Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,800
- 34,189
BUNDI ni jamii ya ndege anayeishi kwa kutegemea nyama kama chakula chake kikuu. Hutafuta mawindo yake nyakati za usiku na mara nyingi hutumia mchana kupumzika. Ni ndege mwenye uwezo mkubwa wa kusikia mirindimo ya sauti iliyo ndogo kiasi kwamba binadamu hawezi kuisikia. Huwasikia na kuwavamia hata wanyama wadogo na kujipatia chakula.
Tafiti zimeonesha kumekuwepo na aina zaidi ya 200 za bundi duniani. Bundi jike ana uwezo wa kutaga mayai 12 lakini hutaga mayai manne hadi manane yakipishana siku moja hadi mbili.
Huishi mabara yote isipokuwa Antaktika na waishio maeneo yenye baridi wana maumbo makubwa zaidi tofauti na wanaoishi maeneo yenye joto.
Uono wa bundi ni mara saba ya uono wa binadamu. Lakini pamoja na sifa hiyo hawezi kuona vitu vilivyo karibu, hupaa kimyakimya bila mabawa yake kupiga kelele, ni kutokana na umbo la mabawa hayo na mfumo wake wa manyoya.
Manyoya yaliyopo miguuni mwa bundi hufyonza kelele zitokanazo na upepo na hivyo kuzuia kelele wakati akipaa angani.
Bundi amejitofautisha na ndege wengine wanaokula nyama wakiwemo tai na mwewe kwa kufanya mawindo yake usiku kwa panya, mijusi, ndege na wadudu ili kuepusha ushindani dhidi ya ndege wengine wanaokula nyama.
Makabila mbalimbali nchini huamini bundi akionekana nyumbani kwa mtu huashiria msiba wa mtu kwani baadhi ya watu husadiki ni mchawi au katumwa na wachawi kuchukua roho za watu.
Lakini, bundi ni ndege kama walivyo wengine, isipokuwa hufanya mawindo yake nyakati ya usiku na si kwa sababu ni mchawi au katumwa na mchawi.
Watafiti wanamtaja ni ndege mwenye uwezo mkubwa na wa kipekee wa kunusa harufu ya mzoga kutoka mbali.
Wanasema nyumba ikiwa na mgonjwa mahututi ambaye seli za mwili wake zimekufa lakini mapigo ya moyo bado yanafanya kazi, bundi hunusa harufu ya seli hizo na kusogea karibu kama atapata chakula, lakini binadamu hana uwezo wa kuhisi wala kuinusa harufu hiyo.
Hata hivyo, hawezi kufanya chochote dhidi ya mgonjwa kwa sababu naye humuogopa binadamu kama walivyo ndege wengine.
Kuonekana kwa bundi kwenye nyumba yenye mgonjwa inaweza kuashiria mgonjwa ameshaanza hatua za kufariki dunia kutokana na seli zake kufa na kuna uwezekano wa kufariki katika kipindi hicho.
Watafiti wanaeleza kwamba inapotokea mgonjwa akafariki ndani ya muda mfupi toka bundi aonekane, si kwamba kifo kimesababishwa na bundi bali ni seli za mwili zilizokufa.
Pamoja na bundi kuhusishwa na imani hizo, ana umuhimu mkubwa katika mfumo wa kiikolojia ya kimazingira kusaidia kudhibiti ongezeko la wanyama waharibifu wa mazao ya kilimo wakiwemo panya na wadudu wengine.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Taasisi ya Kudhibiti Viumbe hai waharibifu kina mradi wa kuendesha utafiti wa kubaini manufaa ya bundi kwenye kudhibiti viumbe hai waharibifu.
Utafiti umeonesha moja kati ya viumbe visumbufu katika mazao ni panya na wanadaiwa kuharibu nafaka kwa asilimia tano hadi 15 kwa mwaka huku wakulima wamekuwa wakitumia kemikali zaidi kukabiliana na viumbe hao.
Kwa msingi huo, SUA kinafanya tafiti hizo ambazo zinalenga kukuza matumizi ya bundi kama njia ya kudhibiti panya na viumbe wengine waharibifu.
Licha ya kufanya tafiti hizo, SUA kimeanza kutoka elimu chini ya mradi huo katika wilaya mbili za Mkoa wa Iringa ambazo ni Mufindi na Iringa kuhusu matumizi ya bundi kudhibiti viumbe hai waharibifu wa mazao shambani hususani panya.
Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Kudhibiti Viumbe hai waharibifu kutoka SUA, Dk Martin Martin anasema watafiti kutoka chuo kikuu hicho wametoa elimu hiyo kwa wakulima wa Mkoa wa Iringa hasa katika Kata ya Isimani.
Dk Martin anasema utafiti wa kutumia bundi ni pamoja na kutambua mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa mazingira na kubadili imani potofu na mtazamo hasi kwa wananchi juu ya bundi.
Anasema kwa kuwa bundi anahusishwa na imani za kishirikina, matumizi ya njia ya kudhibiti visumbufu shambani inaendana na utoaji elimu kwa jamii kabla ya kuwaletea teknolojia hiyo.
“Ukiwa na familia tatu za bundi kwenye shamba la ukubwa wa ekari moja utakuwa na uhakika idadi ya panya shambani itapungua mara dufu na huu tunauita udhibiti wa panya kwa njia ya kibaolojia,” anasema Dk Martin na kusisitiza inapunguza matumizi ya viuatilifu vyenye sumu.
Anasema kwa kutumia njia hiyo inasaidia kutunza afya ya mkulima na viumbe hai wengine pamoja na kutunza mazingira kwa ujumla.
Dk Martin anasema bundi anatumika kudhibiti wadudu waharibifu wakiwemo panya kwa sababu wana uwezo wa kula panya kati ya mmoja hadi 12 kwa siku.
Anataja sifa za kipekee za bundi ni uwezo wake mkubwa wa kusikia na kuhisi, kuona mbali mara kumi zaidi ikilinganishwa na binadamu, na uwezo wa kuzungusha kichwa hadi nyuzi 270.
Anasema katika taasisi hiyo wanaendesha utafiti wa bundi hao ambao si wa kufugwa na kwamba kinachofanyika ni kutengeneza viota vinayowavutia kwa ajili ya kuanzisha familia.
Anasema bundi hawawezi kuanzisha familia bila viota, hivyo huwatengeneza viota na kuviweka shambani ambapo mchana wataingia na usiku watatoka kukabiliana na panya.
“SUA tunatengeneza viota maalumu na kusambaza kwa walengwa ambavyo vinawavutia hao bundi kuingia kuanzisha familia na wakishaanzisha hizo familia chakula chao kikubwa ni panya,” anasema Dk Martin.
Anasema mradi wa utafiti wa bundi unaendelea katika mkoa huo na kwamba matokeo yakiwa kama inavyotarajiwa, viota vya bundi vitasambazwa kwa wakulima walengwa.
Naye Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda, anaeleza matatizo yanayozifanya jamii za Afrika kuona bundi ana mkosi ni kwa sababu ya tabia yake ya kuona vizuri usiku na mchana haonekani.
Profesa Chibunda anamueleza hayo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, aliyetembelea banda la Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu la chuo hicho wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya kumbukizi ya 18 ya SUA ya miaka 39 tangu kifo cha Edward Sokoine kilichotokea Aprili 12, 1984.
Profesa Chibunda anasema, utafiti huo utaleta majawabu katika jamii kwa nini bundi anaona usiku na muda mwingi wa mchana analala na kwenye mwanga anaficha macho yake hadi usiku kwenye mawindo.
“Lakini bundi ni ndege wa kawaida kama walivyo ndege wengine,” anasema Profesa Chibunda.
Nao wakulima wa Mkoa wa Iringa, hasa wa Kata ya Isimani wamekishukuru SUA kwa kuwapelekea teknolojia ya viota kwa ajili ya kuanzisha familia ya bundi kukabiliana na panya wanaoharibu mazao yao.
“Kama ujuavyo Mkoa wa Iringa na hasa wilaya yetu ya Isimani inajihusisha na kilimi cha mahindi na panya wanapenda sana kuharibu mazao haya sasa huu mradi ni ukombozi kwetu,” anasema mkulima, Charles Mgimwa.
chanzo: SUA wanavyotumia bundi kudhibiti viumbe hai waharibifu - HabariLeo