Sababu za kusameheana

John Magongwe

Member
Jan 4, 2024
54
68
Sababu za kusameheana

Msamaha ni Nini

Biblia inaposema achilieni nanyi mtaachiliwa (Luka 6:37) ina maana gani


Neno msamaha, halina tofauti sana na neno ‘kuachilia’ au ‘kufungulia’. Unapomsamehe mtu aliyekukosea ni sawa na umemwachilia huru katika moyo wako. Huna deni naye tena, anakuwa ametoka katika kifungo cha moyo wako.

Na kila mwanadamu anapaswa awe na huo uwezo wa kusamehe. Msamaha ni ufunguo wa kitu kikubwa sana katika maisha.

Ingawa kwa akili za kawaida za kibinadamu ni ngumu kusamehe. Lakini ukiwa Mkristo (uliyeoshwa kwa damu ya Yesu Kristo na kufanyika kuwa kiumbe kipya), ni rahisi kusamehe.

Na msamaha ule unaohusisha vitu ambavyo ni vigumu kusamehe huwa ndio una maana kubwa sana na faida kubwa zaidi kuliko ule wa vitu vidogo.

Nguvu ya msamaha upo katika mistari ipi

Nguvu ya msamaha upo katika mistari kadhaa, ikiwa ni pamoja na ifuatayo:

Luka 6:36 ‘Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

37 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa’.

Hapo anasema ‘achilieni’. Faida za kuachilia ni nini? Mbele kidogo mstari unasema ‘nanyi mtaachiliwa’. Ikiwa na maana kuwa unapomsamehe mtu na wewe umeweka deni mahali fulani la kusamehewa…wa kipimo kile kile na uzito ule ule uliomsamehe mtu…na wewe unalo deni la kusamehewa kwa kiwango hicho hicho mahali fulani, wakati fulani.

Wakolosai 3:13, pia inasema wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa.

Wengi wetu hatujui au hatuna taarifa kuwa kuna Mungu juu anayeyatazama maisha yetu. Ukishaikosa au kupungukiwa na hiyo imani, basi ni ngumu sana kuyaishi maneno ya Mungu. Siku zote kumbuka Mungu yupo juu anatutazama, kila tendo, kila neno na kila tukio tunalofanya na yeye hasahau, wala hasinzii, wala hapumziki. Kwa hiyo kila kitu tunachokifanya, kiwe kibaya kiwe kizuri anakirekodi na kila kitu kina mshahara wake.

Vingine mishahara yake ni hapa hapa duniani na vingine ni kule katika ulimwengu ujao. Ufunuo 22:12 unasema ‘Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo’.

Kwa hiyo kama ulitukanwa na hujasamehe, na wewe pia hujasamehewa matusi ya siri uliyoyatoa moyoni mwako dhidi ya mwingine. Haijalishi unayakumbuka au huyakumbuki, mbele za Mungu hayajasahaulika hata moja.

Tuangalie na mfano mwingine
Mathayo 18:21 ‘Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?
22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
23 Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. 24 Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.

25 Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. 26 Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. 27 Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.
28 Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata, akamshika koo, akisema nilipe uwiwacho.

29 Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. 30 Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. 31 Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.

32 Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; 33 nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? 34 Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. 35 Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake’.

Nguvu ya msamaha ipo kwenye vile unavyovisamehe wewe mwenyewe

Umeona. Nguvu ya msamaha, ipo kwenye vile unavyovisamehe.

Unapomsamehe mtu vitu 100 basi na wewe unastahili kusamehewa vitu 100.

Kadhalika unaposamehewa vitu 100 na wewe una deni la kusamehe vitu 100.

Hakuna njia ya mkato ya kupokea msamaha. Hakikisha unasamehe kwanza ili na wewe pia usamehewe. Bwana Yesu alisema hivyo katika: Mathayo 6:14 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. 15 Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”.

Sasa unaweza kuuliza, hata mtu akinidhulumu vitu vyangu vyote nimsamehe? Ndiyo. Msamehe. Hiyo ni kwa faida yako binafsi.

Utakuwa umemwachia Mungu wako deni kubwa la yeye kukurehemu wewe sawa sawa na jinsi ulivyomsamehe mwingine. Kumbuka mfano hapo juu.

Kumpeleka mtu polisi au mahakamani ni kutomsamehe?
Yapo mazingira ya mtu kupelekwa polisi au mahakamani…ambapo siyo dhambi.

Kwa mfano, imetokea mwizi amekuibia na umemfahamu, na ulipojaribu kumwendea ukakuta kakificha kile kitu au amekwishakitumia na hataki kukiri kwamba yeye ni mwizi wala kutubu.

Mtu kama huyo moyoni unamsamehe kabisa kwa moyo wote, lakini pia anapaswa ashtakiwe kwa watu wa karibu au polisi ili asiendeleze wizi huo kwako na kwa wengine.

(Kwa kufanya hivyo siyo dhambi) na hautahesabika kama hujamsamehe mbele za Mungu.

Kadhalika kama umedhulumiwa mali yako isivyo halali na kuna nafasi ya kuirudisha, pambana kuirudisha kwa hekima.

Mfuate aliyeichukua mwambie akurudishie akikataa na kuna nafasi ya kumshtaki, mshataki ili aogope akurudishie, ili siku nyingine asirudie kufanya hivyo kwako au kwa wengine.

Lakini akija kwako na kutubu na kukiri kwamba ni kweli amekudhulumu lakini mali ile amekwishaitumia na hana tena, na anatubu mbele zako, hapo huna budi kumsamehe na kumkumbatia. Hupaswi kwenda kumshtaki, kwa sababu amekwishakiri kosa lake.

Unapaswa kumsamehe kabisa. (Ukikumbuka siku zote kwamba nguvu ya msamaha ipo katika kusamehe).

Ukiwasamehe waliokuudhi, Bwana atakusamehe uliyemuudhi. Ukiwasamehe waliokudhulumu, Bwana atakusamehe dhuluma ulizozifanya ndogo ndogo hata kama huzikumbuki.

Ukimsamehe mtu aliyekuudhi siku moja na wewe utamuudhi mwingine, lakini Bwana atampa moyo wa kukusamehe wewe.

Ukimsamehe mtu anayetamani kusamehewa na wewe, siku moja na wewe utasamehewa na mtu ambaye ungetamani akusamehe.


Mithali 16:7 “Njia za mtu zikimpendeza Bwana, hata adui zake huwapatanisha naye”.
 
Back
Top Bottom