Jidu La Mabambasi
JF-Expert Member
- Oct 20, 2014
- 16,114
- 26,006
Kati ya sheria za kuchekesha na kuudhi kwa pamoja kwa mlipa kodi, ni hii sheria iliyopitishwa na Bunge wiki hii.
Ati nao WENZA wa viongozi wakuu , nao wapewe mafungu ya pesa zilizokusanywa kama kodi kutoka kwa walalahoi.
Sasa mwenza naye ameshakuwa kiongozi, ambaye hakuchaguliwa na wananchi, lakini mume/mke analipwa mafao ya juu akiwa anatumikia nchi, na analipwa 80% ya mafao yake akimaliza muda wake kiofisi.
Sasa hao wenza inaelekea tamaa imewazidi , wameshajiweka kuwa wanastahili maisha yao yote KUTUNZWA na kodi za walala hoi.
Ati watoto walizoea kupelekwa shule na ma V8, waendelee kuishi hivyo, kwa gharama ya walipa kodi.
Mama Salma Kikwete, mbunge, ndiye alionyesha tamaa hiyo hadharani.
Hilo ni licha ya kwamba mh. Kikwete ana mafao ya urais, na mama Kikwete ana mafao ya ustaafu wa ubunge na mtoto wao Ridhiwani naye mbunge, atakuwa na mafao ya ubunge.
Hii hali kiurahisi sijui utaielezaje.
Ni wizi wa kuaminiwa?
Ni tamaa iliyopitiliza kwa resources za nchi?
Ni kwa kuwaona wananchi kuwa wajinga?
Mwalimu Nyerere pamoja na urais wake, alipong'atuka urais, alirudi Butiama kulima maharage.
Yule mzee alikuwa mtu wa kiasi.
Jakaya Kikwete kwa kweli amelichafua jina lake kwa hili.
Tusipoliondoa hili tutajenga tabaka la watu wanaofyonza hazina kwa kutolifanyia chochote taifa hili.
Na huo utakuwa Usultani.
NYONGEZA NA UPDATE
(Aasemavyo mwandishi maarufu )
TUNAFUTA BIMA KWA MTOTO TUNAENDA KUMLIPA MAFAO MWENZA WA KIONGOZI.
Na Thadei Ole Mushi
1. Hili la kulipa mafao wenza wa Viongozi linatafakarisha. Cha muhimu sana wasiwasahau wenza wa wanajeshi wetu ambao hulala mipikani kulilinda taifa, madaktari na wauguzi wanaolala mahospitalini kuokoa roho za watanzania, wasisahau na walimu wanaowafundisha na kuondoa ujinga kwa watanzania kwenye mazingira magumu kabisa. Wakiwasahau tuwaombee hayo makundi yasije kuwa na wivu na Sheria hiyo.
2. Kama wakiyakumbuka makundi hayo niliyoyataja hapo juu, keki yote ya Taifa itageuka kulipa mafao ya wenza. Kupanga ni kuchagua…..
3. Mimi kama Mwana-CCM natamani sana chama changu kiendelee kushika hatamu, lakini kwa mbali naona umuhimu wa vyama vya upinzani kuwepo bungeni sheria kama hizi zingepata ukosoaji wenye tija na hatimaye ingeundwa sheria nzuri kabisa ambayo isingewakera watanzania. Hili bunge na chama kimoja linapitisha kila kitu hata kesho wakiletewa mswada wa watanzania kula kinyesi chao watapisha… hawana muda wa kuhoji sana.
4. Miswada kama hii inayochochea chuki kwa wananchi kimahesabu haitakiwi kupishwa au hata kujadiliwa mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi. Tumewapa Wapinzani agenda, hata kama ni kucheza hii rafu ingetakiwa ichezwe mara baada ya uchaguzi mkuu 2025 jambo hili lipo karibu sana na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu….. Chama chetu tunakipitisha kwenye misukosuko wenyewe ngoja tuone.
5.Hizi ndio akili zetu, tunaondoa bima kwa watoto tunaenda kuwalipa mafao wake na waume wa viongozi….. Mungu turejeshee akili zetu.
5. Hili kundi la wenza wa viongozi kabla ya mswada huu walikuwa wanapewa kila kitu hata baada ya kustaafu Kama ulinzi,nyumba, na wanaedelea kutunzwa na serikali kwa kila kitu lakini still hawariziki na sasa wamejitungia sheria ya kuendelea kunufaika zaidi na keki ya Taifa. Kwa taifa ambalo vijana wake wanazurura kwenye jua na mvua kutafuta ajira haya ni matusi kwao.
6. Nafikiri Busara ni kuwa Mafao yabaki kuwa ya mtumishi aliyeyachangia tu. Mtu ambaye hajayanchangia asinufaike nayo, hivi katika mazingira yaliyopo nani anayenufaika na keki ya taifa hili kati ya mwenza wa kigogo na mwenza wa mtumishi wa umma kama mwalimu, askari, mwanajeshi, madaktari na kadhalika?
7. Nchi maskini kama hii ambayo bado huduma za jamii hatujamaliza kumpatia kila mtu si sawa kuongeza matumizi ya fedha za Umma kwenye matumizi yasiyo ya Msingi. Kuna watu wanashare maji na mifugo, kuna maeneo watu wanatafuna mizizi badala ya kumeza dawa kutokana na gharama za matibabu hazishikiki…. Haya ni matusi kwao.
8. Wana CCM waliopo nje ya mhilimili wa Bunge tumuombe Rais Samia asisaini huu mswada kuwa Sheria kwanza kuna manufaa makubwa sana kisiasa kutokuusaini kwa sasa.
9. Ukiachana na mishahara mikubwa na minono ambayo viongozi hawa tunaojadili mafao ya wenza wao pia hulipwa mafao manono pindi wanapomaliza utumishi wao na pia huendelea kulipwa mishahara asilimia 80 ya mishahara ya viongozi wenye vyeo kama vyao waliopo madarakani. Yaani huyo kigogo akistaafa bado anaendelea kukamua asilimia 80 ya uliokuwa mshahara wake akiwa nyumbani huyu tunamjadili tena mwenza wake kumlipa mafao kwa kazi gani aliyofanya? Hivi mnawaona watumishi wa umma waliostaafu nusu yao akili zinawaruka kutokana na frustration za kikokotoo na maisha magumu?
10. Jambo hili linaondoa kabisa uzalendo huku chini kwa watumishi wa Umma. Yaani kila atakayepata mrija wa kunyonya akilimnuka huu mswada hataacha kunyonya na kufanya ubadirifu wa mali za umma. Uzalendo hujengwa na mambo mengi hili linawaondolea watanzania wengi uzalendo wao. Nendeni mkaangalie salary slip za watumishi wa Umma wengi wanapokea kiwango cha mwisho cha mishahara yao kutokana na mikopo wakisikia haya wanajisikiaje?
Kila mwanaccm mwenye akili ahoji jambo hili…. Kuwa mwanaccm sio kukubali kila kitu.
Mithali 16: 18-20 inasema “Kiburi hutangulia kabla ya anguko”.
Ole Mushi
0712702602