Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,739
- 13,502
UBORA WA MAUDHUI YA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA 2018
UTANGULIZI
Wanataaluma wa tasnia ya habari, wanahabari, na jamii kwa ujumla wana matarajio sawa kuhusu ubora wa vyombo vya habari. Matarajio haya yanajumuisha kuandika/kurusha habari zenye maslahi kwa jamii, kuzingatia ukweli, kutoa habari sio tu za matukio ya kila siku, bali kwenda mbali zaidi na kuchambua masuala mbalimbali. Uandishi wa namna hii utaweza kujenga ajenda za kisiasa, utazalisha majukwaa ya midajala na kuhamasisha mitazamo mbalimbali, na kuwawajibisha walio na mamlaka.
Utafiti huu unaangazia ubora wa vyombo vya habari kwa kutumia vigezo maalumu vya ubora wa habari. Utafiti huu umefaidika sana na utafiti wa awali wa mwaka 2017 na umeongeza idadi ya vyombo vya habari kutoka 12 kwa mwaka 2017 mpaka 25. Pia, umejumuisha vyombo vya habari kama redio za kijamii, redio za mikoani, blogu, mitandao, vyombo vya habari vya mitandaoni na vyombo vya habari kutoka Zanzibar.
Mazingira ya Kibiashara
Mazingira ya kibiashara yametawaliwa na kushuka kwa mapato yatokanayo na matangazo kwa redio, magazeti na televisheni, watangazaji kuhamishia matangazo yao kwenye vyombo vya habari vya mtandaoni, na kuhama kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji kutoka vyombo vya habari vya jadi kwenda vyombo vya habari vya mtandaoni. Kushuka kwa matangazo kwa sehemu fulani kumechangiwa na maamuzi ya Serikali kupunguza bajeti yake ya matangazo ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza matumizi. Kabla ya uamuzi huu, Serikali ilikuwa ndio mtangazaji mkuu kwenye vyombo vya habari nchini.
MBINU ZA UTAFITI
Moja ya mbinu za kitafiti za kupima namna vyombo vya habari vinavyoripoti habari zao, ni kwa kuchambua maudhui yanayotolewa (habari, makala, na vipindi) kwa kutumia vigezo vinavyofanana.
Utafiti huu umetumia vigezo maalumu vya kupima ubora wa maudhui ambavyo vilijadiliwa na kukubaliwa na wahariri na wadau wa sekta ya habari . Vigezo hivi vimekuwa vikitumika kupima ubora wa maudhui nchini . Vigezo hivi vimegawanyika katika maeneo manne kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini
Mwaka 2017, jumla ya vyombo vya habari 12 vilijumuishwa kwenye utafiti wa majaribio. Wakati wa kujadili matokeo ya awali ya mwaka 2017, ilipendekezwa kwamba utafiti wa mwaka 2018 ujumuishe vyombo vya habari vingine kutoka Tanzania Bara na Zanziabar, na hususani redio za mikoani. Baada ya majadiliano na wadau mbalimbali, jumla ya vyombo vya habari 25 vilijumuishwa kwenye utafiti huu
MATOKEO YA UTAFITI
Sampuli ya utafiti huu umejumuisha habari, makala, vipindi na posti 1,886 kutoka magazeti 7, redio 12, televisheni 4, blogu 1, na mtandao 1. Uwasilishaji wa matokeo unatenganisha redio za mikoani na redio za kitaifa kutokana na tofauti zao.
1. Mada zilizoripotiwa na vyombo vya habari
Masuala yanayoangaziwa na vyombo vya habari ni pamoja na uchumi(29%) hii ikijumuisha miundombinu, mafuta na gesi, usafirishaji, biashara; masuala na maendeleo(28%) ikiwemo afya, elimu, kilimo na mazingira. Masuala yenye mvutano kama matatizo ya kijamii, migogoro, haki za binadamu, masuala ya jinsia, utawala bora nakadhalika yamechukuwa asilimia 16.
Ajali na uhalifu/kesi za mahakamani zimeripotiwa kwa asilimia 12. Kuripotiwa kwa masuala ya kisiasa kuko chini (11%), hii ikijumuisha maudhui ya sera, uchaguzi, usalama wa taifa, na majadiliano ya kisiasa. Masuala ya utamaduni, vyombo vya habari na tafiti vimeguswa kwa kiasi kidogo
Hata hivyo, kila kundi la vyombo vya habari lina namna lilivyoangazia mada hizi kama inavyoonekana kwenye chati hapa chini.
Televisheni zinaongoza kuripoti habari za kiuchumi na ajali/uhalifu, huku zikitoa nafasi kidogo kwa habari za maendeleo na kisiasa. Michuzi blog ina idadi kubwa ya habari zenye maudhui ya ajali/uhalifu, na maendeleo na uchumi, lakini idadi ndogo sana ya habari za kisiasa na zenye utata. JamiiForums inaongoza kutoa taarifa za kisiasa (kama magazeti), na idadi kubwa ya habari zenye utata (kama redio za mikoani).
2. Habari za kitaifa na za mikoani
Redio za mikoani zinaripoti zaidi habari za mikoani (71%, ukilinganisha na wastani wa 60%). Michuzi Blog ina habari nyingi zaidi zenye taswira ya mikoani, wakati JamiiForums imejikita kwenye masuala yenye taswira ya kitaifa.
3. Sababu za kuripotiwa kwa habari
Matokeo yanaonyesha kwamba magazeti yanaweka sababu za kuripotiwa kwa habari fulani (ikipimwa kwa kuwa na paragrafu mbili au zaidi ambazo zinatoa maelezo ya sababu husika) kwa 37%, wakati redio za kitaifa zinafanya hivyo kwa 15%.
Idadi kubwa ya habari zisizokuwa na sababu ya kuripotiwa kwa habari husika ni za redio za kitaifa na Michuzi Blog. Mlengo wa JamiiForums ni wa kujenga mijadala na kubadilishana mitazamo, na sio sana katika kuchimba na kupata sababu za kwanini jambo fulani limetokea. Hii inaonekana kuwa ni wajibu wa magazeti au TV.
4. Ujumuishaji wa mitazamo mbalimbali kwenye habari
Uwepo wa mitazamo mbalimbali kwenye habari/kipindi ni njia nzuri ya kuwajuza wananchi. Inatoa fursa ya kuonyesha kwamba watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti na hivyo kuifanya habari iwe kamili na yenye mizania. Mada zinapaswa kuripotiwa kwa kutumia lensi tofauti, ambayo inaongeza ukamilifu wa habari.
Magazeti yanaongoza kwa kuripoti habari kwa kutumia angalau lensi mbili kwa 24% ya habari zote, yakifuatiwa na redio za mikoani(12%), redio za kitaifa (10%), na TV (10%). Kwenye Michuzi blog na JamiiForums, hali sio nzuri kwani kuna mtazamo zaidi ya mmoja kwa asilimia 1 na 3, mutawalia.
4.1 Ujumuishaji wa maoni kwenye habari
Chati namba 9 inaonyesha kwamba magazeti (32%) na JamiiForums (38%) ndio yanajumuisha maoni mbalimbali kwenye habari/taarifa zao, yakifuatiwa na redio za mikoani (29%). Redio za kitaifa zinafanya hivyo kwa 17%. Michuzi Blog inafanya hivyo kwa 1%.
Kuweka mizania katika habari ni msingi mkuu wa uandishi wa habari kwa kuhakikisha kwamba maoni kinzani yanapewa nafasi. Hili linaonekana kufanywa zaidi na JamiiForums na sio vyombo vya habari.
Ni nadra kwa vyombo vya habari kutoa habari zenye kuikosoa Serikali. Ni JamiiForums pekee ambayo ina maudhui yenye mlengo huo kwa 35%, ikifuatiwa na redio za mikoani na magazeti ambazo zina 4% kila moja. Tayari mwaka 2017 wahariri walishabainisha kwamba vyanzo vya habari vyenye mawazo kinzani na serikali haviko tayari kuzungumza hadharani.
Muundo mzuri wa habari unamwongoza msomaji au msikilizaji kuanzia mwanzo hadi mwisho wa habari husika. Redio za kitaifa ziko chini kidogo ya wastani (56% ya muundo mzuri wa uandishi), ikiwakilishwa na magazeti na redio za mikoani. Vituo vya televisheni na JamiiForums vinafanya vizuri, ingawa tofauti sio kubwa kama inavyoonekana kwenye chati namba 11.
Imeandaliwa na
Baraza la Habari Tanzania likishirikiana na Spurk Media Consulting Ltd., Bern, Switzerland
Watafiti
Christoph Spurk, Bern, Switzerland,
Abdallah Katunzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania