Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC ) yaongeza muda wa usajili kwa Taasisi hadi 30 Aprili, 2025

Mkalukungone mwamba

JF-Expert Member
Aug 29, 2022
748
1,611
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeongeza muda wa mwisho wa usajili kwa taasisi zote za umma na binafsi ambazo hazijajisajili kabisa na ambazo hazijakamilisha hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2025 baada ya muda wa usajili wa hiari kumalizika tarehe 31 Desemba, 2024 kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

Taarifa ya leo Januari 10, 2025 iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia imesema Tume hiyo inatambua juhudi za taasisi ambazo tayari zimesajiliwa na kubainisha kwamba pamoja na jitihada hizo, Tume imebaini idadi kubwa ya taasisi ambazo hazijaanza kabisa zoezi la kujisajili ukiacha taasisi chache ambazo bado hazijakamilisha usajili.

“Ikumbukwe kwamba, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ilianza kufanya kazi tangu tarehe 01 Mei, 2023, hivyo basi kutokuzingatia matakwa ya Sheria hiyo, kunahatarisha juhudi za Serikali za kulinda haki za faragha na taarifa binafsi za wananchi na pia kunadhoofisha uadilifu katika kuboresha usimamizi wa maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.”——imesema taarifa hiyo

Aidha PDPC imesisitiza kuwa Taasisi zitakazoshindwa kujisajili ndani ya muda huo zitachukuliwa hatua kali za kisheria, zikiwemo adhabu na hatua nyingine zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Kuanzia tarehe Mei 01, 2025, PDPC kwa kushirikiana na vyombo vya utekelezaji wa sheria, itaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya taasisi zote ambazo hazijazingatia matakwa ya Sheria husika.

Soma Pia: JamiiForums yashirikiana na DPDC kuendesha Mafunzo ya Uelewa wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa Mahakimu Wakazi wa Mikoa 29

Taasisi ambazo zitabainika hazijasajiliwa zitakabiliwa na adhabu za kisheria, ikiwemo faini kubwa na hatua nyingine za utekelezaji kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

PDPC itaendelea kutoa elimu, maelezo na miongozo kwa umma na kwa taasisi zinazofanya mchakato wa usajili. Aidha, jitihada za kuongeza uelewa wa umma kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi na mahitaji ya uzingatiaji zitaimarishwa katika kipindi hiki.

Snapinsta.app_473336785_516501320794900_8201407474812284890_n_1080.jpg
Snapinsta.app_473426559_955606319312925_7790241316321194790_n_1080.jpg
Snapinsta.app_473130020_1644765136464619_4255198305134731027_n_1080.jpg
 
Back
Top Bottom