Nikiri kwamba huyu Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ameanza kunitia wasi wasi kuhusu baadhi ya maamuzi yake anayochukua.
Kwa mfano, katika hili la kumpa zawadi ya sh milioni moja askari atakayepambana na kulishinda jambazi, ni jambo la hatari sana tena sana. Maana ili ulishinde jambazi mara nyingi lazima ulipige risasi na uliue na ukiliua ushahidi mwingi utakuwa umejificha.
Kama kila kona kumekuwa na shutuma za askari wetu kuwabambikiza raia kesi za mauaji ili kujipatia hongo au kumkomoa mtu, hivi kwa kuahidiwa milioni moja watashindwaje kuwapiga risasi waendesha boda boda au mtu mwingine yeyote na kusingizia kwamba ni jambazi lililokuwa linawakimbia, maiti inaambatanishwa na gobole lililopatikana katika tukio jingine ili mradi tu kuipata hiyo milioni moja. Vinginevyo tukubaliane kwamba sasa Dsm imeruhusiwa yafanywe mauaji ya holela.
Nilidhani, kwa mawazo yangu kwamba kamanda Simon Sirro kwa uzoefu wake badala ya kukubaliana kirahisi rahisi na wazo hili la Makonda ambaye hana uzoefu na mambo haya alitakiwa kuiona hatari hii na kumshauri mapema.
Suala la polisi kupambana na kulishinda jambazi ni moja ya majukumu ya kazi yake na kitendo kinacholiongezea jeshi la polisi na askari husika sifa, si kitendo cha kuahidiwa zawadi.
Ningekubaliana na jambo hili kama zawadi hiyo angetangaziwa raia anayetoa taarifa kwa siri inayosaidia kukamatwa jambazi badala ya askari anayelishinda jambazi, tafsiri ya kushinda hapa ikiwa ni kuua.
Nashauri wasaidizi wa Rais, watu wa Usalama au mheshimiwa Rais mwenyewe walipime jambo hili na wampe maelekezo yaliyo salama zaidi mkuu wa mkoa badala ya kubaki kama lilivyo.