Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 27,103
- 65,407
RIPOTI YA MAMBO YANAYOENDELEA KATIKA SEKTA YA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI KWA MWAKA 2020
Muandaaji, Robert Heriel
UTANGULIZI
Imekuwa ni kawaida yangu kila mwisho wa mwaka kutoa Ripoti ya kile kinachojiri katika Sekta ya wafanyakazi wa ndani ili kuonyesha yanayoendelea humo, mapungufu na maboresho ambayo tumeweza kuyafanya na ambayo serikali inaweza kufanya kusudi kuondoa changamoto katika sekta hii.
Kwa vile mimi mwenyewe (mimi Taikon) ndiye najishughulisha na masuala haya hivyo ni rahisi kuelezea yaliyomo kwa mapana yake. Hivyo ni matumaini Ripoti hii itakuwa msaada mkubwa kwa taifa na jamii ikiwa mapendekezo yake na changamoto zilizomo ndani ya sekta hii zitafanyiwa kazi.
KAZI ZA MAJUMBANI NI NINI?
Kazi za majumbani ni shughuli zote zilizopo nyumbani kama vile usafi kwa aina zake, upishi kwa aina zake, Udobi kwa aina zake, utunzaji bustani kwa aina zake, ufugaji kwa aina zake na malezi kwa aina zake miongoni mwa kazi zingine za majumbani. Ninaposema kwa aina zake namaanisha kwa mgawanyo wake mathalani kwenye Usafi kuna Usafi wa nyumba, usafi wa vyombo, usafi wa eneo la nje,usafi wa vyombo vya usafiri. Au ninaposema Malezi kuna malezi au ungalizi wa mtoto au utunzaji wa watu wazima au wazee wasiojiweza. Nafikiri nimeeleweka na naweza kuendelea.
NANI NI WAFANYAKAZI?
Kwa uzoefu wangu hasa nikizingatia mwaka 2020. Wafanyakazi ni vijana wa umri katika ya miaka 18 mpaka miaka 50.
Wafanyakazi wa kike na wakiume wote wamekuwa wakiomba kazi hizi. Kimahesabu au kiutafiti naweza kusema hivi; Wafanyakazi wakike ndio wengi ambao wamekuwa wakiomba kazi hizi(wakiniomba) Yaani wakiomba kazi wafanyakazi kumi(10) basi nane watakuwa wakike (2) watakuwa wakiume. Kwan habari ya umri hesabu itakuwa kama ifuatavyo;
Kama wataomba kazi watu 100 basi mgawanyo wake ulikuwa hivi;
UMRI ELIMU IDADI ASILIMIA
18 - 22 STD 7 20 20%
18 - 22 Form iv 40 40% Jumla 60% ambao wanaumri kati ya 18 - 22
23 - 27 Std 7 9 9%
23 - 27 Form iv 20 20% Jumla 29% ambao wanaumri kati ya 23 - 27
28 - 32 Std 7 4 4%
28 - 32 Form iv 4 4% Jumla 8% ambao wanaumri wa kati ya 28 - 32
33+ Std 7 1 1%
33+ Form iv 1 1% Jumla 2% ambao umri ni 33 kuendelea
WENYE ELIMU YA KIDATO CHA SITA NA CHUO 1 1% Jumla 1% ambao wanaelimu kuanzia kidato cha sita, diploma na shahada
i. Wafanyakazi wakike ndio wanapewa kipaumbele zaidi kuliko wafanyakazi wa kiume, hii inafanya vijana wengi wanaoomba kulalamika kuwa wanabaguliwa katika kazi.
ii. Wafanyakazi wengi wametoka katika familia masikini sana. Kwa uchunguzi nilioufanya na bahati njema nipo kwenye field hii miaka zaidi ya minne. Wafanyakazi wengi zaidi ya 80% wanatokea familia masikini.
iii. Wafanyakazi wachache wanafanya kazi hii kwa sababu wamechoshwa kukaa nyumbani bila kazi, hivyo huondoka nyumbani ili kujitafutia maisha yao.
iv. Baadhi ya wanawake walioachika au kugombana na waume zao pia huomba kazi hizi kama sehemu ya kujishikiza hii huwafanya wengi kukaa muda mfupi kwenye kazi hali inayowafanya waajiri kukasirishwa na hivyo wengi waajiri hawapendi mtu aliyewahi kuolewa au mwenye mtoto
v. Wafanyakazi wenye watoto ambao wametelekezwa na Baba zao, wengi huomba kazi hasa za kwenda na kurudi ambazo hata hivyo ni chache ukilinganisha na za kulala kwa mwajiri. Na hata wakitaka waende na watoto wao waajiri wengi 99.9% hawataki wafanyakazi waje na mtoto.
vi. Wafanyakazi wengi hawataki kutoa taarifa zao ikiwa ni pamoja na barua za serikali za mitaa wanayotoka, hawataki kutoa namba za watu wao wa karibu, zaidi ya 75% wafanyakazi wa ndani ukiwaambia walete vielelezo vinavyowatambulisha hughairi kuomba kazi. Hali inayowafanya waonekane wanania mbaya.
vii. Wafanyakazi wengi hawataki uwasiliane na watu wa nyumbani kwao kabla hujampa kazi, wengi wanasema hawataki Wazazi wao wajue kuwa wanafanya kazi za ndani. 90% ya wafanyakazi hawataki.
viii. Wafanyakazi ambao tuliwapa kazi bila kuwa na nyaraka zao muhimu wote walitoroka kwa waajiri wao kama sio kuacha kabla ya mwezi kuisha.
ix. Wafanyakazi walioleta nyaraka muhimu za utambulisho na udhamini 80% walikuwa waaminifu, huku 20% wakivunja mkataba aidha kwa kutoroka au kuaga.
x. Wafanyakazi wengi zaidi ya 90% hawana uwezo wa kusema ukweli panapotokea matatizo licha ya kuwaambia kuwa tatizo likitokea waseme, au kila tunapowafuatilia kujua hali zao. Wengi huishia kusema wanaacha kazi au kutoroka kabisa. 10% ndio wanauwezo wa kujieleza na kusema ukweli.
xi. Wafanyakazi wengi 75% ndio wanawaonea na kuwanyanyasa mabosi wao kwa kuwafanyia vitendo vya uhalifu kama kuwalia nauli wanapotumiwa, au wakifika kazini hawakai hata mwezi, hii ni kutokana na kuwa hawatoi nauli. Nilipojaribu kuwauliza wanaishia kusema hawataki tuu kazi, lakini utashangaa mwezi unaofuata anakutafuta anahitaji kazi huku akiomba msamaha na kuahidi kufanya kwa uaminifu.
xii. Wafanyakazi wengi 60% niliowapa nafasi ya pili waliharibu zaidi, huku 40% wakiwa wamejirekebisha.
xiii. Wafanyakazi wengi hasa umri kuanzia 25+ Waliomba kazi za nje ya nchi kama Uarabuni, ulaya na Amerika. 70% walionyesha mapenzi yao kwa nchi za ulaya, Canada na USA. 25% walionyesha mapenzi yao kwa nchi za Asia hasa Dubai na Qatar. 5% Hawa walitaka nchi yoyote ile. Licha ya kuwaambia kuwa Nchi yetu Tanzania hairuhusu kwa sasa wafanyakazi wa ndani kwenda nchi za mbali na kuwaeleza kuwa mimi sihusiki na huduma hiyo bado walinisihi zaidi na zaidi huku wakiahidi kutoa hata chochote. 20% Walishawahi kufanya kazi nje ya nchi na wanauzoefu huo. Mbali na kuwa baadhi walikuwa kama maafisa upelelezi waliokuwa wakinipeleleza.
xiv. Wafanyakazi wengi hawapendi Kuwa na Mkataba hasa wale wasio waaminifu. Wengi hawana elimu ya mkataba hivyo hujikuta katika madhila endapo yatatokea
NANI WANAOWAAJIRI
Waajiri wapo wa aina mbalimbali kulingana na kazi zao na asili yao.
Kulingana na kazi zao wapo waajiri ambao ni watumishi wa umma kama vile waalimu, madaktari, wabunge, mahakimu, askari, wanajeshi, wahasibu miongoni kwa kada zingine. Hawa ndio wengi zaidi wanaohitaji wafanyakazi kuliko waajiri wowote wale.
Wapo pia wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wajasiriamali, wasanii, miongoni mwa wafanyakazi wengine.
Kulingana na Asili yao
Wapo waajiri wenye asili ya Kiafrika wanaotoka bara la Afrika na nje ya bara la Afrika
Wapo waajiri wenye asili ya Asia, ulaya, na Amerika wenye ngozi nyeupe
Kundi hili wapo wachache
I. Waajiri wengi huishi mjini kwenye majiji makubwa, sana sana Dar es salaam,Zanzibar, Arusha, Dodoma, Mwanza na Kilimanjaro
ii. Waajiri wengi hawapendi wafanyakazi wenye watoto au waliokwisha olewa. 99.9% Hawataki
iii. Mgawanyo wa idadi ya wanafamilia ya waajiri waliowengi ni watu watano kuendelea 55%, Wanafamilia watano kurudi chini 45%
iv. Waajiri wengi hupenda wafanyakazi kutoka vijijini na wasio na mambo mengi. 80% hupendelea
v. Wapo waajiri wenye asili ya kitanzania ambao wanaishi mataifa ya nje ambao pia huhitaji
vi. Waajiri wachache 30% ndio wanatabia za kunyanyasa, kudhalilisha, na kuwabagua wafanyakazi wa ndani, ila 70% wanaogopa kutokana na kuwa wafanyakazi wapo chini ya usimamizi wetu.
MISHAHARA YAO
Mishahara ya wafanyakazi ya ndani kwa mujibu wa utafiti wangu na hasa nikizingatia mwaka 2020.
Mishahara ya wafanyakazi wa ndani inatofautiana kwa kulingana na sababu kadhaa, naomba nizitaje.
Mosi, mishahara ya wafanyakazi wengi hasa wanaojitegemea huwa ni shilingi za kitanzania 50,000/= au pungufu ya hapo.
Pili, Mishahara ya wafanyakazi wa ndani walioajiriwa na waajiri watanzania asilimia 97% huwa chini ya laki moja.
Tatu, Mishahara ya wafanyakazi wa ndani walioajiriwa na waajiriwa na raia kutoka nje ya nchi 99% hulipwa zaidi ya 100,000 pungufu ya 200,000 hivyo 100,000<200,000
Nne, mishahara ya wafanyakazi waliochini ya mawakala(agency) kama ofisi yetu Housemaid agency kwa waajiri watanzania kima cha chini 80,000 kwa wageni wa nje kima cha chini 180,000
Hivyo vigezo hapa ni Asili ya muajiri, mfanyakazi anajitegemea au yupo chini ya ofisi au kampuni fulani.
Katika uchunguzi wangu wafanyakazi wengi wa majumbani 90% hulipwa 50,000/= au chini zaidi, sababu kubwa ni kuwa wengi wa waajiri vipato vyao ni duni, wachache wanaweza kuwa na vipato vikubwa lakini kwa vile mfanyakazi anajitegemea hana wa kumsimamia wala kumtetea basi huweza kumlipa 50,000 au pungufu ya hapo.
Wafanyakazi wengi wanaojitegemea wengi wajapo kuomba kazi hulalamika kucheleweshewa mishahara yao zaidi ya miezi miwili mpaka mitatu licha ya kuwa wanalipwa 50,000/=
MIKOA INAYOONGOZA KWA UHITAJI WA WAFANYAKAZI WA NDANI
1. Dar es salaam.
Huu ndio mkoa ambao unaongoza kwa uhitaji wa wafanyakazi wa ndani, nitaeleza sababu.
i. Wafanyakazi wengi hupenda kufanya kazi jijini Dar es salaam tofauti na mikoa mingine
ii. Kipato cha waajiri wa Dar es salaam ni kikubwa kwa wengi wao hivyo kulipa mishahara inayoanzia 80,000 ni rahisi tofauti na mikoa mingine.
iii. Kasumba kwa baadhi ya wafanyakazi
iv. Uwepo wa kazi nyingi hivyo wafanyakazi huamua vile watakavyo, anaweza akafanya kazi siku mbili akaacha kazi licha ya kuwa umemgharamia kutoka kijijini. Pia ni faida kwao kwani akifukuzwa kazi au kuvunjiwa haki zake ni rahisi kuondoka na kupata kazi zingine
2. ARUSHA
Hili ni jiji la pili lenye uhitaji mkubwa wa wafanyakazi wa ndani.
3. Dodoma
Kwa mwaka 2019 kurudi nyuma Dodoma haikuwa kwenye idadi ya mikoa inayoongoza kwa uhitaji wa wasaidizi wa kazi za ndani. Lakini mwaka 2020 mkoa wa Dodoma umefanya mapinduzi makubwa nafikiri sababu kubwa ni watumishi wa serikali wengi kuhamishiwa Dodoma kutokana na kuwa ni mji mkuu wa nchi na wa kiserikali.
4. Kilimanjaro
Huu ni mkoa wa nne kwa mujibu wa uchunguzi wangu na jinsi waajiri wanavyohitaji wasaidizi wa kazi. Mkoa huu waajiri wengi ni watu wazima waliostaafu utumishi wa Umma.
5. Zanzibar
Hii inashika nafasi ya tano kwa uhitaji kulingana na idadi ya wanaohitaji.
Kumbuka, mikoa mingi inahitaji sema uchumi wa watu wake ni duni hali inayopelekea kuwalipa wafanyakazi 50,000/= ambao ni mshahara mdogo. Hivyo mfanyakazi anaposikia Dar es salaam wenzake wanapewa mishahara kuanzia 80,000 au laki moja huamua kuacha.
UTAPELI KATIKA SEKTA HII
Kila kazi inautapeli wake lakini kwa kazi hii ndio kazi inayoongoza kwa utapeli.
Kuna aina tatu za utapeli katika kazi hii
1. Utapeli unaofanywa na Mfanyakazi
2. Utapeli unaofanywa na muajiri
3. Utapeli unaofanywa na madalali wasio na ofisi wala usajili.
UTAPELI WA WAFANYAKAZI
Watu wengi hawajui kuwa wafanyakazi wa ndani wengi wao ndio wanaowaonea Waajiri wao. Ukitaka kujua jambo hili bai nakuomba umuajiri mfanyakazi wa ndani utanielewa vizuri.
i. Mfanyakazi anaweza fanya utapeli wa namna nyingi kwa mwajiri wake, mathalani; Mfanyakazi anaweza kuomba atumiwe nauli kisha akishatumiwa akakataa kuja na nauli akakataa kuirudisha.
ii. Wafanyakazi wengine hutafuta nauli tuu ya kujia mjini, hivyo hujifanya anataka kazi na atakuwa mwaminifu lakini ajapo mjini/kazini atakaa siku mbili tatu kisha ataanza visa na mkasa kisha atataka aondoke arudi nyumbani, na kwa vile huwezi mlazimisha kufanya kazi ataondoka ukidhani amerudi kijijini kumbe yupo hapo hapo mjini.
iii. Mfanyakazi mwingine hudanganya kuwa amefiwa na Mama au Baba yake hivyo umpe nauli ya kurudi kwao, ataondoka na kupanda gari pale Ubungo kama utamsindikiza, akifika mbezi mwisho anashuka au kibaha. Baada ya siku za msiba kuisha utampigia simu atakudanganya kuwa umtumie nauli ya kurudi nawe utamtumia kumbe yupo hapo hapo Dar, Baadaye atakuambia ndugu wamemuambia akae na mzazi kwani hana wa kukaa naye. Kumbe keshapata kazi pengine au anaishi na kijana aliyemdanganya. Waajiri wengi wanalizwa na hawana pa kusemea.
iv. Wafanyakazi wengine wakishajua mwajiri ni mtoaji sana huwaambia ndugu au mtu wa kumtengeneza ajifanye ni Mzazi wake kuwa anaumwa, hivyo anahitaji pesa, hata binti asipokuja lakini akituma pesa kidogo itasaidia. Mwajiri anajikuta anatuma pesa kwa mtu asiyeumwa kumbe ni utapeli.
v. Kutokana na wengi kukataa kutoa taarifa zao hasa nyaraka, baadhi hutoroka na kuiba vitu vidogo vidogo kama mikufu na vito vya thamani ambavyo mpaka mwajiri aje agundue ameibiwa inachukua siku kadhaa. Wengi huiba pesa ambayo haitakufanya uende polisi kwani hawaibi pesa nyingi, huiba laki moja, mbili au elfu hamsini. Hivyo Mwajiri anapiga mahesabu gharama na muda wa kushughulika na mfanyakazi wake aliyemuibia anajikuta anasamehe kishongo upande.
UTAPELI WA WAAJIRI
Hawa kwa kiasi kikubwa kufanya utapeli ni nadra sana kwani wengi wanaanuani na makazi kama sio kazi za kudumu, ila wapo wanaofanya utapeli kama nitakavyoeleza hapa;
i. Kwa waajiri wa kwenda na kurudi, hutumia utapeli kwa mtindo huu, hutafuta mfanyakazi wa kwenda na kurudi. Huyo mfanyakazi atajitegemea kila kitu, kuanzia usafiri na chakula cha mchana. Ataingia kazini saa tatu asubuhi na kutoka saa kumi unusu jioni.
Mfanyakazi atafanyakazi kwa bidii atakapofikisha wiki, mwajiri atamuundia zengwe na kumfukuza kazi bila kumlipa chochote, wakati kamzalishia kwa siku saba. Mfanyakazi kwa vile hana mkataba au kwa kukosa wasimamizi anajikuta amedhulumiwa kama sio kutapeliwa, hii hufanyika zaidi kwa baadhi ya waajiri wa Dar es salaam. Mwajiri ataajiri mwingine hivyo hivyo.
ii. Waajiri wengi huwatapeli wasichana na kuanzisha mahusiano ya kingono, wakishapata wanachokitaka huunda zengwe na kuwafukuza ili kuepusha Mama mwenye familia asijue.
UTAPELI WA MADALALI WASIO NA OFISI WALA USAJILI
i. Baadhi ya madalali wa kazi za majumbani huwatapeli waajiri kwa kuwaletea wafanyakazi wa ndani kisha wakikaa mwezi mmoja huwaamisha kisiri na kuwapeleka sehemu nyingine. Huku wakijifanya hawahusiki na mchezo huo.
ii. Madalali wengine hujifanya kumtumia pesa ya nauli mfanyakazi kumbe hajatuma alafu anakuambia pesa imeliwa na mfanyakazi asiye mwaminifu.
KUOMBA KAZI ZA MAJUMBANI
Wafanyakazi wengi hawaoni umuhimu wa kuomba kazi kwa njia ya kiofisi kama kuandika barua na kuambatanisha vyeti. Hutaka kazi kienyeji na matokeo yake hufanya kazi kienyeji na hata kuacha wengi hupenda kuacha kazi kienyeji. 80% Hawataki kufuata utaratibu wa kuomba kazi kama zilivyokazi zinginge. Hii tosha inawafanya waidharau kazi wanayoenda kuifanya na wao wenyewe kudharaulika.
WAZAZI NA NDUGU WANA MTAZAMO GANI KUHUSU KAZI ZA NDANI?
Wazazi wengi 90% hawapendi watoto wao wafanye kazi za ndani, hii inapelekea watoto wao kudanganya kuwa wamepata kazi fulani ila sio kazi za ndani kwani wengi hukwepa kuzuiwa kufanya kazi hizo.
Sababu za kwa nini Wazazi hawataki,
Katika uchunguzi wangu nilibaini sababu kadhaa zinazopelekea wazazi kutoruhusu watoto wao wafanye kazi za ndani
i. Mishahara duni, wengi huona kazi za ndani kuwa inamishahara midogo tena ya manyanyaso. Hii ni kweli kwa sababu wafanyakazi wengi kama nilivyosema wengi hulipwa chini ya 50,000/=
ii. Matukio mabaya yatokeoayo katika sekta hii. Yapo baadhi ya matukio mabaya yatoeyo katika sekta hii kama vile kunyanyaswa, kupigwa, kufanyiwa ukatili na wakati mwingine mauaji. Hivyo wazazi wengi huona kumruhusu mtoto wake akafanye kazi hizo ni kumtoa kafara mtoto, Wazazi wengi hupenda mtoto akafanye kazi chini ya usimamizi maalumu wenye uhakika wa usalama.
Watu wengi huwadharau wafanyakazi wa ndani licha ya kuwa wengine wamelelewa na hao hao wafanyakazi wa ndani hii inapelekea sekta hii kuonekana sio kitu.
Pia baadhi ya watu huona kazi hii ni utumwa kwani ni ngumu lakini mshahara ni mdogo
MABORESHO NILIYOFANYA KUPUNGUZA CHANGAMOTO
i. Kuanzisha kozi na mafunzo ya kazi za ndani ili kuelimisha wafanyakazi umuhimu wa wao na kazi yao kwenye jamii
ii. Kupandisha mishahara yao kutoka 50,000 mwaka 2018 mpaka 70,000 mwaka 2019, na sasa kima cha chini ni 80,000 kwa wanaokaa hapo hapo. Lengo ni kuwa ifikapo 2024 kima cha chini kiwe 100,000.
iii. Kushirikiana na polisi katika kuhakikisha uhalifu katika sekta hii unadhibitiwa hasa kwa matapeli na wavunjifu wa sheria
iv. Kuwakatia bima ya afya wafanyakazi ile ya gharama nafuu
v. Kuishauri serikali namna bora ya kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani
vi. Kuwadhibiti baadhi ya waajiri ambao wanatabia za kunyanyasa wafanyakazi
vii Kuunda mikataba itakayolinda haki za wafanyakazi na waajiri wao, ila wafanyakazi hapa bado ni changamoto
viii. Tumeelimisha wazazi wengi na kuwaondoa hofu kuhusu usalama wa kazi hii kwa watoto wao
NINI SERIKALI IFANYE
i. Bima ya Afya ya gharama nafuu serikali iiangalie
ii. Serikali iweke utaratibu mzuri wa kusajili makampuni ya uwakala wa kazi za ndani
iii. Serikali ipitia maboresho ya mishahara ya wafanyakazi ya ndani angalau kima cha chini kiwe 100,000/= kwa wanalala. Wanaoenda na kurudi iwe 150,000/= kima cha chini.
iv. Serikali iangalie namna bora ya kuruhusu watu wenye nia ya dhati na wenye mitaji kutoa huduma za housemaid nchi za nje. Utaratibu uhusishe wazoefu, ili kuepuka madhara na wahalifu wa Human Trafficking
v. Serikali ijue umuhimu wa agency wa kazi hizi kwani zinasaidia katika kusimamia haki za wafanyakazi na waajiri wao katika kiwango cha chini na cha kati, hii ni kutokana na kuwa serikali haiwezi kufuatilia kila kitu.
Kutokana na wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana lazima hatua mbalimbali zichukuliwe. Nimeshuhudia makumi ya wanachuo wa ngazi ya shahada wakituma maombi katika kazi za majumbani. Wengi wakiomba nafasi hata za laki moja, jambo hili linaweza kuwa fursa kama serikali itawaachia vijana wabunifu kutengeneza mifumo itakayoajiri watu wengi. Lakini sharti lazima maslahi mazuri ya wafanyakazi yazingatiwe.
Vijana wafundishwe namna bora ya kujiajiri bila kuhofia ikiwa hawatavunja sheria. Uchunguzi wangu unaonyesha kuwa vijana wengi wanapenda kujiajiri lakini wanahofu ya kuanza kwani wengi hawana vipato vya kulipa kodi iwe za TRA au manispaa. Napendekeza, uundwe utaratibu maalumu wa vijana wanaotaka kujiajiri wapewe Grace period ya miaka mitatu ndipo waanze kulipa kodi. Wajisajili kisha wapewe kibali maalumu cha kufungua ofisi wazitakazo, nafahamu serikali haiwezi kutoa mkopo kwa kila Kijana hivyo mbinu hii itasaidia.
Mwisho niipongeze serikali ya awamu ya Tano, mahususi Mhe. Rais, Dkt John Pombe Maagufuli kwa kuweza kujitahidi kutatua baadhi ya changamoto muhimu katika taifa letu. Kwa kazi zangu za kuzunguka zunguka nimeona mambo makubwa aliyoyafanya Mhe. Rais. Safi sana.
Ripoti hii imeandaliwa na;
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Mchunguzi huru