TAHLISO yageuka genge la mtaji wa fedha kwa viongozi wa TAHLISO

Umepigaje Apo

New Member
Dec 30, 2023
2
1
UTANGULIZI

TAHLISO ni Jumuiya ya Wanafunzi wa elimu ya Juu (Vyuo na Vyuo Vikuu) Tanzania. Ilisajiliwa mwaka 2004 ili kuwa sehemu ya kuziunganisha serikali hizi/wanafunzi hawa kwa ajili ya kuwasilisha changamoto, maoni na mapendekezo yanayogusa maslahi ya wanafunzi wote wa Elimu ya Tanzania katika mamlaka mbalimbali za Serikali ya JMT zinazogusa maslahi ya wanafunzi hao.

Jumuiya hii inaongozwa na Katiba inayotambulika kama Katiba ya TAHLISO ya mwaka 2021.
Serikali za wanafunzi kupitia ibara ya 86 (2), (3) ya Katiba hiyo inawataka wanajumuiya kulipia ada ya uwanachama katika mchanganuo kuwa

(1) Kwa vyuo vilivyo na wanafunzi pungufu ya idadi 2000, watatakiwa kulipa TShs. 300,000/= (Laki tatu tu)

(2) Kwa vyuo vilivyo na wanafunzi zaidi ya idadi 2000, watatakiwa kulipa TShs. 500,000/= (Laki tano tu).


Jumuiya hii ina muunganiko wa zaidi ya vyuo 120 kwa Tanzania nzima. Ukusanyaji wa ada hizi za wanachama unaweza kutosheleza utendaji kazi wa jumuiya. Aidha, mpango mkakati wa mapato na matumizi ya ada hizi unapaswa kufanywa kupitia majadiliano ya vikao vya bajeti ambavyo ni Vikao Halali vya Seneti ya Jumuiya hiyo kupitia ibara ya 68 (6), (7), (8) & (11) ya katiba ya TAHLISO. Vilevile kupitia vikao halali vya Mkutano Mkuu wa Jumuiya (General Assembly) kupitia ibara ya 62 ya Katiba ya TAHLISO (a) - (g) wajumbe wanapewa nguvu ya kujadili na kuamua maswala yote yanayogusa maslahi wa wanachama wake.

HOJA KUU
1. Hivi karibuni, menejimenti za vyuo na vyuo Vikuu zimekuwa zikipokea barua ya maelekezo kutoka Wizara ya Elimu ikizitaka kulipa ada za uwanachama kwa kiasi cha TShs. 1000/= kwa kila mwanafunzi kwa idadi ya wanafunzi walioko katika chuo chake kinyume na katiba ya TAHLISO. Kwa barua hii inayotoa maelekezo kwa menejimenti za vyuo na Vyuo Vikuu ambayo wanachama hawajakubaliana katika kikao chochote ongezeko hili la ada inazua taharuki na tafsiri hasi ya matumizi mabaya am uhujumu ya fedha za wanachama.

Kwa mfano, kwa waraka huu vyuo vikuu vinapaswa kutoa mchango unaokadriwa ifuatavyo:-

i. UDOM wanafunzi wanaokadiriwa kuwa elfu 33+, wanapaswa kuchangia MILIONI 33

ii. SUA inayokadiriwa kuwa na wanafunzi elfu 15+ inapswa kuchangia TShs. MILIONI 15

iii. SAUT-Mwanza inayokadiriwa kuwa na wanafunzi elfu 16+ inapaswa kuchangia TShs. MILIONI 16

iv. MZUMBE-Morogoro inayokadiriwa kuwa na wanafunzi zaidi ya elfu 8+ inapaswa kuchangia TShs. MILIONI 8

v. MUM inayokadiriwa kuwa na wanafunzi zaidi ya elfu 7+ inapaswa kuchangia zaidi TShs MILIONI 7

vi. IFM inayokadiriwa kuwa na wanafunzi zaidi ya Elfu 9, inapaswa kuchangia TShs. milioni 9

vii. DARUSO-DUCE yenye wanafunzi zaidi ya elfu 7, inapaswa kuchangia zaidi ya TShs. MILIONI 7.

Hivi ni baadhi ya nyuo ambavyo vimeangaziwa kwa jicho la mkadirio. Aidha, hoja ya ongezeko la ada kuwa TShs. 1,000/= kila mwanafunzi iliwasilisha kwa mara ya kwanza katika mkutano mkuu wa kwanza uliofanyika tarehe 25 Novemba 2023 mkoani Iringa katika Chuo Kikuu Iringa. Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa VIKALI na wajumbe halali kwani iliashiria mazingira ya uhujumu kwa kutaka wanachama kuchangia ada kubwa zaidi ya uwezo wao.

2. Maamuzi ya kuidhinisha uchangiaji wa fedha hizi yalipaswa kujadiliwa na wajumbe ambao ni wanachama halali wa mikutano ya TAHLISO kupitia Seneti au Mkutano Mkuu. Kuandikwa kwa waraka wa maelekezo kwa menejimenti za vyuo na Vyuo Vikuu bila wanachama kujulishwa ni kukiuka katiba na kuashiria utawala mbovu wa uongozi wa TAHLISO

3. Viongozi wa Juu w TAHLSIO, kwa asilimia zaidi ya 80 wameshamaliza Vyuo au Vyuo Vikuu kwa miaka ya masomo ya 2023/24 na wachache wao wanaendelea na masomo. Kushinikizwa ulipwaji huu wa Ada kubwa kuliko uwezo wa wanachama na kutokuwepo na bajeti ya matumizi hata kwa ada halali ya kikatiba kunaashiria mwanya wa kufanya ubadhirifu wa michango ya wanachama.

4. Wizara ya Elimu, mnaombwa kulitazama hili na kulichambua kwa kina kwani kushinikiza maelekezo yaliyotolewa kwa menejiment za Vyuo na Vyuo Vikuu ni kukiuka katiba ya TAHLSO na Katiba za Serikali za wanafunzi ambazo Zinajiendesha zenyewe. Aidha, kuendelea kushinikiza utekelezaji wa jambo ambalo wajumbe halali wa Jumuiya hiyo, ni kupelekea kuvunjika kwa jumuiya hiyo kwani Wajumbe halali hawako tayari kushiriki ubadhirifu wa fedha za wanafunzi.

Hoja ya Ongezeko la fedha hizo za ada imekuja baada ya uwepo wa mdololo wa ulipaji wa ada kutoka Vyuoni kwenda TAHLISO. Mdololo huo umesababishwa na kukosekana kwa mikakati na hamasa ya Viongozi wa TAHLISO kuwakumbusha na kuwataka viongozi wa Serikali za wanafunzi kulipa ada ya kikatiba ya uwanachama. Wajumbe wa mkutano mkuu (IRINGA) walitegemea uwepo wa majadiliano ya Kina kuhusu namna ya kuukata mzizi wa changamoto hiyo. Lakini, yaliyo endelea yalikuwa tofauti na mawazo ya wajumbe, mbadala wake pendekezo na hoja ya ongezeko la ada liligongelewa msumari na Viongozi wa TAHLISO wakiongozwa na Rais wa TAHLISO bila kuwapa wajumbe muda wa kutosha kuamua juu ya suala hilo gumu. Hili lilipelekea wajumbe na wawakilishi kutoka Serikali za wanafunzi kukosa nguvu licha ya Hoja hiyo Kupingwa na Kugomewa na wawakilishi kutoka Serikali za wanafunzi.

Vile vile, ushinikizaji wa utoaji wa fedha hizo kinyume na taratibu na miongozo ya Serikali za wanafunzi, unazidi kutia mashaka kwani, TAHLISO haina mchanganuo wa kanuni za matumizi ya fedha, ni kawaida fedha kutumika bila uwepo wa utaratibu maalum.

Serikali nyingi za wanafunzi zipo katika umoja huo sio kwasababu zimekuwa zikinufaika kwa kiwango kikubwa na uwepo wa jumuiya hiyo la hasha, bali ni kwasababu ya kudumisha umoja, amani na utulivu baina ya Vyuo na Vyuo vikuu.

Kwa kuzingatia kuwa, agizo hilo limetoka baada ya serikali nyingi za wanafunzi kupitisha bajeti zao za mapato na matumizi, matumizi hayo ya fedha kwa kufanya hisani kwa mfuko wa fedha wa TAHLISO (Kinyume na Katiba ya TAHLISO) kunazifanya Serikali nyingi za wanafunzi kuchakata maamuzi ya KUJIONDOA kwenye umoja huo ili walau zipate ahueni.

Tunaomba waandishi wa habari, na wadau mbalimbali, watusaidie kupaza sauti ili iweze kusikika na Wizara ya Elimu, juu ya ongezeko hili la ada ya uanachama TAHLISO kwa vyuo na vyuo Vikuu, kutoka 300000/500000 mpaka zaidi ya Milioni moja, na hata kufikia Milioni thelathini kwa baadhi ya Vyuo, kulingana na idadi ya wanafunzi wake. Kuhalalisha jambo hili bila makubaliano ya wajumbe kutoka Serikali za wanafunzi, ni kuchochea mgogoro utakao athiri afya ya jumuiya hii.

Vile vile, utoaji wa kiwango hicho KIMABAVU kutoka katika mfuko wa Serikali ya wanafunzi, unaweza kuathiri mwenendo wa matumizi ya bajeti lengwa ambazo Serikali za wanafunzi wamekwisha kupitisha Bungeni (Bunge la Serikali ya wanafunzi) na kuzifanya Serikali nyingi za wanafunzi kukwama kufikia maono. Mbadala wake fedha hizo zikatumike na viongozi wa TAHLISO kwa matumizi yasio eleweka, kwani changamoto nyingi za wanafunzi vyuoni, hutatuliwa na Serikali za Wanafunzi huku TAHLISO ikiwa na mchango mdogo mno katika kutatua changamoto za hizo.
 
Back
Top Bottom