Uenezaji wa Injili

John Magongwe

Member
Jan 4, 2024
73
121
Uenezaji wa Injili

Injili ni Nini

Neno injili limetokana na neno la Kigiriki “euaggelion” lenye maana ya Habari Njema. Hivyo, injili maana yake ni Habari Njema. Katika biblia, injili maana yake ni “Habari Njema za Yesu Kristo”. Habari yo yote inayomhusu Bwana Yesu Kristo, kuzaliwa kwake, kuishi kwake, mahubiri yake, kufa kwake na kupaa kwake, na kurudi kwake mara ya pili, hiyo ndiyo injili ya kweli, na ndiyo Habari Njema.

Kueneza Injili
Wakristo wanawezaje kujihusisha na uenezaji wa injili? Ni lazima wenyewe waieneze injili hiyo. Imeandikwa katika kitabu cha Mathayo: "Ndipo alipowaambia wanafunzi wake mavuno ni mengi; lakini watendakazi ni wachache, basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake."

Kueneza injili ni kazi ya wakristo kote ulimwenguni. Imeandikwa katika Mathayo 28:19-20: "Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi, na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari".

Siyo lazima uwe na elimu ya juu kuweza kuhubiri injili. Imeandikwa katika 1Wakorintho 2:1-5: "Basi ndugu zangu mimi nilipokuja kwenu sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno wala kwa hekima maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo naye amesulibiwa, nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu".

MBINU ZILIZOTUMIKA MWANZONI KUENEZA INJILI
Je, Yesu alitumia mbinu gani ili kuzungumza na umati? Je, Wanafunzi waaminifu wa Kristo walifuataje mfano wake, na kwa nini? Umati unakusanyika na kumzunguka Yesu kwenye ufuo wa bahari, hivyo anaamua kupanda mashua na kusonga mbali kidogo. Kwa nini? Anajua kwamba mawimbi ya maji yangekuza sauti yake na watu wengi wangesikia vizuri ujumbe wake (Marko 4:1-2).

Wanafunzi waaminifu wa Kristo walifuata mfano wake na kutumia mbinu mpya ili kueneza habari njema za Ufalme kwa watu wengi. Chini ya mwongozo wa Mfalme, watu wa Mungu wanaendelea kubuni njia mpya na kuzitumia kadiri hali zinavyobadilika na teknolojia mpya kutokea, ili kuwafikia watu wengi iwezekanavyo kabla mwisho haujafika (Mathayo 24:14).

MBINU ZINAZOTUMIKA SASA KUENEZA INJILI
Mbinu zinazotumika kwa sasa kueneza injili ni pamoja na zile zifuatazo.

1. Makanisani
Mungu amewapa wafuasi wa Yesu waliotiwa mafuta madaraka ya kutangaza habari njema duniani kote
. “Kondoo wengine” wa Kristo wanaozidi kuongezeka wanawaunga mkono katika kazi hiyo ya kueneza injili (Yohana 10:16).

Leo, watangazaji wengi wa Ufalme wanatumia nafasi zinazojitokeza za kupanua zaidi kazi yao ya kueneza injili. Maelfu wanaeneza injili wakati wote wakiwa vinara wa kawaida na wasaidizi. Pia, wanaume, wanawake, na watoto wanafanya kazi nzuri ya kutangaza Ufalme kwa bidii. Naam, Yehova anawabariki sana watu wake wote wanapomtumikia bega kwa bega wakiwa waeneza injili (Sefania 3:9).

Kuna baadhi ya watumishi wa Mungu leo, ukiwauliza injili ya Yesu Kristo ni nini hasa, wataishia tu kusema kuwa ni habari njema. Hii inatokana na upungufu wa elimu sahihi ya theolojia na ukosefu wa vitendea kazi kwenye kazi ya huduma kama vile vitabu vizuri ambavyo mtumishi anaweza kujisomea mwenyewe na kuongeza maarifa ya Neno la Mungu.

Injili ni zaidi ya kuhubiri na ushuhuda. Imeandikwa katika Isaya 60:1: "Ondoka ukaangaze kwa kuwa nuru yako imekujia na utukufu wa Bwana umekuzunguka. Imeandikwa pia katika Isaya 61:1: "Roho ya Bwana Mungu i juu yangu kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema, amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao na hao waliofungwa habari ya kufunguliwa kwao".

Kwa sababu ya kukosa ufahamu wa kutosha juu ya injili ni nini, baadhi ya watumishi wanadhani kuwa injili ni kwa ajili ya watu wasioamini ambao wanahitaji kuokolewa na wakishaokoka basi hawahitaji tena injili. Ni kweli injili inawahusu watu ambao hawajaokoka, lakini hata wakishaokoka bado wanahitaji kuhubiriwa/kufundishwa injili ya Yesu Kristo. Kuna sababu nyingi kwa nini ni muhimu sana kufanya hili, yaani kuhubiri injili kwa waaminio. Kubwa ni kupata ufafanuzi zaidi kuhusu Neno la Mungu, na kuimarisha imani, kwa vile shetani yuko vitani muda wote.

Kanisa la Mungu limegawanyika kwenye baadhi ya mambo ya msingi kuhusu injili. Mfano suala la kuhesabiwa haki, suala la utakaso, suala la uhusiano wa sheria na neema, hata juu ya maana ya injili yenyewe, wengine wamelenga kwenye mafanikio na uponyaji tu, Wengine ufalme wa Mungu tu, wengine wokovu kwa imani tu, n.k. Mitizamo ni mingi, na wakati mwingine huzaa mabishano Hivyo, tunahitaji kuendelea kufundishana kwa upendo na uvumilivu juu ya injili ya Yesu Kristo, kwa kuzingatia kanuni sahihi za kutafsiri maandiko ili tuendelee kumfahamu sana Mwana wa Mungu na hata kuufikia umoja wa imani.

Injili ya Yesu Kristo ndiyo mchezaji wa kiungo anayeunganisha mafundisho yote. Timu ya mpira ikikosa mchezaji wa kiungo haiwezi kufanikiwa. Injili ndiyo fundisho linalounganisha, na ndiyo msingi wa mafundisho yote.

Waumini leo wanasikia injili za kila namna kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii na manabii wa uwongo. Wasipohubiriwa injili ya kweli ni rahisi sana kuyumbishwa na kuchukuliwa na upepo wa kila namna.

2. Mikutano ya hadhara

Mikutano ya hadhara hufanywa na watu binafsi au makanisa mbalimbali. Hii ni kuwezesha wale ambao hawakupata nafasi ya kwenda makanisani kutokana na sababu mbalimbali, kuweza kusikia neno la Mungu. Aidha, sababu nyingine ni kushawishi wale ambao hawajaamua kujiunga na Kristo kuweza kufanya hivyo. Maeneo ya hadhara ni pamoja na sokoni, vituo vya mabasi, vituo (centres) vya madukani, na kwenye maeneo ya wazi.

3. Vyama au makundi ya kujifunza biblia
Je, Kuna umuhimu wa kujifunza Biblia katika kikundi?
Ndiyo. Kwa sababu Ukristo haukukusudiwa kuwa juhudi ya mtu binafsi. Mafunzo ya Biblia katika kikundi siyo ya thamani tu, bali ni ya thamani isiyokadirika. Kujifunza katika makundi ya watu wachache ni njia nzuri sana ambayo Yesu aliitumia kuwafundisha wanaume ambao wangetambulika kuwa mitume (Luka 6: 12-16; Marko 4:34).

Ukristo umekusudiwa kuwa wa uhusiano, kwanza, kati yetu na Mungu na, pili, kati yetu na wale wanaotuzunguka. Mafunzo ya kikundi cha watu wachache cha Biblia hutuhamisha kutoka kuwa watazamaji katika ibada ya kanisa ya kila wiki, hadi kuwa washiriki wenye bidii katika jamii yenye nia moja iliyojitolea kwa ukuaji wa kiroho.

Tunapolichambua Neno la Mungu pamoja, tuna nafasi ya kushiriki mitazamo na ufahamu wetu tofauti na tunapanuliwa kwa sababu ya kuamshana. Habari zaidi huhifadhiwa wakati kuna ushirikiano tendaji. Kwa hivyo, ufahamu wetu wa Biblia huimarishwa. Matumizi na uwajibikaji huleta uelewa ambao huhamisha Neno la Mungu kutoka kwa akili hadi moyoni. Mabadiliko yanahimizwa (Warumi 12:2-3), na maisha yetu yanabadilishwa. Wakati maisha yetu yanabadilishwa, maisha ya wale wanaotuzunguka yanabadilishwa pia.

4. Jumuiya za waumini kwenye makazi yao
Hizi ni jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinazoanzishwa ili kutekeleza upendo katika maisha ya kila siku mitaani. Katika jumuiya hizo, waumini hukutana kila wiki, katika siku iliyokubalika na kanisa, ili kusoma Neno la Mungu na kusali pamoja, na kushirikiana katika kukabili changamoto za mazingira yao.

5. Nyumba hadi nyumba
Kristo na wafuasi wake wa mapema waliweka kielelezo gani katika huduma?
Yesu Kristo aliwawekea wafuasi wake kielelezo kizuri cha kueneza injili. Neno la Mungu linasema hivi kuhusu huduma ya Kristo na mitume wake: ‘Alisafiri kutoka jiji mpaka jiji na kutoka kijiji mpaka kijiji, akihubiri na kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu. Na wale kumi na wawili walikuwa pamoja naye’ (Luka 8:1). Namna gani mitume wenyewe? Baada ya roho takatifu kumwagwa siku ya Pentekoste, “kila siku katika hekalu na nyumba kwa nyumba wakaendelea bila kuacha kufundisha na kutangaza habari njema juu ya Kristo Yesu” (Matendo 5:42).

Huduma ya nyumba kwa nyumba wakati mwingine huwa ngumu. Kwa mfano, watu wengine huudhika wanapotembelewa nyumbani kwao kukiwa na ujumbe wa Biblia. Nia si kuwaudhi. Hata hivyo, huduma ya nyumba kwa nyumba inaungwa mkono na maandiko, na huchochewa na upendo wetu kwa Mungu na kwa jirani kutoa ushahidi kwa njia hiyo (Marko 12:28-32).

6. Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii
Vyombo vya habari
vinavyotumika ni pamoja na magazeti, TV na redio.

Mitandao ya kijamii inatumika sana kueneza injili. Hii ni kupitia mtu mmoja mmoja kutuma neno la Mungu kwenye moja ya mitandao au hata zaidi ya mtandao mmoja. Waumini na wasio waumini hupitia mitandao na kusoma injili zilizotumwa humo; hivyo, Neno la Mungu huenea.

Katika hili, taasisi au makundi ya watu wamefungua blogu, ambamo huweka Habari Njema, kwa ajili ya watu kusoma, na wengine kufuatilia (follow). Mitandao mingi hupokea thread/somo fupi za ukurasa mmoja, na mitandao michache mifumo yao huruhusu kupokea thread ndefu kiasi cha kufikia kurasa kumi. Watu huendelea kusoma thread/masomo husika, mwaka hadi mwaka.

Kwa hiyo, injili ni habari yo yote inayomhusu Bwana Yesu Kristo, kuzaliwa kwake, kuishi kwake, mahubiri yake, kufa kwake na kupaa kwake, na kurudi kwake mara ya pili. Hiyo ndiyo injili ya kweli, na ndiyo Habari Njema.

Uenezaji wa injili hufanyika kwa njia mbalimbali. Njia hizo ni pamoja na makanisa, mikutano ya hadhara, vyama au makundi ya kujifunza biblia, jumuiya za waumini kwenye makazi yao, nymba hadi nyumba, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na vitabu mbalimbali.
 
Jiepushe na ukoloni mambo leo kupitia dini za majahazi.
Siku huyo mungu akitaka mumjue aje mwenyewe kwetu Afrika, sio akawatume wazungu na waarabu. Hizo ni dharau.

By the way, dini ni scam iliyo dhahiri kabisa.
 
Jiepushe na ukoloni mambo leo kupitia dini za majahazi.
Siku huyo mungu akitaka mumjue aje mwenyewe kwetu Afrika, sio akawatume wazungu na waarabu. Hizo ni dharau.

By the way, dini ni scam iliyo dhahiri kabisa.
BWANA AKUREHEMU
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…