DR SANTOS
JF-Expert Member
- Mar 11, 2019
- 12,382
- 26,826
MAKABURI YA WASIO NA HATIA (GRAVES OF THE INNOCENTS)- 1
JINA langu naitwa Togolai Mahimba, ni mtoto wa mwisho kati ya watoto saba wa baba yetu, Sinai Mahimba ambaye kwa sasa ni marehemu. Baba yetu alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua ghafla.
Kifo chake kilitawaliwa na utata mkubwa na hata siku ya mazishi yake, kulitokea mambo mengi ya ajabu ambayo mpaka leo siwezi kuyaeleza. Ninayo mambo mengi ambayo ningependa kukusimulia ndugu msomaji lakini kwa kuanzia, naomba nikueleze mambo machache yaliyotokea kabla ya kifo cha baba yetu ambaye mimi ndiye nilikuwa mtoto anayenipenda zaidi.
Kabla hajafikwa na mauti, baba yetu alikuwa mtu maarufu sana kijijini kwetu, Makongorosi, Chunya mkoani Mbeya tulikokuwa tukiishi. Kilichofanya awe maarufu kiasi hicho, ni kazi yake ya uganga aliyokuwa anaifanya ambapo mbali na mambo mengine, alikuwa akiwafanyia matambiko wachimbaji wengi wa dhahabu ili wakiingia mgodini, wapate dhahabu kwa urahisi sambamba na wafanyabiashara wengine.
Umaarufu wa baba ulisababisha hata sisi watoto wake tuwe maarufu sana, hasa mimi ambaye muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kila alikokuwa anakwenda, kuanzia kwenye matambiko maporini, kwenye mazindiko migodini, kuchimba dawa msituni mpaka kilingeni kwake alikokuwa akifanyia shughuli zake za uganga.
Wengi walikuwa wakifupisha jina langu kwa kuniita Togo na hilo ndiyo lililokuwa maarufu kuliko hata jina langu halisi. Nakumbuka maisha yangu ya utotoni yalikuwa ya raha sana kutokana na jinsi baba alivyokuwa akinipenda. Hata ndugu zangu wengine tuliozaliwa pamoja, walikuwa wakinionea gere kwa jinsi nilivyokuwa nikipendwa.
Maisha yaliendelea vizuri, nikawa naendelea kukua huku pia nikijifunza mambo mengi aliyokuwa akiyafanya baba katika kazi zake. Mambo yalianza kubadilika siku moja tukiwa msituni na baba kutafuta dawa.
Baba akiwa ameinama akichimba mizizi ya mti wa mtangetange ambao ulikuwa ukitumika kwa kutibu magonjwa mengi, hata yale yaliyoshindikana hospitalini, ghafla alivamiwa na kundi la popo waliokuwa wanapiga kelele kwa nguvu. Baba akawa anahangaika kujaribu kuwazuia popo hao ambao waliendelea kumzonga hasa sehemu za kichwani.
Akiwa anaendelea kupambana nao, nilimshuhudia akifanya tukio ambalo sikuwahi kumuona baba akilifanya hata mara moja. Kwa kasi ya kimbunga, aliyeyuka na kupotea eneo hilo, nikabaki nimepigwa na butwaa, nikiwa ni kama siamini.
Ghafla wale popo baada ya kuona baba amepotea kimiujiza, walitawanyika na kupotea eneo hilo huku wakiendelea kupiga kelele kwa nguvu. Nikawa nageuka huku na kule kumtazama baba bila mafanikio, hofu kubwa ikatanda kwenye moyo wangu.
“Unashangaa nini Togolai,” sauti ya baba ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashtuka kwa nguvu. Cha ajabu, baba alikuwa amesimama palepale alipokuwepo, akiendelea na kazi yake ya kuchimba mizizi ya mtangetange kama hakuna kilichotokea.
“Baba mbona sielewi?”
“Huelewi nini tena?”
“Popo.”
“Popo? Wamefanya nini?”
“Hawajakuumiza?”
“Mbona sikuelewi Togo?” alisema baba huku akiacha kazi aliyokuwa anaifanya na kunisogelea. Sikutaka kuamini kama kweli baba alikuwa haelewi nilichokuwa nakizungumza, akanisogelea na kunishika begani.
“Uko sawa?”
“Ndi..yo baba, niko sawa,” nilibabaika kidogo, nikamuona baba akigeuka huku na kule kama anayeangalia kitu fulani. Na mimi nikawa nageuka kufuata usawa wa macho yake, ghafla macho yetu yakaganda eneo moja, nilipigwa na butwaa kubwa kwa nilichokuwa nakiona, nikajikuta nikianza kutetemeka.
Wanaume wawili waliokuwa uchi wa mnyama, walikuwa wakining’inia kwenye tawi la mti mkubwa uliokuwa mita chache kutoka pale tulipokuwa, wote wakitukodolea macho yao mekundu.
“Unawaona wale washenzi?” baba alisema huku akionyesha kutokuwa na hata chembe ya wasiwasi. Nikatingisha kichwa kama ishara ya kumjibu ‘ndiyo nawaona’.
“Wale ni wachawi wanaosumbua watu kijijini kwetu, naona wametangaza vita na mimi, hawanijui hawa,” alisema baba na kama ilivyotokea mara ya kwanza, aliyeyuka na kupotea eneo lile, wale wachawi nao wakapotea kwenye upeo wa macho yangu, nikasikia kelele za watu waliokuwa wakilia kwa sauti kubwa kama wanaolalamikia maumivu makali.
“Ndiyo dawa yao, na siku nyingine wakirudia watanikoma,” alisema baba, nikashtuka tena baada ya kumuona amesimama palepale alipokuwa mara ya kwanza, pembeni yangu lakini safari hii alikuwa akihema kwa nguvu kama mtu aliyetoka kukimbia. Nilijihisi kama nipo ndotoni.
“Baba mbona sielewi kinachotoke…” nilisema lakini kabla sijamalizia kauli yangu, macho yangu yalitua kwenye mkono wa baba uliokuwa na jeraha na alama kama ameng’atwa na mnyama mkali, huku damu nyeusi zikimtoka kwa wingi.
“Ninii!” baba alinihoji baada ya kuona macho yangu yameganda kwenye mkono wake.
“Umeumia baba, pole,” nilisema lakini baba hakunijibu kitu zaidi ya kuusogeza ule mkono wenye jeraha karibu na uso wake, akawa analichunguza vizuri lile jeraha.
Akasogea pale kwenye mti wa mtangetange na kuchuma majani yake, akayatia mdomoni na kuanza kuyatafuna kisha muda mfupi baadaye, aliyatoa mdomoni na kuyabandika juu ya kidonda chake, nikamuona akifumba macho kama ishara ya kuonyesha jinsi alivyokuwa akihisi maumivu.
“Nitakuwa sawa usijali, nimeshazoea kusumbuana na hawa wachawi. Inabidi na wewe uwe jasiri,” alisema baba huku akiendelea kujisafisha pale kwenye jeraha lake. Zile damu nyeusi zilizokuwa zinamtoka zikakata, akashusha pumzi ndefu na kuendelea na kazi ya kuchimba dawa.
Kwa kweli matukio yale niliyoyashuhudia yaliufanya moyo wangu uingiwe na hofu kubwa mno. Sikuwahi kudhani baba anaweza kuwa na nguvu za giza kiasi kile, siku zote niliamini alichokuwa anakifanya ni kutibu watu kwa mitishamba tu, basi! Hata hivyo, nilijikaza kiume na kuuficha mshtuko nilioupata, nikaendelea kumsaidia baba na hatimaye tukamaliza kazi yetu.
Wakati tunarudi kutoka msituni, baba alinisisitiza njiani kwamba sitakiwi kumwambia mtu yeyote kuhusu nilichoshuhudia, hata ndugu zangu wa tumbo moja. Akaniambia kwa kilichotokea, anahisi kuna madhara makubwa yatakuwa yametokea kijijini kwetu.
“Unamaanisha nini baba?”
“Wale wachawi waliotuvamia kule msituni, mmoja nimemuumiza sana sijui kama anaweza kuwa yupo hai mpaka muda huu.”
“Kwani ni akina nani wale?”
“Kwani wewe huwajui wale? Au hujawatazama vizuri?” baba alinihoji na kuanza kunifafanulia, akaniambia yule mmoja ni mzee wa kanisa pale kijijini kwetu, aliponitajia jina lake ndiyo nikamtambua vizuri. Alikuwa ni mzee Mwankuga, ambaye mara kwa mara alikuwa akiingia kwenye migogoro na baba kutokana na kugombea mpaka wa shamba kwa sababu shamba letu na lake yalikuwa yemepakana.
Nakumbuka kuna kipindi waliwahi kupelekana mpaka kwa balozi kutokana na ugomvi wao huo. Hata familia zetu hazikuwa na uhusiano mzuri, sisi tulikatazwa kabisa kuongea wala kucheza na watoto wa mzee Mwankuga na yeye hali kadhalika.
“Kwa hiyo unataka kusema mzee Mwankuga naye ni mchawi? Si mtumishi wa Mungu yule na kila Jumapili anaenda kanisani tena anakaa siti za mbele?”
“Mwanangu dunia ina mengi hii! Hutakiwi kumuamini mtu, pale kanisani waumini karibu wote huwa wanakuja kutafuta dawa kwangu, wengine wanataka wapandishwe vyeo, wengine wanataka kujikinga na wengine wana shida mbalimbali, usiwaamini binadamu,” alisema baba, nikabaki nimeduwaa. Hizo zikawa ni habari nyingine za kushangaza sana kwangu.
“Sasa pale si walikuwa wawili? Huyo mwingine ni nani?”
“Si yule mwalimu wenu, Mwashambwa?”
“Mwalimu wetu Mwashambwa anayetufundisha hesabu naye ni mchawi?” niliuliza kwa mshangao mkubwa huku mdomo nikiwa nimeuacha wazi.
“Ndiyo, hata ule mguu wake anaochechemea nasikia alikutana na kombora la kichawi ndiyo likampa ulemavu wa kudumu, siyo mtu mzuri kabisa, we turudi nyumbani utasikia chochote kuhusu watu hao wawili,” baba alisema kwa kujiamini, ukimya mrefu ukatanda kati yetu, hakuna aliyezungumza chochote.
Niliendelea kutembea huku nikiwa na furushi langu la dawa kichwani pamoja na panga, baba yeye alikuwa ametangulia mbele, naye akiwa amebeba dawa na jembe tulilokuwa tunalitumia kuchimbia dawa.
Ili kufika nyumbani kwetu, ilikuwa ni lazima upite nyumba kadhaa za nyasi na nyingine za bati zilizokuwa pembezoni mwa kijiji ndiyo uelekee nyumbani. Miongoni mwa nyumba hizo, ilikuwepo pia na nyumba ya mzee Mwankuga ambaye muda mfupi uliopita baba alikuwa akinisimulia mambo yake kwamba ni mchawi.
Tulipokaribia nyumbani kwa mzee huyo, baba alinionyesha ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo, tukawa tunasikia sauti za watu wengi wakilia kutoka nyumbani kwa mzee huyo, baba akanionyesha ishara kama anayesema ‘unaona?’, nikashika mdomo kwa mshangao. Sikutaka kuamini kwamba kweli mzee Mwankuga alikuwa amefariki dunia.
Je, nini kitafuatia?