Hivi karibuni meli maarufu sana ya jeshi la wanamaji la China “Peace Ark” ambayo kwa Kichina inajulikana kama ‘Heping Fangzhou’ ilitia nanga katika bandari ya Dar es Salaam, ikiwa tayari kutoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali. Meli hii ya kwanza ya hospitali ya China yenye uwezo wa kubeba zaidi ya tani 10,000, iliwasili kwenye bandari ya Dar es Salaam tarehe 16 Julai mwaka 2024, ikiwa na madaktari bingwa zaidi ya 100 waliobobea katika magonjwa mbalimbali, huku ikiwa na seti ya vifaa tiba zaidi ya 2000.
Tangu wakati huo meli hiyo ilianza kutoa huduma za matibabu bila malipo kwa wananchi wa Tanzania hadi ilipong’oa nanga Julai 23. Watanzania wengi, hawakutaka kupitwa na fursa hii adimu ambayo labda inaweza kupatikana mara moja tu katika maisha, yaani kushuhudia kwa macho yao meli kubwa ya hospitali inayotembea ikifika nchini kwao pamoja na kupata matibabu.
Kwa Tanzania tunaweza kuihesabu kuwa ni nchi yenye bahati na inayopendwa sana na China, kwasababu hii ni mara ya tatu sasa China kuonesha mshikamano wake kwa nchi hii, kwa kupeleka meli hiyo kutoa huduma za matibabu bure. Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alieleza kuwa hii ni ziara ya tatu kwa meli hiyo ya matibabu kwenda nchini Tanzania, na kubainisha kuwa Tanzania ni taifa la kwanza kutembelewa na meli hiyo mara tatu.
Madaktari hao walipofika bandarini walilakiwa na wenyeji wao na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na maafisa wa jeshi la China, ambao wamekuwa wakitumikia nchini humo. Meli hii imekwenda Tanzania ikiwa ni sehemu ya mpango wa maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Ukombozi la China (PLA)
Katika salamu zake za makaribisho, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliyehudhuria kwenye sherehe za mapokezi, aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupata huduma za matibabu bure zinazotolewa kwa pamoja na madaktari kutoka China na wenzao wa Tanzania. Kwa maoni yake hii ni fursa adhimu ya kupata huduma za matibabu kutoka kwa madaktari wabobezi wa China. Mbali na kutoa matibabu, lakini ujio wa meli hiyo katika taifa hilo la Afrika Mashariki pia unaashiria uhusiano wa kindugu kati ya China na Tanzania ambao upo tangu enzi na dahari.
Kwa kuzingatia kanuni ya kujenga "jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja " na "jumuiya ya baharini yenye mustakabali wa pamoja," meli hii ya hospitali inalenga kuleta huduma za matibabu bila malipo zinazohitajika kwa watu wa maeneo yote duniani. Madaktari hao wakiwa nchini Tanzania, wamewanufaisha wagonjwa 4074 kwa huduma za matibabu bila malipo ambazo pia zilijumuisha kufanya upasuaji 11 wa magonjwa mbalimbali na kufanya uchunguzi 1280 kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Akieleza furaha yake baada ya kwenda kutembelea kwenye meli hiyo ili kujionea mwenyewe jinsi madaktari wa China na Tanzania wanavyotoa huduma za matibabu, Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu, alisema meli hii ilipanga kuona na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa 600, lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa wananchi, wataalamu hawa walionana na wagonjwa zaidi ya elfu 1,000 kwa siku.
Kilichomfurahisha zaidi waziri Ummy ni kwamba katika kipindi hiki cha utoji wa huduma za afya mama mmoja alipata mtoto kwa kujifungua salama kwenye meli hii, ambapo amesema hii inaonesha kuwa uhusiano ya nchi hizi mbili umegusa maisha ya watu, na mtoto huyu amepewa jina la ‘Peace Ark’.”
Ikizingatiwa kuwa mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, ni dhahiri kwamba ziara hii ya meli ya Peace Ark imezileta nchi hizi mbili karibu zaidi.