Sikukukataa mwanangu; Umasikini ulifanya mama yako anikimbie

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
26,639
64,204
SIKUKUKATAA MWANANGU; UMASIKINI ULIFANYA MAMA YAKO ANIKIMBIE.

Kwa Mkono wa, ROBERT HERIEL.
© maandishi ya Robert Heriel Kwa lugha ya Kiswahili.

Taikon wa Fasihi Anawasilisha

"Sasa nimebaki Peke yangu, hata waliowangu hawanitaki, sio wangu tena, ingawaje ni Mali yangu kiasili lakini dunia imenigombanisha nao. Sijui mambo haya yataisha lini, Mwanzoni nilitaka kujua yanamaana gani lakini nafikiri hata ningeijua maana yake wala isingenisaidia kitu. Mambo haya yamenichosha!

Niliamini na kuaminishwa tangu nikiwa kijana shupavu, mwenye nguvu na moduli Imara yakiwa; mvumilivu hula mbivu na mchumia juani hulia kivulini lakini kumbe sio mara zote maneno hayo ya wahenga huwa kweli. Nilivumilia Pasi ya kulia machoni nikiwa na subira ambaye angemualika Kheri, lakini haikuwa hivyo. Mambo yalizidi kunichachamalia, mpaka unachokiona hivi leo sijawahi pata ahueni.

Umasikini ni laaana mbaya Sana. Umasikini ndio huo ushetani, unaweza niita Shetani, kwani yeye ndiye hapendwi na watu wote Duniani. Hakuna ampendaye masikini, hata yeye mwenyewe hajipendi. Umasikini ni chuki! Chuki inayopikwa ikaiva na Kunuka watu wakereke.

Haya nambie ni Nani alikuelekeza nipo huku na Mimi ndiye Baba yako?"
Nikasema nikimtazama binti yangu

" Niliipata hii barua kutoka katika Sanduku la Mama, nilishtuka nilipoiona, moyo wangu ulianguka katika mhimili wake, nashindwa Kueleza ilivyokuwa, nilipoisoma nilijikuta machozi yakinidondoka, ndani ya barua hii kuna mtu imemtaja anaitwa Evitha, huyo ni rafiki wa Mama, yeye ndiye alinambia mambo ambayo sikuwahi kuyafikiri, na sikuwahi kujua kuwa Mimi naitwa TABASAMU, lakini Evitha alinambia yote, akanielekeza Kwa rafiki yako wa zamani aitwaye SADIKI, nikaenda Kwa SADIKI ingawaje ni mbali na nyumbani, ilinichukua masaa matatu ndani ya Gari.."

"Ooh! SADIKI! Bado yupo, rafiki wangu wa muda mrefu Sana, tangu tukiwa Vijana wadogo, siku zile tukiwa ndio tumekuja mjini kutafuta maisha. Vipi maendeleo yake na Familia yake, hajambo?" Nikamkatisha binti yangu baada ya kusikia jina la rafiki yangu, Sadiki.

" Hajambo, maendeleo sio mabaya Sana ukilinganisha na yako, Sadiki alinihadithia kila kitu alichokijua kuhusu wewe, alisema kuwa Wewe ni mtu mwema, mkarimu, mcheshi na ati ulikuwa kijana mtanashati Sana, akanipa picha mlizopiga wote, hizi hapa"
Binti akatoa picha kwenye mkoba wake akiwa karibu yangu, akanikabidhi. Nikawa nazitazama;
" Ulikuwa kijana Mzuri, sio ajabu Mama yangu alishindwa kukukataa, sasa sijui ilikuwaje mkatengana..."
" Uzuri hauna maana yoyote ukiwa masikini, tena mbele ya mwanamke mwenye tamaa ya Mali, sisemi kumtukana Mama Yako, Hasha! Ila utanashati wangu haukushinda nguvu za umasikini. Tukaachana"
Nikajibu huku macho yangu yakiendelea kuzitazama picha alizokuja nazo binti yangu alizopewa na Sadiki.

Zilikuwa picha tatu,
Picha ya Kwanza ilikuwa ikinionyesha Mimi na Kundi kubwa la Vijana wapatao kumi, watano wakiwa wamesimama, watano wakiwa wamechuchumaa. Nikamuuliza binti yangu;
" Umenitambua kwenye picha hii Mimi ni yupi?"
" Aaanh! We.ewe ni huyu hapa aliyechuchumaa, aliyevalia suruali na Shati la mikono mirefu,, mwenye Afro nyingi kuliko wote. Picha hii ya zamani Sana mpaka rangi imebadilika" TABASAMU akasema akinionyesha.

" Yes, wala hujakosea, Jambo gani limekufanya unitambue?" Nikamuuliza.
" Mbali na Sadiki kuwa alinionyesha lakini mtu yeyote akipewa picha hii atasema Kama nilivyosema; tunafanana Sana Baba" TABASAMU akajibu huku wote tukicheka.

"Picha hii inaonyesha tulikuwa wengi mno, nilikuwa nafanya kazi katika kiwanda cha nguo, Nilifanya kazi Kwa nguvu sana, nikiwa na ndoto kubwa, licha ya Mshahara ulikuwa mdogo lakini nilijibana, nikanunua mahitaji yangu ya ndani Kama kitanda, Godoro, na vitu vingine vya ndani, maisha yaliendelea nami nikiendelea yasiniache nyuma,
Sikutaka maisha yaniache na kunifarakamisha na waliokuwa nami nyakati ngumu, hivyo kidogo nilichokuwa napata nilikuwa natuma nyumbani Kwa Baba na Mama yangu,
Sikutaka kuwaacha wazazi wangu wala kipato changu kidogo hakikuwa kisingizio cha kutowahudumia. Nilipopata Mia niliwapa kumi, nilipopata Elfu niliwapa Mia, niliwapa nikijua wanastahili kikubwa zaidi ya kidogo niwapacho" nikameza mate kisha nikaendelea.

" Atoaye hubarikiwa, awatunzaye wazazi kuongezewa ndiyo ilivyosemwa na ndivyo nitakavyo kuusia binti yangu. Maisha yangu yalibadilika, baraka zikafunguka, nikaongezwa Cheo na kamshahara kakaongezeka, hii ni kutokana na kujituma Kwa nguvu zote Pasi na kuchoka, pamoja na baraka za wazazi wangu.
Kipato kikiongezeka matumizi huongezeka, nikajaza makazi yangu niliyopanga vitu vya ndani, Kwa kweli Kwa kijana wa wakati ule ningeweza kusema nilijivunia kuwa na mahali pazuri pakujishikiza"
Hayo yote niliyasema nikiwa namtazama binti yangu, Tabasamu. Kuna wakati hisia zilifanya misuli ya macho ilegee nusura nitoe machozi, lakini nikawa nayazuia. Haipendezi Baba kulia mbele ya mtoto. Lakini mambo mengine yanaumiza.

" Upweke!" Nikameza fumba la mate kisha kimya kikatokea Kwa kitambo kidogo kabla hakijafukuzwa na TABASAMU;
" Upweke!"
" Yes upweke, pengine hujawahi kuishi mwenyewe, ikiwa uliwahi basi utanikubalia kuwa Upweke ni zaidi ya kaburi, upweke ni njia ya kifo, upweke unaua. Upweke haukupi Raha ukafurahi, upweke unaathiri namna ya kufikiri.
Nilikuwa mpweke pindi nikirudi nyumbani nikitokea kazini, chakula hakiliki kikalika Kwa UTAMU, usingizi hauwi mtamu. Kuamka amka usiku inachosha kujikuta upo mwenyewe Kama kaburini. Ndipo wazo la kuoa liliponijia akilini.
Dawa ya kijana mpweke ni Kuoa, usioe au kuolewa Kama haujisikii mpweke, ndoa haimfai mtu asiyejihisi mpweke"

Tabasamu alikuwa akinisikiliza Kwa umakini mkubwa Kama mtu asikilizaye hotuba ya Karne, huenda maelezo yangu yalimsisimua, au pengine ni hamu tuu ya kumsikiliza Baba yake mzazi kwani tangu azaliwe hajawahi kumuona.

"Nimetoa maelezo mengi Sana, lakini picha hii inaelezea mwanzo wa mapambano yangu. Siku zote Mwanzoni watakaokusapoti wanaweza kuwa Wengi, Marafiki huwa wengi lakini mambo hubadilika kadiri siku ziendavyo, watu hao hupungua na kupungua na kubaki mmoja au asibaki hata mmoja aliyeupande wako. Kupandishwa daraja na Cheo kazi kulipunguzia marafiki, niliokuwa nikicheka nao wakanichukia, penye riziki hapakosi fitna binti yangu, rafiki wakapungua nikabaki na rafiki mmoja, ndivy huyu SADIKI"
Nikasema huku nikimuonyesha Kwa kidole Sadiki aliyeko katika Ile picha. Tabasamu akasogeza USO wake kumtazama Sadiki katika Ile picha yenye watu kumi.

" Waaoh! Kumbe mmetoka mbali Sana na Sadiki, ndio maana alisema wewe ni rafiki yako wa kweli" Tabasamu akasema.

"Kipato kinapoongezeka watumiaji huongezeka pia, ukiwa na kipato duni utajipangia bajeti na wala hakuna atakayekusumbua, lakini kipato kinapoongezeka na kuwa maradufu utashangaa wapanga bajeti yako nao wanaongezeka, wao hupanga pesa yako utadhani yakwao, na ukithubutu kuwazuia chuki na maneno yasiyofaa wanakuzushia"
Nikasema.

Nikachukua picha ya Pili;
Picha hii ilionyesha watu wanne, mwanamke akiwa mmoja.
" Je unamtambua yeyote katika picha hii?" Nikamuuliza binti yangu, ndiye huyo Tabasamu.

" Huyu ni wewe, huyu ni rafiki yako Sadiki, hawa wawili siwajui; mlikuwa mmependeza Sana" Tabasamu akasema akiwa ameukunjua USO wake Kwa Tabasamu.

" Vizuri, umejibu vyema; Ni kweli tulikuwa tumependeza, pesa ilishaanza kutuzoea, na siku zote pesa ikikuzoea utapendeza" wote tukacheka.

" Huyu mwanamke katika picha hii aliyekaribu yangu anaitwa Isabella, huyu ndiye Mama yako..."
" Mama yangu!!! Unatania" Tabasamu akanikatisha Kwa sauti ya kushangaa.
Mimi nikawa namtazama, Tabasamu akaichukua Ile picha mikononi mwangu, akawa anaitazama Kwa hisia, alikuwa akiitazama Kwa nusu dakika kisha ananitazama usoni, alafu anaitazama tena vivyo hivyo mpaka dakika mbili zilipoisha. Nami nikawa kimya kumpa nafasi ya hisia zake kufanya kazi.

" Alikuwa mrembo Sana Isabella, uzuri wake ulivuka mpaka katika mbingu, habari za uzuri wake zilienea katika jiji zima, mpaka nchi nzima ikamtambua Isabella. Urembo wake ulivuka bahari mpaka nchi za mbali. Alikuwa mwanamke wa gharama na alistahili kugharamiwa. Nafikiri unamuona Isabella ndiye Mama yako huyu.
Ingawaje Sura umechukua kwangu lakini mambo mengine mengi umeyarithi kutoka kwake, si unaona macho yako yalivyo, unaona rangi, angalia umbo piah, huyu ndiye Isabella Mama Yako"
Nikameza fumba la mate na Kusafisha koo kisha nikaendelea;

" Mwanamke huvurugwa na kijana mtanashati, mzuri na mwenye mvuto, hilo ni Jambo la Kwanza. la pili, mwanamke huvutiwa na kijana mcheshi na mwenye akili za kutosha kumdhibiti,. La mwisho, mwanamke huvutiwa na Mwanaume mwenye kipato kizuri atakayeweza kumhudumia.
Mimi nilikuwa na sifa mbili Kati ya hizo, nilipungukiwa sifa moja ya kutokuwa na kipato kizuri cha kumtunza mwanamke mzuri Kama alivyokuwa Mama yako.
Lakini mengine mvuto na haiba nilikuwa nayo, ucheshi na akili ya kumtuliza Kwa maneno mazuri nilikuwa nayo.
Mama Yako mara Kwa mara alikuwa akikiri kuwa Mimi ninamaneno mazuri Sana.
Nami nilijua kuwa wanawake hupenda maneno mazuri kuliko kitu kingine chochote kile baada ya pesa."

"Hahaha! Baba bhana! Unaonekana ulikuwa mtundu na. Muongo muongo mpaka mama akaingia kingi" Tabasamu akasema akiwa kanikatisha.

" Uongo unaladha yake Kwa mwanamke, uongo Kwa mwanamke huuona kama akili ya ubunifu, pasipo uongo mwanamke yu akuona huna ubunifu, huna akili ya kujiongeza, hata hivyo sio kila Jambo ni lakusema uongo Kwa mwanamke, Ila walau ujue kuwa kuna mambo mwanamke anataka adanganywe ili Moyo wake ufurahi. Zingatia binti yangu, mwanamke anahitaji Moyo wake ufurahi pasipo kujali ni uongo au ni kweli" Nikasema kisha nikamtazama binti yangu.

"Mmh! Baba unamambo Sana, enhee! Ikawaje"
Tabasamu akasema.

" Akanikubalia na Rasmi tukaingia kwenye Mahusiano. Sikutaka kumuonyesha ninapoishi Kwa sababu Kwa jinsi umuonavyo Isabella asingekubali kuishi na Mimi katika Mazingira Yale. ingawaje nilikuwa nimejitahidi kujijenga lakini bado niliamini sijakidhi vigezo vya kumpeleka Isabella ninapoishi.
Mwanamke mzuri hustahili mambo mazuri, labda ningeamua kujiongopea tuu lakini ukweli ndio huo. Mbinu ya kukutana naye hotelini ilisaidia.
Baada ya miezi mitatu Kuisha tukiwa katika mapenzi motomoto, Isabella akapata ujauzito.
Zilikuwa habari njema Sana kwangu, ulikuwa ni ushindi ambao katika maisha yangu mpaka leo sijawahi kuupata, kupata mtoto na Mwanamke mzuri Kama Isabella ni zaidi ya bahati.
Isabella akaniambia kuwa Kwa vile sasa anamimba basi nimpeleke ninapoishi ili akapaone, nikamwambia haina shida, lakini sikutaka nimuwahishe kumpeleka kwani mimba ilikuwa changa angeweza kuitoa. Nilipata wazo kuwa nisubiri ikue ifikie miezi isiyowezekana kutolewa, nilijua Kama nitampeleka Isabella mapema ninapoishi anaweza akapachukia na kuitoa mimba yangu kisha tukaachana. Hilo sikutaka litokee.
Miezi Saba ilipoisha, Isabella akiwa kachoka kabisa nikaona ule ndio ulikuwa muda sahihi wakumpeleka mahali ninapoishi. Kwa kipindi kile mimba za miezi hiyo kuzitoa isingewezekana kwani Teknolojia ilikuwa duni.
Nikampeleka, Kama nilivyokuwa nimetarajia, Isabella hakupendezwa na makazi yangu niliyokuwa nimepanga, USO wake ulikuwa na hasira, sikuwa kumuona Isabella katika Hali Ile.
Hakutaka hata kuingia ndani, alikasirika Sana. Akaondoka licha ya jitihada nilizofanya ili aingie walau apaone humo ndani"
Nikameza mate na kushusha pumzi alafu nikamtazama Tabasamu, niliuona USO wa Tabasamu ukiwa umebadilika Sana, tayari Huzuni ilimuingia, alinitazama Kwa kunionea huruma.

"Pole Sana Baba" Akasema . Nikamtazama kisha nikaendelea.

" Mama Yako akajifungua, nilienda kumuona Hospitalini, nilimkuta akiwa amefurahi Sana kumpata mtoto wa kike, Kwa jinsi nilivyomuona akiwa ametabasamu ndio maana nikakuita wewe Tabasamu, ingawaje sina uhakika kama bado unatumia jina hilo"
Tabasamu akanikatisha akasema;

" Hapana, natumia jina la Angelica, jina la Tabasamu sijawahi kusikia yeyote akiniita na wala sikuwa kufikiri naitwa jina Hilo, barua hii ndio ilinishangaza nilipokuta jina hilo, na nilipofika Kwa Evitha rafiki yake na Mama nilipomueleza hayo akaniambia "Tabasamu" ndio jina nililopewa na Baba yangu. Na hata nilipofika Kwa SADIKI japo hakunitambua lakini baada ya kujitambulisha akaniambia mtoto wa Rafiki yake aliitwa "Tabasamu""
Akasema huku uso wake ukiwajawa na simanzi.

" Hakuna apendaye kurithi jina la Baba Masikini, Nani atakayekubali ubin wa masikini, Mimi sijawahi kuona na utu uzima wangu huu, wengi hujilazimisha tuu lakini ukweli hakuna apendaye kuitwa jina la Baba Masikini. Ndoto ya wengi hupenda majina makubwa, hutamani Baba zao wangekuwa watu wakubwa wenye majina ya heshima. Sio majina yenye vinasaba vya ufukara"

" Habari za huyu mtu wa nne nitakueleza habari zake baadaye" Nikasema kisha nikachukua picha ya mwisho ambayo ni yatatu alizokuwa amezileta Tabasamu kutoka Kwa SADIKI.

Picha ya tatu,
Ilikuwa inaonyesha watu watatu, mwanaume mmoja aliyebeba mtoto mchanga, na Mwanamke mmoja.

" Hii nayo kuna yeyote unayemfahamu?"
Nikamtazama Tabasamu nakuuliza.
" Huyu ni wewe, Huyu ni Mama unayemuita Isabella, sitaki kuamini huyu uliyembeba ndio mimi!" Tabasamu akasema huku akimtazama mtoto mchanga aliyekuwa kabebwa na Mwanaume mmoja pichani.

" Uamini usiamini, huyu ni wewe, hapa ulikuwa na miezi miwili baada ya kuzaliwa. Picha hii inamambo mengi Sana, unaona nyuso zetu, zilikuwa bado na nguvu ya ujana. Mama Yako licha ya mahusiano yetu kuwa mabaya kutokana na Simulizi nitakayokusimulia muda mfupi ujao, lakini siku moja Malaika mwema alimshauri vyema, siku hiyo alimtuma rafiki yake Evitha aje kuniiita kwani alikuwa nashida na Mimi, Evitha akanichukua mpaka kwenye makazi mapya ya Isabella ambayo alihama kunikwepa nisimsumbue sumbue. Yalikuwanmakazi Bora kabisa yenye kutamanika na wanadamu wengi Duniani. Yalikuwa pembezoni mwa ufukwe wa bahari.
Nilipofika nikiwa na Evitha, Isabella alinilaki kisha akanirukia na kunikumbatia Kwa nguvu nyingi, akiwa kanikumbatia niliyasikia mapigo yake yakidunda Kwa nguvu sana mithili ya mtu anayekata roho Kwa kifo cha kikatili,
Isabella alilia Sana akiwa kanikumbatia, kila alipojaribu kutaka kusema Kwikwi ilikuwa ikimzuia. Moyoni nikajiuliza mambo haya yanamaana gani. Asiwepo wa kunijibu"
Nikanyamaza, nikamuomba Tabasamu animiminie maji kwenye Bilauri ilivyokuwa pale mezani. Akafanya hivyo, nikanywa maji kisha nikaendelea kuongea;

" Akaniachia kunikumbatia, kisha tukaelekea katika sebule yenye samani za kisasa kabisa, hapo akamuagiza Msaidizi wa kazi akamlete mtoto chumbani, akaletwa, moyo wangu ulilipuka Kwa furaha nilipombeba mtoto. Kalikuwa katoto kazuri Sana kenye uso mzuri Sana usio na hatia, kalikuwa kamelala, nilifurahi kumbeba mwanangu katika mikono yangu hii; Isabella na Evitha walikuwa wakinitazama Kama wanawake wanaofurahia kumuona mwanaume abebaye mwanaye Kwa mapenzi yote.
Isabella akaniambia; hapana Shaka huyu mtoto ni wako, na Mwanamke timamu Kama mama WA dunia mwenye jukumu la kuleta watoto duniani hawezi fanya Dhulma kubwa kwa mwanaume aliyempa mtoto. Huyu mtoto ni wako, siwezi kukudhulumu kilicho chako. Ninaweza kukudhulumu mambo mengine lakini kamwe siwezi kukudhulumu Damu yako. Huyu ni mwanao. Lakini maisha haya yanataka kunitenganisha nawe, sipendi kulisema hili lakini nafikiri unalielewa, Mimi ni mwanamke mzuri, ulipenda kuniiita Malaika niliyeomba hifadhi Duniani, hukuwa mbali na ukweli kwani ndivyo nionekanavyo, siwezi ishi maisha ya dhiki Mpenzi wangu. Nakuomba Jambo moja, naomba ukae mbali na Mimi, usinitafute wala kunitafuta, niambie ni kiasi gani nikupe ili usinitafute Mimi na mwanangu? Nikamtazama mama Yako, nikamuuliza Kwa mshangao; unataka nikuuzie mwanangu?' akanitazama kisha akajibu, unaweza ukasema hivyo Mpenzi. Tukagombana Sana na Mama yako, siku Ile nililia Kama mtoto mdogo, hata hivyo muda wa kuondoka ulikaribia, akaniambia mume wake anayeishi naye anakaribia Kurudi kutoka kazini, hivyo tupige picha ya ukumbusho ndipo niondoke, tukapiga picha, akaisafisha palepale kwani ñyumba Ile ilikuwa na vifaa vingi vya kisasa kutoka nchi za Magharibi. Akanipa Nakala moja nyingine akabaki nayo, akaniondoa"

Nikachukua Bilauri nikameza fumba la maji kisha nikaendelea;

" Niliondoka Kwa hasira, nisingekubali kumuuza mwanangu wa kumzaa, hata Kwa taabu ipi, isingewezekana, nilikuwa tayari kwa lolote. Wakati narudi nikapitia Kwa SADIKI na kumuelezea Yale yote yaliyotokea, akanipa pole na kunishauri niachane na Isabella kwani mtu anayetoka naye ni tajiri na mtu anayeogopwa na watu wote katika jiji hili. Mimi sikuwa tayari kupokea ushauri wa Sadiki, nilimuona Kama naye ni Wale Wale. Nikatoka Kwa hasira na kuisahau hii picha. Masikini Sadiki, kumbe aliitunza;
Baadaye nikajikuta katika matatizo makubwa yaliyosababishwa na huyu mtu"
Nikaichukua Ile picha ya pili inayoonyesha watu wanne, ambao watatu nilishawatambulisha,

" Ndio namuona, ulinambia utanielezea habari zake"
Tabasamu akasema huku akimtazama akijaribu kumfahamu lakini hakuweza kumtambua kabisa.

" Mtu huyu ndiye aliyekuwa akiishi na Mama yako, ndiye alikuwa mmiliki wa kiwanda cha nguo nilichokuwa nafanyia kazi,ukaribu wangu naye ulizidi kuimarika baada ya Mimi kumpata Isabella, sikujua Kwa nyuma mtu huyu alikuwa akinilamba kisogo na ulimi wenye makali ya Upanga, pesa zake zilimsomba Isabella, licha ya kujua Isabella ni mchumba wangu na tayari alikuwa na mimba lakini Hilo halikumzuia katika mpango wake wa kumnasa Isabella. Alifanikiwa.
Siku moja, akaniita ofisini kwake, akanipa barua ya kufukuzwa kazi, nilipomuambia sababu ya yote hayo ni nini, hakunijibu zaidi ya kuita walinzi wanitoe mule ofisini kwake na kuweka amri kuwa nisionekane tena katika kiwanda kile. Siku zile sikujua sababu ya hayo yote.
Mambo yangu yakaanza kuniendea Mrama, maisha yakawa yashida Sana, ilifika wakati nakosa pesa ya kununulia sabuni na dawa ya Meno, Isabella hakutaka tena kunijua, aliniacha solemba, Wale waliosubiria anguko langu wakagweka sherehe, wakashangilia, na kunizomea. Kodi ya nyumba ikawa ni shida.
SADIKI alikuwa msaada mkubwa kwangu, lakini nilijua kuwa naye anafamilia yake nisingekubali kumpa mzigo wakati wote, nikaona ni busara kuuacha mji na kusogea nje kidogo ya mji ambapo nilinunua kiwanja,
Hapo nikajitengenezea kibanda changu cha miti na kuezeka Kwa nyasi ili niweze kujisitiri"

Nikameza mate kisha nikamtazama Tabasamu aliyekuwa alitokwa na machozi, nikamshika usoni na kumpangusa machozi yake Kwa viganja vyangu vigumu.
Kisha nikasema;
" Usilie binti yangu"
" Nilimkumbuka mwanangu, nikasema nitaenda mjini kumsalimia na kumuona Isabella Kwa vile nilijua walipokuwa wakiishi, nikabangaiza kukusanya nauli, wala haikuwa nauli kubwa ya kusema kubwa Sana, ni nauli hizi za daladala tuu kwani nilikuwa nje ya mji lakini sio mbali na mji. Lakini licha ya nauli kuwa ndogo lakini huwezi amini binti yangu, Ile Ile nauli ndogo ilikuwa ikinishinda, sikuwahi fikiri ipo siku nauli ya Daladala itanishinda, lakini ndio hivyo mwanangu, maisha yanaenda mbele, maisha hayana macho, hatujui yaliyombele yetu kwani Sisi ni vipofu"

" Nikafika alipokuwa anaishi Isabella, siku Ile ilikuwa siku mbaya kwangu, nilipofika baada ya kugonga Geti, likafunguliwa na Mdada wa kazi, na Kwa vile alikuwa akinifahamu alifurahi kuniona, akanikaribisha Kwa hamasa, lakini tulipofika sebuleni nilishtushwa kumuona Isabella akiwa na mtu huyu, jina lake utalifahamu"

" Sikuwahi kuhisi maumivu Kama Yale ya Ile siku, yalikuwa maumivu makali Sana yasiyoelezeka. Kumbe mapenzi yanauma, wivu mkali ulinishika, nikamfuta mtu yule aliyekuwa akinywa Wine nyekundu nikaichukua Ile chupa na kumpiga nayo usoni, akachanika, lakini sikumuacha, nilikuwa Kama mwendawazimu, nilimpiga haswa lakini kamwe huwezi shindana na mwenye pesa, nikajikuta nipo korokoroni, nikakaa mahabusu Kwa wiki tatu nikiteswa na Askari magereza waliolipwa pesa nyingi na mtu Yule. Siku ya nane Isabella alikuja akiwa akiwa kabakiza siku chache ajifungue, akanitoa mahabusu na kunionya kuwa Kwa Usalama wa maisha yangu niachane naye tuu. Isabella akasema; siwezi kwenda Leba wakati Baba mwenye mtoto nikiwa katika Hali Ile, yaani nikiwa mahabusu. Akanitoa kisha akanipa milioni moja, akaniambia tarehe ya kujifungua aliyoambiwa Hospitalini, hivyo itapendeza nikienda kumuona mtoto siku hiyo yakujifungua"

Hapo nikameza fumba la mate kisha nikaendelea;

" Tukaachana nikiwa nimerudi nyumbani kwangu nje ya mji, nikiwa na milioni moja, ilikuwa pesa nyingi Kwa wakati ule. Japo nilianza kumchukia Isabella lakini siwezi jiongopea kuwa bado niliona ananipenda, siku ya Isabella kujifungua ilipofika nilifika Hospitalini Kwa kufuata maelekezo aliyonipatia, nilienda nikiwa na zawadi ndogo, Isabella alivyoniona alifurahi, alitasabasamu, na hapohapo nikambeba mtoto nikamsema; utaitwa Tabasamu. Hilo ndilo jina lako.
Punde wakaingia watu waliovalia kiaskari wakiwa na mtu Yule, wakanitoa mule wodini, nilipiga kelele waniache, mtoto alilia Sana lakini Wale Askari hawakujali. Wakanipeleka tena korokoroni. Nikakaa mwezi mahabusu nikisubiria kesi yangu ya kubambikiwa ya madawa ya kulevya. Lakini siku isiyo na jina nikiwa mahabusu Askari magereza akaja kunichukua na kunipeleka mapokezi, hapo nikakutana na Evitha, akaniambia Isabella amemuagiza aje kunitoa. Basi nikatolewa mahabusu. Evitha akiwa kwenye Gari yake akaniomba anipeleke kwangu nikamkatalia kwani sikutaka mtu yeyote apajue isipokuwa Sadiki tuu. Nilifanya hivyo Kwa sababu mbili; moja, niliishi kwenye makazi duni nilijisikia vibaya watu wanaonijua kujua ninaishi mahali Kama pale, lakini Jambo la pili, ni usalama wangu"

Nikameza mate kisha nikaendelea;

" Miezi miwili baada ya mtoto kuzaliwa, Sadiki alikuja ninapoishi akanipa habari kuwa Evitha ananitafuta, akaniambia amesema nikutane naye siku ya jumamosi kwenye hoteli maarufu hapa jijini. Nilipokutana na Evitha ndio akanipeleka kwenye makazi mapya ya Isabella, tukapiga picha hii, na akataka nimuuzie mtoto"

"Nilipokataa baada ya kuondoka, nilifuatiliwa mpaka wakanikamata, nikafungwa Kwa kesi ya kubambikiziwa miaka kumi jela. Kwa kweli maisha yangu yalibadilika mno. Yalikuwa magumu. Dunia iliyokuwa inaenda mbele Kwa Kasi kwangu niliiona Kama inanitumbukiza shimoni. Baada ya kutoka siku na hata Mia ya kuanzia maisha, nilienda kwenye eneo langu lile nililonunua nyakati zile, Kwa vile lilikuwa eneo kubwa na mji ulikuwa umesogea kutokana na watu kuongezeka, nikaligawa nusu na kuuza, ndipo nikajenga nyumba hii hapa uliyonikuta nayo. Nilipojaribu kumtafuta Isabella ili nimuone mwanangu sikuweza kumpata tena. Pale alipokuwa akiishi walinambia wala hawamjui mtu huyo. Miaka kumi ni mingi Sana, mambo hubadilika, hivyo nikaona wanahaki ya kutomjua Kama alihama muda mrefu. Leo ni miaka zaidi ya thelasini tangu nilipouacha USO wa Isabella na mwanaye"

" Leo Mungu kanikumbuka, nilikuwa nimetengwa na Dunia, niliishi Kama mchawi, kuna wakati nilihisi Mungu naye kaniacha, mambo niliyoyapitia ni magumu Sana. Mengine siwezi kuyaeleza Tabasamu,

Vipi Mama Yako hajambo?"
Nikasema huku nikiziweka picha mezani kisha nikamtazama Tabasamu;

" Pole Sana Baba, sikuyajua mambo haya. Ama kweli dunia kuna mambo ukiyajua yanaumiza Sana. Siku ya Leo ninafuraha iliyochanhanyika na Huzuni Nyingi. Jiandae tuondoke hapa"
Tabasamu akasema,

" Binti yangu, tuondoke hapa tuende wapi?"
Nikamuuliza.
" Nataka nikupeleke kwangu, siwezi ondoka bila wewe Baba yangu"
" Sidhani Kama ni wazo zuri mwanangu"
" Tuondoke Baba"
Tabasamu aliongea akiwa anamaanisha, tulitoka nje nikaoanda Gari la binti yangu, wote nyuso zetu zikitoa machozi yasiyokauka licha ya kujitahidi kuyazuia.

" Kwa hiyo Baba huna Mtoto mwingine tena au hukuweza kuoa?"
Tabasamu akasema huku akiendesha Gari.
" Baada ya kutoka jela mambo mengi yalibadilika, sikuwa naendana na Dunia ya utandawazi, wanawake wa utandawazi wengi hupenda wanaume wenye vipato tuu, angalau mama Yako alikuwa anavigezo vitatu lakini wanawake WA sasa kigezo Chao ni pesa. Sikutaka yajirudie yaliyonikuta, niliamua nisiwe na Mwanamke, hivyo sikubahatika kupata mtoto"
Nikaongea Kwa uchungu na hapo nikamuona Tabasamu akianza kulia Kwa sauti.
Huzuni ilijaa mule ndani huku mngurumo WA gari ukifanya hisia za majonzi kuongezeka.

Baada ya kitambo cha masaa mawili tulisimama nje ya Geti kubwa lenye jumba la kifahari ndani yake.
Tukaingia ndani, kisha tukatoka ndani ya Gari, Tabasamu akanikumbatia na kunishika Mkono mpaka tulipoukabili mlango wa sebuleni. Tukafungua mlango.

Tabasamu akanikaribisha, sebuleni ilikuwa sebule kubwa Sana yenye thamani za Hali ya juu. Baadaye Tabasamu akaenda kwenye jokofu akaja na birika lenye Juisi akiwa kabeba na Bilauri ya thamani, akanimiminia Juisi kisha akanikaribisha. Baada ya kunikaribisha akaondoka kuelekea ndani huku akinambia anakuja sasa hivi.

Nikawa nakunywa huku nikaendelea kusanifu uzuri wa mandhari ya juamba lile. Kitambo kidogo nikashtuka kumuona Isabella akiwa na wheelchair ambayo juu yake aliyekuwa kakaa alinipa mshtuko mkubwa, macho yangu yalishindwa kushangaa kumuona Isabella akiwa kwenye wheelchair, moyo wangu ulifadhaika Sana kumuona Isabella katika Hali Ile.
Isabella aliponiona akajaribu kujinasua pale lakini ikashindikana, alitaka kuja kunilaki na kunikumbatia, Mimi nilikuwa nimesimama nikiwa nimeduwaa Bilauri ikiwa mkononi. Nilimkimbilia na kumkumbatia Isabella, mwanamke niliyempenda Kwa moyo wangu wote, lakini aliyeyajeruhi maisha yangu.

Tulikumbatiana na Isabella akiwa pale kwenye wheelchair Kwa kitambo huku Isabella akilalamika kuwa amenikosea Sana, anaomba nimsamehe Kwa yote.
Alikuwa keshakuwa mtu mzima Sana umri unaokimbilia miaka sitini, Hakuwa amepishana kiumri Sana na Mimi.
Uso wake bado ulikuwa na uzuri wa kizee, macho yake yalificha majuto ya miaka nenda Rudi.

Tukakaa kwenye sofa.
" Tabasamu naomba uniweke karibu na Taikon Baba yako" Isabella akasema. Tabasamu alishtuka kuitwa Tabasamu na Mama yake, alimzoea mama yake akikutumia jina la Angelica.
Baada ya Isabella kuwekwa karibu yangu alinishika miguu yangu akanitoa kwenye wheelchair akapiga magoti nakuanza kulia aliomba nimsamehe.
"Usilie Isabella, maisha hayana macho, na Sisi ni vipofu hatukujua mambo yote haya Kama yangetukia, ujana wetu ulikuwa WA taabu, sasa tunaukabili mwisho wetu, ukingoni tumefikia, hatuwezi kulaumiana"
Nikasema kisha nikaendelea.

" Nimekusamehe Kwa yote uliyoyatenda na pia nimekusamehe Kwa yote utakayotenda. Hiyo ndio maana ya samehe Saba mara sabini. Nawe nakuomba unisamehe Isabella"
Nikasema huku machozi yakiingiwa na ukungu WA machozi. Hakika nilijihisi simanzi kuu.

" Taikon, nimekudhulumu maisha ya ujana wako, najuta kubeba uhusika mbaya katika maisha yangu kwako, nimekutenda mambo ya kikatili. Nahisi sistahili msamaha wako. Hukuwahi kunikosea Mpenzi, ulikuwa na Mapenzi ya dhati kwangu, umasikini wako ulinifanya nikuone hufai. Lakini nimepata nini sasa hivi. Nauliza kipi nilichokipata, pesa zimenisaidia wapi hivi leo, majumba yamenisaidia nini Mimi. Tazama sasa Nina miguu lakini natembelea wheelchair, hivi nilihangika kutafuta yote Kwa ajili ya nini"

" Inatosha Isabella, usiseme yote hayo,huna sababu ya kujihukumu, wewe ni mwanamke Bora kwangu hata Kama ulifanya mabaya. Nimekusamehe nami naomba unisamehe. Tuusubiri mwisho wetu unaobisha hodi mbele yetu.."

Nikasema lakini kabla sijamaliza mlango wa sebuleni ukafunguliwa, akaingia kijana wa miaka ishirini na Saba, kisha akafuatiwa na binti wa miaka ishirini na mbili, ambaye alikuwa kashikana mikono na mvulana WA miaka kumi hivi. Niliwatazama na kabla mlango wa sebule haujajifunga nikiwa nadhani wamemalizika, USO wangu ukashtuka kumuona Yule mtu aliyeniharibia maisha, alikuwa na kovu usoni, nilikumbuka kuwa Mimi ndiye nilimuweka kovu lile Kwa kumpiga na chupa ya wine nyekundu.

Naye alishtuka kuniona.

Nikamgeukia Tabasamu,
" Tabasamu!" Nikamuita, Tabasamu akanigeukia.
,* Mtu Yule wa nne kwenye Ile picha ndio huyu hapa" nikasema nikiwa namtazama Tabasamu kisha nikamnyooshea Yule mtu kidole.

" Whaaat!!! Wewe ndiye umemfanyia Baba yangu mambo haya!" Tabasamu akasema Kwa kufoka na kustaaajabu kisha akakimbia chumbani wote tukistaajabu. Kabla hatujapumua Tabasamu akarudi akiwa kabeba bastola,

" No! No! Hapana, usifanye hivyo Tabasamu." Nikainuka upesi na kusimama mbele ya mtu Yule ambaye jina lake utalifahamu punde tuu.

" Baba Acha nimuue, hawezi kunitesea Baba yangu kiasi hiki. Miaka yote niliamini yeye ndiye Baba yangu, lakini kumbe walikuwa wakinidanganya, kumbe ni watu washenzi, wadhalimu, makatili Kama wanyama Pori. Acha niwaue"
Tabasamu akasema.

" Usifanye hivyo..." Nikasema lakini nikakatishwa.
" Please sister don't do that" Binti wa miaka ishirini na mbili akawa anamsihi dada yake.

" Mwanangu, sikukataa kukulea, umasikini wangu ndio ulimfanya Mama Yako anikimbie. Sikukukimbia. Wasamehe wote Kwa maana msamaha ndio macho ya maisha. Maisha pasipo msamaha ni Sawa na safari ya vipofu"

Nikahitimisha,

Ulikuwa nami taikon wa Fasihi, Yule Mtibeli kutoka Nyota ya Tibeli.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
The best story na ina mafundisho makubwa sana ndani yake ukiangalia kwa umakini
Taikon hamlaumu Isabella kwa yote aliyomtendea bali Anaulaumu umasikini adui mkubwa adui namba moja wa Taikon ni umasikini
Hii ina maanisha ukiwa na kila kitu lakini ukawa masikini ww ni bure, Mwanadamu hakamiliki kuwa bora kama hana pesa

Umasikini ni laana nitapambana kuupinga maisha yangu yote
 
The best story na ina mafundisho makubwa sana ndani yake ukiangalia kwa umakini
Taikon hamlaumu Isabella kwa yote aliyomtendea bali Anaulaumu umasikini adui mkubwa adui namba moja wa Taikon ni umasikini
Hii ina maanisha ukiwa na kila kitu lakini ukawa masikini ww ni bure, Mwanadamu hakamiliki kuwa bora kama hana pesa

Umasikini ni laana nitapambana kuupinga maisha yangu yote


Umesema kweli Kabisa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom