Uchaguzi 2020 Pazia la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania urais wa Zanzibar kupitia CCM, lafungwa, Vikao vya mchujo vyaanza

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,569
9,429
PAZIA la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), limefungwa rasmi jana jioni. Sasa wagombea 31 wanasubiri mchujo wa vikao vya chama hicho tawala Tanzania, ili kumpata mrithi wa Dk Ali Mohamed Shein, anayemaliza muda wake.

Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, Cassian Nyimbo aliwaambia waandishi wa habari kwamba kazi hiyo imekwenda vizuri. Alisema wanachama wote hao 32, wamekidhi vigezo walivyotakiwa kuvitimiza katika mchakato huo wa awali wa kupata mrithi wa nafasi ya urais wa Zanzibar.

Kwa mfano, Nyimbo alisema baadhi ya wagombea walipata wadhamini zaidi ya 250 katika mikoa mitano ya Unguja, kitendo ambacho sio kosa, kwani kinaonesha ukomavu wa kuwafikia wanachama wa CCM.

“Wagombea 32 waliochukua fomu kuomba ridhaa kwa nafasi ya urais wa Zanzibar wamekidhi vigezo na sifa zilizowekwa na leo hii wamerudisha fomu...yupo mgombea mmoja amejiengua baada ya kuzipitia fomu alisema mbio hizo ni kubwa na yeye binafsi anastahiki kutoa nafasi kwa wengine,” alisema Nyimbo.

Mgombea aliyechukua fomu na baadaye kujiengua ni Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu. Katika kinyang’anyiro hicho, jumla ya wanawake watano wamejitosa, wakiweka rekodi, ambapo katika mchakato wa urais wa Zanzibar wa mwaka 2000, mwanamke mmoja tu, Balozi Amina Salum Ali ndiye aliyejitokeza.

Wanawake waliochukua fomu ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, Mouldine Castico, Mwatum Mussa Sultani, Fatma Kombo Masoud na Hasnat Atai Masoud. Pia wamo watoto watatu wa marais waliowahi kuiongoza Zanzibar.

Hao ni Balozi Ali Abeid Karume (mtoto wa Mzee Abeid Amani Karume), Dk Hussein Mwinyi (mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi) na Mussa Aboud Jumbe (mtoto wa Mzee Aboud Jumbe).

Wagombea wengine ni Mbwana Bakari Juma, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Hussein Ali Mussa, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Jafaar Jumanne, Mohamed Haji Mohamed, Issa Suleiman Nassor, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Haji Rashid Pandu, Abdulhamid Mohamed Ali, Jecha Salum Jecha na Dk Khalid Salum Mohamed.

Wamo pia Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Majwiri, Hamad Yussuf Masauni, Mohamed Aboud, Bakari Rashid Bakari, Ayoub Mohamed Mahmoud, Hashim Salum Hashim, Pereira Ame Silima, Iddi Hamad Iddi na Shaame Simai Mcha.

Nyimbo alisema baada ya wagombea hao kukamilisha mchakato huo, kazi inayoendelea ni kukaa kwa vikao vya chama ambavyo vitapitia wagombea hao ikiwemo kuchambua sifa na vigezo mbali mbali ikiwemo elimu.

“Kuanzia kesho (leo) tutakuwa na vikao mbali mbali vya chama ikiwemo Sekretarieti pamoja na kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama na Maadili na baadaye tutakuwa na kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM,” alisema.

Kwa mujibu wa ratiba ya kuwapata wagombea wa CCM wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, jana ilikuwa siku ya mwisho ya kurejesha gomu.

Ratiba hiyo inaonesha leo kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar, itakutana wakati keshokutwa kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar kitafanyika Kisiwandui, Unguja.

Aidha, ratiba hiyo inaonesha Julai 4 kikao cha Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, itakutana kwa ajili ya kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu kuhusu wanachama wanaoomba nafasi ya urais wa Zanzibar.

Julai 9, kikao cha Kamati Kuu ya NEC kitakutana jijini Dodoma kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa NEC juu ya majina ya wanachama wasiozidi watatu, wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Zanzibar.

Jina la mgombea wa urais wa Zanzibar atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu litafahamika Julai 10, mwaka huu jijini Dodoma ambako kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitachagua jina moja la mwanachama atakayesimama kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar.

Mgombea wa mwisho kurejesha fomu alikuwa Waziri wa Uwezeshaji Wanawake, Watoto na Vijana, Moudline Castico ambaye alikipongeza Chama Cha Mapinduzi, kwa kuweka utaratibu mzuri unaofahamika kwa mujibu wa Katiba katika kuwapata viongozi wake wa nafasi za juu za uongozi wa chama.

“Nimekuwa mtu wa mwisho kurudisha fomu... namshukuru Mungu nimepata wadhamini zaidi waliokusudiwa kwa mujibu wa masharti ya fomu hii kwa kutembelea mkoa mmoja wa Kusini Pemba na mingine Unguja,” alisema.
 
Mbio, mbwembwe, sifa zote huishia hapa:-


"....Jina la mgombea wa urais wa Zanzibar atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu litafahamika Julai 10, mwaka huu jijini Dodoma ambako kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitachagua jina moja la mwanachama atakayesimama kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar..."
 
Back
Top Bottom