RAIA wa Kenya, Stanley Mwaura (38), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka 58, yakiwamo kughushi, kijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa Sh. milioni 805.3
Mwaura alisomewa mashtaka yake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi.
Wakili wa Serikali Simon Wankyo, alidai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 28 ya kughushi na mengine kama hayo ya kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa katika Benki ya Azania na kujipatia fedha hizo.
Alidai kuwa katika shtaka la kwanza, Mei 7, mwaka jana, alighushi hundi ya tarehe hiyo yenye thamani ya Sh. milioni 9.8 akionyesha kuwa ilitiwa saini na Ahmad Zacharia na Vida Zacharia.
Ilidaiwa katika mashtaka 27 katika tarehe tofauti mshtakiwa alighushi hundi akionyesha zimetiwa saini na Ahmad Zacharia na Vida Zacharia zenye viwango tofauti vya fehda. Katika shtaka lingine, Mei 7, mwaka 2015, mshtakiwa anadaiwa kwa nia ya kudanganya aliwasilisha hundi ya Sh. Milioni 9.8 katika benki ya Azania.
Aidha ilidaiwa katika mashtaka mengine 27 kwa nia ya kudanganya aliwasilisha hundi zenye viwango tofauti vya fedha katika benki ya Azania. Katika shtaka la 57, ilidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2013 na Mei 31, mwaka huu, mshtakiwa alijipatia Sh. 805,358,880.50 kutoka benki ya Azania kwa kudanganya kuwa fedha hizo zilikuwa malipo ya kampuni ya Professional Paint Centre Ltd kwenda Stano Enterprises kwa ajili ya kusambaza kazi.
Katika shtaka la mwisho, mshtakiwa anadaiwa kufanya utakatishaji wa fedha haramu kutoka kwenye akaunti ya Kampuni ya Professional Paint Centre Ltd iliyopo benki ya Azam zilizotokana na kughushi.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika. Hata hivyo kwa kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha haina dhamana kwa mujibu wa sheria ya makosa hayo, mshtakiwa alirudishwa rumande hadi Juni 20, mwaka huu.
Source: IPP