Riwaya Mpya: Mpelelezi Ray Shaba katika

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,720
40,804
promo2.png
SURA YA KWANZA:


Ray Shaba alikuwa kwenye kikao ambacho mjumbe wake alikuwa ni yeye peke yake. Mikono yake ikiendelea kurusha ngumi kwenye begi la mchanga lililokuwa linaning’inia kwenye chumba chake cha kufanyia mazoezi. Begi lile la mchanga la ngozi nyeusi lilikuwa na maandishi makubwa ya EVERLAST likionesha limetengenezwa na kampuni gani. Alipiga ngumi mfulilizo huko akiruka ruka kama bondia machachari ulingoni. Alikuwa anathema kwa nguvu huku jasho likimtiririka.

Sijui nimfanye nini.

Alipiga ngumi tena. Jab, Jab, Cross, Hook, Jab Jab, Cross, Hook. Jasho lilimdondokai kama mtu aliyekuwa aliyeingia ndani akitoka nje alikonyeshewa mvua. Zilikuwa zimepita karibu wiki tatu tangu yeye na mke wake wakutane katika mapenzi. Mke wake alikuwa hataki Ray amguse. Ray alikuwa anaona kama ananyima kile ambacho aliamini kuwa ni haki yake. Mara ya mwisho nusura amlazimishe mke wake kwa nguvu. Hata hivyo kama Afisa wa Polisi alijua kabisa kuwa kufanya hivyo ingekuwa sawa na kumbaka mkewe. Kila akimfikiria alizidi kupata hasira kwani alikuwa anajishangaa kuna wasichana wangapi ambao walikuwa wanajilengesha kwake ofisini.

Ray Shaba alikuwa ni kijana wa miraba mine, mrefu wa wastani na aliyekaa kama mtu ambaye ni mcheza filamu mashuhuri. Uso wake alijaliwa uso wa utoto wenyewe waliita babyface. Lakini umbo lake lilikuwa la mtu mkakamavu. Jasho lililokuwa limetanga mwili lilimfanya ang’are mwili mzima kama mtu aliyepakwa mafuta Nywele zake zilikuwa zimekatwa vizuri, kwani alikuwa na kawaida ya kukata nywele zake kila wiki.

Kwa miezi kadhaa uhusiano na mke wake ulikuwa una mushkeli. Walikuwa hawawezi kuzungumza vizuri bila mkewe, Sofia Shaba kusema jambo ambalo lingemtibua kichwani Ray. Sofia akianza kusema maneno yake yalikuwa ni kama kujaribu kupima uvumilivu wa mmewe. Mara kadhaa Ray alijikuta anacharuka wakati mwingine hata kutamani kumzaba kibao mkewe. Lakini alikuwa ni miongoni mwa watu wenye uwezo mkubwa wa kujitawala; akifika katika hali hiyo huwa anaamua kutoka nje na kwenda kutembea kufanya jambo jingine.

Asubuhi ile alikuwa amejaribu kupata haki yake ya ndoa kwa mkewe aliyekuwa amelala naye pembeni tena akiwa kama alivyozaliwa. Ray alianza kumchokoza kuona labda safari hii angefanikiwa.

“No, Ray, No” Sofia alisima nusu akiwa usingizini, akiutupilia mbali mkono wa Ray uliokuwa umeanza kutambaa kwenye kifua chake.

“Sofia, mbona unakuwa hivi lakini”

“Bwana, nimechoka bana”

“Sasa kuchoka gani huku wiki sasa?” Ray alisema akionesha kukasirishwa.

“Sijisikii vizuri kweli”

“Sasa wewe unafikiri mimi nifanyaje?”

“Nenda bafuni kajimwagie maji ya baridi” Sofia alisema na kujigeuza upande wa pili huku akijifunika Zaidi. Ray alitamani alivute lile shuka na kulitupilia mbali na afanye vitu ambavyo angeweza kuvifanya. Kama angeamua kutumia nguvu, Sofia hakuwa na nafasi wala uwezo wa kumzuia Ray. Hasira zilimuwaka na akaamua kutoka pale kwenye bafuni kupiga kunawa uso na kuenda kwenye mazoezi.

Ray aliendelea na mazoezi yake ya kupiga ngumi na baadaye akaanza kunyanyua vyuma. Chumba chake kilikuwa kikubwa na alikitenga mahsusi kwa ajili ya mazoezi ya viungo. Kutokana na kazi yake alijua inamapasa kuwa fiti kabisa. Pamoja na utaalamu mwingine mwingi, Ray alikuwa anashikilia Mkanda Mweuzi Ngazi ya Nne wa Karate za Goju Ryu za Okinawa Japan. Baada ya kunyanyua vyuma na kusisimua misuli yake, alipanda kwenye mashine ya kukimbia na kuanza kufanya mazoezi ya kukimbia katika kuinua uwezo wa mapafu yake na ustahimili wa moyo wake. Alikimbia kwenye mashine ile kwa saa moja hivi.

Baada ya hapo Ray alifanya mazoezi ya kawaida ya taratibu huku akiangalia habari kwenye TV iliyokuwa inaning’inia kwenye ukuta mmoja wa chumba kile cha mazoezi. Hakukuwa na sauti nyingine yoyote isipokuwa ile TV ikirusha habari za kimataifa kwa sauti ya chini. Alikuwa anendelea kujiuliza kama mke wake anafanya vile kumshinikiza kukubaliana naye katika mambo ambayo Ray alishafanya uamuzi, au anafanya vile kama adhabu.

Wanawake bana, wanafikiri sex ni zawadi au adhabu.

Alitaka kucheka lakini alijua ukweli wa wazo hilo. Miaka yake ya ndoa na Sofia ilikuwa ni ya furaha sana mwanzoni. Lakini kwa kadiri walivyokuwa wanachelewa kujaliwa kupata mtoto, ndivyo Sofia alivyokuwa anazidi kuonekana kutokuwa na furaha na kuchukulia tendo zima la mapenzi kati ya mume na mke kama silaha au kifaa Fulani ambacho anaweza kukitumia. Akiwa na furaha na Ray basi atajitoa kwake, lakini Ray akimuudhi kidogo basi anabana miguu yake kwa hasira. Mara nyingi Ray inapokuwa katika hali hiyo alikumbuka wimbo wa Christian Bella, wa Mapenzi Gani. Hakuelewa kwanini ilikuwa ni lazima abembeleze kitu ambacho Sofia mwenyewe alisimama altarene na kusema “Ndio”.

Alipomaliza mazoezi alichukua tauno jeupe na kuanza kujipangusa huku akielekea bafuni kujimwagia maji katika bafu lililokuwa limetengenezwa kwenye chumba kidogo pembeni ya chumba kile cha mazoezi. Alioga kwa haraka na baada ya hapo alielekea chumbani kwenda kubadili nguo na kujiandaa kwenda kazini. Alimkuta mke wake bado amejilaza, tena amejisaula kabisa jinsi alivyomwacha, shuka likiwa limemfunika sehemu ya kiuno tu. Ray alijihisi damu inapanda tena na hamu kwa mke wake ikimpanda, lakini hakuwa na muda wa kubembeleza. Kuna mambo makubwa ya kitaifa yalikuwa yanamsubiria, kuna Jiji linatakiwa liwe salama, kuna kesi zinahitaji kufungwa. Alikuwa ni mpelelezi nambari moja Tanzania. Taifa lilimtegemea,

Alipomaliza kupata kifungua kinywa mke wake alikuwa anaoga. Hakutaka hata kumuaga kwani na yeye alikuwa anajua kulipiza kisasi; kama yeye anabania na mimi nitabania alijiambia. Alipoingia kwenye gari lake, simu yake ya mkononi ikaita.

“Ray”

“Yeah”

“Kuna majambazi yamevamia Benki NMB Barabara ya Azikiwe na Kamanda anataka ufike mara moja”

“Ok, niko njiani”

Alikata sima kumuaga Katibu Muhtasi wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar-es-Saalam, SACP Rama S. Msangi. Alipotoka getini, alijisemea moyoni kuwa siku ile ilikuwa ni siku mbaya sana kumtibua, majambazi yalichagua siku mbaya sana kumuingiza Ray kwenye kuwashughulikia. Na itakuwa siku mbaya kwao, Ray alijiambia. Ilikuwa siku nyingine ya kazi ya kulinda raia, usalama wao na wa mali zao.

Mpelelezi Ray Shaba, aliingia kazini.

SURA YA PILI

ASKOFU MKUU, NABII, Mtume, Mwinjilisti na Mtumishi wa Mungu Damien Zeloth Ndondo alikuwa amefumba macho yake katika hali ya sala mkono wake wa kulia ukiwa umeshikilia Biblia kwenye mapaja yake. Biblia yake ilikuwa ina gamba jeupe na zipu ya rangi ya dhahabu, iliyoendanana na zile nyuzi za kuweka alama kwenye ukurasa usipotee. Mkono wake wa kushoto aliuegemeza kwenye kiti chake huku vidole vya mkono huo wa kushoto vikiwa vinacheza cheza vikifuata taratibu mapigo na mdundo wa wimbo wa sifa uliokuwa ukiendelea kupasua angala la uwanja wa Jangwani. Kila baada ya dakika kadhaa mkono wake wa kushoto ulishika kitambaa cheupe na kumpangusa uso wake.

Damien Ndondo alikuwa ameketi kwa utulivu kwenye kiti kikubwa cheupe kilichoweka nakshi ya rangi ya dhahabu kwenye kingo zake huku kikiwa kimeinuliwa juu kidogo ya viti vingine vilivyokuwepo jukwaani pale. Yeye mwenyewe alikuwa amevalia suti nyeupe na viatu vyeupe. Ndani alikuwa amevaa shati la KiAskofu linalong’ara la rangi ya dhambarau huku kifuani kwake akiwa amevaa msalaba mkubwa wa rangi ya fedha. Kiegemeo cha kiti hicho kilikuwa kikubwa na kukifanya kiwe ni kama kiti cha enzi cha kifalme. Askofu Mkuu Ndondo alikuwa ameketi pale akisubiri muda ufike akaribishwe tena na Mchungaji Msaidizi Asegelile Mwakilembe aliyekuwa mwongozaji wa mkutano ule ili aendelee na mahubiri yake.

Siku ile ilikuwa ni siku ya tano ya mfululilzo wa siku saba za mahubiri makubwa katika mkutano uliopewa jina la Siku Saba za Uweza – Dar Yarudi kwa Yesu. Maelfu ya watu kutoka kona zote za Jiji la Dar-es-Salaam na wageni wengine kutoka mikoani walifurika katika viwanja vile. Kina mama na kina baba, wazee kwa vijana na watoto wengine wakiwa wametoroka kwenye shule za sekondari na za msingi walikuwa wamejazana pale. Wafanya biashara na wachuuzi wa vitu mbalimbali nao walitumia nafasi ile kufanya biashara zao ndogondogo kuzunguka viunga vya mkutano ule.

Jukwaa lilikuwa la kisasa zaidi kuliko majukwaa yote ambayo yamewahi kutengenezwa huko nyuma kwenye viwanja vya Jangwani iwe kwa mambo ya dini au ya kijamii. Lilikuwa ni jukwaa lenye sehemu tatu ambazo zote zingetosha kabisa kuwa majukwaa yanayotegemea. Yaliunganishwa kwa aina ya mapaa matatu; sehemu mbili za pembeni zilikuwa na mapaa ya nusu mviringo wakati jukwaa la kati ambapo Askofu alikuwa amekaa na kwaya yake lilikuwa na jukwaa kubwa la pembetatu. Kwenye majukwaa yale mawili ya pembeni kulikuwa na TV kubwa juu yake zikirusha mkutano ule. Juu ya jukwaa kuu kulikuwa na bango kubwa ambalo lilikuwa na maandishi yakimulikwa na taa “Yesu Jana na Leo”. Kwamba baada ya mkutano huo jukwaa lile lingekuja kupanguliwa ingekuwa vigumu kuamini kwani lilionekana kama jengo la kudumu mahali pale.

Majukwaa yale mawili ya pembeni yalikuwa yamegawanywa huku upande wa kushoto kulikuwa na safu tano ya viti nane nane ambavyo vilikuwa vimekaliwa na wachungaji na mashemasi waandamizi wanaume na wanawake wa kanisa lake ambao walikuwa hapo pia kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali za kiroho. Wengi wao walikuwa wametoka kwenye matawi mbalimbali ya kanisa la Ndondo ndani na nje ya nchi. Kumi tu ndio walikuwa wanatoka Makao Makuu pale Dar. Wachungaji wale wote pale walikuwa wamevaa mashati meusi ya kichungaji yenye kola nyeupe za kiroma.

Upande wake wa kulia kwenye lile jukwaa jingine kulikuwa na safu nyingine tano ya viti nane nane vikiwa vimekaliwa na wageni kutoka serikalini, viongozi mashuhuri wa kisiasa, viongozi wa makanisa na dini nyingine waliokubali mwaliko. Watu wengine mashuhuri waliokuwepo Jijini Dar ambao walikuwa wamealikwa kwenye mkutano huo ambao ulikuwa unafanyika kwa mara nyingine nao walikuwa kwenye upande huo. Kila mwaka wakati wakati wa kuelekea msimu wa Krimasi na kufunga mwaka ndio ulikuwa wakati wa mkutano mkubwa kwa ajili ya Jiji la Dar na watu walikuwa wanasubiria kwa hamu kwani kwa muda wote wa mwaka Askofu Damien anakuwa katika mikutano katika mikoa mbalimbali nan je ya nchi hasa katika nchi za Kiafrika.

Mkutano huo ulirushwa moja kwa moja kupitia TV ya kanisa lake na kusikilizwa nchi nzima kupitia radio ambayo pia kanisa lake lilimiliki; au kwa usahihi zaidi familia yake ilimiliki. Magari ya kurushia matangazo yalikuwa yameegeshwa mita chache tu nyuma ya jukwaa ambalo wenyewe walikuwa wanaita madhabahuni. Pamoja na vyombo hivyo vya habari mkutano huo wa kiroho ulikuwa ukirushwa moja kwa moja pia kupitia mitandao ya kijamii ya YouTube na Facebook pamoja na kwenye tovuti ya Askofu Ndondo. Kulikuwa na wafanyakazi wengine vijana ambao walikuwa na jukumu la kutoa yanayoendelea na kurusha picha mbalimmbali kwenye mitandao ya Twitter, Instagram na JamiiForums.

Kwenye viti vya wageni mashuhuri walikuwepo Mkuu wa Mkoa wa Dar Bw. Dotto Rangimoto ambaye alikuwa anatajwa kama rafiki wa karibu sana wa Rais. Alikuwepo pia Mstahiki Meya wa Jiji la Dar Nelson Kibonge ambaye alikuwa anatoka chama cha upinzani cha CHADEMA, Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar Kamishna Mwandamizi wa Polisi Rama S. Msangi, Waziri wa Jinsia na Watoto Rehema Faraja, Waziri wa Ulinzi David Mpogoro na wengine viongozi wa vyama vya siasa. Kiongozi Mkuu wa kambi ya upinzani Bungeni Dkt. Butho Mtenzi naye alikuwe ameungana nao kwani alikuwa pia ni muumini wa kanisa la Ndondo.

Jukwaa kuu lilikuwa na ukubwa wa mita 30 x 30 likiwa na seti ya viti nane upande mmoja ambapo Askofu Mkuu Ndondo na mke wake Rebecca – Mama Askofu – au maarufu kama First Lady pamoja na wazee wawili wa kanisa pamoja mwongozaji wa mkutano. Viti vitatu vilivyobakia vilikuwa kwa ajili ya walinzi wao binafsi. Nyuma yao ilikuwepo Kwaya Kuu ya Kanisa la Mavuno ya Siku za Mwisho iliyojulikana kama End Time Harvest Mass Choir ikiwa na waimbaji mia moja waliotoka katika kwaya mbalimbali za kanisa hilo zinazoongoza ibada mbalimbali za Jumapili.

Wote walikuwa wamevalia majoho ya rangi ya dhambarau inayong’ara huku yakiwa na utepe mweupe uliozunguka shingoni na kuangukia pembeni ya kiuno karibu na magoti hivi. Walionekana kama wahitimu waliokuwa wanasubiri kupewa shahada zao. Tepe zilizoanguka mabegani zilikuwa na michoro ya msalaba. Wote walikuwa wamesimama kwenye jukwaa la ngazi lililokuwa nyuma ya jukwaa kuu wakipaza sauti zao kwa sifa, huku wakinesanesa kufuata mapigo ya nyimbo mbalimbali.

Askofu Mkuu Ndondo alikuwa ndiye mhubiri maarufu zaidi nchini akiongoza mojawapo ya makanisa makubwa kabisa katika bara la Afrika. Kanisa lake la The End Times Harvest Tabernacle –Maskani ya Mavuno ya Nyakati za Mwisho - lilitajwa na jarida maarufu la Times la Marekani katika orodha ya makanisa makubwa duniani. Lilikuwa ni mojawapo ya Makanisa makubwa kabisa kwa uwezo wa kuchukua waumini Afrika nyuma ya lile Kanisa Katoliki la mji wa Yamoussoukro, Cameron. Kanisa la Mavuno kama lilivyojulikana kwa waumini wake na sehemu nyingine nchini lilikuwa limejengwa katika eneo lililowahi kuwa la Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam Taasisi ya Maendeleo ya Maji, Ubungo.

Miaka michache nyuma serikali iliuza maeneo kadhaa yaliyokuwa ya wazi Jijini Dar kwa wawekezaji na mojawapo ya maeneo ni pale alipojenga kanisa lake. Askofu alinunua eneo lile kwa shilingi milioni mia tatu na hamsingi tu jambo lilizusha mjadala mkali Bungeni na kwenye jamii kwani ilidaiwa kuwa ni eneo ambalo kama lingeuzwa kwa bei halali lisingechukulika bila bilioni kumi na tano. Wengine walidai kuwa thamani ya eneo lile lilikuwa si chini ya bilioni hamsini. Kutokana na ukwasi wake na ukaribu wake na baadhi ya viongozi mjadala ule ulizimwa kinyemela na mambo kuendelea kimya kimya. Viongozi wa upinzani na baadhi ya wale kutoka CCM walitishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu lakini juhudi zao hazikufika mbali.

Mchungaji Ndondo alinunua eneo hilo bila ya kufikiria mara mbili akiwashinda wawekezaji kutoka Afrika ya Kusini waliotaka kujenga nyumba za kisasa za kupanga. Ndani ya mwaka mmoja na nusu tu toka anunue alihamishia kanisa lake toka maeneo ya Kipawa ambako lilianzia na kukua kwa kasi kuliko Kanisa lolote katika Afrika ndani ya miaka kumi. Kutokana na kuwa na waumini wapatao elfu thelathini wanaohudhuria ibada tano kila Jumapili hakukuwa na jinsi isipokuwa kuhamisha Kanisa ili kuweza kuwapokea watu wengi zaidi na kutoa huduma nyingine nyingi mbalimbali.

Pamoja na kanisa hilo kuu, Ndondo alikuwa na matawi ya makanisa katika mikoa mitano nchini ya Iringa, Morogoro, Mwanza, Arusha na Dodoma. Alikuwa anatarajia kufungua matawi mengine kumi kwenye mikoa mingine baada ya mwaka mpya. Ibada zake za Jumapili ambapo akiongoza kutoka mojawapo ya makanisa zilikuwa zinarushwa moja kwa moja kupitia mtandao wa intaneti kwenda makanisa yake mengine na kwenye mitandao ya Facebook na Youtube huku wafanyakazi wake wengine wakirusha vipande vipande vya kilichokuwa kinaendelea kanisani kupitia Twitter na Instagram.

Mkutano huo wa Jangwani ulikuwa unafanyika ikiwa ni mara ya mwisho kwa viwanja hivyo kuwa sehemu ya makusanyiko makubwa ya watu. Hii ni baada ya kukamilika kwa stendi ya mabasi yaendayo kwa kasi na kuuzwa kwa eneo lililobakia kwa ajili ya ujenzi wa magorofa ya kisasa ambayo minong’ono ya mitaani ilikuwa inadokeza kuwa ilikuwa mali ya rais mmoja wa zamani na familia yake. Wakazi wa Dar waliahidiwa kuwa eneo jipya jingine litatengwa kwa ajili ya shughuli za mikutano, michezo na burudani. Hivyo, pamoja na mahubiri ya Ndondo watu wengine walienda pale kama kutoa heshima zao kwa uwanja huo maarufu ambao umekuwa ukitumika kuwakutanisha maelfu ya watu wa Dar tangu enzi za harakati za Uhuru. Wazee wa Dar wanakumbuka eneo hilo ambapo Nyerere alikuwa akifanya mikutano ya kuhamasisha watu kuelekea kukomesha ukoloni. Masimulizi ya jinsi Nyerere alikuwa anawahamasisha wazee wa Dar yaliandikwa katika simulizi na Mzee Mohammed Said ambaye wazazi wake walikuwa ni mashuhuda wa harakati za uhuru.

Majira ya saa kumi na moja kamili yalipokaribia mwimbaji Skola Kanuti alikuwa anamalizia kuongoza wimbo wa kuabudu uliokuwa ukisindikizwa na sauti maridadi za ala za muziki kutoka bendi yake. Jua lilikuwa tayari linaelekea kuzama na upepo ulikuwa unavuma taratibu kutokea baharini. Kulikuwa na mawingu kidogo upande wa Magharibi na makundi ya nyangenyange yalipita kukata mawingu hayo kila baada ya dakika chache kama vile yanalifuata jua liendako.

Wimbo wa Skola Kanuti wa El-Shaddai Tunakuabudu ulikuwa unapanda chati za nyimbo za Injili nchini na nchi za jirani zinazozungumza Kiswahili. Hata kwenye nyimbo za kidunia bado ulikuwa unaongoza nambari moja nchini na watu hata wasiokuwa waumini walipenda kujikuta wanauimba wakiwa katika shughuli zao mbalimbali. Ulipigwa katika mtindo wa RnB huku sauti ya Skola ikiupamba kama Whitney Houston katika wimbo wake wa I Look to You.

Askofu Mkuu Ndondo alijikuta akisimama huku akinyosha mikono yake juu kupunga na akifuatisha wimbo huo wa kuabudu. Wachungaji waliokuwa pale jukwaani na wageni wengine waliokuwa naye pale jukwaani walisimama huku wakipunga mikono yao hewani katika hali ya kumtukuza Mungu na kuoneshwa kuguswa. Kwaya ya End Times Harvesters ilikuwa inaunga mkono katika kiitikio cha wimbo wakifuatia uongozi wa bendi ya muziki wa Injili ya Skola Kanuti.

Skola aliongoza wimbo wa kuabudu kwa umahiri mkubwa akiwa amezama katika hisia za ibada kwelikweli; machozi yalikuwa yakitiririka kwenye mashavu yake kama vijito vya maji kwenye bustani nzuri. Alikuwa amevaa sketi nyeusi ndefu hadi miguuni, ikimbana kwa kiasi ikiacha dokezo tu umbo lake la namba nane alilojaliwa na Mungu. Juu alikuwa amevaa blauzi nyeupe yenye mikono mifupi yenye marinda mabegani. Nywele zake nyeusi zilikuwa zimechanwa na kufungwa nyuma katika fundo lililosindikizwa na kibanio kidogo cheusi. Mkufu wa rangi ya dhahabu ulining’inia shingoni mwake huku kidani chake cha msalaba kikiangukia katikati ya kifua chake ambapo blauzi iliachia kidogo. Kama ilivyokuwa kawaida yake miguuni alikuwa amevaa viatu vya mchuchumio vya rangi nyekundu ambavyo vilikuwa vikionekana zaidi akitembea pale jukwaani.

Mbele ya maelfu ya watu waliokuwepo pale uwanjani umati huo mkubwa wa watu Skola aliimba kwa sauti ya aliyokuwa anaimiliki kwa madoido yenye kuonesha upeo wake wa sauti. Wimbo ule wa kuabudu uliunguruma kwenye seti sita za maspika makubwa nane nane yalikuwa yamegawanywa pale uwanjani katika pande mbili. Kulikuwa na seti ya kwanza ya spika iliyoukwa pembeni ya jukwaa kubwa ikining’inia kwenye minara mikubwa miwili ambayo pia ilikuwa imewekwa pia taa kubwa za usiku zikiangaza chini jukwaani, nyingine zikimulika nyuma na mbele ya jukwaa hilo kubwa.

Seti nyinginge mbili zilikuwa upande wa kushoto na wa kulia kama mita hamsini tu kutoka jukwaani na seti nyingine mbili zikifuatia mita mia hivi kutoka seti zile za pili. Seti ya mwisho ilikuwa nyuma kati ya maelfu ya watu waliokuwepo pale uwanjani yakining’inia manne manne kwenye kibanda cha fundi mitambo ambacho nacho kilikuwa kimezungukwa na taa kubwa za usiku zikining’inia kwenye milingoti mikubwa ya chuma.

Maelfu ya watu waliokuwa wanahudhuria mkutano huo mkubwa wa Injili nao walikuwa wakinyosha mikono yao katika hali ya kuabudu wakifuata sauti ya Skola Kanuti. Wengine kama Skola nyuso zao zilikuwa zikibubujika machozi. Siyo wote waliokuwepo pale uwanjani walikuwa hapo kwa ajili ya mahubiri ya kusisimua ya Askofu Ndondo. Wapo waliokuwepo kwa ajili ya yale yaliyodaiwa kuwa ni miujiza ambayo huambatana na mahubiri ya Ndondo. Kila mkutano wa Ndondo ulipokuwa ukitangazwa mojawapo ya chombezo zilizokuwa zinarushwa sana ni madai ya uwepo wa watu waliokuwa wanapona kutoka matatizo mbalimbali kama uziwi, ububu, magonjwa mbalimbali na hata madai ya watu walioondolewa vizazi wakirudishiwa na wengine wakidaiwa kuwa waliweza kupata watoto licha ya vizazi vyao kuondolewa na hivyo kupata ujauzito kwa njia ya miujiza.

Hata hivyo walikuwepo wengine pale na labda kundi kubwa kuliko mengine ambao walikuwa wanasubiri muziki mwanzoni mwa mahubiri na mwisho wa mahubiri. Baada ya watu kuitwa kukata shauri mwishoni mwa mahubiri na watu walipoagwa kuahirisha krusedi ile kwaya zilipiga nyimbo za kusisimua. Askofu Ndondo alijulikana kwa jinsi kwaya yake ilivyokuwa inapenda kile kilichoitwa “ndombolo ya Yesu”; aina ya muziki wa Kikongo lakini ukitumika kanisani. Watu walipenda kucheza nyimbo hizo wengine wakikatika kabisa na kushtulia utadhani wanacheza miziki ya kina Christian Bella au wanacheza kwa madoido kama vijana wa Yamoto Band.

Ndondo alifumbua macho yake wakati wimbo ule wa kuabudu unaelekea ukingoni na mhamasishaji akisogea taratibu mkononi akiwa ameshika kipaza sauti ili kupokea taratibu majukumu kutoka kwa Skola. Kutoka Askofu alipokuwa amesimama Skola alikuwa mbele yake mita chache tu. Ndondo alimuangalia mdada yule na mawazo fulani ambayo hayakumpasa mtu aliyejitambulisha kama mtu wa Mungu yalianza kumpanda taratibu kama mchwa kwenye tegu la kitanda. Mawazo yale yalifika sehemu za viungo mbalimbali vya mwili wake na kuamsha ashki na hamu za kiume ambazo mahali pake hasa ni chumbani kwake na mke wake. Hisia zile zilimfanya asahau kwa sekunde chache kuwa alikuwa mbele ya mkutano wa Injili, mbele ya maelfu ya watu na yumkini mamilioni wakimuangalia kwenye luninga. Ndondo hakuwahi kuyakemea wala kuyakataa kama alivyokuwa akiwafundisha wengine mara kwa mara katika semina zake maarufu zilizojulikana kama Maisha ya Ushindi Katika Kristo.

Hayakuwa mawazo tu ya tamaa ambayo mwanamme au mwanamke yeyote yanaweza kumpitia wakati fulani; yak wake yalivunja ukuta wa tamaa na kupitiliza. Yalikuwa yanajenga mafuriko ya tamaa katika mwili na hisia za Askofu Mkuu Ndondo. Mafuriko hayo ya tamaa yalikuwa ni sehemu ya maisha yake tokea ujana. Yalikuwa ni mafuriko ya maji machafu yaliyoanza kuujaza moyo wake na kuchafua ibada yote rohoni mwake. Hakumuona Skola kama mtumishi wa Mungu akiwa katika huduma yake ya uimbaji. Ndondo hakujali kabisa kuwa Skola alikuwa ni mke wa mtu katika ndoa ambayo yeye mwenyewe ndiyo aliyeifungisha miezi sita tu nyuma.

Aliapa moyoni mwake dakika chache tu kabla hajakaribishwa kuendelea na mahubiri yake kuwa vyovyote vile ilivyo au itakavyokuwa alitaka kuona mubashara kile kilichofichika chini ya mavazi yale mazuri. Askofu alidhamiria kuwa siku moja atahakikisha anamjua Skola Kanuti. Alikuwa anamjua ndiyo; lakini alitaka kumjua Kibiblia japo ilikuwa ni kinyume na Biblia yenyewe.

“Halleluya, Halleluya” alisema kwa sauti ya taratibu wakati akisogea mbele ya mkutano huku Skola naye akielekea kwenye ngazi upande wa kulia wa jukwaa kwa ajili ya kujiandaa kusikiliza mahubiri. Muziki uliendelea taratibu huku mkutano ukilipuka kwa makofi na kushangilia. Kulikuwepo na kundi la mashabiki wa Askofu ambao walikuwa wanakimbia kimbia pale chini ya jukwaa wakipulia vipenga kama watu walivyokuwa wanafanya wakati wa enzi za Mhubiri Moses Kulola.

Mkono wake wa kulia ukishikilia kipaza sauti Askofu Ndondo aligeuka macho yake yakimsindikiza Skola akielekea kwenye ngazi. Aliwataka watu wamshangilie Mungu kwa uimbaji mzuri wa Skola moyoni mwake hata hivyo akisia uumbaji alivyoumbwa Skola. Sauti ya Askofu ilipopaa kwenye maspika yaliyokuwa pale uwanjani, kelele za shangwe zililipuka watu waliokuwa na mapepo walianza kuanguka, nguvu fulani ya Kimungu ilitanda uwanjani; aliponyosha mkono wake juu na kurudia maneno yale ya “haleluya” huku akikimbia upande huu wa jukwaa na upande ule wa jukwaa karibu nusu ya watu wote waliokuwa wamesimama pande zile alizoelekezea mkono wake wa kushoto walirudi nyuma kama waliopulizwa na upepo mkali. Wakayumba na wengine wakianguka chini katika kile kilichoitwa ni upako. Askofu Mkuu Damien Ndondo alijitangaza kama mhubiri aliyekuwa na upako maradufu. Mwenyewe aliuita upako wa Eliya.

SURA YA TATU​

FELA NKASI ALIKUWA amefikia mwisho wa uwezo wake wote wa kujitahidi. Alikuwa amegota kwenye ukingo wa matumaini; kwenye ukuta wa kukata tamaa. Alijikuta akiyatafakari maisha yake yote na kuamua moyoni mwake kuwa hayakuwa na umaana wowote ule. Moyo wake ulikuwa mzito kwa majuto, huzuni, uchungu na kujiona duni. Katika maisha yake yote Fela hakuwahi kujua kitu kinachoitwa furaha.

Marafiki zake wengi walimuona kama ni mcheshi na mwenye furaha usoni lakini hawakupata nafasi ya kujua kilichokuwa moyoni mwake kwani hakuwa mtu anayefungua hisia zake kwa watu wa nje. Watu waliojaribu kumkaribia sana alitafuta namna ya kuwaweka mbali naye; mahusiano yake yote yalikuwa ni ya juu juu tu; hakujiachilia kuzama sana katika urafiki au mapenzi.

Fela alikuwa ni binti wa miaka ishirini na mitatu. Alikuwa ni mrefu kupita mabinti wengi na akivalia viatu vya mchuchumio aliwapita hata wanaume wengi. Alikuwa ni mweusi aliyeiva; alifanana kama watu wanaopatikana Sudan Kusini waitwao Wanubia. Kwa Tanzania weusi wake ulikuwa ni kama wa mabinti wa Kinyakyusa wanaotokea Mwakalelil Tukuyu, Mbeya. Alikuwa na midomo minene yenye rangi nyekundu ya asili. Akipaka rangi yoyote ya midomo inaendana naye na kuuongezea uso wake sifa. Macho yake makubwa na angavu yalikuwa ya rangi ya kahawia kibichi yakiwa yameumbwa kama kungu hivi. Alikuwa amejipaka wanja kama kawaida yake.

Hakuna mahali ambapo Fela alipita ambapo watu hawakugeuza shingo zao mara mbili kuthibitisha aliyewapita alikuwa ni binadamu na siyo malaika. Waliothubutu kurusha maneno ya mapenzi walirusha yale ya kusifia na wale ambao hawakuwa na ujasiri huo waligunia moyoni na kujiuguzia. Haikujalisha kama walikuwa ni wanawake au wanaume wote waligeuka kumwangalia ama kwa ajili ya tamaa, kumshukuru Mungu kwa uumbaji wake, au kwa wivu wa kutamani jinsi Fela alivyoumbwa. Alikuwa ni tishio kwa mabinti wengine mahali popote alipotokea.

Wenye waume zao au mabwana zao waliwabana kwa karibu wasiwaache wacheze karibu na Fela au kumzoea. Alikuwa ni miongoni mwa mabinti ambao walikuwa kwenye lile kundi la kipekee la wazuri wa kuzaliwa. Ingetokea Fela ametumbukia kwenye matope, akiwa hajajipodoa vyovyote vilevile, na akaibuka kuna watu bado wangepiga magoti kubusu kila hatua aliyopiga na kubusu kila tope lililodongoka ardhini kutoka viungo vya Fela; huku wakiapa kwa kila mzimu waliyemjua. Fela akipigwa na vumbi unaweza kusema kajipodoa. Sifa hizi nyingi watu waliosimuliwa hawakuamini; hadi walipokutana na Fela na midomo yao ikaachama na macho yakatumbua.

Fela alijua anao ule uzuri wa kuzaliwa na hakuacha kuutumia uzuri ule ipasavyo katika maisha yake. Alitumia uzuri wake kuepuka mazingira mbalimbali asiyoyataka na hata kupata nafasi mbalimbali alizozitaka. Mwaka mmoja nyuma alijaribu kuomba kazi mbalimbali, na kote alikoenda kufanyiwa usahili hakuna ambako alikataliwa kazi; tena alibembelezwa kukubali. Mwisho wa siku hakutaka kukaa ofisini kama mabinti wengine. Uzuri wa Fela haukuwa uzuri tu wa nje nje, uzuri wake ulisindikizwa na ucheshi na uchakaramu wa mjini.

Alikuwa ni binti aliyependa maneno ya mzaha na utani. Fela hakuwa binti mwenye majivuno hilo lilimtengenezea marafiki kwa haraka sana. Tabasamu lake liligeuza hasira kuwa kicheko na kicheko chake kilimfanya mtu mgonjwa ajisikie nafuu na kutamani kupona haraka. Jinsi alivyojua kutumia uzuri wake hasa kwa kumwangalia mtu ilikuwa ni balaa kwa aliyeangaliwa. Akikuangalia ukiwa amehuzunika utatamani umbembeleze kwa nyimbo na mapambo. Fela akikuangalia kwa hasira unaweza kujikuta unaomba msamaha kwa makosa hadi yale ya mababu zako na yale ya mababu wa mababu zao. Huyo alikuwa Fela binti wa pekee wa marehemu Mzee Nkasi.

Kwenye ulimwengu wa mapenzi yenye kuenzi na mahaba yasiyo na vibaba, Fela alikuwa ni moto uchomao, ule moto unaotajwa kwenye misemo kuwa ni wa kuotea mbali. Alikuwa ni moto uchomao na ukapendwa zaidi na wale wachomwao. Hakuna mwanamme aliyeweza kummiliki Fela na kudai kuwa ni wake peke yake katika mapenzi. Uzuri wake huo alikuwa anautumia vizuri kwelikweli mtoto wa kike; kama kuutumia huko kunaweza kuitwa ni kuzuri.

Wakati akiwa binti mdogo hajapevuka weusi wake na umbile lake halikuwa na mvuto wowote kwa yeyote. Alikuwa anaonekana kama mtoto wa kiume na alipenda kucheza nao. Mwili wake ulipoanza kuchukua umbo la kike, shingo, miguu, kiuno na kifua chake vilipoanza kutii amri ya Mungu ya uumbaji wa mwanamke Fela alianza kuumbika na kushtua mioyo ya watu. Mwendo wake ulibadilika na hatua zake zilianza kunesanesa. Mwanzoni hakuelewa kwanini alikuwa anaonekana anapata marafiki wengi, anasemehewa makosa mengi, na anabembelezwa kwa kila chozi alilotoa.

Walimu na wanafunzi pale shuleni walikuwa wanajibamiza kwake kitu ambacho alijua kinampa nguvu ambayo wanawake wachache walikuwa wanayo. Kuna wanawake ambao wanasifiwa kuwa ni wazuri; wapo wanaoambiwa ni wazuri; wapo ambao wanaamini ni wazuri na wapo ambao wanajijua ni wazuri. Lakini, pia wapo wanawake ambao wanasifiwa, wanaambiwa, wanaamini na wanajijua kuwa ni wazuri. Fela alikuwa ni mmojawapo wa wanawake kwenye kundi hilo dogo.

Fela alikuwa akiishi kwenye ghorofa ya kupanga ya NHC ambayo ilikuwa ni sehemu ya maghorofa makubwa matano maeneo ya Masaki karibu na maduka ya Slipway. Usiku huo kwa mara nyingine tena Fela alikuwa amegubikwa na dimbwi la huzuni; dimbwi lililokuwa kama wingu zito jeusi likiwa limetanda kwenye anga ya moyo wake likisubiri kunyesha mvua kali ya uchungu iliyoambatana na radi na ngurumo ya mateso yenye kutikisa kina cha mtima. Alikuwa amepanga sehemu yenye vyumba viwili, sebule kubwa na jiko la kisasa ambalo lilikuwa na meza ya wastani ya marumaru iliyokuwa kama mpaka na sebule. Meza ilikuwa imezungukwa na viti sita, vitatu vitatu upande na upande huu na kiti kimoja kimoja upande mwingine. Kulikuwa na makabati makubwa ya kuwekea vyombo ya rangi nyeuepe yalikuwa wamepamba kuta zake kuanzia upande lilipo jiko hadi upande wa kushoto ukipita sinki la maji. Ilikuwa ni miongoni mwa majengo ya kisasa ambayo yamekuwa yakijengwa katika jiji la Dar na sehemu nyingine nchini kwa ajili ya kupangishwa hasa kwa watu wenye kipato cha kati. Yalikuwepo maghorofa mengine katika miji mbalimbali ambayo yalikuwa ni kwa watu wenye kipato cha juu.

Ndani alikuwa amekupamba kwa vitu mbalimbali vya kifahari; kuanzia samani, TV kubwa ya nchi 55 ya Samsung huku akiwa na spika za kisasa za UBL. Fela mwenyewe na peke yake hakuwa na kazi wala kipato cha kumuwezesha kumudu pango hilo wala vitu vilivyomo mle ndani. Alikuwa amepangiwa hapo na Waziri mmoja mtu mzima ambaye alikuwa na mke na watoto sehemu nyingine pale pale Jijini Dar. Fela hakuwa nacho lakini alikuwa na wenye nacho na wale wenye nacho hawakuacha kuwa naye kwani naye alikuwa anacho wakitakacho.

Fela alikuwa amekaa kwenye kochi kubwa mbele ya televisheni yake huku ameshikilia glasi ya kinywaji kikali cha Whisky. Alikuwa amevaa kujiandaa kutoka kwenda kwenye starehe na kikundi cha mashosti wake kama wenyewe walivyoitana. Lilikuwa kundi la wasichana watano ambao walikuwa wanaishi mjini kijanjajanja. Walikuwa ni mabinti wasomi wa fani mbalimbali wakiwa wamehitimu vyuo vikuu vikubwa vitatu; Mlimani UDSM, Dodoma na Mzumbe.

Wasomi hao warembo hakuna hata mmoja aliyekuwa anafanya kazi ya alichokuwa amesomea. Hakuna hata aliyetaka kutafuta kazi ya kutaka kuajiriwa. Waliamua kuishi mjini kwa kutumia uchunaji. Walikuwa ni majemedari wa kuchuna na makamanda wa kuchanua. Na kuwachuna watu pale mjini mashosti wale sita walikuwa wanawachuna kwelikweli kama wenye akili mbovu. Siku hiyo hata hivyo Fela hakujisikia kabisa kutoka kwenda mahali popote; alikuwa amejiandaa ndiyo lakini moyoni alijisikia vibaya na hisia ya hatia ilikuwa imemng’ang’ania isimuachilie. Alijikuta akitamani kuachana maisha hayo ya kiujanja na kuishi maisha yenye heshima na furaha hata kama siyo ya kifahari kama aliyokuwa akiishi wakati ule.

Kilichokuwa kinamsumbua zaidi siku hiyo hata ilikuwa ni hisia iliyomjaa moyoni na kumfanya ajisikie duni, mchafu, aliyepotea na ambaye hakuwa na njia nyingine ya kuishi kwa furaha. Akiwa na miaka hiyo ishirini na mitatu tu Fela alikuwa ameshatoa mimba nne; mimba ya kwanza akiitoa akiwa na miaka kumi na sita tu, kidato cha tatu tena ya Mwalimu wake wa Kemia kule Iringa Girls. Mwalimu mwenyewe ndiye aliyempeleka kwa daktari ili kuhakikisha kuwa binti anaweza kuendelea na masomo na mwalimu anakwepa jela. Zoezi la kutoa mimba nusura limtoe roho Fela; aliponusurika alianza kujihisi kuhitimu mambo ya mapenzi.

Hilo la Iringa Girls lilikuwa ni mwendelezo wa matukio yaliyomkuta kuanzia akiwa kidato cha kwanza pale ambapo wazazi wake walipofariki kufuatia maambukizo ya HIV. Fela alikuwa mtoto wa pekee kwa kwa wazazi wake.Wote wawili walikuwa ni watumishi wa serikali – baba akiwa Kanali wa JWTZ akiongoza kambi ya Nyegezi na mamake akiwa Muuguzi Mwandamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Walikuwa wakiishi maeneo ya Isamilo ukipita maghorofa ya benki. Baba yake aliambukizwa kwanza na ndani ya mwaka mmoja wote wawili walikuwa wamekufa; alitangulia babake kisha mama akafuatia. Ingekuwa wakati wa watu kupewa dawa ARV, Fela alikuwa anaamini labda wazazi wake wangekuwa hai na maisha yake yasingegeuka yalivyogeuka.

Msiba wa babake yake uliivuruga kabisa familia yake na mahusiano na ndugu wa upande wa baba yake yalikoma kabisa Baada ya msiba wa mama yake alichukuliwa kuishi na mjomba wake mjini. Mjombaake alikuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Wakati wazazi wake wanafariki alikuwa ndio ameanza Mwanza Sekondari lakini baada ya msiba alipelekwa bweni kule Iringa Girls na mjomba.

Akiwa Iringa Girls Mzee Chakupewa mjombake Fela alianza kufunga safari za mara kwa mara kumjulia hali. Zilikuwa zinafanyika karibu kila mwezi. Safari hizi ziliambatana na zawadi nyingi ambazo hata mtoto wake mwenyewe Beatrice George Chakupewa, binamu yake na Fela aliyekuwa anasoma shule ile ile hakuzipata na kusababisha kuwepo kwa wivu mkali baina ya ndugu hao. Ilifika mahali hata kuzungumza hawazungumzi. Hazikuwa safari za kawaida kwani mara kwa mara Mzee Chakupewa alimchukua Fela na kwenda kumpa maisha Iringa mjini. Mazoea hayo yalianza kumfunga Fela katika mazoea mabaya kabisa ambayo hakudhania angeweza kuyaingia katika maisha yake. Mazoea ya mahusiano haramu ya kingono kati yake na mjombake. Hakujilaumu, wala kujutia; aliona kwa vile mzee anamhudumia basi alikuwa anastahili pia kupewa mwili wake.

Tukio kubwa kabisa hata hivyo ambalo lilimuumiza Fela na kumsumbua mawazoni mwake mara kwa mara halikuwa hilo la mahusiano na mjombaake kwani alishaachana naye alipomaliza shule na hakutaka kuendelea naye kwani alikuwa na watu wengine bora zaidi wa kuwachuna. Tukio lililomuumiza lilikuwa ni lile lililotokea siku ya mahafali ya kidato cha nne pale shuleni. Tukio ambalo lilimfanya moyo umuende mbio kila alipofikiria; lilimjaza hasira na hisia za kutaka kupaza sauti alie. Alipoanza kufikiria tena wakati ule amekaa machozi yalianza kumlenga, vinyweleo vya mwili vilisimama kama aliyepigwa na baridi ghafla na midomo yake ilimkauka. Hisia zake zilikuwa zimechanganyika kati ya hasira na huzuni, uchungu na aibu. Tukio lile liliacha alama isiyofutika katika moyo na maisha ya Fela labda kuliko tukio jingine lolote ukiondoa msiba wa wazazi wake.

Simu yake ya mkononi iliyokuwa mezani pembeni yake ilitetemeka na kuita huku ikirukaruka kama bisibisi zinazokaangwa. Fela aliona jina la mpigaji na hakushangaa kwani alikuwa anamsubiria; aliinyakua na kuitikia.

“Hey Girl, uko tayari shosti” ilikuwa sauti ya mmoja wa rafiki zake aliyeitwa Tina. Tina alikuwa na sauti ya juu sana kuliko watu wengi. Hata akinong’ona utadhani anapayuka na kwenye simu ndio ilikuwa kama kichaa kapewa spika. Fela ilibidi asogeze simu yake mbali kidogo na sikio lake kabla Tina hajampasua ngoma ya sikio.

“Aah, mmeshafika?” Fela aliuliza kwa sauti ya unyonge na uchovu kama mtu aliyezinduka toka usingizini.

“Eh, Vipi, uko Ok? Mbona unasound uko down sana?” Tina aliuliza sauti yake ikionesha hali ya wasiwasi. Fela aliweza kuficha hisia zake mara nyingi kwa kuwa mchangamfu karibu wakati wote. Hakutaka Tina aanza kumpekua.

“No, niko Ok bwana, nilipitiwa tu na usingizi hapa. Ngoja nije basi; give me a few minutes” Fela alisema huku akijilazimisha kunyanyuka kutoka kwenye kochi. Angekuwa na uwezo wa kuwatimua hao rafiki zake angewatimua ili abakie katika dimbwi lake la majonzi.

“Powa, fanya haraka basi” Tina alisema huku akitafuna Big G.

Fela alielekea bafuni kwa kujisuasua kujiangalia na kujipangusa machozi ambayo yalikuwa yamejikusanya machoni yakisubiri nyongeza ya uchungu ili yabubujike. Kwa haraka haraka alijipaka tena vipodozi na kupaka wanja vizuri tena kwenye nyusi zake pamoja na kubandika kope za bandia kama ilivyokuwa ada yake anapoenda kujirusha. Alipitisha tena rangi ya mdomo, na kuibana midomo yake ili kuisambaza vizuri. Uso wake uliokuwa wa mviringo kama ule wa yai la tausi ulikuwa umerembeka. Alijiangalia tena na kujiona yuko safi hasa kwa mida hiyo ya usiku; alikuwa amevaa gauni jekundu la kumetameta lililoishia kwenye magoti, mkononi akishika pochi nyekundu vile vile. Alikusanya vitu vyake alivyohitaji na kuchukua kiasi kikubwa cha hela mfukoni na kuamua kuondoka kuwafuata rafiki zake waliokuwa wakimsubiri kwenye gari kubwa la Nissan Armada la rangi nyeupe.

Alipowaona rafiki zake mawazo yake yote ya huzuni yalitoweka ghafla na lile wingu lililokuwa limeanza kutanda likayeyuka kama mvuke. Alirudisha uchangamfu wake wala marafiki zake hawakuhisi chochote. Wenzie nao walipomuona walimchangamsha kwa kumpigisha stori mbalimbali; stori za mambo yaliyowakuta tangu mara ya mwisho walipokuwa pamoja; wiki moja tu nyuma. Gari lilipoanza kuondoka pale ni vicheko na stori za mambo ya maisha na mabwana zao vilitawala ndani ya gari. Mabinti wale hakuwa wanajali kushea mabwana zao kwani hakuna ambaye alikuwa ni bwana wa kwao kweli. Kwa wao walikuwa ni wanaume tu wa kuwachuna na mtu akimchoka mwanamme mmoja anawashakizia wengine; mtu akikutana na kituko anawaambia wenzie ili nao wakakione. Tina alikanyaga mafuta kuelekea Club Paradise kwa ajili ya kujirusha na kula raha. Wote walikuwa wamevalia nguo ambazo ziliwafanya waonekane mabinti waliojaliwa kweli kweli, kama si kifua miguu, kama si kiuno nyuma. Hakuna aliyekuwa na uso wa changamoto.

Fela hakutaka kufikiria tena mambo yale yaliyowahi kumkuta; alitambua moyoni mwake kuwa wakati ni sasa na kula maisha ni sasa. Alijishangaa sijui ni kitu gani kilikuwa kimemuingia usiku ule hadi kumfanya afikirie kufanya kitu kibaya ili asije tena kusikia ile huzuni na aibu ambayo ilimkumba. Ilikuwa ni hisia mbaya sana. Alijiambia tena na tena kuwa yeye bado ni msichana mzuri, mrembo wa nguvu na ambaye amebahatika kutumia usichana wake vizuri kuweza kuwa na maisha mazuri tu. Maisha ambayo maelfu kama siyo mamilioni ya mabinti wangetamana kuyaishi hata kwa siku moja. Alisema moyoni kuwa yaliyopita si ndwele, bora agange yajayo. Kwamba, hakuna mtu anayeweza kubadilisha mambo yaliyowahi kumtokea, anaweza tu kubadilisha yale yanayoweza kumtokea. Fela alirudi na kuwa Fela tena.

Sauti nyingine ambayo ilikuwa inanong’ona usiku na mchana; sauti ambayo Fela hakutaka kuisikia kabisa katika maisha yake. Sauti ambayo ilikuwa kama inambembeleza kila siku kumtaka arudi katika maisha mazuri aliyolelewa na wazazi wake kabla ya vifo vyao. Sauti ile ilikuwa inazidi kufifia ndani ya moyo wake. Na katika kelele za ukumbi wa disco na vinywaji alivyokuwa akikata na marafiki zake Fela alijitahidi kwa nguvu kubwa kabisa kuizimisha sauti ile ya upole.

Na kwa masaa machache ya anasa na starehe alifanikiwa. Hakukumbuka kile kilichomtokea siku ya Mahafali ya Kidato cha Nne kule Iringa Girls miaka kadhaa iliyopita. Hakutaka kukikumbuka. Aliilinda siri hiyo ndani ya moyo wake na kuifungia kwa kufuli; na ufunguo akautupa; au aliamini ameutupa.
 
Afadhali; ngoja nami nirudi kwenye fani yangu pendwa ya utunzi manake dah!

Siku hizi huwa napata stimu za kuandika pale ninaposoma simulizi au kuangalia filamu ya kuvutia!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom