SHIRIKA la Maendeleo la Ufaransa (AFD) limeeleza kuwa, lina mpango wa kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo ifikapo mwakani.
Emmanuel Baudran, Mwakilishi wa AFD nchini Tanzania ametoa kauli hiyo leo wakati alifanya mazungumzo na Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini alipokwanda kumtembelea.
Baudran ameeleza fedha ambazo zimetolewa kupitia mkopo wenye masharti nafuu zimeelekezwa katika Sekta za Maji, Nishati na Miundombinu ya usafirishaji.
Amesema mwakani shirika hilo limepanga kuongeza kiasi cha fedha kutoka Euro milioni 50 hadi Euro milioni 100 kwa mwaka kupitia mikopo ya masharti nafuu huku kipaumbele kikiwa ni sekta hizo za nishati, maji na miundombinu ya usafirishaji.
Akizunguza na Prof. Muhongo pia watumishi wengine wa wizara hiyo Baudran amesema, Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele na shirika hilo.
Amesema, katika miezi ijayo AFD itajikita katika utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa Gridi ya Umeme ya Taifa, uboreshaji wa vituo 10 vya kupooza umeme pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kutoka Geita mpaka Nyakanazi (220 KV).
Huu ni mpango wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kupanua Gridi ya Taifa kwa upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ambapo itaunganisha Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.
Prof. Muhongo amelishukuru shirika hilo kwa ushirikiano wanaouonesha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini.
Amesema, juhudi hizo zitasaidia kutimiza lengo la serikali la kuwa na umeme wa kutosha na wa bei nafuu ambao utasaidia kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali.
Source: Mwanahalisi