Nimeona andiko fulani linalosemekana ni la Yeriko Nyerere akihoji uhalali wa Zabuni ya Chakula MNH na Hoja kuwa kila Kabila lina utamaduni wake wa Chakula. Naomba kwa ufupi sana nitofautine na ndugu yangu huyu kama ifuatavyo;
1. Hoja ya kuwa kila kabila lina utamaduni wake wa Chakula
Hoja hii haina mashiko. Swali la msingi ni kuwa je Wachaga waendapo kutibiwa India kwa mfano huenda na Mtori? Wahaya hubeba Matoke na Senene? Jibu ni hapana.
Hili suala la vyakula vya kimila kwa mgonjwa naamini haviishi mtaani na mgonjwa atavipata kwa wingi akishatoka hospitalini.
Binafsi naamini suala la ugonjwa halina utamaduni. Mgonjwa awapo ktk mazingira ya Hospitali ni muhimu apate chakula kulingana na masharti ya madaktari ili kuwezesha kupona haraka.
Pengine Yeriko anasahau mambo manne muhimu. Moja, Yeriko anasahau kuwa MNH siyo hospitali kwa matatizo madogo madogo. Hii ni "tertiary hosp" ambayo kimsingi wagonjwa wake wanatakiwa wawe wameshindikana kutibiwa huko ngazi za chini. Sina uhakika kama hili linafuatwa lakini mara nyingi kila mgonjwa wa aina hii ana mahitaji maalumu ya virutubisho na naamini kuwepo kwa mzabuni na utaratibu mzuri utawezesha wagomjwa kupata virutubisho stahili.
Mbili, bei hii bado si mbaya sana, kama sikosei ni elfu 30 kwa wastani wa elfu 6 kwa siku. Watu wengi hutumia fedha nyingi zaidi ya hizi kwenye starehe na "shughuli" zisizo na tija na hata gharama za kuandaa chakula cha mgonjwa.
Tatu, Yeriko anasahau kuwa uandaaji wa vyakula na usafirishaji hauna ulinganifu wa usalama wa kiafya na waweza pia kuchangia magonjwa mahispitalini. Ni bahati kubwa kuwa hatujawahi kusikia matatizo ya aina hii lakini kutosikia hakuondoi uwezekano wa kuwepo. Uwepo wa mzabuni na utaratibu ukiwa mzuri utahakikisha usafi wa uhakika wa chakula cha mgonjwa.
Nne, naamini hospitali itaweka utaratibu maalumu wa wagonjwa kupewa chakula kwa upendo . Pengine ni vema kuuliza kupata undani wa uzingatiwaji wa "upendo" na lugha laini wakati wa wagonjwa kupewa chakula pasipo kuhukumu kwa kutumia "press release".
2. Hoja ya Zabuni
Kwa hali ya kisiasa ilivyo na utumbuaji majipu sidhani kuwa MNH watafanya kosa eneo hili. Hata hivyo, ni vizuri tujifunze kuaminiana ili twende mbele.
Binafsi naona uamuzi huu umechelewa sana. Ni fedheha kwa ndugu wa wagonjwa kubeba masahani na mahotipoti kuingia Hospitali ya Taifa.
Lazima tukubali kuwa MABADILIKO hayawezi kumfurahisha au kumnufaisha kila mtu. Na sijawahi ona mabadiliko ambayo yanapendwa na kila mtu. Lakini iwapo wengi wananufaika, sioni sababu ya kuyapinga. Tutoe nafasi kwa mabadiliko kabla ya kuyahukumu.
Ni hayo tu...