Msafara wa Naibu Waziri Nishati na Madini, Dk.Medard Kalemani ukikagua ujenzi wa kituo kipya cha mjini Singida cha kutawanya umeme kilovoti 400 wa gridi kutoka nchini Kenya na Tanzania. Kituo hicho kitasambaza umeme kutoka Singida kwenda mkoa wa Iringa na Shinyanga.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk.Medard Kalemani (wa kwanza kushoto mwenye miwani) akizungumza na maafisa kutoka ofisi na madini kanda ya kati mkoa wa Singida na wa wilaya ya Manyoni, kwenye ofisi ya Mkuu wa wa wilaya hiyo ya Manyoni Fatma Touefiq.Wa pili kushoto ni Afisa Madini kutoka osifi ya madini kanda ya kati ambaye jina lake halikufahamika mara moja, Kamishina msaidizi wa madini kanda ya kati, Sosthenes Massola na Meneja wa kampuni ya Spencon inayosambaza umeme (REA) vijiji vya mkoa wa Singida, Machil Rao.
Serikali imeiagiza Kampuni ya Spencon ya jijini Nairobi, Kenya, kumaliza kazi ya usambazaji umeme katika vijiji 73 vya mkoa wa Singida ambavyo bado havijapata umeme wa (REA) kabla ya Mei mwaka huu.
Endapo kampuni hiyo itashindwa kumaliza kazi katika kipindi hicho itanyang’anywa vifaa vyake, ili kufidia hasara itayotokana na kuchelewa kumaliza kazi kwa mujibu wa matakwa ya mkataba.
Hayo yalisemwa juzi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani,muda mfupi baada ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme kupitia mradi wa REA 11 katika kijiji cha Heka wilayani Manyoni mkoa wa Singida.
Alisema kwa mujibu wa mkataba wa serikali na kampuni Spencon, kazi ya usambazaji wa umeme iliyoanza Oktoba 2013 katika vijiji 90 vya mkoa wa Singida, ilitarajiwa kuwa imemalizika Novemba mwaka jana lakini hadi sasa ni vijiji 17 pekee ndio vilivyopata umeme huo.
“Serikali imelipa kampuni ya Spencon malipo yake yote, kwa sasa haina sababu ya kuendelea kuvumilia wananchi wasipate nishati hii ya umeme kwa maendeleo yao. Nakuagiza meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, simamia kazi hii usiku na mchana ili vijiji vyote vilivyopo kwenye mradi wa REA II, viwe vimepata umeme kabla ya Mei mwaka huu,” alisema.
Aidha Naibu Waziri huyo, ameiagiza Kampuni ya Hainan International Limited ya nchini Korea, inayojenga kituo mbadala mjini cha kusambaza umeme wa Kilovoti 400, kumaliza kazi hiyo ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.
Dkt. Kalemani alisema kazi hiyo ya kuunganisha umeme wa gridi kutoka nchini Kenya na wa nchini na kisha umeme huo kusambazwa hadi mikoa ya Iringa na Shinyanga na hatua hiyo itasaidia kurahisisha utekelezaji wa ahadi ya serikali ya awamu ya tano ambayo iliahidi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo, aliwataka wachimbani wa madini mbalimbali wadogo, wajiunge au waanzishe vikundi na kuvisajili kisheria, ili serikali iweze kuwapatia ruzuku kuboresha shughuli zao.
“Serikali ya awamu ya tano, inatambua na inathamini shughuli zinazofanywa na wachimbaji madini wadogo, wakati na wale wakubwa, sababu kuu ikiwa ni kwamba sekta hiyo ina fursa nyingi za ajira na pia inapatia mapato(mrahaba) kwa maendeleo ya nchi,” alisema Naibu Waziri..
Alisema kwa hali hiyo,serikali kuu itaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kwa wachimbaji na kutoa ruzuku kwa vikundi vitakavyokidhi vigezo.
Dkt. Kalemani pia amewakumbusha wachimbaji hao, kutunza mazingira katika maeneo wanayochimba madini kwa kupanda miti na kufukia mashimo baada ya kumaliza kuchimba madini.
Aidha Naibu Waziri aliahidi viwanda vidogo vya kutengeneza chaki mkoani Singida kuwa Wizara ya Nishati na Madini itashirikiana na Wizara ya Elimu na Ufundi kuwasaidia kutafuta soko la biashara zao ili waweze kunufaika na kazi wanayoifanya.