Thabit Madai
Member
- Oct 8, 2024
- 52
- 138
NA THABIT MADAI, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba, Serikali itaendelea kukuza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji pamoja na kuweka mkazo wa kurahisisha michakato, kuimarisha mifumo ya udhibiti na kutoa motisha za kuvutia uwekezaji nchini.*
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipofungua maonesho ya Utalii na Uwekezaji Zanzibar, 2024 huko viwanja vya maonesho ya Biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa kupongeza mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya nane anayoiongoza.
Amesema, Zanzibar imefungua milango wazi kwa fursa za biashara na uwekezaji na tayari imewakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nao kwenye maono ya ukuaji wa Uchumi endelevu na ustawi wa utalii wa muda mrefu.
Amesema, maonesho hayo yamedhihirisha thamani ya ushirikiano baina ya wadau wa utalii nchini, Sekta ya Umma na Kibinafsi (PPP) na kueleza kuwa ushirikiano wao ni njia muhimu za kufikia malengo ya pamoja.
Rais Dk. Mwinyi aliwashauri wadau wa Utalii kuendeleza utamaduni na shauku ya kufanya Maonesho ya Utalii na Uwekezaji si kwa mnasaba wa Zanzibar pekee bali kwa Afrika Mashariki na medani za kimataifa ili kuendelea kuitangaza nchi na vivutio vyake duniani kote.
Alisema, hatua hiyo itaiwezesha Zanzibar kuwa kituo bora cha ushindani kwa utalii kwenye ramani ya dunia.
Pia, Dk. Mwinyi amesema maonesho hayo ni fursa nzuri za kubadilishana uzoefu, kuweka harambee, misingi ya miradi ya kuleta mabadiliko kwenye sekta ya utalii nchini na kuwahimiza wadau wa utalii kushiriki kikamilifu na kuchangia katika kuunda mustakabali wa utalii na uwekezaji Zanzibar.
Ameeleza kuwa maonyesho hayo yanaashiria mwanzo wa mashirikiano mapya na wa kudumu na ubunifu tu sio dhamira ya utalii na uwekezaji peke bali ari ya pamoja ya kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa kinara wa ukuaji endelevu, uhifadhi wa utamaduni na maendeleo ya kiuchumi.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi amesema Sekta ya utalii licha ya kuwa ni utii wa mgongo wa pato la Uchumi wa nchi lakini, inaakisi nadharia nzima ya maisha ya Wazanzibari, elimu kwa vizazi vilivyopo pamoja na kuhifadhi utamaduni wa utambulisho wa taifa.
Dk. Mwinyi alibainisha kwamba faida za utalii na uwekezaji zinufaishe visiwa vyote vya Unguja na Pemba kwa kutengeneza fursa kwa watu wote.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amepongeza juhudi za Maendeleo zinazofanywa na Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopo kwenye sekta ya Utalii ni kazi kubwa inayofanywa Dk. Mwinyi.
Aidha, amelielezea miaka minne ya mafaniko kwenye uongozi wa Dk. Mwinyi imeakisi maendeleo enedelevu ya Sekta ya utalii na kukuza biashara na uwekezaji nchini.
Maonesho hayo ya Utalii na uwekezaji Zanzibar, 2024 yameandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kamisheni ya Utalii, na sekta binafsi.
Katika hafla hiyo pia kulisainiwa makubaliano ya Ushirikiano baina ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji na vitega Uchumi, ZIPA katika kuendeleza kazi za utalii na kurahisisha uwekezaji kwa kuendeleza vivutio vipya kwa maeneo ya utalii nchini na makubaliano baina ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Baraza la Sanaa Zanzibar katika kuondosha changamoto zinazotokana na utalii, hususan eneo muziki, sana ana burudani.