Sera ya Elimu ya Tanzania inahitaji mabadiliko

Voice of wise

Member
Jul 2, 2023
18
19
Ili Taifa liwe na maendeleo ni sharti liwe na watu wenye elimu sahihi. Watu wakiwa na elimu sahihi, Taifa litapata viongozi bora, watumishi wa serikali wenye weledi na uaminifu mkubwa, wataalamu bora, wanateknolojia sahihi, wanasheria mahili, mafundi bora, wahandisi, madaktari bingwa, askari polisi wenye weledi, wabunifu/wagunduzi, watafiti, watunga sera wazuri n.k.

Katika ELIMU iliyo bora pia utapata wananchi wenye uzalendo halisi na siyo wa mdomoni tu wakati ukipewa rushwa uko radhi nchi ipate hasara. Utapata wanasiasa halisi badala ya wanafiki wenye kulindana wenye kupangiana marupurupu makubwa yasiyoendana na hali halisi ya maisha ya watanzania wenzao. Kama hiyo haitoshi waliotayari kupokea rushwa kubwa kubwa bila kuangalia maslahi ya nchi. Na mengine mengi.

Sera na mfumo wa elimu wa sasa ni wazi kuwa unazalisha watu wenye kukariri kwa sababu haumwongozi mhitimu kwenye maadili ya kazi na nini anapaswa kufanya ili kutoa tija kwa kutumia maarifa aliyoyapata na kuchanganya na kipaji chake alichozaliwa nacho. Aidha mfumo wetu wa elimu hauendelezi vipaji vya kuzaliwa vya vijana wetu. Kwa kifupi mfumo wa elimu unatakiwa marekebisho makubwa.

Nafahamu kuwa sasa hivi serikali yetu inakamilisha mchakato wa maboresho ya sera ya elimu, mfumo na mitaala. Lakini naamini bado nafasi ya kuchangia maoni ipo. Kwa hiyo tunaweza kuendelea kuchangia.

Maoni yangu ni kwamba mfumo wetu utoe nafasi ya watoto katika ngazi ya elimu msingi kujitambua vipaji vyao wenyewe. Na kuanzishwe michepuo kuanzia darasa la 4 ambayo watoto wenye vipaji vya kundi fulani watajikita zaidi kwenye eneo lao la kipaji, wakiboreshwa vipaji vyao kuendana na soko la biashara na ajira.

Na kuelekezwa jinsi wanavyoweza kujiajiri au kuajiriwa kwa kutumia vipaji vyao vya kuzaliwa navyo. Michepuo hiyo inaweza kuwekwa kwenye makundi ya ufundi ambao nao utawekwa kwenye aina zake (useremala, ushonaji, vipuri, makenika, uwashi, radio, umeme, computer n.k.), sanaa na aina zake (uchoraji, mziki, uchongaji vinyago, ususi, soka, n.k.), michepuo mingine ni pamoja na biashara, kilimo, ualimu, dini n.k.

Mafunzo ya kwenye michepuo yatolewe kwa vitendo zaidi kuliko nadharia. Pamoja na masomo ya vipaji vyao kunakuwa na masomo ya general kama vile sayansi, uzalendo, historia, lugha za kibiashara (kiswahili English, French, Chinese, German, Espanol n.k.). Kwa upande wa lugha za lazima ni kiswahili na English, nyingine ziwe optional. Mfumo huu uendelezwe vivyo hivyo hadi chuo kikuu.

Najua utekelezaji wake unahitaji uwekezaji mkubwa kwa shule ya msingi kuwa na vitendea kazi kwa mafunzo ya vitendo vya aina zote za michepuo. Ufumbuzi wake ni kuzigawanya shule ili kila moja ijikite na mchepuo mmoja au miwili. Watoto wanapomaliza darasa la 3 watakuwa tayari wameshatambuliwa vipaji vyao, kwa hiyo kila mmoja atahamishiwa kwenye shule yenye mchepuo unaomhusu ili akaendeleze kipaji chake. Walimu husika nao wapewe elimu maalum ndani na nje ya nchi.

Mimi naamini kwamba kwa utaratibu huu kila mtoto atakayehitimu darasa la 10 (Form 4, kwa mfumo mpya), ataweza ama kuajirika ama kujiajiri mwenyewe.

Kwa upande wa vyuo vikuu. Wapunguze sana nadharia waongeze vitendo zaidi. Ili kumwandaa mhitimu kuwa kiongozi anapaswa ajifunze mambo halisi atakayokutana nayo kazini. Lakini pia afundishwe miiko mikuu na ale kiapo serious ambacho akikikiuka apate adhabu kali sana ikiwemo kifungo (liende sambamba na kutungiwa sheria kali).

Baadhi ya maadili ni pamoja na kukataa rushwa. Afundishwe madhara makubwa (the bigger picture) ya rushwa kwenye maendeleo ya Taifa. Mambo ya utawala bora ya human resources na impact zake kwenye tija. Kujali utu na haki za binadamu n.k.

Katika ajira za watumishi wa umma nako kuwe na mchakato wa haki kwenye kuajiri. Kuwe na mwiko kabisa wa umangi meza ambao mwl JKN aliupiga sana vita bila mafanikio. Hadi sasa ajira za watumishi wa serikali zimejaa undugu, rushwa na "technical know who". Vijana wazuri wenye kujali kazi hawapati ajira kwa gharama ya wazembe, waroho, na wapenda fedha wasiokuwa na passion ya kazi.

Kukiwa na seriousness kwenye ajira na hata kwenye teuzi za watumishi na wale wa kisiasa, nina uhakika kilio cha kukosekana watanzania wenye uadilifu kazini kitakufa kifo cha asili. Hatutategemea eti mpaka waje wawekezaji wa nje ndio tuendeleza raslimali zetu nyeti kama bandari zetu. Ambao wanatuchezea na lugha za kutufunga kwenye mikataba isiyo maslahi kwa Taifa letu. Matokeo yake inapotokea dispute tunapigwa faini kubwa kubwa kwa sababu tunakuwa na wawakilishi weak.

Makampuni makini kama Microsoft yanaendelea kwa sababu yako makini sana katika ajira zao. Hakuna cha upendeleo wala mtoto wake na rushwa kwenye ajira zao. Ni quality na uadilifu ndio vipau mbele vya kumpa mtu ajira. Mpaka upate ajira kwao lazima ufaulu mitihani ya ngazi zisizopungua 5. Nyingine wanakuangalia jinsi unavyo behave kwenye makundi mbalimbali huku wakiku monitor bila wewe kujua. Hawakurupuki tu wala hawapokei vi memo, wala hawaangalii cheti cha mtu eti amefaulu with honours. Ni ubora wako wewe kama wewe ndio unaopimwa nao. Pamoja na ufaulu mzuri, je kichwani kuna wanachokitaka?

Je, ni mwadilifu na mwaminifu kiasi Gani? Je unaweza kujieleza kwa ufasaha? Je, unataalumu wanayoihitaji bila shaka yoyote? Maana mtu anaweza kuwa alifaulu sana kwa ubora Wake wakukariri au kwa kupendelewa ama kwa kununua mitihani.

Serikali yetu mara nyingi wanakagua tu vyeti, na kufanya usaili wa kutimiza wajibu. Walimu ndiyo kabisa hawasailiwi vinachambuliwa vyeti kwa baadhi plus wenye ujanja ujanja wao ndiyo wanaajiriwa. hata vyuo vikuu nao wanaangalia vyeti zaidi bila ufahamu wa mtu. Nasikia siku hizi wamekubali/wamelazimishwa kubadilika. Matokeo yake baadhi ya maprofesa wanaozalishwa wanapoaminiwa na serikali wanaiangusha mazima.

Hii ni kwa sababu wamepata ajira kwa kuangalia ufaulu tu wa mitihani badala ya uhalisia wa mtu. Na tunajua kuwa baadhi ya watu hupata ufaulu kwa michongo na kuendelea hadi kuwa maprofesa kwa sababu mfumo unawalazimu. Ni shida tupu.

Wasilisho langu hili ni maoni yangu binafsi ambayo yametokana na uzoefu wangu wa kupita kwenye mifumo yetu ya elimu ya msingi hadi chuo kikuu. Baada ya kuhitimu darasa la 7 na kutofanikiwa kuchaguliwa kwenda kidato cha 1 (pamoja na kwamba nilikuwa ninakiwasha sana darasani), nilitamani sana niende chuo cha ufundi nikasomee kipaji changu cha uchoraji. Lakini nilipuuzwa na walezi wangu, kwa hiyo sikufanikiwa. Badala yake nikatafutiwa shule ya kurudia darasa la 7 ndipo nikafaulu kwenda sekondari.

Aidha, nilitamani nisome sekondari yenye kufundisha uchoraji (mfano Azania) lakini haikuwa hivyo. Hapo ndiyo ikawa mwisho wa kuendeleza kipaji changu cha uchoraji kitaaluma, ingawa cha asili bado ninacho.

Nilipokuwa najiandaa kwenda chuo kikuu pekee kwa wakati huo UDSM (maana badae kidogo kitivo cha kilimo morogoro ndiyo kilirasmishwa kuwa chuo kikuu cha pili) nilifurahi kwamba nakwenda kusomea kazi ya uhandisi nikitegemea ku-specialize mambo ya uhandisi per see. Kama ni civil basi nitajifunza ujenzi mwanzo mwisho. Naingia mwaka wa kwanza nakutana na masomo general duh. Kukariri pale pale kumbe!

Mwaka wa pili nikaangukia idara ya uhandisi kilimo mambo kwa mbaali yanaonekana lakini bado nasomea mitihani zaidi kuliko taaluma ya kueleweka. Mara nasoma masomo ya civil, mara ya mechanical, mara ya survey, sijielewi niko vipi. Kwa kweli hadi nahitimu taaluma ya chuo kikuu kule sokoine nilikuwa sijielewi kabisa nikiajiriwa nitakwenda kufanya majukumu Gani.

Basically nilikuwa najua tu masomo meengi niliyosoma lakini siyo kazi gani naenda kuifanya, sijui ndo ukilaza (lakini hapana ni mfumo haukuniandaa vyema). Hata kujiajiri tu nilikuwa nahitaji niongozwe. Na kweli nilipoajiriwa serikalini nilifanya majukumu yasiyo na uhusiano dhahiri na mambo niliyosomea chuo kikuu. Ni mwendo wa kujiongeza tu.

Hii ndiyo hali halisi kwa nionavyo mimi. Nawakaribisha na wengine mtoe maduku duku yenu kwa ushauri mzuri kwa serikali yetu katika kuboresha zaidi sera yake ya elimu. Najua baadhi ya taaluma, kama udaktari na nyingine, mifumo yao iko vyema maana wana hadi internship ya mwaka mzima. Tafadhalini leteni uzoefu wenu na maoni yenu ya nini kifanyike. Naamini wahusika wataona na kuchukulia serious maoni yetu.

Nawasilisha.
 
Back
Top Bottom