Petro E. Mselewa, majibu mengi unayopewa humu yanazidi tu kuthibitisha hayo unayosema...ni kweli kuwa uelewa wa Watanzania walio wengi ni mdogo sana. Wachache wenye uelewa kiasi unafiki umewetawala mioyo yao na ulafi matumbo yao. Wamebaki wanatumia ushabiki wao kuliko akili na bahati mbaya hata jamvi letu hili halikupona.
Ukiwauliza hawa watu kwa nini Magufuli angalau haipi hoja ya Katiba mpya kipaumbele ili hatua zake zipate nguvu kisheria hawana majibu. Inakuwaje watu waliopinga Rasimu ya Katiba ya Warioba sasa wachangamkie kukurupuka kwa viongozi bila kuzingatia sheria zinasemaje? Huku ni kuonesha kiwango cha kutisha cha ulemavu wa fikra.
Kwa upande wangu nitazidi kumuomba Mh. Tundu Antipas Lissu asichoke na azidi kutoa elimu kwani gharama za ujinga siku zote ni kubwa sana. Utalaumuje dhambi za watumishi wa awamu zilizopita huku unajua vitendo vyao vilikuwa na baraka za Viongozi wao wakuu ambao kama Katiba ingeruhusu, wangetakiwa kutangulia Keko.
Mkapa anatamba mitaani akiwa huru na Kikwete anapeta mitaani akiwa huru, huku kila moja anajua wao ndio walikuwa vinara wa ufisadi nchini. Fikiria Rais wa nchi anajimilikisha migodi wa Kiwira, Rais anaingia madarakani kwa hela ya wizi na rushwa au Rais anaiingiza nchi kwenye mkataba mkubwa wa umeme nchini na kampuni hewa!
Lakini baya kupita yote, ni chama tawala kujimilikisha miradi, rasilmali za taifa na mali za wananchi bila ridhaa yao na kuzitumia kwa manufaa ya wachache. Kama Magufuli angekuwa na dhamira ya kweli kulinusuru taifa hili kutoka kwenye tope la maovu angeanza kwa kutuomba radhi, tumsamehe yeye na chama chake halafu tuanze upya.
Ukitaka mti ufe kabisa na usije ukachipuka tena unahakikisha umekata mizizi na siyo matawi kama anavyofanya Magufuli, hapana, huu ni usanii. Huanzi kujenga ukuta wa nyumba, unajenga msingi kwanza unaoweza kustahimili uzito utakaotua juu yake...Magufuli tafadhali, fufua mara moja mchakato wa Katiba mpya, Rasimu ya Warioba.