Uhusiano wa karibu kati ya China na nchi za Afrika, ambao umekuwa wa kina zaidi baada ya China kuwa na maendeleo makubwa kiuchumi, umekuwa unafuatiliwa kwa karibu na nchi za magharibi, na katika baadhi ya nyakati umekuwa ukipakwa matope kwa kila njia bila mafanikio, kujaribu kuleta migongano kati ya China na nchi za Afrika. Hata hivyo wanaojaribu kuupaka matope uhusiano kati ya China na Afrika, wanajaribu kuiiga China.
Tangu mwanzoni mwa miaka ya 90 hasa baada ya vita baridi kwisha, nchi nyingi za magharibi ziliamua kujiegemeza zaidi kwa nchi za Ulaya Mashariki, na kuziacha pembeni nchi za Afrika na sehemu nyingine za dunia. Wakati huo China iliendelea na moyo ule ule wa urafiki wa karibu kati yake na nchi zilizokuwa zimewekwa pembeni na nchi za magharibi. Bahati ni kwamba huko kuwekwa pembeni, kulikuwa ni kichocheo cha mafungamano ya karibu kati ya China na nchi za Afrika, hadi kufikia ukaribu wa kina ulipo sasa.
Bahati mbaya kwa nchi za magharibi ni kwamba, ule ushawishi uliokuwepo kwa muda mrefu tangu enzi za ukoloni sasa umekuwa ukififia, na ukaribu wa China kwa nchi za Afrika umeendelea kuimarika. Lakini kumekuwa na maswali mengi ya kwanini ushawishi wa China barani Afrika umekuwa ukiongezeka, na kwanini ule wa nchi za magharibi umekuwa ukififia.
Kwa nchi za Afrika China imekuwa ni nchi ya mfano, ambayo imezifahamisha kuwa umaskini au kuwa nyuma kimaendeleo si jambo la kudumu, ni jambo linaloweza kuondolewa kwa juhudi na sera nzuri. Lakini pia China imeimarisha ukaribu wake na nchi za Afrika kwa kuendelea na ukaribu uleule iliokuwa nao na nchi za Afrika hata kabla ya kuwa na maendeleo makubwa kama iliyo nayo sasa.
China kwa upande mwingine imekuwa inarudia kauli yake ya mara kwa mara kuwa maendeleo yake ni maendeleo ya dunia. Nchi za Afrika zimekuwa ni mashahidi wa kauli hiyo ya China. Kupitia mipango mbalimbali ya ushirikiano, iwe ni “Ukanda mmoja, Njia moja” au Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, China imekuwa ikitoa fursa mbalimbali za kuhimiza maendeleo kwa nchi za Afrika. Hii imekuwa ni tofauti na program mbalimbali zilizowekwa na nchi za magharibi au kupitia taasisi za kimataifa za nchi za magharibi, ambazo kimsingi zimekuwa zinaendelea na mifumo kandamizi ya kinyonyaji iliyokuwepo wakati wa enzi za ukoloni.
Tunaweza kuangalia pia jinsi China ilivyojenga sura mpya ya ushirikiano kati yake na nchi za Afrika. Nchi za magharibi mara nyingi zimeweka mifumo ambayo inafanya nchi za Afrika ziendelee kutegemea misaada, na mara nyingi misaada inayotolewa na nchi hizo, au ile inayotolewa na taasisi za kimataifa inazozidhibiti imekuwa na masharti mengi magumu ambayo ni kandamizi kwa nchi za Afrika. China imekuwa inapigania zaidi ushirikiano wa kunufaishana, na kuendeleza dhana kuwa kunakuwa na manufaa zaidi kama pande mbili zinanufaika na ushirikiano na sio upande mmoja tu.
China pia kupitia ushirikiano na nchi za Afrika imekuwa ikitoa fursa za moja kwa moja kwa watu wa Afrika. Tofauti na nchi za magharibi ambazo mara nyingi zimejikita kwenye ushirikiano na nchi za Afrika kupitia makampuni makubwa na mashirika makubwa, China kwa upande mwingine ni zaidi ya hapo, kwani imekuwa ikitoa fursa za moja kwa moja kwa wafanyabiashara wa kawaida wanaopenda kuja China kununua bidhaa au hata kuanzisha shughuli zao na kujiendeleza China. Kwa sasa miji ya Guangzhou, Yiwu na hata Changsha imekuwa ni miji ambayo ina milango mingi ya fursa kwa mwafrika mmoja mmoja.