Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 29,013
- 69,673
RIWAYA: MLIO WA RISASI HARUSINI
Mtunzi: Robert Heriel
WhatsApp 0693322300
Akajitazama kwenye kioo kikubwa cha kabati akiwa chumbani kwake. Kila alipojitazama hakuona kasoro yoyote katika mwili wake. Aligeuka huku na huku akiendelea kujitazama. Macho yake yalimuambia yeye ni mrembo mwenye mvuto wa viwango vya kimataifa, ni kweli wala macho yake hayakuwa yamemdanganya. Ismaiya alikuwa mwanamke aliyeumbwa akaumbika. naweza kusema alikuwa ni moja ya wanawake wazuri kuwahi kutokea katika dunia. Alikuwa na urefu wa futi sita kasoro. Mwenye umbo matata kama chungu cha kimakonde ambalo lililaza na kulewesha nyoyo za wanaume waliobahatika kumuona. Uso wake wenye macho makubwa kiasi yaliyolegea ulizidisha maradufu uzuri wake. Pua iliyochongoka huku chini yake ikipokelewa na midomo minene kiasi ilizidi kumpa kura muhimu katika urembo wake, hakuna ambaye hakutaka kumuona mwanamke kama Ismaiya akitabasamu kutokana na mpangilio mzuri wa meno yake meupe pee yenye mwanya wa kichokozi. Kichwani alikuwa na nywele fupi zilizokatwa kwa ustadi mkubwa huku masikioni kukiwa na hereni za duara. Kifua chake laini kilibeba maziwa madogo kiasi huku kiuno chake chembamba kikishikilia makalio makubwa yenye nyonga nene zilizotesa nguo aliyokuwa ameivaa. Mapaja yake laini yalimeta meta mithili ya bilauri ya dhahabu. Huyo ndiye Ismaiya binti Ndossi. Mwanamke mwenye uzuri usiyosemeka. Rangi yake ya kahawia alimaarufu kama maji ya kunde.
Pamoja na uzuri wote huo lakini Ismaiya aliuona si chochote wala si lolote. Uzuri ulikuwa na faida gani ikiwa kiberenge tuu kilimshinda. Hakuamini kabisa kwamba rafiki yake Adele angeweza kumnyang'anya mchumba wake. Sasa aliuona uzuri wake siyo kitu tena. Alijilinganisha na Adele ambaye hakumfikia kwa lolote lile. Siyo kwa sura wala kwa umbo. Siyo kwa kimo wala kwa rangi. Alimzidi karibu kila kitu. Sasa iweje Adele amnyamng’anye mchumba wake. Kwa kipi hasa. Kwa lipi hilo lililompiku mpaka Adele ampindue katika penzi lake.
"Kile kinyago cha mpabure kinanizidi kwa lipi. Msichana hana mvuto wa kumvutia mwanaume yeyote. Mtu mwembamba kama mlingoti wa kupandishia bendera. Embu cheki! Tazama mzigo huu. Embu ona " akaongea mwenyewe akijitazama kwenye kioo huku akitingisha makalio yake yaliyoshiba haswa.
‘’Nimetimiza vigezo na masharti ya kuitwa mwanamke mrembo, wapo wanaonifananisha na malaika, wapo wanaoniona malkia wa sheba wa kizazi hiki. Lakini iweje! Iweje Yule ngedere anipiku! Au yule kiberenge kanizidi mambo ya chumbani. Mmmh!’’ akaongea kwa sauti ya upole huku uso wake ukionyesha kukata tamaa baada ya kuwaza jambo hilo. Ni akama alikaribia ukweli.
Basi kama kuna jambo ambalo Adele alibobea ni suala la kummudu mwanaume kitandani. Adele alikuwa fundi msanifu wa masuala ya kitandani. Alijua ni vipi ammiliki mwanaume yeyote yule. Adele alikuwa na kipaji cha kukata mauno katika mkao wowote ule jambo ambalo wanawake wengi linawashinda. Kama hiyo haitoshi Adele alifuzu mafunzo ya kumdumaza mwanaume akili kwa kumpa mahaba na kumdekeza. Wapi alijifunza mambo hayo siyo mimi wala wewe, hakuna aliyekuwa anajua. Mtoto Adele alikuwa kisanga kwenye shuka na godoro. Alikuwa mwepesi kushuka katika mabonde na mito bila kudondoka.
Ismaiya akajibwaga katika kitanda kama mzigo. Alikuwa amechoka. Katika chumba cha Ismaiya kulikuwa na kabati kubwa lenye kioo. Karibu na kitanda kulikuwa na dressing table iliyosheheni vipodozi na mafuta ya kila namna. Chini lilikuwepo zulia la manyoya. Kilikuwa chumba kilichobeba choo na bafu ambacho kilisheheni vitu vilivyomtosha mtoto mrembo kama alivyo yeye. Ismaiya aliiangalia saa ya ukutani iliyoonyesha ni saa mbili kasoro, asubuhi. Kisha akachukua kadi iliyokuwa kwenye dressing table. Akaitazama kama mtu ambaye haamini. Akasoma majina yaliyokuwa kwenye ile kadi. Majina yalikuwa ni Adele kisena na Robert Gabriel. Aliposoma jina la Robert alijikuta akitoa machozi. Alikuwa akimpenda sana; Robert alikuwa mwanaume ambaye aliuteka moyo wake kikamilifu. Hakuwahi kufikiri kuwa siku moja wataachana . Hata hicho kifo chenyewe aliahidi kupigana nacho kama kingekuja kuwatenganisha. Kama alikuwa tayari kupambana na kifo sembuse mwendawazimu mmoja aitwaye Adele. Alitaka kumuonyesha Adele kuwa yeye siyo mwanamke wa kuchezewa. Alitaka kumfunza Adele kama mfano kwa wanawake wengine wenye tabia za kuiba waume au wachumba za watu.
Akanyanyuka na kuvaa nguo zake. Akashika simu yake na kubonyeza bonyeza kisha akaiweka sikioni.
"hello! Ndio natoka nyumbani" Ismaiya aliongea na mtu aliyeupande wa pili kisha akakata simu. Kama kawaida yake alikuwa amependeza mno. Alivalia suruali nyekundu iliyochora umbo lake kikamilifu. Juu alivalia blauzi ya maua ua iliyoachia sehemu kubwa ya kifua chake ambapo kulikuwepo na mkufu wa dhahabu aliouvaa shingoni. Huyo ndiye Ismaiya bhana. Binti ambaye kama angegombea umiss wa dunia angeshinda bila kupingwa.
Msafara wa magari ya harusi uliowabeba Adele na Robert ulikuwa upo njiani ukiwa umefunga barabara kuelekea ukumbi wa harusi. Ulikuwa msafara wa aina yake kutokana na uwepo wa magari mengi ya gharama. Magari hayo yaliongozwa na Polisi wa barabarani.
"pipipi..pipipipi..pipipi.pipipipi.!" Ilikuwa ni honi ya magari yaliyotoa mlio uliopokelewa na ngoma na matarumbeta. Wapita njia walisimama kushangaa msafara huo wa aina yake. Baadhi ya watu waliacha shughuli zao ili waangalie msafara wa harusi ya aina yake ambao ulikuwa nadra sana kwa jiji la Dar es salaam . Baadhi ya watu wengine walikuwa wapo madirishani wakichungulia tukio hilo lililoibua msisimuko mkubwa kwa kila mtaa ulipokuwa ukipita. Adele akafarajika sana kuona mpango wake wa kuolewa na Robert umekamilika. Akachungulia dirishani akiwa ndani ya gari akaona jinsi watu walivyokuwa wakiutazama msafara wa magari ya harusi yake. Akaachia tabasamu jepesi huku akijisifu na kuona fahari kwa siku ile. Aliwaona watoto wakizuiwa na wazazi wao wasiufuate msafara wa harusi yake ili wasije kupotea. Adele muda wote alikuwa anatabasamu kwa kila alichokuwa anakiona. Hata hivyo ilikuwa ni haki yake kutabasamu. Hiyo ilikuwa ni siku yake kufurahi sasa kwa nini anune.
Alimkumbuka rafiki yake Ismaiya. Alikumbuka siku ya kwanza walipokutana chuoni wakiwa mwaka wa kwanza. Akakumbuka siku Ismaiya alivyokuja kwa mara ya kwanza akiwa na Robert ambapo alipomuona Robert moyo wake ulimpasuka. Adele alikumbuka jinsi alivyomuonea wivu rafiki yake Ismaiya kisa yupo na Robert . Bado aliendelea kukumbuka mambo mengi ambayo mengine yalimfanya atabasamu mengine yaliusononesha moyo wake. Mawazo ya Adele yalikatishwa baada ya mlango wa gari alilokuwa amepanda kufunguliwa. Tayari walikuwa wamefika ukumbini. Alijiweka sawa akisubiri maelekezo ya namna atakavyotoka. Ukumbi ulikuwa umepambwa ukapambika. Watu walikuwa wamefurika wakiwa wamependeza sana. Mbele alisimama mshehereshaji ambapo kushoto kwake alikuwepo Dj aliyekuwa akiweka muziki kuhakikisha tukio lile linavutia zaidi. Maputo yaliranda randa na mapovu yenye rangi za kupendeza ya shampoo yalikuwa hewani. Watu walikuwa wametulia tuli wakisubiri maharusi waingie ili sherehe ianze. Muziki mwororo uliendelea kupiga ukizibembeleza nyoyo za wazazi, ndugu, jamaa na wageni waalikwa waliokuwamo ukumbini. Upande wa kulia mbele kabisa karibu na jukwaa walipoandaliwa maharusi, walikuwa wameketi wazazi na ndugu wa Adele Kisena. Mama na baba yake Adele pamoja na kaka zake walikuwa wamevaa sare zilizokuwa zimewapendeza sana. Upande wa kushoto mbele waliketi wazazi wa Robert Gabriel wakiwa na ndugu na rafiki zake. Nao walikuwa wamevaa sare nzuri za kuvutia zilizokuwa tofauti na wazazi wa Adele.
Punde mshehereshaji akaagiza dj aweke muziki wa kuwaingiza maharusi ukumbuni. Kwa sauti yenye bashasha na ucheshi uliojawa na utani mshehereshaji aliwahamasisha watu wote waliokuwa ukumbini kushangilia. Hapo ukumbi wote ulitikisika na kurindima.
Bibi harusi aliingia akiwa na bwana harusi kwenye lango kuu. Macho yote yaligeuka nyuma kuwatazama. Waooh! Walikuwa wamependeza sana. Walipendeza kupita kiasi mithili ya malaika. Kila mtu alitamani aseme neno kuwasifia lakini midomo ya ikawa mizito. Maharusi wakaendelea kutembea kuelekea mbele walipokuwa wamewekewa siti zao. Adele akainua uso wake uliokuwa ndani ya shela akatazama mbele kabisa lilipojukwaa. Moyo wake ukalipuka kwa shangwe. Alijawa na kiwewe cha furaha. Aliona picha kubwa ikimuonyesha yeye akiwa kakumbatiwa na Robert . Aliikumbuka picha hiyo walipiga studio jana yake. Chini ya ile picha yaliandikwa majina yao, Robert na Adele. Ilikuwa picha iliyovuta hisia zake. Polepole akageuza macho yake kumtazama Robert ambaye naye alikuwa anaitazama ile picha iliyokuwa mbele kabisa jukwaani huku wakicheza polepole wakisonga mbele. Hapo Robert akageuka wakatazamana. Wote kwa pamoja wakatabasamu wakiendelea kucheza taratibu kufuatana na ala ya muziki huku ukumbi ukiendelea kupiga vigelegele.
Wakafika, wakapokelewa na washenga wao. Hatimaye walifika katika sehemu zao walizokuwa wameandaliwa. Ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na chereko wakiwapongeza. Wakati wengine wakiwapongeza, washenga walikuwa na kazi ya kuwahudumia. Mshenga wa Adele alikuwa na kazi ya kulishika na kuliweka sawa shela alilokuwa amelivaa Adele ili lisijemtega akaanguka. Hivyo kila mara alikuwa akilibeba na kumfuta uso wake uliokuwa umerembwa ukarembeka.Maharusi walikaa kwenye viti vyao. Adele akamuuliza mshenga wake.
" Usalama upo Ramla?"
"Kila kitu kipo sawa kama tulivyopanga"Ramla ambaye ndiye mshenga wa Adele akajibu huku akimfuta jasho usoni.
"Vizuri.. Yule malaya sijui huko yupo katika hali gani?" Adele aliongea kwa sauti ya chini huku akifutwa jasho na Ramla.
Hata hivyo Ramla hakumjibu. Harusi iliendelea lakini jambo ambalo Adele hakulitegemea lilijitokeza. Adele moyo wake ulilipuka kwa hofu. Akapoteza utulivu. Ni kama hakuwa na uhakika na kile alichokuwa amekiona. Alishangaa kumuona mshenga wake akiwa kavaa saa ya Ismaiya. Iweje Ramla avae saa ya Ismaiya. Aliitazama kwa umakini akajiridhisha kabisa ilikuwa ni ileile saa ya Ismaiya waliyonunua wote pale mlimani city. Adele akili ikamzunguka. Hofu ikamkumbatia. Alihisi kuna mchezo hauelewi. Akamtazama Ramla ambaye alikuwa hana hili wa lile akiwatazama watu waliomo ukumbini uso wake ukiwa kama mtu anayewaza jambo fulani. Punde Ramla akamgeukia Adele hali iliyomfanya ashtuke. Kilichomshtua ni kukutana na macho ya Adele yenye wasiwasi mwingi. Wote wakatabasamu, Ramla akachukua kitambaa akamfuta Adele usoni. Wakatabasamu tena lakini Adele alishtuka sana, Kitendo cha Ramla kutabsamu kilimtia hofu. Adele aligundua jambo ambalo liliipindua akili yake. Aliona mwanya kwenye kinywa cha Ramla, “hakuwa na mwanya”. Adele alikuwa akiwaza. Marafiki zake wote hawana mwanya isipokuwa rafiki mmoja tuu, Ismaiya! Iweje leo hii Ramla awe na mwanya wakati siku zote hana. Au ameenda kuchonga meno. Mbona ni jana tuu tuliongea naye hakuwa hivi. Huu mwanya umetoka wapi. Adele aliwaza mwenyewe akiwa haelewi, wasiwasi ukamuingia kuwa yule hakuwa Ramla bali alikuwa Ismaiya. Hakuamini kuwa jambo lile lingeweza kutokea. Alianza kumuogopa Ismaiya. Akajiuliza ni kwa kivipi Ismaiya acheze mchezo mgumu kama ule. Hata hivyo akajiuliza kama huyu siyo Ramla. Je Ramla yupo wapi. Akiwaza na kuwazua huku moyo wake ukipoteza utulivu alishtuka kumuona Ramla halisi akiingia mlangoni akiwa kavaa nguo zake kawaida. Moyo ulimlipuka. Alihisi kijasho kikimtoka. Ni kama presha ilimpanda. Akamtazama Ramla akiwa kule mlangoni akiingia, wote walitazamana. Adele akagundua jambo kwenye uso wa Ramla, macho yalikuwa mekundu kama mtu aliyekuwa analia. Hapo wasiwasi ukaongezeka. Akili yake ilichanganyikiwa. Akageuka kumtazama mshenga wake ambaye hapo mwanzo alijua ni Ramla kumbe siye. Ismaiya akatabasamu.
"Unashangaa! Mchezo ndio umeanza bi. harusi muiba waume za watu" Ismaiya aliongea kwa sauti ya chini akimtazama Adele.
Adele bado alikuwa ametekewa akiwa amekodoa macho akiwa haamini. Sasa ilikuwa ni dhahiri aliyekuwa ameketi pale alikuwa ni Ismaiya. Adele aliliona shela zito alitamani alivue ili apate ahueni. Alihisi joto huku kijasho kikimtoka. Ismaiya bado aliendelea na kazi yake ya ushenga. Adele alikwepesha uso wake huku akijitahidi kuwafanya watu ukumbini wasielewe kilichokuwa kinachoendelea.
Kitendo cha Ismaiya kumfuta Adele jasho kilimuumiza sana moyo wake. Aliumia kugeuka mshenga wa bibi harusi aliyemuibia mchumba wake. Hasira zilimpanda. Roho yake ilichafuka. Alitamani ampige Adele muda uleule lakini alikumbuka kuwa yupo mbele za watu. Jambo lolote angelifanya lingemponza na kumharibia mipango yake. Ismaiya alijua kuwa anahitaji uvumilivu kutimiza mipango yake. Ismaiya akamtazama Robert ambaye mara kwa mara alikuwa akimshika mkono na kumpiga mabusu Adele. Roho yake ilimuuma alihisi uvumilivu kumshinda. Alijikaza kuzuia machozi yasidondoke lakini lilikuwa ni zoezi gumu sana. Machozi yalishalamba mashavu yake laini ambayo hayakustahili dhuluma ile.
Ismaiya akakumbuka miaka minne nyuma alipokutana na Robert . Ilikuwa siku ya maonyesho ya sabasaba katika viwanja vya sabasaba pale temeke. Ni siku hiyo ya sabasaba iliyobadilisha muelekeo wa moyo wake. Siku ambayo kamwe hawezi kuisahau. Siku aliyokutana na mwanaume aliyempenda kwa dhati yote. Ismaiya pia alikumbuka siku walipoenda Zanzibar wakiwa na Robert kuosha macho. Ilikuwa ni kumbukumbu iliyomfanya azidi kutoa machozi.
"Maiya nitakupenda siku zote za maisha yangu" Ismaiya alikumbuka maneno ya Robert walipokuwa Zanzibar. Robert alizoea kumuita maiya kama kifupi cha Ismaiya. Huku ndiko kunipenda. Huku ndiko kunipenda Robert . Ismaiya alilalama kimoyo moyo huku akimtazama Robert kwa macho ya uchungu. Robert alishangaa kumuona Ramla akilia. Alijiuliza nini kinamfanya Ramla alie. Masikini, laiti angejua kuwa yule hakuwa Ramla bali ni Ismaiya wala asingejiuliza maswali hayo ya kipuuzi. Angejua majibu ya kinachomfanya binti huyo kulia. Angejua kuwa yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha machozi ya Ismaiya ambaye muda huo alijua ni Ramla. Basi ndio hivyo hakuwa anajua. Walitazamana kwa kitambo kisichozidi sekunde kumi. Robert alimsogelea Adele na kumuuliza kwa sauti ya chini kuwa mbona Ramla alikuwa analia. Adele alimjibu kuwa wala hakuwa analia bali ni matatizo ya macho yaliyokuwa yakimsumbua.
"Pole shemeji Ramla. Sikujua kuwa unamatatizo ya macho" Robert akasema. Maneno ya Robert yaliongeza hasira kwa Ismaiya. Donge zito la hasira lilimkaba kooni. Leo Robert ni wakuniita mimi shemeji. Leo mimi nina matatizo ya macho. Ismaiya alilalama peke yake kimoyo moyo. Huku akimtazama Robert. Adele akaanza kufikiria namna ya kumkabili mshenga wake. Ilikuwa vita baridi baina ya bibi harusi na mshenga wake. Kitendo cha Ismaiya kumkaribia Adele mpaka kuwa mshenga kilimpa Adele hofu kubwa. Akili yake ikamuambia anapaswa afanye jambo la haraka kumkabili Ismaiya. Adele alimnong'oneza Robert jambo fulani. Kisha Robert naye akalifuata sikio la mshenga wake ambaye ni Onesmo Kitoi akamdokeza jambo fulani. Onesmo ni mme wa Ramla. Punde mshehereshaji alitoa taarifa fupi kuwa kutakuwa na mapumziko ya dakika kumi. Kisha harusi itaendelea. Mc aliita band ya muziki kutumbuiza wakati huo bibi harusi Adele na bwana harusi Robert wakitoka kuelekea maliwatoni. Ismaiya akagundua kuwa Adele anataka kumfanyia ujanja ili amtoroke. Hakutaka kumuachia Adele hata sentimita moja. Alijua kufanya hivyo anaweza akampoteza adui yake. Akili yake ikafanya kazi haraka kujua afanye nini. Akataka kumsindikiza bibi harusi lakini yeye na mshenga wa kiume waliambiwa wabaki palepale. Hapo alijua tayari Adele amemkimbia. Na kama ishu ikibumbuluka inaweza hatarisha usalama wake. Adele alitoka kwenda msalani akiwa kashikwa mkono na mume wake, Robert . Watu walishangalia sana jinsi walivyokuwa wakitoka huku band ya muziki ikiimba mubashara. Adele aliyainua macho yake kuangalia kule alipomuona Ramla akiingia lakini hakumuona. Akaangalia pande zote, Robert akamvuta kutokana na kupunguza mwendo.
"Unashangaa nini. Twende. Tunadakika kumi tuu" Robert akasema. Adele hakumjibu zaidi ya kuongeza hatua huku mkono mwingine ukishika shela lisiburuzike lisije likamtega akaanguka. Akaingia chooni. Huko alijiuliza maswali ambayo hakupata majibu yake. Ramla aliyemuona ameingia kaenda wapi. Alijihisi kama amechanganyikiwa.
" ninaota? Lakini hapana! Nimemuona kwa macho yangu kabisa" Adele aliwaza. Alihisi kama anaota. Lakini hakutaka kupuuzia. Alitoka chooni akamkuta mume wake akimsubiri. Kwa jinsi alivyomkuta ni kama alikuwa akimlinda. Unaweza sema alikuwa bodyguard wa Rais. Ilikuwa zamu ya Robert kuingia chooni. Robert alimkabidhi simu Adele ili isijeikaanguka chooni. Robert alipoingia chooni Adele alibinya binya kwenye ile simu kisha akaweka sikioni.
"Mambo yameharibika, Maiya… Ndiye mshenga mpigeni risasi nitakaporudi... Wee usibishe wewe mpige risasi mshenga.." Adele akakata simu baada ya kuona kitasa cha chooni kimetekenywa na Robert kutokea. Robert alisikia kwa mbali maneno “risasi mshenga”
"Nani anataka kumpiga risasi mshenga?" Robert akauliza akichomekea vizuri shati lake kwenye suruali.
"Mume wangu jamani, umesikia vibaya. Au ndio unawaza leo usiku!nitakupa vitu mpaka leo upagawe " Adele aliongea kwa sauti ya kike haswa akiilegeza sauti yake. Kama ni ulaghai Adele alikuwa amesomea. Adele alifanana kabisa na Delila wa Samson. Robert akajikuta akilipotezea swali hilo baada ya Adele kumpelekea mdomo. Wakanyonyana ndimi kwa kitambo kisha wakarudi ukumbini. Ukumbini walimkuta Ramla na Onesmo ambao ni washenga wakipiga stori. Adele alijua dakika fupi zijazo Ismaiya ambaye mle ukumbini watu wanajua ni Ramla atakuwa amekufa kwa kupigwa risasi na watu aliokuwa amewapanga. Adele akarudi sehemu yake akaketi. Muda huu alikuwa na ahueni kutokana na kujua kuwa mwisho wa Ismaiya unakaribia. Alipoangaza kule nyuma ya ukumbi alimuona yule mtu aliyefanana na Ramla. Akamtazama kwa udadisi alafu akashtuka. Sasa waligongana macho. Yule mwanamke ambaye Adele aliamini ndiye Ramla halisi akatabasamu. Moyo wa Adele ulichanganyikiwa baada ya kumuona anamwanya. Akageuka kumuangalia mshenga wake lakini kabla hajafanya lolote ghafla mshenga akadondoka sakafuni huku damu ikitambaa kwenye sakafu. Mshenga alikuwa amepigwa risasi kama Adele alivyoagiza. Adele alihisi kuchanganyikiwa kutokana na kuhisi kuwa aliyepigwa risasi ni Ramla halisi wala siyo Ismaiya. Ukumbi ulishikwa na taharuki kubwa kutokana na tukio la mshenga kudondoka kwa kupigwa risasi. Adele aliamka nakumfuata Ramla aliyekuwa amelala sakafuni
"Ramla! Ramla! Amka Ramla! Ramlaaaaa!" Adele akaita kwa kupagawa huku ukumbi mzima ukiwa tuli umetulia watu wakimtazama kwa macho ya taharuki. Onesmo alibaki amepigwa na butwaa. Aliishiwa nguvu mwishowe akapoteza fahamu. Harusi iligeuka sinema ya kikatili na kutisha. Adele akainua uso wake uliojawa na machozi akamtazama Ismaiya ambaye alikuwa amevaa kinyago chenye sura ya Ramla. Ismaiya akatabasamu kisha akaongea maneno bila kutoa sauti lakini Adele aliyaelewa sawia.
Itaendelea........
Riwaya ya Mlio wa Risasi harusini softcopy Tsh 3,000/= Hardcopy Tsh 10,000/=
Piga simu 0693322300
Mtunzi: Robert Heriel
WhatsApp 0693322300
>>>>>>>>>>>>>>>>>>> Episode 01 <<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<

*************************************************