Sina mashaka na uwezo wa Omog

Betterhalf

JF-Expert Member
Dec 20, 2016
2,881
2,558
Habari za asubuhi wana JF,

Mimi ni mdau wa michezo, na ninaipenda sana Simba SC.
Katika harakati za kuijenga timu, mwaka jana uongozi wa klabu yetu ulimsainisha Joseph Marius Omog kuwa kocha mkuu akiliongoza benchi la ufundi lililokuwa chini ya Jackson Mayanja.

Omog ni Mcameroon aliyezaliwa 30/11/1971 ambaye ni muumini mkubwa wa 4-3-3. Amepita nyingi katika kuipata taaluma yake, akianzia kwao na baadae Ujerumani ambako alifuzu leseni daraja B ya UEFA.
Kikazi amepita sehemu nyingi ikiwamo timu ya taifa ya Cameroon ambako hakuwa mafanikio sana. Kwa ngazi ya vilabu, kwao na kwingineko amekuwa na mafanikio ikiwamo kutwaa Kombe la Shirikisho la CAF akiwa na AC Leopards ya Congo Brazaville mwaka 2012.

Baadae alijiunga na Azam FC ya Tanzania ambayo aliipa taji la ligi kuu ya VPL msimu wa 2013/2014. Pamoja na kwamba sina utaalam mkubwa wa kuchambua masuala ya kiufundi, binafsi ninamkubali sana Omog kimbinu katika kujenga kikosi ambacho kina uwezo mkubwa wa kujilinda, kupanga mashambulizi na kucheza kitimu.
Kwa hili kikwazo kikubwa kwa makocha wa VPL alikuwa ni Pluijm ambaye pia alikuwa ni mzuri kimbinu. Aidha, sababu nyingine ya kutokuwa na wasiwasi nae, inatokana na kuchukua kombe katika ngazi ya vilabu barani Afrika Ni jambo linaloashiria kuwa ana uwezo na anastahili pongezi.

Kwa nini apongezwe? Ni kwa sababu timu aliyoiongoza haitoki katika mojawapo ya nchi zenye fitina katika soka la kiafrika. Hapa unamaanisha Misri, Tunisia, Algeria, Morocco, Ghana na Nigeria (hasa enzi za ubora wa Enyimba). Kwa nini nimjadili Omog? Hii inatokana na ugeu ugeu ambao wana-Simba wengi tumekuwa nao hasa timu inapopata matokeo mabaya. Ushauri wangu, kila timu imejiandaa kivyao, ili tuweze kupambana lazima tuwe kitu kimoja katika kila hatua ya mapambano haya.

Pia lazima tuwaunge mkono wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa ujumla. Panapolazimika kutoa neno, basi litolewe kama ushauri badala ya kulaumu tu. Kimsingi tupo kwenye wakati mgumu lakini muhimu sana kwetu. Tukiutumia vizuri, tutaumaliza ukame wa miaka takriban minne na tukiteleza tunaweza kusahau ubingwa.

Aidha, ikiwa tumeweza kufikia hapo tulipo, kiufundi tumefanikiwa sana na hatuna haja ya kumtimua Omog kwa kuwa ameshaanza kuitengeneza chemistry ya timu.
Kila la kheri Simba SC, kila la kheri Omog.

Nawasilisha.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…