Twaweza leo wamezindua Ripoti ya utafiti wao inayoitwa "Safi na Salama"?
Ripoti hii inawasilisha takwimu juu ya upatikanaji wa maji, njia za kutibu maji na usafi wa mazingira kwa ujumla.
Takwimu hizi zinajibu maswali kama:
Je, jitihada na uwekezaji katika Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji na ule wa Matokeo Makubwa Sasa vimeleta tija katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa wananchi?
Je, ni njia kuu zipi za kutibu maji zinazotumiwa na wananchi?
Je, ni wananchi wangapi walioshiriki kwenye kampeni ya jamii ya kufanya usafi iliyohamasishwa na Rais Magufuli?
Moja ya Matokeo ya utafiti huu yaliyojumuishwa kwenye ripoti ni hali ya upatikanaji wa maji safi na salama:
========
Ili kupata picha halisi ya mwenendo wa upatikanaji wa maji, hasa katika maeneo ya vijijini, tunalinganisha takwimu juu ya upatikanaji wa maji kutoka awamu kadhaa za utafiti wa Sauti za Wananchi na takwimu zilizokusanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupitia tafiti zake za kaya, pamoja na takwimu zilizoripotiwa na Wizara ya Maji (MoW) na matokeo yaliyoripotiwa na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Mwenendo wa takwimu zilizokusanywa na NBS pamoja na Sauti za Wananchi zinanonesha kwamba upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijijini haujabadilika tangu mwaka 2015. Kati ya tafiti kumi na nne, kumi na mbili kati ya hizo zilikadiria kwamba kati ya asilimia 41 na asilimia 48 ya kaya zinatumia vyanzo vilivyoboreshwa kwa ajili ya maji ya kunywa.
Hata hivyo, takwimu za Sauti za Wananchi zinaonesha kuwa upatikanaji umepungua kutoka asilimia 55 mwaka 2014 hadi asilimia 46 mwaka 2016.
Wizara ya Maji imeripoti kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji kati ya asilimia 50 na asilimia 60, na takwimu za Matokeo Makubwa Sasa pia zinaripoti ongezeko la kasi kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi asilimia 67 mwaka 2015.
=====