SoC04 Tanzania ya Sekta za Kisasa za Maendeleo

Tanzania Tuitakayo competition threads

KiuyaJibu

JF-Expert Member
Aug 29, 2007
848
191
Utangulizi

Tanzania tuitakayo ni ile ambayo imejenga sekta za kisasa za maendeleo na sekta mojawapo kuu ikiwa ni viwanda; ambayo itachangia hali ya maisha ya watu wake kuwa bora kwa kuongeza pato la mmoja mmoja ambapo kwa ujumla wake pato la Taifa linakua pia. Kukua kwa uchumi wa mmoja mmoja kuna pelekea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla, kwa mujibu wa ripoti ya Tathimini ya Ustawi wa Kiuchumi (MEO) iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Februari, 2024 sehemu ya ripoti hiyo imesema, uchumi wa Tanzania utakuwa kwa asilimia 6.1 zaidi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki isipokuwa Rwanda asilimia 7.2 kwa mwaka huu; hivyo, Serikali itakuwa na uwezo wa kutoa na kuboresha huduma za msingi kwa wananchi wake kama vile afya, elimu, miundombinu, nishati. Kuwezekana kwa hayo yote tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi kwenye kila sekta; hata hivyo, hayo yote pekee yake hayatoshi bila kuwepo kwa utawala bora.

Pamoja na mambo mengine na kuzingatia hali halisi ilivyo hapa nchini, ili tuweze kuwa na uchumi imara kwa ngazi zote hadi kufikia Taifa kwa ujumla wake yafuatayo inabidi yafanyiwe kazi

Ujenzi wa viwanda na uzalishaji viwandani

Eneo hili lina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yeyote ile duniani; ili tuweze kuwa na uchumi imara kama Taifa hatuna budi kuwekeza kwenye eneo hili. Tunaweza kuanza na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo hadi vikubwa kwa kuhakikisha kila mkoa unakuwa na kiwanda angalau kimoja kinachofanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa halafu tunashuka hadi kwenye kila wilaya na kuendelea zaidi ya hapo; eneo hili linaajiri watu wengi kwa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Ili viwanda hivi viweze kuleta nafuu inayotarajiwa na visiwe mzigo kwa wazalishaji, vinatakiwa vijikite kwenye uzalishaji unaolenga

  • kukidhi mahitaji ya ndani-chakula, mavazi, madawa, malazi na mitambo na mashine zitakazosaidia uzalishaji wa mahitaji hayo ya ndani;
  • uzalishaji unaotegemea zaidi mali ghafi kutoka ndani na siyo nje;
  • matumizi makubwa ya rasilimali Watu wa ndani na siyo wataalamu kutoka nje; na
  • kuwepo mahusiano ya kutegemeana baina ya shughuli za kilimo na viwanda.
Ni muhimu kufahamu kuwa uchumi wa Taifa unatakiwa kujikita zaidi katika uzalishaji na siyo uchuuzi. Pamoja ya kuwa, shughuli za biashara na huduma zingine ni muhimu lakini msingi wake ni uzalishaji.

Hata hivyo, nashukuru kwa jitihada zinazofanywa na Serikali hasa kwenye kuwezesha uanzishwaji wa Viwanda vipya na Kongani za Viwanda (Industrial Parks) za Kwala-Pwani, TAMCO pamoja na Kongani ya kisasa ya viwanda (Modern Industrial Parks)-Pwani; ifafanuzi wake uko kwenye hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Kuimarisha fedha yetu dhidi ya fedha za kigeni

Hii inawezekana kwa kufanya yafuatayo:

  • Malipo yote ya bidhaa na huduma hapa nchini yanatakiwa kufanyika kwa fedha ya Kitanzania (Tshs.) hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 kifungu 26 pamoja na tangazo la ukumbusho kwa Umma la Agosti, 2007 lilorudiwa tena Disemba, 2017 likisisitiza malipo yote ya bidhaa na huduma hapa nchini yatozwe kwa fedha ya Kitanzania.
  • Kupunguza utegemezi wa kuagiza na kununua bidhaa na huduma zinazopatikana nchini kutoka nje ya nchi.
  • Kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
  • Kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi
Usalama wa chakula

Ili tuwe na utulivu katika nchi pamoja na mambo mengine ni lazima tuweze kujitosheleza kwa chakula ikiwa inamaanisha usalama wa chakula ambayo maana yake ni (i) upatikanaji (ii) kukifikia (iii) matumizi na (iv) uhakika

Tunapokuwa na usalama wa chakula, inatupa matokeo chanya kwenye maeneo yafuatayo:

  • Kukua kwa uchumi na kuzalisha ajira
  • Kupunguza umasikini
  • Fursa za kibiashara
  • Utaongeza usalama na uhakika wa chakula duniani
  • Utaboresha afya na huduma za afya
Kujitosheleza kwa nishati

Ili uzalishaji kwenye viwanda na uwepo wa viwanda uwe na maana na kuleta matokeo chanya; ni muhimu kuwa na nishati ya uhakika jambo ambalo linawezekana kulingana na hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2024/2025 hadi kufikia Machi, 2024 kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye gridi ya Taifa ni MW 2138 kutoka awali MW 1872.1 kwa mwaka 2022/2023 na inategemewa kuongezeka MW 2115 ifikapo Disemba, 2024 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere (JNHPP) pamoja na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa.

Kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati uliyopangwa itatupa uhakika wa nishati ya umeme ifikapo mwaka 2025, ni ishara nzuri kwenye kutekeleza dhana nzima ya uchumi wa viwanda ambayo ina mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi.



Kuboresha matumizi ya TEHAMA

Ni matumizi ya taarifa na maarifa ya kidijitali katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vipengele muhimu vya uzalishaji. Uchumi umeanzisha miundo mipya na bunifu ya biashara ambayo kwa kiasi fulani inalingana na miundo ya kitamaduni ya biashara, kwa mfano, huduma za malipo kwa mtandao, biashara ya mtandaoni, na maduka ya maombi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Matumizi ya TEHAMA yanachochea ukuaji wa sekta za kiuchumi nchini kama ilivyo katika nchi nyingine katika kutoa huduma mbalimbali zinazotolewa na sekta ya umma na binafsi.

Ili kukuza na kuendeleza uchumi kwa kutumia TEHAMA ninapendekeza yafuatayo kutekelezwa: kuendelea kuwekeza katika miundombinu migumu na laini hasa maeneo ya pembezoni ya miji na vijijini; kuwezesha upatikanaji wa intaneti kwa bei nafuu na kuimarisha mifumo ya kielektroniki katika utoaji wa huduma hasa za kifedha ili kuwezesha malipo kwa njia ya kielektroniki badala ya fedha taslimu; kukuza ujuzi wa kidijitali na kuongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi; kuimarisha programu za kubadilishana ujuzi kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa kama vile kujifunza kwa mashine (machine learning), Akili Mnemba (AI), uchambuzi taarifa (data analytics); kuimarisha mfumo wa kusimamia ikolojia ya ujasiriamali wa kidigitali, ubunifu na ukuaji wa kampuni changa; kuimarisha utambuzi wa makazi kwa kuanzisha miundombinu ya taarifa za anga (Spatial Data Infrustructure) ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kijiografia; kubainisha chombo mahususi kitakachokuwa na dhamana ya kusimamia na kuendeleza biashara mtandao; na kuanzisha maeneo maalum ya biashara ya Teknolojia ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya mawasiliano.
 
Back
Top Bottom