Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inashikilia jumla ya tani 400 za pombe zinazofungashwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu kama Viroba zilizopatikana katika msako wa siku 3 pekee ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Wakili Mwandamizi wa Serikali kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Manchare Heche Suguta amewataka wasambazaji na wafanyabiashara wakubwa pamoja na viwanda kutoendelea na biashara hiyo na kutoa ushirikiano kwa serikali kubaini kiwango cha pombe za viroba kilichopo sokoni kwa hivi sasa wakati utaratibu mwingine ukitafutwa.
Aidha, Bw. Suguta amesema wamejipanga kudhibiti waingizaji wa bidhaa za pombe ya viroba kutoka nje ya nchi kwa kuweka udhibiti maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kuwa hakuna uingizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi inayoingia katika soko la Tanzania.