Nimeuliza wenyeji wakasema kuwa mbu hawa ni spesheli wameletwa kwenye mradi wa utafiti wa malaria.
Hii ni ajabu sana.
- Tunachokijua
- Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) ni shirika linaloongoza la utafiti wa afya barani Afrika, lenye rekodi nzuri ya kuendeleza, kupima na kuthibitisha ubunifu wa afya. Linaendeshwa na jukumu kuu la kimkakati la utafiti, mafunzo na huduma ikijumuisha taaluma mbalimbali za kisayansi, kuanzia sayansi ya msingi ya matibabu na ikolojia hadi majaribio ya kimatibabu, utafiti wa mifumo ya afya, tafsiri ya sera, na utekelezaji wa programu za afya.
Kazi ya Taasisi ya Afya Ifakara imepangwa katika idara tatu za utafiti, vitengo sita vya utafiti na vitengo saba vya msaada wa kiufundi. Idara za utafiti ni Afya ya Mazingira na Sayansi ya Ikolojia (EHES), Afua na Majaribio ya Kliniki (ICT), na Mifumo ya Afya, Tathmini ya Athari na Sera (HSIEP).
Madai ya kuzalisha Mbu
JamiiForums imezungumza na Dkt. Dickson Wilson Lwetoijera, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wadudu akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 12 katika utafiti wa kudhibiti wadudu wa Malaria anafafanua kuhusu taarifa hizo.
Dkt. Lwetoijera ambaye pia anatambulika kama Mwanasayansi Mwandamizi anasema:
Taasisi imekuwa ikifanya taafiti mbalimbali kuhusu Ugonjwa wa Malaria, kuna vipengele tofauti kuhusu utafiti wa Malaria unaofanywa na Ifakara (IHI), upo ambao unahusu chanjo na upo pia unaohusu kudhibiti Mbu.
Ni kweli tunazalisha Mbu kwa ajili ya kufanyia tafiti mbalimbali na tunapata vibali vyote vya Serikali, Mbu wanaozalishwa Maabara hawasambazi Malaria.
Tunazalisha kulingana na idadi ya mahitaji ya utafiti, kuwazalisha ni gharama kubwa kwa kuwa kuna kuwalipa watu mishahara na vitu kama hivyo.
Mara nyingi mbu hao wanakunywa damu ya ng’ombe, tunaweza kuwapeleka ng’ombe au kuchukua damu yao kisha kuiingiza katika mifumo maalumu isigande kisha inakuwa chakula cha Mbu.
Kuzalisha Mbu inategemea na baiolojia ya Mbu anayezalishwa lakini mara nyingi kuanzia hatua ya yai hadi kuwa Mbu mzima inaweza kuchukua siku 15 na Mbu mmoja anaweza kutaga mayai hadi 300.
Mafanikio ya tafiti
JamiiForums ilitaka pia kufahamu mafanikio ya taasisi hii katika kutekeleza majukumu yake ya kitafiti ambapo Dkt. Lwetoijera amebainisha;
Kuna faida nyingi kwa uchache utafiti wa Ifakara wa Mwaka 2004 ulisaidia Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitisha usambazaji wa vyandarua, kuna chanjo ya Malaria kwa Watoto chini ya miaka mitano iliyopitishwa na WHO pia, kuna dawa ya kutibu Malaria inaitwa ALU, dawa ya Watoto (pediatric medication) Ifakara ilihusika katika kufanya tafiti.
Ifakara tuligundua uwepo wa Usugu wa Malaria, tafiti zetu zilisaidia kuifanya Serikali ipitishe mabadiliko ya Dawa za Malaria.
Kwa mujibu wa Dkt. Lwetoijera, njia ya kuwamaliza mbu hao baada ya utafiti fulani kukamilika ni kutowapa chakula au dawa, usipofanya chochote ukiwafungia bila chakula ndani ya siku tatu hadi nne wote utakuta wamekufa.
Pia, wakimng’ata mtu hapati Malaria kwa kuwa hawana vimelea, saizi ya ukubwa wao ni kama mbu wengine wa kawaida, ni ngumu kutofautisha na mbu wa kawaida.
Mbu hao hawasambazwi, wanabaki Maabara, ni mbu wa majaribio hawatoki kwenda sehemu nyingine.