Pfizer
JF-Expert Member
- Mar 25, 2021
- 532
- 753
Bandari Kavu ya Kwala iko katika eneo la Vigwaza Wilayani Kibaha-Mkoa wa Pwani, kilomita 15.5 kutoka barabara kuu ya Morogoro kwa kutokea katika Mzani wa Vigwaza na kilomita 105.5 kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi kufika katika Bandari Kavu hiyo. Bandari Kavu ya Kwala hii iko katika eneo la ukubwa wa Hekta 502 na kati ya hizo Hekta 120 tayari zimesafishwa, Hekta 60 zimesawazishwa na Hekta 5 zimejengwa kwa kiwango cha zege. Eneo lililowekewa uzio wenye urefu wa Kilomita 2.96 lina jumla ya Hekta 60 ambazo ndizo zimeanza kujengwa miundombinu ya Bandari Kavu kwa awamu ya kwanza.Changamoto Zilizokuwa Zinaikabili Bandari ya Dar es Salaam
Moja ya changamoto kubwa zilizokuwa zinaikabili Bandari ya Dar es Salaam kuanzia miaka ya 2008 ni msongamano wa meli uliotokana na mrundikano wa Shehena katika Bandari ya Dar es salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na wadau wa Bandari ikiwa ni pamoja na SUMATRA (sasa TASAC) na Wizara ya Miundombinu (kwa sasa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi) walichukua hatua mbalimbali za kupunguza tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Bandari Kavu (Inland Container Depots – ICDs).
Mchango wa Kamati ya Kuboresha Ufanisi wa Bandari ya DSM
Mnamo mwaka 2010, TPA pamoja na Wadau wa Bandari wanaounganishwa kupitia Kamati ya Kuboresha Ufanisi wa Bandari (Port Improvement Committee (PIC)) ambayo hujadili na kutoa maamuzi mbalimbali yanayosaidia uboreshaji wa utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam, walipanua wigo kwa kuanzisha “Car Freight Stations” (CFSs) kwa ajili ya shehena ya magari. Sababu kubwa ya kuanzishwa kwa ICDs na CFS ni pamoja na kupunguza msongamano wa meli bandarini, kuondoa mrundikano wa shehena bandarini, kuharakisha utoaji wa shehena bandarini na kuhudumia meli kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Uwezo mdogo wa Bandari Kavu Zilizokuwepo (ICDs)
Katika Jiji la DSM kulikuwa na jumla ya Bandari Kavu (ICDs) 11 zenye uwezo wa kuhifadhi kontena 24,300 kwa vipimo vya TEUs kwa wakati mmoja. Kati ya hizo, kulikuwa pia na Bandari Kavu (CFS) 9 zenye uwezo wa kuhifahi jumla ya magari 19,100 kwa wakati mmoja, ambazo zilionekana kutokidhi mahitaji makubwa kwa wakati huo na baadae.
Umiliki wa Eneo la Bandari Kavu ya KwalaSerikali kupitia TPA imeamua kujenga Bandari Kavu eneo la Kwala “Quarantine” Ruvu. Katika awamu ya kwanza, Hekta 502 zimetwaliwa na TPA ikiwa ni sehemu ya Hekta 52,000 ya eneo linalomilikiwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambapo kihistoria, eneo hili lilikuwa chini ya usimamizi wa “Tanzania Livestock, Marketing Company (TLMC) na baadaye kuwa chini ya Tanzania, Livestock Marketing Project (TLMP).
Shughuli kuu zilizokuwa zikifanywa katika eneo hili ni pamoja na kuhifadhi mifugo kwa muda mfupi (Holding ground), iliyokuwa ikisafirishwa kutoka maeneo ya bara kwa njia ya reli kwenda mikoa ya DSM, Mtwara, Lindi na mingine; kusafirishwa nje ya nchi hususan Kusini mwa Bara la Afrika kwa ajili ya kusaidia harakati za Ukombozi. Kwa sasa ni sehemu ndogo tu ya eneo hili ambayo bado inaendelea kutumiwa kama “holding ground” na kituo cha mauzo ya mifugo kwenda nje ya nchi, hususan visiwa vya Comoro na Shelisheli.
Eneo la Bandari ya Kwala lilitolewa na Serikali kwa TPA ili kuendeleza miundombinu ya Bandari Kavu ikiwemo Yadi, Majengo, Barabara na Reli zinazounganisha Bandari hiyo na reli za TRC na barabara kuu ya Morogoro. Bandari ya Kwala ipo karibu na stesheni za Msuwa na Ruvu kwa reli (SGR na MGR) za TRC. Mchoro ufuatao unaonesha Eneo la Kwala.
Sababu za Ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala
Uamuzi wa kujenga Bandari Kavu ya Kwala unatokana na sababu kuu zifuatazo:
Kiufundi na Kiuchumi
Eneo la Ruvu liko karibu na miundombinu ya barabara kuu inayounganisha nchi jirani za Burundi, Rwanda, DR Congo, Malawi, Zambia na Uganda; zinazotumia Bandari ya DSM na reli. Aidha, katika siku za usoni, eneo hili litaweza kuunganishwa kiurahisi na barabara ya Chalinze – Dar es Salaam “Express Highway”. Vilevile eneo la Kwala ni tambarare na hivyo gharama za ujenzi wa Bandari Kavu la Kwala zinatarajiwa kuwa nafuu.
Kijamii
Eneo la Kwala linamilikiwa na Serikali na hivyo halikuhitaji fidia ili kupisha mradi jambo ambalo mara nyingi huambatana na migogoro na athari mbalimbali za kijamii.
Mpango wa Utekelezaji wa Mradi
Utekelezaji wa Ujenzi wa mradi wa Bandari Kavu ya Kwala umegawanyika katika Awamu mbili (2), zenye jumla ya gharama ya TZS: 88,849,938,598.95. Kama inavyooneshwa kwenye Jedwali namba 2 hapa chini.
Jedwali Na.2: Awamu na Gharama za Mradi wa Bandari Kavu ya Kwala
Awamu | Aina ya kazi za kutekeleza | Gharama (TZS) |
1 | Kusafisha eneo Hekta 60 na Ujenzi wa Ukuta | 9,465,643,798.00 |
2 | Ujenzi wa Yadi hekta 5 kiwango cha Zege | 39,213,592,863.58 |
Ujenzi wa Reli Mchepuko (1.3 Km) | 1,365,132,380.00 | |
Barabara 15.5 Km Kiwango cha Zege | 38,805,569,557.37 | |
JUMLA | 88,849,938,598.95 |
4.1.1 Awamu ya Kwanza
Awamu ya Kwanza ilihusisha kusafisha eneo lenye ukubwa wa Hekta 60 ambalo liligharimu kiasi cha TZS:9,465,643,798.00, ikijumuisha malipo ya VAT kwa TRA ya asilimia 18. Awamu hii ilianza kutekelezwa mwezi Februari 2017 na kukamilishwa mwezi Desemba 2017. Kazi hiyo zilitekelezwa na Kampuni ya SUMAJKT Construction Company Limited.
4.1.2 Awamu ya Pili
Awamu ya Pili ilihusisha Ujenzi wa Yadi yenye ukubwa wa Hekta 5 kiwango cha Zege, Ujenzi wa Barabara yenye urefu wa 15.5 Km kwa Kiwango cha Zege pamoja na Ujenzi wa Reli Mchepuko yenye urefu wa 1.3 Km, kama ifuatavyo: -
Ujenzi wa Yadi Hekta 5 kiwango cha Zege
Kazi hii ilihusisha ujenzi wa eneo la Hekta 5 za Yadi ya Bandari Kavu kwa kiwango cha Zege na ulitekelezwa na Kampuni ya SUMAJKT Construction Company Limited, kwa gharama za TZS: 39,213,592,863.58. Mradi huu ulianza mwezi June, 2019 na ilipangwa kukamilika mwezi Oktoba 2019. Baada ya Mkandarasi kutokamilisha kazi za Mkataba katika muda uliopangwa, TPA iliingia mkataba mpya ulionza mwezi Agosti 2022 na ulikamilika tarehe 07 Julai 2023, mpaka sasa utekelezaji wa mradi huu umekamilika.
Barabara 15.5 Km Kiwango cha Zege
Ujenzi wa barabara hii yenye urefu wa kilomita 15.5 na upana wa njia mbili kutoka Vigwaza mpaka Bandari ya Kwala-Ruvu, unatekelezwa na Mkandarasi Estim Construction Ltd, akisimamiwa na TANROADS chini ya Mhandisi Mshauri Tanroads Engineering Consulting Unit (TECU). Gharama ya mradi huu hadi kufikia sasa ni TZS:38,805,569,557.37 ikijumuisha VAT. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 07.10.2020, Muda wa mkataba wa awali ulikuwa miezi 12, kutokana na changamoto zilizojitokeza kipindi cha utekelezaji (baadhi ya wananchi kukataa kupisha mradi wakidai fidia, kuongezeka kwa kazi mfano Round about zilisababisha mkandarasi kuongezewa muda hadi 07th Desemba 2022. Hadi sasa mradi umekamilika kwa asilimia 100.
Ujenzi wa Reli Mchepuko (1.3 Km)
Ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ulihusisha ujenzi wa reli mchepuko (rial siding) kutoka Stesheni ya TRC Kwala hadi Bandari Kavu ya Kwala. Makubaliano kati ya TPA na Shirika la Reli Tanzania (TRC) yaliingiwa 18th Agosti, 2017 kwa ujenzi wa reli yenye urefu wa Kilomita 1.3. kwa gharama ya TZS: 1,766,626,180.00 kwa mchanganuo ufuatao (TRC kuchangia TZS: 401,493,800.00 na TPA kuchangia TZS: 1,365,132,380.00).
SHEHENA INAYOTARAJIWA KUHUDUMIWA KATIKA BANDARI KAVU YA KWALA
Bandari ya Kwala inayotarajiwa kuhudumia shehena ya makasha yanayokwenda nchi jirani, inakadiriwa kuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 823 kwa siku, na hivyo kuifanya Bandari hiyo kuhudumia hadi makasha 300,395 kwa mwaka; sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayohudumiwa na Bandari ya DSM kwa sasa.
UTAYARI WA BANDARI KAVU YA KWALA KATIKA KUHUDUMIA SHEHENA
Katika kuhakikisha kuwa, Bandari Kavu ya Kwala inakuwa tayari kutoa huduma kwa shehena mbalimbali, TPA imefanikiwa kupata leseni ya Bandari Kavu inayotolewa na Mdhibiti wa Usafiri Majini, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania na Leseni ya Forodha inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa sasa, Bandari Kavu ya Kwala inafanya kazi na takwimu mpaka tarehe 10 Februari 2024 kuna jumla ya makasha 232 yenye mzigo na makasha matupu 78 yaliyokuwa yamekaa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa zaidi ya siku hamsini (50) yalihamishiwa katika Bandari Kavu ya Kwala na zaidi ya makasha 100 yameshaondolewa kwa kuchukuliwa na wateja Aidha, taratibu za kuhamisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kwala zinaendelea.
MANUFAA YA KUANZA KWA SHUGHULI KATIKA BANDARI KAVU YA KWALA
Faida zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ni pamoja na zifuatazo;
Kuongeza ufanisi na kiasi cha shehena inayohudumiwa katika Bandari ya DSM;
Kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia huduma zitolewazo katika Bandari za DSM na Kwala;
Itapunguza gharama za uendeshaji hivyo kuvutia wateja kutumia Bandari ya DSM;
Kuongeza ushindani wa Bandari ya DSM kikanda ukizingatia uwekezaji wa Bandari za nchi jirani katika Bandari Kavu;
Kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na biashara za mikoa ya DSM na Pwani kwa kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa;
Kuimarishwa kwa usalama barabarani kwa kuwa idadi kubwa ya shehena ya Bandari ya DSM kutumia usafiri wa reli;
Maisha marefu ya miundombinu ya barabara za mikoa ya DSM na Pwani;
Utaongeza ajira kwa wakazi wanaoizunguka Bandari Kavu ya Kwala na Taifa kwa ujumla; na
Ongezeko la viwanda katika eneo la Kwala vitakavyovutiwa na uwepo wa Bandari Kavu na usafiri wa uhakika kuelekea lango kuu la biashara nchini-Bandari ya DSM.
VIVUTIO VYA BIASHARA KATIKA BANDARI KAVU YA KWALA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imeainisha vivutio vya wafanya biasha ili waweze kutumia Bandari Kavu ya Kwala ambapo ni pamoja na:
Kuongeza siku za msamaha za gharama za kuhifadhi mzigo (Storage) kutoka siku 7 kwa mizigo ya ndani ya nchi hadi siku 30. Aidha, kwa upande wa mizigo ya nje ya nchi (transit cargo) siku zimeongezwa kutoka siku 15 kwa sasa hadi kufikia siku 60.
Gharama za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya Reli ya TRC kutoka mizigo yao Kwala ambapo kiasi cha USD 125 kwa kasha la 20ft imekubalika.
Punguzo kwa gharama za kupakia mizigo kwenye kasha (Staffing) kutoka USD 70 hadi kufikia USD 65 kwa kasha la futi 20. Kwa upande wa kasha la futi 40 gharama zimepunguzwa kutoka USD 140 hadi USD 130. Aidha, gharama nyingine zilizopunguzwa ni katika ‘lift on na lift off’ na ‘extra movement’.
MAOMBI YA WADAU WA NJE KUENDELEZA MIUNDOMBINU YA BANDARI KAVU
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania katika nyakati tofauti imekuwa ikipokea maombi na maelekezo mbalimbali ya Serikali kwa ajili ya ugawaji wa ardhi ya Kwala kwa ajili ya kuhudumia nchi Jirani. Mpaka sasa tayari ardhi Hekta 100 zimegawiwa kwa nchi 8 ambazo zinapata huduma kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Vilevile, TPA imeendelea kupokea maombi kutoka kwa Wafanyabiashara mbalimbali wakitaka kukodishwa ardhi kwa ajili ya uanzishaji na kuendesha Bandari Kavu ya Kwala. Mpaka sasa Kampuni mbili (2) zimeomba kuendesha bandari Kavu na Kampuni zaidi ya tano (9) zimeomba kuokdishwa ardhi wastani wa hekta 5 kila moja kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Bandari Kavu. Maombi hayo yote kwa sasa yanafanyiwa kazi.
HITIMISHO
Bandari Kavu ya Kwala inatarajiwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio lango kuu la kibiashara nchini. Manufaa mtambuka ya Bandari Kavu ya Kwala kama vile kupunguza msongamano wa Malori na mizigo Bandarini yatapelekea Tanzania kufunguka kiuchumi hivyo, ushirikiano na wadau wote ni muhimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.