TCRA: Tumia simu vizuri, ukimdhalilisha mwanamke mtandaoni jela inakuhusu

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,688
6,484
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaonya watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake mitandaoni, ikisema kufanya hivyo ni kosa la kihalifu kwa mujibu wa sheria za nchi na kunaweza kumpelekea mtu kutozwa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Meneja wa TCRA Kanda ya Kati Boniface Shoo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake yaliyolenga kufahamu hatua mamlaka hiyo inachukua kukomesha vitendo vya udhalilishaji wanawake mitandaoni ambavyo wadau wamebainisha kushamiri kwa kasi.

“Makosa ya jinai, na makosa mengine yoyote yale ambayo mtu unaweza kufanya kama kawaida ukiyafanya kwenye simu bado umefanya kosa,” alibainisha Shoo na kuongeza:

“Kwa hiyo, tusitumie hizo simu zetu kufanya makosa yeyote yale. Unyanyasaji mtandaoni, sijui wizi tusifanye, hivyo. Tutumie simu kwa ajili ya maendeleo yako binafsi na maendeleo ya nchi.”

Takriban asilimia 77 ya wanawake Watanzania wanaojihusisha na siasa nchini wameacha, au kusimama kwa muda, kutumia mitandao ya kijamii kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni unyanyasaji wa kijinsia uliokithiri ambao wanawake hao wamebainisha kupitia kwenye majukwaa hayo.

Hali hii imepelekea wadau mbalimbali kama vile shirika la kimataifa linalojihusisha na masuala ya habari la Internews kuandaa mafunzo kwa wadau mbalimbali kama vile waandishi wa habari kama sehemu ya kuunganisha nguvu za wadau kupambana na kukomesha vitendo hivi.

Mafunzo hayo ya Internews yalifanyika Machi 8, 2022.

Moja kati ya wadau muhimu katika kukomesha vitendo vya udhalilishaji wanawake mitandaoni ni shirika lisilo la kiserikali linalojikita kwenye kuwajengea uwezo wanawake kwenye eneo la usalama wao kidijitali la Zaina Foundation.

Neema Olle Ndemno ambaye wakati wa mazungumzo mdau huyo wa usalama wa wanawake kidijitali alieleza mtazamo wake wa nini kinasukuma vitendo vya udhalilishaji wanawake mitandaoni.

Njia ya kuendeleza udhalilishaji
“Kwa namna moja ama nyingine matumizi ya mitandao yamekuwa kama njia pia ya kuendeleza yale matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, hususani kwa wanawake, ambayo tayari yapo kwenye jamii,” anaeleza Ndemno. “Mtu anaweza akatuma picha yake kwenye mtandao na pale pale watu wakaibuka kuanza kumnyanyasa na kuanza kumtolea maneno mabaya ambayo hayafai.”

Hoja ya Ndemno kwamba kinachotokea mitandaoni kinaakisi kile kilichopo kwenye jamii za Kitanzania inapata nguvu tukiangalia hali ya udhalilishaji wanawake nchini.

Watafiti wanabainisha kwamba tatizo la ukatili wa kijinsia ni kubwa sana nchini Tanzania huku takwimu zikionesha kwamba asilimia 40 ya wanawake na watoto wa wakike wenye umri kati ya miaka 15 na 49 wamekutana na ukatili wa kimwili katika maisha yao na asilimia 17 wakisema wamekutana na ukatili wa kingono.

“Huu ukatili wa kijinsia tulikuwa nao kabla ya ujio wa mitandao ya kijamii na tulikuwa tunapambana nao,” anaeleza Godwin Asenga, mtaalamu wa TEHAMA kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) akikubaliana na hoja ya Ndemno.

“Baada ya ujio wa mitandao hii tumeona kundi lile lile limehamishia ukatili huu mtandaoni,” anongeza Asenga. “Sasa tunaona ukatili wa kijinsia mitandaoni wanawake wamekuwa wakikatiliwa.”

Akieleza aina ya udhalilishaji ambazo yeye binafsi amewahi kuzishuhudia zikielekezwa kwa wanawake mitandaoni, Asenga alitaja wanawake kudhihakiwa maumbile yao pamoja na picha za utupu za wanawake kurushwa mitandaoni bila ya ridhaa zao.

Ndemno anaamini kwamba hatua kali za kisheria zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya watu wanaodhalilisha watu mitandaoni, siyo wanawake tu bali hata udhalilishaji unaoelekezwa dhidi ya wanaume.

Uhalifu wa mtandao nchini Tanzania unaongozwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, na wakati zipo kesi za watu walioshitakiwa kwa kukiuka sheria hiyo, kwa kiwango kikubwa kesi hizo hazihusishi watu wanaodhalilisha watu wengine mitandaoni.

Kesi moja ya mfano
“Tungechukua kesi moja ya mfano ambayo itaenda hadharani watu wataona na yule mtu [anayedhalilisha] akikutana na hatia aadhibiwe na umma ujue mtu fulani alikosea hivi na ameadhibiwa hivi,” ni maoni ya Ndemno. “Ili ionekane sheria imekamata msumeo. Mimi nashauri hilo.”

Kwa upande wake, Asenga anapigia chapuo umuhimu wa kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi bora ya mitandao ya kijamii, akionesha wasiwasi wake kwamba kushitaki tu pekee kunaweza kusiwe suluhu ya muda mrefu ya tatizo husika.

“Tunaweza kuipongeza TCRA kwa maana ya kwamba ndiyo mamlaka husika inayosimamia masuala yanayohusiana na haya maudhui ya mtandaoni,” anaeleza Asenga. “[TCRA] wamekuwa wakitoa elimu kupitia kurasa zao za mitandao. Sasa elimu ya namna ile inahitajika kuongezwa nguvu.”

Asenga anaamini kwamba pia ipo haja ya TCRA kutoa mrejesho kwenye jamii ya wale ambao wanakutwa na hayo makosa na ni adhabu gani ambazo wameshachukuliwa.

Hatua Hii anasema inaweza kusaidia watu kujifunza kutokana na zile adhabu ambazo watu wengine wamepewa.

Source: The Chanzo
 
Ufafanuzi wa neno Kudhalilisha ni Upi? Wengine ukiwatongoza wanasema umewadhalilisha wakati ni haki yao..
 
wao ndiyo wanaojidhalilisha, waanze na wale wanaotembea 'uchi' kwa public kwa kisingizio cha 'joto'
Hapo hakuna kujidhalilisha mkuu,si umeshasema anaona joto? Ni km wazungu Tu kule Zanzibar wanatembea nusu uchi tena Hadi kipindi cha ramadhani lkn wenyeji hawawafanyi chochote...abae mswahili kutoka mchambawima sasa,utasikia anadhalilisha utu,wengine huenda mbali anadhalilisha uislamu..anapigwa

mentality za hovyo kbs
 
Hapo hakuna kujidhalilisha mkuu,si umeshasema anaona joto? Ni km wazungu Tu kule Zanzibar wanatembea nusu uchi tena Hadi kipindi cha ramadhani lkn wenyeji hawawafanyi chochote...abae mswahili kutoka mchambawima sasa,utasikia anadhalilisha utu,wengine huenda mbali anadhalilisha uislamu..anapigwa

mentality za hovyo kbs
endelea kutetea ujinga
 
Hapo hakuna kujidhalilisha mkuu,si umeshasema anaona joto? Ni km wazungu Tu kule Zanzibar wanatembea nusu uchi tena Hadi kipindi cha ramadhani lkn wenyeji hawawafanyi chochote...abae mswahili kutoka mchambawima sasa,utasikia anadhalilisha utu,wengine huenda mbali anadhalilisha uislamu..anapigwa

mentality za hovyo kbs
Umenena wabongo wengi wana mentality za hovyo sana!
 
Mwenye picha tafadhali ya jambo hili atupie tuone huo udhalilishaji basi
 
Kwa nini wanakubali kujirekodi picha na video za ngono???

TCRA hao wanawake wakijichanganya mtandaoni lazima tuwaonyeshe njia sahihi ya kupita
 
Back
Top Bottom