SI KWELI Tundu Lissu apongeza Tume Mpya ya Haki Jinai, iliyoundwa na Rais Samia

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Source #1
View Source #1
Kuna Taarifa zilizosambaa kwenye Mitandao ya Kijamii, zinazodai Tarehe 31 Januari 2023 wakati Tundu Lissu akifanya Mahojiano ya channel ya YouTube ya Jambo TV, kwamba alimpongeza Rais Samia kwa kuunda Tume mpya ya Kuchunguza Haki Jinai. Taarifa hizo ni Uzushi.

Uzushi huo ulidai kuwa Tundu Antipas Lissu alisifia kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai, hata hivyo, kwa mujibu wa video iliyorekodiwa wakati wa mahojiano hayo Lissu hakupongeza kuundwa kwa tume ya haki jinai wala hakuzungumzia kundwa kwa tume ya haki jinai bali alizungumzia mfumo wa haki jinai kwa kukosoa mfumo huo.

SWAHILI TIMES FAKE.jpg
Tarehe 31 Januari 2023 Rais Samia alizindua Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai. Rais Samia alisema Tume hiyo imeundwa kutokana na kuvurugika kwa mifumo ya haki jinai ambayo inachangiwa na kupuuzwa kwa mifumo ya maadili na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi wasio na uwezo kupoteza haki zao.

Taasisi zitakazofanyiwa tathmini na Tume hiyo ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Tathmini imeanza 1 Februari 2023 na matokeo yatakabidhiwa 31, Mei 2023. Itafanya kazi kwa muda wa miezi minne.

Tarehe 06 Januari 2023, Rais Samia aliunda Tume hii ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mohamed Othman Chande na Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue. Wajumbe wengine ni pampoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk Eliezer Feleshi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Utumishi) Dk Laurean Ndumbaro, Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu Said Mwema na Mkuu wa Jeshi la Polkisi mstaafu Balozi Ernest Mangu. Wengine ni pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dk Edward Hosea, Askari Polisi mstaafu, Saada Makungu, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco Omar Issa, Ofisa mwandamizi Ofisi ya Rais Baraka Leonard na Mkurugenzi wa Utafiti katika Chuo Kikuu cha Zanzibar na Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Yahya Khamisi Hamad.

6-26-scaled.jpg
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Mhe. Mussa Azan Zungu, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini Mhe. Eng. Hamadi Masauni, Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Zena Said pamoja na Wajumbe wa Tume ya kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 31 Januari, 2023.
 
Tunachokijua
Kwenye video iliyorekodiwa Lissu alisema kuwa:

" Hawa Mapolisi wastaafu ni mapolisi waliokuzwa kwenye mfumo gani, walikuwa MaIGP wa jeshi gani Hili hili, wanaleta uzoefu na ufahamu wa jeshi lipi hili hili. Falsafa ya upolisi wanayoleita kwenye hiyo kazi ni falsafa ya upolisi hii hii halafu mnategemea maajabu hilo la kwanza la pili.

Ingekuwa bora zaidi kazi ya polisi reform iwe ni sehemu ya constitutional reform kuna matatizo ambayo yameshakuwa makubwa kiasi kwamba kuyatibu kwa kuyaundia tume ni kupoteza muda na pesa za umma.

Nchi hii imeshaunda tume ngapi za kushughulikia maswala hayo tangu mwaka 61". Ameongeza kwamba haya mambo yanayozungumzwa yamo kwenye Tume ya Jaji Nyalali, Kwenye ripoti ya Warioba Utayakuta, Tume ya Jaji Chande Utayakuta. Hivyo sio kitu kigeni. Aliongeza Tundu Lissu.

"Ukitaka kuzima jambo Wanasema Wenyewe, Ukitaka kufunika kombe ili Maharamia yapite, Unaliundia Tume". Halafu ukiuliza wanasema Jamani, Si Mheshimiwa rais ameunda Tume? Subirini, Mnapunguza moto, Maharamia yanapita". Alisema Tundu Lissu.

Tundu Antiphas Lissu ni Makamu mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria nguli, aliyepata kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Pia aligombea Urais wa Tanzania Mwaka 2020.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom