Ferruccio Lamborghini
JF-Expert Member
- Apr 15, 2020
- 1,667
- 2,594
TRENI ya abiria kutoka bara iliwasili kwenye Stesheni ya Dar es Salaam majira ya saa tano asubuhi. Kuwasili huko kuliwafanya baadhi ya watu waliokuwa wakisubiri, kuanza kuangalia kwenye madirisha ya mabehewa ili kuwaona wageni wao.
Treni hiyo iliposimama kukaligeuza eneo hilo kuingia kwenye hekaheka za watu kupishana kati ya abiria waliokuwa wakiteremka na waliokuwa wakiwasubiri wageni wao.
Sauti zilizokuwa zikikumbushana kutoisahau mizigo kutoka kwa abiria waliokuwa wakiwahadharisha wenzao wanaoteremka, nazo zikasikika. Uchangamfu kwa wenyeji wenye furaha waliokutana na wageni wao na wengine hata kukumbatiana baada ya kuonana ulijitokeza.
Harakati za wenyeji kuwasaidia mizigo wageni waliowapokea ziliendelea, huku wageni wengine walionekana kutokuwa na wenyeji waliofika kuwapokea, wakikatisha katikati ya watu, huku baadhi yao wakiwa wamebeba masanduku vichwani wakielekea nje. Eneo lote lilikuwa limetawaliwa na harufu mbaya na nzito ya jasho lililotokana na abiria wengi kukosa maji ya kuoga kutokana na kusafiri kwa siku mbili mfululizo au zaidi.
Ndani ya behewa moja kulikuwa na abiria aliyekuwa ametulia kimya kwenye kiti akiwaangalia abiria wenzake waliokuwa kwenye harakati za kuondoka.
Mtu huyo aliyeonekana kutokuwa na haraka, alikuwa amekaa kwa kuuegesha mguu mmoja juu ya mwenzake kana kwamba alikuwa bado akiendelea na safari.
Mtu huyo ambaye safari yake ilianzia kituo cha treni cha Kingolwira mkoani Morogoro wakati treni iliposimama, alipanda akiwa hana mzigo wowote aliobeba au kushika chochote mkononi.
Akapata kiti ndani ya behewa aliloingia, na tangu hapo hakuzungumza na abiria yeyote na wala hakuinuka kwenda popote. Hakutikisika, wala hakumwangalia yeyote.
Baadhi ya abiria walimwangalia kwa mashaka, wengine wakimdhania ni mwendawazimu.
Dhana hiyo ikawajengea woga dhidi ya mtu huyo. Hadhari ikajengwa na kuwa makini naye muda wote wa safari. Moja ya kiashiria kilichowafanya wamuone ni mwendawazimu na kumuogopa ni ukimya alioujenga baada ya kuingia.
Kingine kilichowaongezea mashaka kuwa mtu huyo ana matatizo ya akili ni miwani meusi ya jua aliyoivaa.
Wakati alipokuwa akipanda treni hiyo ilikuwa ni usiku na alikuwa ameivaa. Imekuwa ni kawaida kwa wasanii, hasa wa muziki katika kile kinachoitwa ‘swaga ya mavazi’, kuonekana wakivaa miwani ya aina hiyo nyakati za usiku kama kujenga mwonekano wa kisanii mbele ya mashabiki wao.
Lakini ilikuwa tofauti na huyu mtu aliyeingia. Hakuonekana kuwa na dalili zozote zilizomuonyesha kuwa ni msanii wa fani yoyote.
Hivyo, uvaaji wake wa miwani hiyo katika muda kama huo, kulimfanya kila abiria aliyekuwemo ndani ya behewa hilo kumuona ana matatizo ya akili.
Na hakuivua hadi walivyowasili hapo jijini Dar es Salaam.
Kuwasili jijini Dar es Salaam kukawapa baadhi ya abiria waliokuwemo kwenye behewa hilo ahueni ya kujiona wamefika salama safari yao wakiwa na mtu huyo. Wakateremka na kumwacha akiwa amekaa vilevile kwenye kiti kilekile huku miwani yake ikiendelea kuwepo usoni kwake!
Mtu huyo ambaye ni mwembamba na mrefu, mweusi na mkakamavu, ana nywele fupi zilizoonekana kunyolewa siku chache zilizopita kama siyo jana au juzi. Mwonekano wa sura yake ulitoa taswira ya misukosuko iliyomkosesha amani ya maisha.
Hali hiyo ingemfanya yeyote ambaye angemwona, isingekuwa ajabu kubuni kwa kuuzidisha umri wake na pengine kumlengesha kwenye miaka hamsini na mitano au kwenda mbele wakati miaka yake halisi haikuzidi arobaini na mitano.
Akiwa bado amekaa kwenye kiti ndani ya behewa alilomo, mtu huyo aligeuka na kuangalia nje ya dirisha lililokuwa kando yake.
Akaiona ile vurugu iliyokuwepo awali iliyofanywa na abiria walioteremka na kupokewa na wenyeji wao waliokuwa wakiwasubiri, ikiwa imepungua kwa kiasi kikubwa.
Akaurudisha uso wake taratibu kuangalia tena ndani ya behewa alilomo. Akamuona abiria aliyemhesabia kuwa ni wa mwisho kwenye behewa hilo, akimalizia kutoka huku akiwa na begi begani. Akajiona amebakia peke yake ndani ya behewa hilo. Taratibu alijiinua kivivu kutoka kwenye kiti alichokaa na kuelekea mlangoni.
Akiwa nje ya jengo la stesheni, mtu huyo alisimama katika moja ya nguzo zilizopo kwenye baraza ya jengo hilo la kituo cha treni na kuiangalia barabara iliyokuwa mbele yake.
Akawa ametulia kuyaangalia magari madogo yaliyokuwa kwenye foleni iliyosimama yakipigiana honi muda wote.
Tukio hilo la kuuona msongamano wa magari, lilimfanya aifikirie miaka ya nyuma alipokuwa ameliondoka jiji hilo la Dar es Salaam.
Hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kuliona jiji hilo. Aliondoka kukiwa hakuna msongamano mkubwa wa magari kama anavyoushuhudia hapo.
Magari yalikuwa yameenea kuanzia mzunguko wa mnara wa Clock Tower na kuingia hadi Barabara ya Nkrumah na kuendelea kwenye Barabara ya Uhuru na mengine yakitokea Mtaa wa Samora na kuzunguka mzunguko wa Clock Tower na kujigawa.
Baadhi yalionekana yakija Barabara ya Sokoine na kukata kuelekea maeneo ya Kurasini, huku mengine yakiongoza kwenye barabara za Uhuru na Nkrumah. Mji umebadilika! mtu huyo aliwaza huku akiendelea kuyaangalia magari hayo.
Akiwa bado amesimama nje ya jengo hilo la stesheni ambalo aliliona likiwa limebakia katika taswira ileile ya miaka aliyokuwa ameondoka jijini humo, mtu huyo aliyaangalia majengo yaliyokuwa mkabala na uso wake.
Zilikuwa ofisi za Shirika la Reli na Kituo cha Kati cha Polisi. Aliyabaini majengo hayo kutokuwa na mabadiliko yoyote kwa miaka aliyokuwa ameondoka. Badiliko pekee aliloliona ni kwenye jengo la Tanesco alilolifahamu kwa jina la ‘Tanesco Training School’ kwa miaka hiyo.
Hakuwa na uhakika kama bado lilikuwa chini ya shirika hilo na kuendelea kutumiwa kwa matumizi hayo.
Kwa eneo alilokuwa amesimama na taswira aliyoiona pale, akaamini jiji la Dar lilikuwa bado halijawa kwenye mabadiliko makubwa. Aliliona kutokuwa tofauti na miaka aliyokuwa ameondoka.
Miaka ambayo alikwenda kutumikia kifungo cha jela cha miaka arobaini na kuhenya nacho kwa wastani wa miaka ishirini na mitano.
Sasa anarudi katika jiji hilo akiwa raia huru!
Miaka imekatika! aliwaza huku akianza kuteremka kwenye ngazi kuliteremka jengo hilo. Akaivuka barabara kwa kukatiza kwenye magari yaliyokuwa kwenye msongamano.
Akaelekea kituo cha basi cha stesheni kwa kupitia Barabara ya Sokoine. Alipoifikia barabara hiyo ya Sokoine, hapo ndipo aliposhtuka baada ya kuliona jiji likiwa na mabadiliko ambayo hakuyatarajia kuyaona.
Mungu wangu, mji umebadilika hivi! alishangaa huku akikifuata kituo cha mabasi ya daladala cha Stesheni. Aliiangalia barabara hiyo ya Sokoine kwa mshangao ikiwa na taswira tofauti na ile aliyoiacha.
Majengo marefu yalikuwa yameibuka kadri upeo wake wa macho ulivyokuwa ukienda mbele huku macho yake yakiangalia kila kona ya anga ya jiji hilo iliyomuonyesha kuwepo kwa jengo refu.
Hali hiyo ikaanza kumuweka kwenye wasiwasi huenda hata mabasi aliyokuwa akiyafuata kwenye kituo anachoelekea yanaweza yasiwe yanakitumia tena kituo hicho. Akiwa amejipanga kumuuliza mtu endapo hataliona basi analolihitaji, ghafla mbele yake akaliona basi lililoandikwa, M’MBUSHO/STESHENI.
“Mwananyamala, Mwananyamala!” alimsikia na kumuona kondakta wa gari hilo akiita abiria wa kupanda basi hilo.
Kuliona basi hilo, mtu huyo alichepuka kwa mwendo wa haraka na kwenda kuingia. Sijui nauli itakuwa shilingi ngapi? alijiuliza wakati akikaa kwenye kiti kilichopo dirishani.
*******
Macho yake yakiwa wakati wote yanaangalia nje kwenye mitaa ambalo basi hilo likipita, mtu huyo alikumbana na mabadiliko yaliyokuwa yakimuonyesha kuwa, Dar es Salaam aliyoiondoka, siyo Dar es Salaam anayoishuhudia akiwa humo kwenye basi.
Alikiri mabadiliko anayoyaona yalikuwa makubwa. Majengo marefu yenye ghorofa zilizokwenda juu yalionekana yamechipua katika maeneo tofauti kila alimokuwa akipita.
Kulikuwa na majengo mapya na yapo yaliyokarabatiwa; yote hayo yalimshangaza, huku akijaribu kuuficha mshangao wake usionekane na abiria aliokuwanao ndani ya basi.
Kadhalika, alishangazwa na magari madogo ya kifahari yaliyojazana barabarani huku akishtushwa na idadi kubwa ya wanawake, hasa wasichana waliokuwa wakiyaendesha. Mabadiliko! aliwaza.
Kitu kingine kilichomshangaza ni idadi kubwa ya wasichana aliowaona wakitembea barabarani. Wengi aliwaona wakiwa warembo, lakini pia maeneo ya makalio yao yakionekana kuwa na afya njema. Wanakula nini? alijiuliza huku macho yake yakiambaa kumwangalia msichana aliyekuwa amevaa suruali iliyobana vyema sehemu zake za nyuma, akitembea kando ya barabara.
Daladala alilopanda likaingia Barabara ya Kinondoni. Mabadiliko aliyokutana nayo kwa kuanzia uwepo wa Benki ya Stanbic na majengo mengine yaliyofuatia, yalimfanya kutochoka kuangalia nje wakati akipita barabara hiyo, huku akiiona Shule ya Sekondari ya Kinondoni -Bakwata ikiwa na mabadiliko makubwa.
Itaendelea kesho
©Mwanaspoti