ACT Wazalendo
JF-Expert Member
- May 5, 2014
- 620
- 1,543
UCHAMBUZI WA BAJETI YA OFISI YA RAIS- MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA KWA MWAKA WA FEDHA 2024/2025
Utangulizi
Ijumaa tarehe 19 April 2024, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawalabora Ndg. George Simbachawene (Mb) amewasilisha Bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025. ACT Wazalendo kupitia waziri kivuli wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ndg. Riziki Shahari Mngwali tumeisikiliza na kuichambua na haya ni maeneo sita tuliyoyamulika.
1. Kanuni za mafao (Kikokotoo) bado zinaendelea kuwaumiza wazee wetu wastaafu.
Kumekuwepo na malalamiko mengi juu ya watumishi wa umma wanaostaafu kupunjwa mafao yao tangu kuanza kutumika kwa kanuni mpya ya kikotoo cha mafao Julai 01, 2022. Kanuni mpya ya ukokotoaji wa asilimia 33 na kikotoo cha 1/580 badala ya 1/540 kinapunguza malipo ya mkupuo (lumpsum) ya kiinua mgongo cha mtumishi anayestaafu kwa asilimia 50.5 ukilinganisha na kanuni za awali (kabla 2018). Kanuni hizi zilipingwa na wafanyakazi, wanaharakati na wanasiasa ila baadae zikarejeshwa kinyemela.
ACT Wazalendo tunaamini kuwa kanuni hizi mpya za kikokotoo hazisaidii kulinda maisha ya watu na kutoa uhakika wa kuishi vizuri unapokutwa na majanga au kupoteza uwezo wa kufanya kazi kwa namna yoyote ile. Hatupaswi kuwaadhibu wazee wetu kwa kukubali kanuni hizi kandamizi zinazoenda kuwapunja mafao yao na kufupisha muda wa kuwahudimia kwa kuwakadiria kifo mapema zaidi. Aidha, hatukubaliana na uamuzi wa serikali kuwabebesha wastaafu mzigo wa gharama kwa makosa ya utendaji mbovu wa menejimeti za mifuko na madeni ya serikali.
Tumeona waziri ameliambia Bunge kuwa marekebisho ya Sheria ya mafao ya kustaafu katika utumishi wa Kisiasa sura ya 255 yamekamilika, Serikali ya CCM ba wabunge wao, hawaoni haya kurekebisha maslahi ya wanansiasa na kuacha vilio kwa wananchi, hakuna hata sehemu moja ambapo wameanza kusikia kilio cha watumishi wa Umma, na badala yake wafanyakazi wanabaki na matumaini hewa. ACT Wazalendo ili kuhakikisha wafanyakazi wastaafu wananufaika na michago yao baada ya kustaafu.
i. Tunaitaka serikali kurejesha kanuni za zamani za mwaka 2017 (Social security Schemes- Pension benefits harmonization rules), wastaafu walipwe 50.5 kiinua mgongo, kwa kikoktoo 1/540 na kwa miaka 15.
ii. Vyama vya wafanyakazi nchini vishikamane kama ilivyofanya miaka mitatu nyuma kupinga udhalimu huu.
iii. Tunaitaka serikali kulipa madeni yote inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mkupuo mmoja ili kuiwezesha mifuko kujiendesha na kuhudumia wateja wake kwa wakati.
2. Wabadhirifu wa fedha za Umma wanaendelea Kuliumiza Taifa.
Sekta ya Utumishi wa umma ni muhimu sana kwenye mapambano dhidi ya ubadhirifu au kuchunga matumizi mazuri ya fedha za umma. Ingawa, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala bora ina wajibu huo. Bado tumeendelea kuona upotevu wa fedha, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma kwenye Ofisi, Idara na Halmashauri mbalimbali nchini.
Hoja ya ubadhirifu imekuwa ikirudiwa rudiwa kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za kila mwaka. Katika ripoti ya mwaka 2022/23 iliyotoka mwaka huu imeonyesha hali imendelea kuwa mbaya zaidi kuhusu upotevu wa fedha na ubadhirifu wa zaidi ya shilingi Trilioni 6.6.
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliohusika katika ubadhilifu wa fedha za umma.
3. Madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara ya Watumishi wa umma.
Katika uchambuzi tulioufanya mwaka 2022/2023 wa bajeti na ripoti ya CAG tulionyesha kuwepo kwa malimbikizo ya muda mrefu ya mishahara, madeni na stahiki zilizotakiwa kulipwa kwa Watumishi wa Umma kiasi cha Shilingi bilioni 429.80 mwaka 2020/2021 kutoka shilingi bilioni 334.15 mwaka wa fedha 2019/2020, mwaka wa fedha wa 2021/22 iliyotolewa na Waziri Bungeni ni imeonyesha kuwa Serikali imelipa jumla ya madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 119,098 yenye thamani ya shilingi bilioni 204.42. katika mwaka a fedha 2023/24 Bilioni 39 ya watumishi 26,331 na madai ya watumishi waliokoma utumishi kwa sababu mbalimbali Bilioni 7.02 hivyo kufanya madai na malimbikizo ya watumishi kuwa shilingi Bilioni 179.31.
ACT Wazalendo tunarudia wito wetu kwa kuitaka Serikali kumaliza kwa mkupuo madai malimbikizo ya watumishi kupitia mfumo wa hatifungani maalum. Aidha, tunasisitiza Serikali kuyatambua madeni haya katika takwimu za deni la taifa na kuimarisha mfumo wa kulipa madai ya watumishi ambao utahakikisha kuwa madeni mapya hayatoozalishwa tena siku za usoni.
4. Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) zinatumiwa kwa Manufaa ya kisiasa kuinufaisha CCM
Katika mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2024/25 wizara ya utumishi imeendelea na jukumu la kuratibu na kusimamia Miradi ya Maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). ACT Wazalendo katika kuangazia jukumu hili, tumekuwa tukielezea changamoto, hoja na mapendekezo ya namna bora ya kusimamia fedha za TASAF kufuatia na malalamiko mbalimbali tuliyoyapokea kutoka kwa wananchi.
Mosi, Kufanyishwa kazi wazee na watu wenye ulemavu, wazee wamekua wakifanyinshwa kazi za kuchimba mitaro, mabwawa, kufanya usafi kwenye shule au kufyatulishwa matofali badala ya kupatiwa fedha hizo kama ruzuku kutokana na kundi lao.
Pili, fedha hizo sasa hivi zinatolewa kwa ubaguzi au kutumika vibaya na viongozi wa Chama cha Mapinduzi ili kujinufaisha kisiasa kwa kuwatisha watu wenye vigezo vya kunufaika na TASAF kuwa hawatonufaika iwapo hawatajiunga na CCM au kuwaondoa kwenye mfumo ikiwa watakuwa Wapinzani wa CCM.
ACT Wazalendo tunaendelea kumtaka Waziri nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa umma na Utawala bora kufuatilia na kuchukua hatua za kumaliza changamoto hizo Nchi nzima.
Mwisho, tunaona ili kumaliza tatizo hili ni lazima Serikali iimarishe mfumo wa hifadhi ya jamii ili kutoa pensheni kwa wazee wote badala ya kutegemea fedha za Mkopo ambazo zinaweza kusitishwa muda wowote.
5. Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) iondolewe Ikulu na irejeshwe katika Wizara ya Uchukuzi.
Tunaendelea kusistiza kwamba wakala wa ndege za Serikali (TGFA) kuondolewa Ikulu rai hii tumekua tukiirudia mara kwa mara. Miongoni mwa maamuzi mabovu yaliyofanywa na Serikali 2016 ni kulichukua Shirika la ndege la serikali na kuwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kutoka wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wakala kuongezewa jukumu la kuratibu ununuzi wa ndege, kuzikodisha kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kusimamia mikataba ya ukodishwaji wa ndege hizo kwa niaba ya Serikali, mbali na jukumu lake la asili la kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa Kitaifa.
Tulieleza athari za uamuzi huo ambao unaendelea kuthibitishwa na ripoti ya CAG, ambayo imeonyesha ATCL wanaendelea kupata hasara ya Shilingi bilioni 56.64 hasara hii inayopata ATCL kwa sehemu kubwa inatokana na mfumo wa umiliki wa ndege. Mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. Ndege zote zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za walipa kodi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL. Mfumo huu unaoleta hasara kwa taifa unatokana na uamuzi wa mwaka 2016.
Aidha, bado tunaona Wakala wa Ndege za Serikali kuwekwa chini Ofisi ya Rais Ikulu ni uamuzi usiofaa. Kwasababu haukufanywa kwa ajili ya manufaa ya umma badala yake ulilenga kuzuia uwazi na uwajibikajika katika mikataba ya ununuzi wa ndege. Kitendo kilichopelekea kurudisha nyuma jitihada za kudhibiti ubadhirifu na ufisadi katika manunuzi ya ndege ambayo sasa yanadhihirika kwa ndege hizo kuwa mbovu ndani ya muda mfupi tu.
ACT Wazalendo tunarudia wito wetu wa kuitaka Serikali kuirejesha TGFA wizara inayohusika na Uchukuzi ili kudhibiti ubadhirifu na wizi kwa kuimarisha uwazi, tunaitaka Serikali ifanye mapitio ya mikataba yote ya manunuzi ya ndege kwa lengo la kuiboresha kwenye mapungufu. Pili, Serikali imilikishe kwa Kampuni ya Ndege ya Taifa ndege zote inazokodishiwa na ATCL.
6. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanyiwe ukaguzi.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Sheria hii ilitungwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) Sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
TAKUKURU inaingia kwenye kundi la taasisi zilizowekwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kiasi cha kushindwa kumulikwa ufanisi wake kwa kuwianisha na matumizi inayofanya. TAKUKURU inatengewa fedha na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha TAKUKURA inapaswa kukaguliwa kila mwaka lakini tangu mwaka 2007 ilipoanzisha haijawahi kukaguliwa.
Kutokana na uzoefu wa utendaji, historia na tafiti mbalimbali licha ya kuwa ni chombo kilichoanzishwa ili kuimarisha uwajibikaji na kuchunga matumizi mazuri ya rasilimali yapo malalamiko na tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi kwa baadhi ya watumishi, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuweka taarifa za fedha zinazojitegemea za TAKUKURU sio kufichwa kwenye fungu la 20 la bajeti. Pia, tunaitaka Serikali kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuifanya ukaguzi TAKUKURU kama sheria zinavyotaka na taarifa yake iwe wazi kwa umma.
Hitimisho
Mpango wa utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Menejimeti, utumishi wa Umma na utawala bora kwa mwaka 2024/25 unaonyesha kwa kiasi kikubwa mambo ni yale yale. Dhana ya utawala bora inazidi kudorora kufuatiwa na hoja za ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma katika ofisi mbalimbali za Serikali kuu, idara na Halmashauri nchini. Aidha, kuendelea kuruhusu kutumika kwa kanuni mpya ya kikotoo cha mafao kwa watumishi wanaoenda kustaafu kunaporomosha ari na utendaji wa watumishi. Vilevile, suala la matumizi ya fedha za maendeleo ya jamii kutowekewa utaratibu mzuri kutaendelea kuchomwa fedha hizo bila kuleta matokeo tarajiwa.
Imetolewa na;
Ndg. Riziki Shahari Mngwali,
Waziri Kivuli wa Utumishi wa umma, Utawala bora
ACT Wazalendo.
23 April 2024.