Kwa hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya Tano, ni dhahiri kuna dalili za nchi kurejesha heshima katika tasnia ya utendaji na itapelekea watumishi wake kujitafakari wanapokuwa wanachukua hatua ama kuhudumia wananchi. Ninaposema kujitafakari namaanisha hakutakuwa na rushwa tena katika ofisi za masjala na hakutakuwa na njoo kesho kwai kila jambo litashughulikiwa kwa ratiba yake.
Nchi inahitaji kupona, Yes ni jambo lisiloepukika. Sote tumemsikia Rais wa Awamu ya Tano akikiri kwamba ndani ya chama chake kuna majizi, wabadhirifu na mafisadi. Pia imeandikwa katika Biblia takatifu kwamba ASIYEWAANGALIA WA NYUMBANI KWAKE HUYO HAFAI KABISA... ingawa waliowengi wanatafsiri kuangalia kuhudumia, lakini katika hili natafakari hata kuwaona na kuwachungua walio ndani mwake maana usaliti ndani ya familia hukaribisha majahili na michepuko. Lakini kwa rais kung'amua kuwa ndani ya nyumba yake kuna ndugu adui basi uponyaji unaanzia hapo. Ameomba tumuunge mkono. Mimi ninamuunga mkono na ninamuombea.
Taarifa na takwimu nyingi za taasisi na mataifa ya magharibi (wakopeshaji wetu kwa jina la wafadhili wa maendeleo) zilimulika nchi za Afrika hususani na Tanzania ikiwemo kama nchi ambazo zimekubuhu kwa rushwa na kukosekana utawala bora. Kwao utawala bora ni pamoja na kuruhusu mahusiano ya jinsia moja bila kuangalia athari zake kitamaduni na kijamii. Pia suala la rushwa, ni kweli nchi zetu zilikubuhu kwa rushwa. Ingawa rushwa zinazoongelewa hapo zinafichwa lakini ndiyo zile za BAE, STANBIC Bank, Uwekezaji katika Nishati na kadhalika. Mataifa hayo kupitia mashirika ya nchi zao wamekuwa watoa rushwa wakubwa kwa viongozi wa Afrika.
Leo hatua kubwa zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa na serikali yetu kudhibiti mianya ya rushwa na kuwachukulia hatua wote wanaobainika kushiriki matendo hayo. Lakini mataifa hayo hayo sasa yanaumbuka kwa kuhusishwa na sakata baya zaidi la ukwepaji kodi na kuficha fedha katika makampuni hewa (Panama Papaers). Viongozi wa nchi hizo ni wahusika wakubwa wa sakata hilo na mpaka sasa hakuna hata mmoja aliyemnyooshea kidole Mmagharibi mwenzake kwa tuhuma hizo. Hakuna mali zao kukamatwa na kuzuiwa, hakuna sheria kufuata mkondo, hakuna kesi.
Kwa unafiki huu wa Wazungu, ninawaasa Watanzania wenzangu, tusisubiri kusifiwa na hao mabwanyenye. Tuchape kazi, tusafishe nchi yetu. Wanaotubeza leo na kusema wanakata misaada watakuja kuomba hiyo misaada kwetu. Ukiona mtu mweupe anakusifia ujue huyo ni MNAFIKI na ujichunguze kasoro ulizonazo.