Shairi: Swali juu ya mabadiliko ya wajawazito

MakaDik

JF-Expert Member
May 31, 2019
238
135
SWALI JUU YA MABADILIKO YA WAJAWAZITO

1. Leo nakuja na swali, msione la kitoto
Linahusika na mwili, wamama wajawazito
Ni swali gumu ukweli, linaleta tumbo Joto
Hivi nini kinajili, kipindi cha huu wito

2. Hivi nini kinajili, kipindi cha huu wito
Mabadiliko ya hali, awapo ndani mtoto
Usipokuwa mahili, hugeuka changamoto
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

3. Leo switi usioge, namisi harufu yako
Mara sitaki Pelege, Nitafutie Choroko
Sitaki kupanda ndege, leta bodaboda yako
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

4.Shati hilo ni kituko, vaa burauzi yangu
Baki na kitanda chako, nalala kwenye uvungu
Nenda kwa hawala yako, usinitie machungu
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

5.wengine wanadiliki, kusema nilikosea
Wanaweza toka nduki, badae wakajutia
Leo hii huondoki, zamu yako ya kufua
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

6. Nipe mboga chukuchuku, sitaki mimi mafuta
Tutembee pekupeku, ukivaa nitadata
Sitaki ugali kuku, Nipe ndizi na mbatata
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

7. Nataka uvae jinsi, sitaki hizo zingine
Navaa nikimmisi, shati lake mi nipone
Kwa wakwezo vaa pensi, Ili ukaonekane
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

8. Udogo wa shamba lenu, Ule kula ni mtamu
Nimeshapata fununu, wa hapa hauna hamu
Wamama wapewe tunu, wanapitia magumu
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

9.Balojia sikusoma, muwezao nipe jibu
Swali limeleta homa, ninataka mnitibu
Tukiona tunakwama, tuwatafute mababu
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

10. Najua kwa Mungu wetu, huko hakukosi jibu
Yeye ndiye kila kitu, sisi bora tuwe bubu
Tunaweza kuwa fyatu, swali likitusurubu
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

11. Niwape pole wamama, hali inapowakumba
Ni kipindi cha lawama, penginepo twawachamba
Twaombea uzima, tusiwafanye mitumba
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

12. Ninawaomba wababa, tubebe uvumilivu
Hata wanapotukaba, jua mbele kuna mbivu
Tujifanyeni mazoba, Ili kuzikwepa mbovu
Hivi nini kinajili kipindi cha huu wito

13. Penginepo nimekwaza, watu wengi hapa ndani
Jamani sijawabeza, nianueni juani
Ni wengi lawatatiza, swali hili nafusini
Bila Mungu ndani yetu, uvumilivu ni ziro
 
Back
Top Bottom