Tahadhari: Usikope Fedha Kwa Ajili Ya Kwenda Kufanya Uwekezaji

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Kwenye uwekezaji, faida ambayo huwa inapatikana ni ndogo sana kwenye muda mfupi. Ila faida hiyo huwa inakuwa kubwa kadiri uwekezaji unavyofanyika kwa muda mrefu.

Kwa kuwa watu wengi hawana subira ya kuwekeza kwa muda mrefu ndiyo wapate faida, huwa wanatafuta njia za mkato za kupata faida ya uwekezaji haraka.

Kwa mfano kwa uwekezaji ambao unampa mtu riba ya asilimia 12 kwa mwaka, akiwekeza milioni 10, kwa mwaka anapata milioni moja na laki mbili tu. Hapa mtu anaweza kuona ili apate faida kubwa, inabidi afanye uwekezaji mkubwa.

Lakini tatizo linakuja kwamba mtu anakuwa hana kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa pamoja. Na hapo ndipo wengi huangalia ni njia gani rahisi kwao kupata fedha nyingi za kuwekeza.

Kukopa fedha kwa ajili ya kufanya uwekezaji huwa ni kitu ambacho baadhi ya watu hukifikiria na hata kukitekeleza. Kwa kuona wakichukua mkopo na kwenda kuwekeza, watapata faida kubwa.

Kwa hesabu za haraka haraka na juu juu unaweza kuona kuwekeza fedha nyingi ni kupata faida kubwa. Lakini tukurudi kwenye hesabu za msingi, kuchukua mkopo kwa ajili ya kwenda kufanya uwekezaji ni hasara kubwa.

Mikopo na uwekezaji vyote vinatumia kanuni moja, ila ambayo inafanya kazi kinyume. Unapowekeza, kunakuwa na riba, ambapo wewe uliyewekeza unalipwa kutokana na fedha uliyowekeza. Unapochukua mkopo, kunakuwa na riba, ambayo wewe uliyekopa unalipa kutokana na fedha ulizokopa.

Hivyo kukopa ili ufanye uwekezaji kwa sehemu kubwa unaishia kupata hasara kwa sababu kubwa tatu.

Moja ni mikopo inakuwa na riba kubwa kuliko uwekezaji.

Uwekezaji mwingi unakupa marejesho ya kati ya 10% mpaka 15% kwa mwaka. Huku mikopo mingi ikitoza riba kati ya 18% mpaka 20% kwa mwaka. Kwa hiyo ukienda kuchukua mkopo ili uwekeze, utalipa gharama kubwa kuliko faida unayopata.

Kwa mfano ukichukua mkopo wa milioni 10 kwa riba ya 18% kwa mwaka, utapaswa kulipa milioni 1 na laki 8 kwa mwaka. Ukiwekeza hiyo milioni 10 mahali ambapo unapata riba ya 12% kwa mwaka, utapata faida ya milioni 1 na laki 2 kwa mwaka. Ukifanya hesabu za kujumlisha na kutoa hapo, unaona wazi kwamba kwa hiyo milioni 10 unapata hasara ya laki 6.

Mbili ni mfumuko wa bei unapunguza thamani ya fedha na faida ya uwekezaji.

Kila mwaka huwa kunakuwa na mfumuko wa bei ambao unapandisha bei ya vitu na kupunguza thamani ya fedha. Kwa Tanzania, mfumuko wa bei huwa ni 4% mpaka 5% kwa mwaka, hivyo kila mwaka fedha inapungua thamani kwa kiasi hicho.

Kwa maana hiyo pamoja na faida unayopata kwenye uwekezaji, bado sehemu hiyo ya uwekezaji inamezwa na mfumuko wa bei. Hivyo hata kama unapata mkopo ambao riba yake iko chini sana, bado ukiweka mfumuko wa bei unajikuta unapata hasara.

Kwa mfano kama umepata mkopo wenye riba ndogo ya 6% kwa mwaka unaweza kuona ni sahihi kuchukua na kwenda kuwekeza mahali ambapo unapata riba ya 10% kwa mwaka. Lakini kwenye hicho unachopata ukitoa 4% ya mfumuko wa bei, unajikuta unarudi kwenye hasara.

Tatu ni riba ya deni ni uhakika wakati riba ya uwekezaji siyo uhakika.

Ukichukua mkopo na kuambiwa utalipa riba ya 10% kwa mwaka, utalipa hiyo bila kujali nini kimetokea kwenye uchumi. Wakati ukiwekeza mahali ambapo umeambiwa utapata riba ya 10% kwa mwaka, itategemea na hali ya uchumi, inaweza kupanda au kushuka, isipokuwa uwekezaji wa hatifungani ambao riba ni uhakika.

Kwa maana hiyo, unakopa fedha ambayo lazima ulipe kwa kiwango mlichokubaliana, lakini unapoenda kuwekeza unachopata siyo uhakika. Hapo unaona jinsi ambavyo kukopa kwenda kuwekeza, hata kama hesabu zimekaa sawa, bado siyo maamuzi sahihi.

Ufanye nini ili kunufaika na uwekezaji?

Kama ambavyo tumekuwa tunajifunza, njia bora ya kunufaika na uwekezaji ni kuwekeza kidogo kidogo kwa muda mrefu bila kuacha wala kutoa. Usitegemee faida ya uwekezaji kwenye kiasi unachowekeza, badala yake tegemea faida ya uwekezaji kwenye muda unaowekeza.

Na muhimu zaidi, usijaribu kutafuta njia ya mkato ya kupata faida kubwa kwenye uwekezaji. Utaishia kupoteza zaidi kuliko unavyopata. Njia ya wewe kuweza kupata faida kubwa kwa fedha zako ni kuzifanyia kazi moja kwa moja, kitu ambacho unapaswa kuwa unakifanya. Na ile faida unayopata ndiyo uiwekeze na kuwa na subira badala ya kulazimisha faida kubwa.

Karibu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2024 ambapo utakwenda kujifunza na kuweka mpango huu kwa vitendo kisha kusimamiwa kwenye kuutekeleza kwa msimamo bila kuacha. Tuma sasa ujumbe wenye maneno SEMINA 2024 kwenda namba 0713 604 101 upate nafasi ya kushiriki semina.

SIKILIZA SOMO HILI KWENYE ONGEA NA KOCHA.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili ambapo washiriki wamekuwa na maswali na michango mbalimbali. Karibu usikilize hapo chini ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi.


View: https://youtu.be/qLnwE0sygAs

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Faida ya uwekezaji huwa inaamuliwa na nini?

2. Kwa nini kukopa kwa ajili ya kuwekeza siyo maamuzi sahihi?

3. Kama unapata mkopo kwa riba ya 10% kwa mwaka na kuna uwekezaji wa riba ya 12%
kwa mwaka, je ni sahihi ukope na kwenda kuwekeza? Kama jibu ni ndiyo eleza kwa nini na kama ni hapana eleza kwa nini.

4. Unaivukaje tamaa ya kutaka kutumia njia za mkato kufaidika zaidi kwenye uwekezaji?

5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekez
o na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Back
Top Bottom