SIKU chache baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamis Kigwangalla, kutoa tamko la kuwataka watoa huduma za tiba asili na mbadala, tamko hilo limepingwa na Jukwaa la Tiba Asilia na Mbadala Tanzania.
Katika tamko lake, Dkt. Kigwangalla alipiga marufuku matangazo yote yanayotolewa na Matabibu kwa ajili ya elimu kwa umma katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, kuwasilisha nyaraka zote muhimu kuhusu huduma wanazotoa ndani ya siku 14.Pia Dkt. Kigwangalla aliwataka
Matabibu hao kuwasilisha nyaraka zote za kumiliki mashine zinazotumika kufanya uchunguzi wa tiba asili, mbadala na kulitaka Baraza la Tiba Asili na Mbadala, kupitia nyaraka zote ambazo zinahusu usajili wa watoa huduma, vituo na maduka ya dawa asili ndani ya siku 14 kuanzia Desemba 24 mwaka huu.
Dkt. Kigwangala alitoa tamko hilo siku chache baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye Kituo cha Tiba Asili na Mbadala cha Foreplan Clinic, kilichopo Ilala, Bungoni, kinachomilikiwa na Tabibu Juma Mwaka.
Baada ya kufanya ukaguzi kituoni hapo, alitoa siku saba kwa Baraza hilo kuchunguza huduma zinazotolewa katika kituo hicho ambacho Tabibu wake amejipatia umaarufu mkubwa kama mmoja wa Matabibu wa tiba mbadala kutokana na vipindi vyake vinavyoelezea tiba ya maradhi mbalimbali ya binadamu kwa kutumia tiba asilia.
Kutokana na tamko hilo, jana Matabibu wa tiba hizo kutoka mikoa mbalimbali nchini, walikutana Dar es Salaam na kulipinga kwa hoja ya viongozi wa Jukwaa la Tiba Asili Tanzania kutoshirikishwa.
Jukwaa hilo limewataka baadhi ya viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, kutoichukulia dhana ya 'Hapa Kazi Tu' kufanya maamuzi yasiyofaa mbele ya jamii badala yake waangalie namna ya kutoa mwongozo kwa Matabibu kuhusu sheria ya utoaji elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
Nao wanachama wa Jukwaa hilo, waliitaka Serikali kuitambua tiba asili na mbadala kwani Watanzania wengi wamenufaika na dawa hizo.
Walisema yapo magonjwa mengi yanayowasumbua Watanzania ambao kwa muda mrefu wametumia tiba za kisasa hospitalini bila kupona lakini walipotumia tiba asili na mbadala, zimewasaidia na kupona.
Akitoa tamko la Jukwaa hilo, Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Bonaventura Mwalongo, alisema tamko la Wizara hiyo limelenga kudhoofisha nia njema ya utoaji huduma za tiba asili.
Aliwataka Matabibu wote wa tiba asili na mbadala, kuwa wavumilivu katika kipindi hiki akiwataka watoe ushirikiano wa hali na mali kwa viongozi wa taasisi zinazosimamia masuala ya tiba asili ngazi ya Taifa ili kupata mwafaka baina yao na Serikali.
"Kusiwe na matamko mengine zaidi ya hili, tamko la mtu mmoja mmoja linaweza kudhoofisha umoja tulionao hasa kwa kuzingatia kuwa, asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba asili kupata tiba," alisema Mwalongo.