Tetemeko la ardhi Bukoba litetemeshe wanasiasa

mcubic

JF-Expert Member
Mar 3, 2011
10,310
6,544
WATU 16 wameripotiwa kupoteza maisha baada ya tetemeko la ardhi (earthquake) kadirio kubwa kutikisa Bukoba, Kagera na watu zaidi ya 200, imeelezwa wamejeruhiwa kwa viwango tofauti vya majeraha.

Maumivu hayapimiki kwa watu waliopoteza ndugu na wanafamilia wanaowapenda, hasara ni kubwa kwa walioharibikiwa na mali, mtikisiko wa Bukoba na Mkoa wa Kagera ni wa kiwango cha juu, na taifa zima lipo msibani.

Tetemeko la ardhi linapotokea kwa kawaida huwa haliwi lawama kwa mtu, maana tangu Tetemeko la Ardhi la Shaanxi 1556, lililotokea katikati ya Karne ya 16, wanasayansi wamekuwa wakiumiza kichwa ili kutabiri matukio yajayo kuhusu tetemeko bila mafanikio.

Tetemeko la Ardhi la Shaanxi 1556, lilitokea Januari 23, 1556, Jimbo la Shaanxi, China. Watu zaidi ya 830,000 walipoteza maisha. Hiyo ndiyo rekodi kubwa zaidi ya maafa kwa matukio ya tetemeko la ardhi. Kuanzia hapo wanasayansi wamekuwa wakijitahidi kufanya utafiti ili wapate uwezo wa kubashiri yajayo lakini hakuna mafanikio.

Shabaha ya wanasayansi kutafuta vipimo vyenye usahihi wa kujua tarehe, eneo na kiasi kijacho cha tetemeko la ardhi ni ili kupunguza madhara, kubwa zaidi kuokoa maafa na uharibifu wa mali.

Mathalan, ingebashiriwa mapema kuwa Septemba 10, mwaka huu tukio la tetemeko la ardhi lingetokea, Bukoba, maana yake maafa yasingetokea. Kazi kubwa ingefanyika kuhamasisha watu wasiwepo eneo ambalo tetemeko lingepita. Vilevile mali zinazohamishika zisingeharibika. Nyumba sawa, maana hazihamishiki.

Tatizo tememeko la ardhi siyo sawa na tukio la kupatwa kwa jua, kwamba tarehe, saa na eneo ambalo muonekano unakuwa sawia zaidi kuhusu tendo lenyewe, kila kitu kinajulikana mapema kutokana na vipimo vya kisayansi. Narudia; Tetemeko la ardhi si tukio la kumbebesha mtu lawama.

Shida kubwa ni kuwa tetemeko la ardhi linapotokea na kuondoka huacha ujumbe wa kurudi tena. Hivyo basi, linapotokea vilevile huweza kurejea wakati wowote. Zaidi haijulikani litarudi lini, ukubwa wake na eneo mahsusi.

Ni kama ambavyo mwandishi maarufu duniani, Salman Rushdie katika kitabu chake The Ground Beneath Her Feet, aliandika: “Unapokuwa kwenye tetemeko la ardhi, hata kama utapona bila kupata madhara yoyote, lakini bado utakuwa na kiharusi kwenye moyo, kumbukumbu ya tetemeko hubaki kwenye kifua cha dunia. Tetemeko la ardhi linapoondoka huacha ahadi ya kurudi tena, inawezekana likarudi kwa kishindo kikubwa zaidi.”

Kubwa naona tetemeko la ardhi ambalo limesababisha maafa Bukoba, linatosha kabisa kuingia ndani ya kichwa cha kila mwanasiasa na kuzitetemesha fikra zake. Tetemeko likishatetemesha fikra sasa likumbushe kuwa sasa hivi hakuna mjadala wenye viulizo vya waliopoteza maisha ni watu wa chama gani?

Kugha ni moja kwamba “tumepoteza ndugu zetu.” Haupo mjadala kuhusu majeruhi ni wa chama gani, wote ni Watanzania. Hapa ndipo tetemeko linatosha kutoa ukumbusho.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli aliahirisha ziara yake ya kwenda Zambia kwenye shughuli ya kuapishwa kwa rais wa nchi hiyo, Edgar Lungu. Uamuzi wenye kukiri kuwa taifa limekumbwa na maafa.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, siku mbili baada ya tukio la tetemeko, alisafiri mpaka Bukoba kujionea hali halisi, ikiwa ni pamoja na kwenda kuwajulia hali majeruhi na kuwafariji. Alifanya safari yenye kusadiki kuwa maafa yaliyotokea yanalihusu taifa kwa umoja wake, si vyama na upande wa kiitikadi.

Siku moja kabla ya Mbowe, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifika Bukoba kujionea hali ya maafa, uharibifu wa mali pamoja na kuwatembelea majeruhi, kuwaona, kuwajulia hali na kuwafariji.

Jimbo la Bukoba Mjini, mbunge wake ni Wilfred Lwakatare wa Chadema. Katika tukio zima la maafa kulikuwa na ushirikiano wa kutosha kwa mbunge na viongozi wengine wa wilaya na mkoa ambao ni wateule wa Rais Magufuli. Ushirikiano huo hauna tafsiri nyingine, zaidi kwamba madhara ya tetemeko la ardhi yana mguso wa pamoja kama jamii na nchi kwa jumla kuliko vyama na itikadi za wanasiasa.

Sasa niulize swali; Je, kuna vifo vyenye kuibua mshtuko wa nchi na vingine havina? Je, watu 16 waliopoteza maisha Bukoba wanaweza kuwaunganisha Watanzania, sasa ni kwa nini kuwe na maandalizi ya vifo ambavyo vinaweza kuwagawa Watanzania?

Vema tukubali kuwa vifo ni vifo tu. Kila nafsi inayoonja mauti huacha simanzi isiyoelezeka kwa watu waliompenda. Kila halaiki inayokumbwa na maafa ni msiba wa kitaifa, iwe ajali kama ya tetemeko, kimbunga, barabarani, majini na hata angani, maafa ni maafa tu.

Tetemeko la ardhi litetemeshe fikra za wanasiasa kutambua kuwa hawapaswi kuunganishwa na maafa ya Bukoba, wakati wao wenyewe kwa vitendo vyao vya kutotaka kuzungumza na kupata mwafaka wa yale wanayopingana, wanaweza kusababisha upotevu wa nafsi nyingi zaidi.

Siasa za kuvutana kwa misimamo ya kuingia barabarani huweza kusababisha madhara makubwa mno kuliko yale ya tetemeko la ardhi la Bukoba. Hivyo, kitendo cha kuonesha kujali ya Bukoba huku wakiendelea kutunishiana msuli tafsiri yake ni maigizo.

Tukio la Zanzibar, baada ya maandamano ya Chama cha Wananchi (Cuf) na mapambano ya polisi, Januari 26 na 27, 2001, ripoti zinasema zaidi ya watu 60 walipoteza maisha, wengine wengi wakijeruhiwa, kupata ulemavu wa kudumu, huku kundi kubwa la Wazanzibari wakikimbilia nchi jirani.

Piga hesabu, siasa za CCM na Cuf ziligharimu maisha ya watu wengi zaidi kuliko tetemeko la ardhi. Haiwezekani kuzuia maafa ya tetemeko la ardhi lakini maafa ya kisiasa yanaweza kuzuilika. Inafaa kuungana katika kuzuia maafa yanayozulika kisha kushirikiana kwenye majanga yanayokuja bila taarifa.

Haina maana leo kuonesha kuguswa na tatizo lisilozuilika lililosababisha maafa ya watu 16, wakati huohuo Chadema wanaweka misimamo ya kujenga Ukuta (Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania), huku Rais Magufuli akiweka ahadi ya kuubomoa (Vunja Ukuta), misimamo ambayo inaweza kuyagharimu maisha ya watu wengi zaidi.

Badala ya Rais Magufuli na wapinzani kukutana kwenye meza ya mazungumzo, wanashindana na kutishiana kupitia vyombo vya habari. Nchi ambayo watu wake wanakuwa na nidhamu dhidi ya umwagaji damu hujitahidi zaidi kuzuia yanayozuilika halafu huunganishwa zaidi kwa yale ambayo hayazuiliki.

Tetemeko la Bukoba linatoa muongozo kuwa kama ambavyo vyama vyote vimeguswa na maafa hayo, vitambue kuwa vitapaswa kuguswa na kujilaumu kwa gharama ya maisha ya Watanzania kama hali ya sasa ya kutunishiana misuli itaipeleka nchi kwenye machafuko.

Kuelekea Oktoba Mosi, mwaka huu ambayo Chadema wamesema ndiyo tarehe ya kujenga Ukuta, kwamba yatafanyika maandamano ya kuupinga udikteta nchi nzima baada ya kuahirisha Septemba Mosi, mwaka huu, dirisha la maridhiano liwe wazi, si kwa ajili ya upande fulani kuonesha kushindwa au kunyenyekea, bali lengo kuu ni kulinda usalama wa nchi na maisha ya watu wake.

Maisha ya Mtanzania yanatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote ile. Hakuna tofauti zozote za kisiasa ambazo zinaweza kutoa leseni ya kuingia barabarani kupigana. Wakati wote wanasiasa wanatakiwa kuwa Watanzania kabla ya kuweka misimamo yao.

Wapinzani wanapaswa kutii mamlaka ya nchi, wamtii Rais Magufuli kama Mkuu wa Nchi. Vilevile Rais Magufuli hana hiyari kukutana na wapinzani na kujadili namna bora ya kufanya shughuli za kisiasa ili kuachana na hii vuta nikuvute.

Hii hali ya vuta nikuvute, wapinzani waking’ang’ania kuwa watajenga Ukuta, serikali ikisisitiza kuwa itabomoa, inawaweka wananchi kwenye hali ya wasiwasi, zaidi inaamsha sura ya kuvunjiana heshima, kati ya wapinzani na mamlaka za nchi kitu ambacho si kizuri.

Ni matumaini yangu hai kuwa kama amabavyo tetemeko la ardhi Bukoba limebeba hisia za jumla pasipo itikadi za vyama, hata malumbano ya kisiasa wakati huu na nyakati zijazo, utazame maslahi kama nchi kuliko matakwa ya vikundi au vyama. Mwisho kabisa, hekima huonekana pale ambapo majanga au machafuko yanayozulika yanaposhughulikiwa katika namna ambayo hayatokei kabisa.

Wakati huu na hata ujao, hakuna ambaye atalaumiwa kwa tetemeko la ardhi Bukoba, maana si tukio lenye kutoa viashiria vyovyote kabla ya kutokea, ila wanasiasa watabeba lawama wakati wowote kama wataisababishia nchi maafa. Kama ambavyo Januari 26 na 27, 2001 inabaki kuwa lawama kwa CCM, Cuf, polisi pamoja na serikali kwa jumla.

Vilevile, maafa ya watu wawili Arusha mwaka 2011, lawama ni kwa Chadema, polisi na serikali yote, kwamba wangetenda mambo yao kwa busara hasara ya vifo vya watu isingetokea. Maafa ya kisiasa yana lawama, ya tetemeko hayana lawama.

Chanzo: Maandishi Genius
 
Nyuzi ndefu kama hii yenye maono chanya haipati uungwaji mkono......ila mathread ya umbeya na kumention watu yanajaza watu balaa
 
Vijana wanataka ubuyu wa zari na mobeto ndio Tanzania yetu hii
Nyuzi ndefu kama hii yenye maono chanya haipati uungwaji mkono......ila mathread ya umbeya na kumention watu yanajaza watu balaa
 
Back
Top Bottom