PSSSF: Wastaafu wanachelewa kupata Mafao kwa kuchelewesha uwasilishaji wa taarifa zao za kustaafu

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
1,137
1,958
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema wastaafu wengi wanachelewa kupata mafao yao kutokana na kuchelewesha taarifa zao za kustaafu miezi sita kabla.

Pia, umesema kuwa hakuna watumishi wanaowafanyia mpango wastaafu wengine kupata mafao mapema badala yake uwahishaji wa taarifa zao ndio unawasaidia kupata stahiki zao haraka.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 6, 2022 na Meneja wa PSSSF Temeke, Rajabu Kinande katika mkutano mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari cha Dar es Salaam (DCPC).

“Watumishi wanaokaribia kustaafu hupata barua zao miezi sita kabla ya tarehe ya kustaafu,” anasema Kinande.

Anabainisha kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, mtumishi anatakiwa kuanza kufuatilia mafao yake kwa kupeleka taarifa zote muhimu katika ofisi hizo ili zianze kufanyiwa kazi ikiwemo kufuatilia kama waajiri wamechangia miezi yote kama inavyotakiwa na sheria.

“Unajua asilimia kubwa ya wastaafu huanza kufuatilia mafao yao baada ya kustaafu na barua alishaipata miezi sita kabla, jambo hili linawafanya kuchelewa kupata mafao yao,” anasema Kinande na kuongeza:

“Wapo wanaochelewa hata kurudisha fomu wanazotakiwa kujaza baada ya kustaafu sasa, akiona mwenzake amepata mafao mapema kabla yake anasema wamefanyiwa ‘michongo’ hii si kweli.”

Katika hatua nyingine, Kinande amesema mfuko huo pia una huduma za kidigitali ambazo zinatoa fursa kwa wanachama, wastaafu na waajiri kutumia mifumo hiyo kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma bila kufika ofisini.

Amesema kila mwaka mfuko huo hufanya uhakiki wa wastaafu na wategemezi wanaopata pensheni kwa lengo la kusafisha daftari la wastaafu na kuhakikisha pensheni inalipwa kwa walengwa na si vinginevyo.

“Niwatake waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya watumishi wao kwa wakati ili kuepuka tozo ya ucheleweshaji wakati wa kulipa mafao kwa wanachama" anasema na kuongeza.

“Ili kupunguza malalamiko ni vyema waajiri kutimiza wajibu wao kisheria wa kulipa michango ya watumishi wake ndani ya mwezi mmoja baada ya mwisho wa mwezi husika. Kwa sasa mwajiri ana uwezo wa kutengeneza namba za kumbukumbu ya malipo itakayomuwezesha kulipa michango na kupata risiti kupitia mtandao,” alieleza.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom