Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,828
- 13,585
Serikali imesaini mikataba mitano itakayowezesha kuanza ujenzi wa madaraja 13 katika sehemu za barabara zilizoathiriwa na Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya katika Mkoa wa Lindi ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 140 zitatumika katika utekelezaji huo.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba hiyo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi leo Oktoba 07, 2024, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua ukubwa wa athari ya miundombinu ya madaraja na makalvati katika Mkoa wa Lindi na kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kurudisha upya miundombinu hiyo.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais katika Mkoa wa Lindi ni kujenga upya madaraja yaliyoathiriwa katika maeneo yote ili mvua zitakapoanza kunyesha wananchi watakuwa salama na mawasiliano ya barabara yanakuwa ya uhakika”, amesema Bashungwa.
Amesema ujenzi wa madaraja hayo utatekelezwa katika barabara kuu ya Malendego – Nangurukuru – Lindi – Mingoyo na barabara za Mkoa za Nangurukuru – Liwale, Kiranjeranje – Namichiga, Liwale – Nachingwea na barabara ya Tingi – Chumo – Kipatimu.
Bashungwa amemshukuru Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kwa kutoa msukumo wa kuharakisha upatikanaji wa Wakandarasi watakaotekeleza ujenzi wa madaraja na makalvati na amewapongeza Wananchi kwa subira waliyoonesha kipindi ambacho Serikali ilikuwa inatafuta suluhu ya kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya katika Mkoa wa Lindi.
Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa kazi za ujenzi wa madaraja 13 yatatekelezwa kwa muda wa Miezi 10 kwa kufuata taratibu zote za kitaalam na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka kwa Wakala huo.
Pia soma
~ Daraja la Mbwemkuru-Lindi linamaliza malori na watu, Serikali fanyeni jambo
~ TANROADS yaweka kambi kurejesha mawasiliano barabara ya Tingi-Kipatimo mkoani Lindi
~ Hidaya akata mawasiliano, daraja lasombwa Somanga