Profesa Ndalichako alilia Serikali mambo manne jimbo la Kasulu Mjini

peno hasegawa

JF-Expert Member
Feb 24, 2016
14,253
23,937
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako ameiomba Serikali kutatua changamoto ya maji, barabara, umeme na upatikanaji wa mbolea jimboni kwake.

Mwanza. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako ameiomba Serikali kutatua changamoto ya maji, barabara, umeme na upatikanaji wa mbolea jimboni kwake.

Akitoa salamu zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Oktoba17, 2022 wakati wa ufunguzi wa barabara ya Kidahwe- Kasulu na uwekaji jiwe la msingi barabara ya Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo, Profesa Ndalichako licha ya kuishukuru Serikali ameiomba itoe kipaumbele kwa barabara za Kasulu.

“Kwenye barabara niombe sana pamoja na shukrani ninazo zitoa lakini kwenye kazi ya barabara bado sana.

Ukienda kwenye Kata ya Muhunga wakati wa mvua hakupitiki kabisa, tuombe suala la barabara katika mji wa Kasulu lipewe kipaumbele

“Barabara za kuunganisha Kata na Kata za Mitaani bado ni changamoto kubwa. Barabara nyingi hazina makalavati wakati wa mvua inakuwa ni adha kubwa, huwezi kuamini sehemu nyingine mitaani wananchi wanapanda mipunga kwenye barabara kwasababu hakuna njia ya maji kwenda,” amesema.

Kuhusu Maji, Ndalichako amesema licha ya kupatikana kwa wingi baada ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango kumuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuchimba visima lakini usambazaji bado haujakamilia.

“Niombe sana usambazaji wa maji ukamilike ili wananchi waweze kunufaika, visima vimechimbwa tangu Septemba mwaka jana mpaka leo wananchi hawajasambaziwa maji,” amesema.

Amesema pamoja na nia ya Rais Samia ya kuona wakulima wanapata mbolea kwa bei nafuu lakini upatikanaji wake ni changamoto kubwa akidai wananchi wanapanga foleni, mawakala wachache na kusababisha wananchi kukesha kutafuta mbolea.

“Lipo changamoto ya uandikishaji watu ili wapate mbolea. Ili mwananchi aweze kupata mbolea lazima awe na namba ya utambulisho.

“Wananchi ambao wamejiandikisha mpaka sasa ni zaidi ya 8,000 hawajapata namba za utambulisho maana yake hawa hawawezi kabisa kununua mbolea. Tunaomba namba za mbolea zipatokane na vituo viongezwe,” amesema.

Kuhusu umeme amesema “Mji wangu wa Kasulu una mitaa 108, mitaa 77 mpaka sasa mingi haijasambaziwa umeme wa Rea. Kwahiyo namuomba sana kaka yangu (Waziri wa Nishati, Januari Makamba) awaambie wananchi nini kinaendelea,” amesema.

Hata hivyo, Makamba amesema baada ya mkoa huo kuonganishwa kwenye gridi ya Taifa changamoto ya umeme mkoani humo inaenda kukoma.

Akijibu changamoto ya kuchelewa kutolewa namba za wanaojisajili kwa ajili ya kununua mbolea pamoja na uchache wa mawakala, Rais Samia amesema wataongeza mawakala baada ya wiki mbili, huku akitaja tatizo la kimtandao ndiyo chanzo cha kucheleweshewa namba zao.

Awali akitoa taarifa ya miradi ya barabara hizo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila amesema wakazi wa mkoa huo wataondoka a na changamoto ya kukaa barabarani saa saba au siku nzima kipindi cha mvua badala ya saa nne kwa barabara ya lami.

Baada ya barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa Kilomita 260.6 kujengwa ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Nyakanazi, Kibondo, Kasulu hadi Manyovu inaunganisha Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga na Mwanza.

“Pia inaunganisha nchi jirani ya Burundi kupitia mpaka wa manyovu. Barabara hii imekuwa ikipitika kwa shida sana kipindi cha mvua,” amesema.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara kuu zinazounganisha mikoa na nchi jirani.

Amesema barabara hiyo itapunguza gharama za usafiri, usafirishaji, muda pamoja na kuimili mzigo wa kwenye magari.

“Kutokana na umbali mrefu wa barabara hii, usafiri kati ya Nyakanazi na Kigoma umekuwa ukichukua masaa karibia saba hadi zaidi ya siku moja kipindi cha mvua badala ya takribani masaa manne kwa barabara ya lami.

Hali hii inasababisha adha kwa wasafiri na wasafirishaji wa mazao mbalimbali,” amesema.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom