NYUMA YA PAZIA: Kutoka Romario, Ronaldo, Messi na sasa Traore

Ferruccio Lamborghini

JF-Expert Member
Apr 15, 2020
1,667
2,561
WAINGEREZA huwa wana msemo wao ‘Falling from the grace’. Kiswahili chake kinaweza kwenda na mfano. Yaani mfano wa mwanadamu aliyekuwa na nguvu za kubeba magunia matatu kwa wakati mmoja inapofika mahala akaishiwa nguvu kiasi kwamba akawa hawezi kunyanyua rimoti ya televisheni iliyo kando yake.

Mfano mwingine? Himaya ya Warumi ilivyoanguka. Ilikuwa himaya yenye nguvu zaidi duniani chini ya Julio Cesar. Warumi walikuwa zaidi ya Wamarekani. Kwa mbali zaidi. Baadaye walianguka na hawakuwahi kusimama tena.

Mfano mwingine? Huu hapa wa Barcelona. Nyakati zimekwenda wapi? Nawafahamu Barcelona tangu enzi za kina Hristo Stoichkov, Gheorghe Hagi, Ronald Koeman, Romario na wengineo. Hawajawahi kukaukiwa na watu ambao wasingeweza kufananishwa kirahisi na watu wa timu nyingine.

Halafu zikaja zama za kina Rivaldo. Unamkumbuka Rivaldo? Yule Mbrazil mwenye kipaji kikubwa ambaye mwanzoni mwa miaka ya 2000 yeye na Patrick Kluivert walisababisha watu waipende Barcelona. Baadaye nyakati zikasogea na Barcelona wakaendelea kulinda himaya yao. Walikuja kuibuka kina Samuel Eto’o, Deco na zaidi ya yote, Ronaldinho.

Barcelona wakaendelea kulinda himaya yao tena. Alikuja ‘mpuuzi’ mmoja anaitwa Pep Guardiola akatushangaza kwa kuwaondoa hawa watu watatu ghafla ghafla tu. Lakini ni yeye ndiye aliyeilinda Barcelona kwa kutuletea utatu wa Lionel Messi, Andres Iniesta na Xavi Hernandez.

Usidhani walikuwa wao tu. Ni kwa sababu majina yao yalikuwa makubwa zaidi lakini Barcelona ilijaza aina ya wachezaji wanaoitwa World Class. Walikuwepo kina Cesc Fabregas, David Villa, Dani Alves na wengineo.

Baadaye kidogo wakati kina Xavi wakianza kuchoka, Barcelona iliongezewa makali katika eneo la ushambuliaji ambalo liliibeba zaidi timu. Messi aliletewa Neymar na Luis Suarez na hivyo kutengeneza utatu mtakatifu kutoka Amerika Kusini. Tulidhani Barcelona ingeendelea kuwa hivyo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, baada ya hapo Barcelona wamegeuka Warumi. Himaya imeanguka. Kama ulikuwa shabiki wa damu wa Barcelona unaweza kulia. Wiki iliyopita walikuwa wakikamilisha uhamisho wa mchezaji anayeitwa, Adama Traore.

Subiri kwanza, kabla haujamjadili Adama inawezekana utakuwa unamuonea. Kabla ya hapo alishatanguliwa na wachezaji wa kawaida kina Memphis Depay. Nadhani Lionel Messi alishaamua kuondoka baada ya kuanza kuletewa kwa wachezaji wa namna hii kabla habari za ugumu wa masuala ya fedha Camp Nou. Depay na Messi wapi na wapi?

Lakini sasa wana Adama Traore. Ni kinda aliyekulia kwao, kama ilivyo kwa baadhi ya makinda wengine wa La Masia. Tatizo Adama hajakaa kuwa mchezaji wa Barcelona. Aina yake ya soka na kipaji chake ni vitu tofauti na Barcelona.

Adama ana kasi, mwepesi, lakini uamuzi wake wa mwisho haustahili kumfanya kuwa mchezaji wa Barcelona. Wenyewe waliporuhusu enzi hizo aondoke kwenda Aston Villa nadhani kuna kitu walikuwa wamekiona. Walikuwa wameona hastahili kuwa mchezaji wao.

Amezura kwenda Middlesbrough halafu Wolves lakini sasa amerudishwa tena Barcelona. Sababu? Hatuwezi kujua. Kwanza kabisa tulidhani Xavi Hernandez angeweza kujaribu kuichezesha timu yake kwa staili ambayo yeye mwenyewe alikuwa anacheza akiwa mchezaji Camp Nou. Staili ya Tiktak.

Kwa wachezaji kama hawa wanaokimbia kama faru sijui Xavi anataka kuichezesha timu yake kwa staili gani. sio kwa Adama tu, bali hata aina ya wachezaji ambao Barcelona imeendelea kujikusanyia katika miaka ya karibuni. Inaonekana wazi kwamba staili ya Tiktak kwa sasa itakuwa marehemu.

Kwa miaka nenda rudi, hasa katika eneo la ushambuliaji, Barcelona ilikuwa na wachezaji ambao wangeweza kuingia katika vikosi vya kwanza vya timu yoyote kubwa barani Ulaya. Lakini kwa Adama unamzumzungia mchezaji ambaye alishindwa hata kupata namba katika kikosi cha kocha mpya wa Wolves, Bruno Lage.

Kama unakuwa mwandishi wa gazeti fulani na unaandika kichwa cha habari kuhusu uhamisho wa Adama kwenda Barcelona unaweza tu kuandika ‘Barcelona yamnyakuwa mchezaji wa akiba wa Woles’. Hakuna ambaye anaweza kukulaumu. Ni hali halisi.

Kitu kilicho wazi zaidi ni kwamba Barcelona imeanguka ndani na nje ya uwanja. Kitu kibaya zaidi katika klabu kubwa kama Barcelona ni pale linapotokea anguko la nje ya uwanja. Hili ndilo ambalo linazaa anguko la ndani ya uwanja.

Barcelona haina pesa. Katika dunia huru na ya maisha halisi ya Barcelona nadhani ni wazi kwamba Xavi angewekewa majina matatu ya kuchagua mchezaji mmoja mzuri na jina la Adama lisingekuwepo. Angeweza kuwekewa Bukayo Saka, Mohamed Salah au Riyad Mahrez.

Hata hivyo, amewekewa jina la Adama. Unaweza kusema kwamba Adama yupo Camp Nou kwa mkopo lakini kama unaona kuna kipengele ambacho kinaweza kuifanya Barcelona wamchukue Adama moja kwa moja basi ujue kiasi hapo ndipo mkono wao ulipofikia.

Matokeo yake Barcelona itaendelea kuanguka. Mchezaji mwingine amefukuzwa Arsenal kijanja lakini wao wamemtwaa. Pierre Emerick-Aubamayeng. Msimu mmoja ulioipita Xavi akiwa Falme za Kiarabu alidai kwamba Auba hakuwa aina ya mchezaji wa kucheza Barcelona. Sio kwamba ni mbaya, hapana, ni kwa sababu ya staili yake ya soka.

Leo Xavi pia amemchukua Auba. Sio mchezaji ambaye atakabia juu, umri umekwenda, lakini pia hawezi kucheza Tiktak kwa ufasaha. Atakachompa ni umaliziaji wa haraka katika nafasi ndogo. Labda hapo tu ndipo Barcelona watafaidi kipaji cha Auba.

Nyakati zimepita na Barcelona hatimaye wameanguka chali. Hapo katikati walikuwa kama vile wanachechemea lakini sasa hivi wameanguka chali kabisa. Unategemea Adama awe mchezaji wa kuipa Barcelona mafanikio ya Ligi ya Mabingwa? Sidhani.

Angalia pengo lililopo kati ya kundi hili la Romario, Rivaldo, Ronaldinho, Eto’o, Messi, Iniesta na Xavi kisha wafananishe na Adama aliyetokea Wolves. Utagundua kwamba kwa sasa Barcelona imelala chali. Itachukua muda mrefu kuweza kunyanyuka, kujipangusa mchanga kisha kuanza kukimbia.

Kama Xavi anadhani anaweza kuinyanyua timu kwa kuwatumia kina Adama na Memphis Depay nadhani atasubiri sana. Na unapozingatia kwamba mwisho wa msimu wapinzani wao wanaweza kuwa na Erling Haaland na Kylian Mbappe kwa pamoja nadhani pengo la El Clasico litazidi kutanuka, lakini zaidi pengo la Barcelona na wakubwa wengine wa Ulaya litatanuka zaidi.



MwanaSpoti
 
Wakati Real Madrid wanajenga timu, Barcelona walikuwa wanapambana kumbakiza Messi, na kununua wachezaji kwa bei kubwa ambao WAmekuja kuwa flop. Madrid wanajiandaa kusepesha Ronaldo wao wanapambana na Messi astafu soka akiwa Barca, philosophy ya rais wa Barca ilikuwa mbovu na haikuwa na long-term projection. Ukishindwa kufanya long term projection lazima uwe specialist in failure, with short term success.
 
Nimependa aina ya usimuliaji wako ni mzuri,Kwanza unaijua vyema timu,pili umetulia kwenye kuandika

I'm Madrid fan lakini nasikitika anguko la Barca.

Hakuna Madrid bila Barca
 
Nimependa aina ya usimuliaji wako ni mzuri,Kwanza unaijua vyema timu,pili umetulia kwenye kuandika

I'm Madrid fan lakini nasikitika anguko la Barca.

Hakuna Madrid bila Barca
Huyo ni Eddo Kumwembe wa Mwanaspoti.
 
Back
Top Bottom