MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema serikali haina nia ya kumwonea mtu, inapochukua hatua ya kutumbua majipu kwa watumishi wa umma.
Samia aliyasema hayo juzi baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Morogoro, iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk Steven Kebwe akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.
Alisema lengo la kutumbua majipu ni kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji serikalini, kama ilivyoangizwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili Watanzania wote wafaidike na matunda ya nchi yao.
“Mtasikia katika serikali tunarekebisha, majipu yanatumbuliwa... kwa kweli hatuna nia ya kumwonea mtu, tunarekebisha kama ilivyoagizwa katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ili Watanzania wote wafaidi matunda ya nchi yao,” alisema Samia.
Alisema katika marekebisho hayo, serikali imechukua hatua ya kukata mishahara ya walio juu na kunyanyua ya walio chini waje juu kidogo na kwamba jitihada zote hizo ni katika kufanya mambo yaende vizuri nchini.
“Tunapozungumzia amani na utulivu ni pamoja na kuhakikisha kwamba walio chini wapo vizuri, wasipokuwa vizuri hakuna amani na utulivu, kazi itawapata watu wa kamati ya ulinzi na usalama, kuwatuliza kila siku na hawatatulizika kwa sababu wana shida,” alisema Makamu wa Rais na kuongeza: “Lakini tukiwatuliza kwenye mambo yao wana maji, wana umeme, wana chakula, mtoto anaenda shule vizuri, anapata afya, akienda zahanati dawa zipo, watatulia tu.”
Alisema kwa hivi sasa kuna tatizo la watumishi hewa na wengine wamediriki kumdanganya mkuu wao wa kazi na hayo ndiyo mambo ambayo hayaleti picha nzuri katika serikali.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuunga mkono jitihada hizo za serikali ili kurejesha nidhamu na uwajibaikaji kwa watumishi wote. Wakati huo huo, Makamu wa Rais ametembelea kiwanda cha kutengeneza nguo cha Mazava, ambapo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuzingatia masharti ya ajira na wafanyakazi kuchapa kazi kwa bidii ili Taifa lipate kodi na wao wapate mapato.
Akizungumza na wafanyakazi, Samia aliuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa serikali itazifanyia kazi changamoto za eneo na ukosefu wa ujuzi kwa kuwapeleka vijana wengi kwenye vyuo vya elimu ya ufundi stadi (VETA) kujifunza ushonaji.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo kwenye viwanda na kusisitiza kwamba kupitia mpango wa EPZ, viwanda vingine vinatarajiwa kujengwa mkoani humo, jambo ambalo litaongeza ajira kwa vijana.
Kiwanda hicho ambacho kilianza uzalishaji mwaka 2010 kina wafanyakazi zaidi ya 2,000 na kwamba asilimia 100 ya nguo zinazozalishwa kiwandani hapo, zinauzwa nje ya nchi, ambapo soko kuu liko Marekani.