Uadilifu unatakiwa fedha za elimu bure

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
WIKI iliyopita Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa taarifa kwamba tayari Sh bilioni 18.77 kwa ajili ya mpango wa kutoa elimu bure, zimeshapelekwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari nchi nzima.

Fedha hizo ni kwa ajili ya mwezi huu wa Januari ambao shule zinafunguliwa. Hatua hiyo imethibitisha kwamba ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba imedhamiria kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne, haikuwa maneno ya kuombea kura majukwaani bali ni ya dhati.

Hii pia inaashiria kwamba ahadi nyingi za Rais John Magufuli zitafanyiwa kazi, hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kuwa na utayari na kutimiza wajibu wake kadri anavyoweza huku akitanguliza mbele uadilifu na uzalendo kwa nchi yake.

Katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, serikali imewataka wahusika kuweka wazi fedha walizopokea kutoka serikalini, ikiwa ni pamoja na kubandika kwenye mbao ili wananchi wafahamu alichopewa mhusika na matumizi yake.

Bodi za shule zimepewa, pia kazi ya kuhakikisha zinasimamia matumizi ya fedha hizo na kutoa taarifa kwa atakayebainika kutumia fedha hizo, vinginevyo ili achukuliwe hatua stahili. Mikoa mingi imekiri kupokea fedha hizo.

Kwa mfano, mkoa wa Mwanza ulikiri Alhamisi iliyopita kupokea Sh 642,643,000 na kwamba pesa hizo tayari zimeshatumwa kwenye shule za msingi za serikali 850 mkoani humo na sekondari 197.

Mkoa wa Rukwa pia ni miongoni mwa mikoa iliyokiri kupokea Sh milioni 336 kwa ajili ya shule za msingi 360 na sekondari 105. Kwanza tunaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuanza kutekeleza ahadi hiyo ya kutoa elimu bure, ambapo mzazi atabaki na jukumu dogo la kununua sare, madaftari, kalamu na vitabu vya rejea.

Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema kwamba namna nzuri ya kumsaidia mtoto wa maskini ni kumpa elimu na hakuna ubishi kwamba ada na michango mashuleni zimekuwa zikichangia familia kadhaa maskini kushindwa kusomesha watoto wao.

Hata hivyo, hofu yetu iko kwa baadhi ya watendaji wenye dhamana ya kuzitumia pesa hizi kwa malengo yaliyokusudiwa. Na hili haliko kwetu tu bali takribani kila aliyezungumzia pesa hizi, kuanzia Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said Magalula na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk Faisah Issa, wameonya na kuapa kuwashughulikia watakaotumia pesa hizo kwa malengo tofauti.

Hofu hii inatokana na tabia iliyojijenga huko nyuma ya baadhi ya watu kuamini kwamba fedha za umma ni za kula tu; na hivyo huenda wakawepo watu watakaotaka kula fedha hizi au kuzitumia kwa namna isivyokusudiwa, licha ya makemeo haya na hatua za kutumbua majipu zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Ni imani yetu kwamba uadilifu utatawala katika matumizi ya fedha hizi, na wale wote watakaokiuka matumizi yake, tunaamini watashughulikiwa mara moja na mamlaka husika bila kuonewa haya.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…