Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 2,201
- 5,585
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela Deus Sangu ametoa wito kwa wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa wa Chama Cha Mapinduzi.
Sangu ametoa kauli hiyo Novemba 22, 2024 kwa nyakati tofauti wakati akifanya mikutano ya kimkakati ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hasan ya kuwachagua viongozi katika Kata ya Mfinga, Kalumbaleza, Mwadui na Muze zilizopo katika Jimbo la Kwela, Mkoani Rukwa.
Amesema CCM ina kila sababu ya kushinda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa jinsi ilivyojipambanua kushughulikia kero zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
Amesema wananchi wa jimbo hilo wana kila sababu ya kuwapigia kura viongozi wa Serikali za Mitaa waliogombea kupitia chama hicho ikiwa ni ishara ya shukrani kutokana na bilioni za fedha ambazo Rais Samia Suluhu Hassan anazitoa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo.
" Tumejiandaa vilivyo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha tunashinda kwa kishindo", amesisitiza Sangu.
Amesema katika kipindi chake cha uongozi, Mkoa wa Rukwa hususan Jimbo la Kwela limefunguka ambapo kila kona barabara zimeboreshwa huku zingine zikiendelea kuwekwa lami ili ziweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka.
Amesema huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, umeme pamoja maji zimeimarika ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Diwani wa Muze, Kalolo Ntalli amesema kwa jinsi walivyojipanga na kutokana na ubora wa wagombea waliopitishwa na chama hicho, hakika ushindi ifikapo tarehe 27 Novemba mwaka huu hauepukiki.