- Tunachokijua
- Teknolojia ya Akili mnemba (AI) ni seti ya teknolojia zinazoiwezesha kompyuta kutekeleza majukumu mbalimbali ya kina na kwa uwezo mkubwa na haraka kadri ya maelekezo ya mtumiaji, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuona, kuelewa na kutafsiri lugha inayozungumzwa na maandishi, kuchanganua data, kutengeneza picha na video na kutoa mapendekezo ya utatuzi wa matatizo mbalimbali.
Pamoja na kuwa na lengo zuri na muhimu teknolojia hii ya Akili Mnemba (AI)imesaidia kurahisisha na kuongeza ufanisi wa kazi ambazo huweza kufanya kwa muda mfupi huku ikiwa na makosa ambayo yanarekebishika. Baadhi ya watu wasio na nia njema wamekuwa wakiitumia katika kupotosha taarifa mbalimbali katika Jamii.
Hivyo ni vema kila mara kujifunza mbinu zitakazokuwezesha kutambua maudhui aidha ya maandishi, picha, video au sauti yaliyotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba ili kuepuka kupotoshwa.
Kuna utata unaoibuka kuwa kati ya picha hizi mbili juu ya uhalisia wake kama zimetengenezwa kwa akili mnemba ama ni halisi.
Je uhalisia wa picha hizo ni upi?
JamiiCheck imebaini mapungufu kadhaa ambayo yanadhihirisha kuwa picha zote mbili zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili Mnemba (AI).
Katika picha ya kwanza, mwanamke aliyejifunika kichwa chake anaonekana kuwa sehemu kubwa ya nywele iliyosukwa ikiungana na kitambaa chake sehemu ya juu na unywele huo kushuka upande wa nyuma, ukitazama kwa makini sehemu hiyo ya nywele ni tofauti kabisa na nywele zinazooneka sehemu ya mbele ambapo kitambaa hakijafunika.
Pia mkufu uliovaliwa shingoni hauonekani kuungana kwenda upande wa pili tofauti na uhalisia wa namna ya uvaliwaji wa mikufu. Vile vile kiganja cha mkono kinaonekana ikmefungamana na kiganja cha mkono wa pili ambao hauonekani huku vidole vikiwa pungufu na hali isiyokuwa ya kawaida.
Hata hivyo mtu wa pili anayemfuatia mwanamke huyo haonekani kuwa na mkono kuanzia begani licha ya kuwa na sweta linaloonekana kuwa halina kitu ndani yake. Sehemu ya madhaifu haya na mengine yaliyopo yanadhihirisha kuwa picha hii imetengenezwa kwa akili mnemba.
Vilevile kifaa cha utambuzi wa maudhui yaliyotengenezwa kwa kutumia akili mnemba kinabainisha kuwa picha hiyo imetengenezwa kwa teknolojia hiyo kwa asilimia 99.
Aidha picha ya pili pia imebainika kuwa na mapungufu kadhaa ambayo yanathibitisha kuwa picha hiyo imetengenezwa kwa akili mnemba. Mapungufu hayo ni pamoja uwepo wa watu wawili mwishoni mwa picha ambao wanaonekana wameungana licha ya kuonekana wamepakatana.
Pia mzee anayeonekana kuwa na ndevu zenye rangi sawa na ukuta, sehemu ya miguu yake haiendani na ukubwa wa umbo la mwili wake ambapo miguu hiyo inaonekana kuwa na hali ya wembamba iliyopitiliza (zingatia sehemu ya magoti) vilevile rangi ya suruali ya mguu mmoja ni tofauti na mguu mwingine.
Vilevile kifaa cha utambuzi wa maudhui yaliyotengenezwa kwa kutumia akili mnemba kinabainisha kuwa picha hiyo imetengenezwa kwa teknolojia hiyo kwa asilimia 99.