Kuna namna nyingi za kushughulikia yanayoendelea nchini sasa hivi na hasa madai makali dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa. Mengi tumeshazungumza juu ya Idara hii na kwa muda mrefu. Bahati mbaya inaonekana hata wabunge wetu hawajaona njia rahisi na ya haraka ya kusafisha idara hii. Tayari inaonekana wapo wabunge wengi kutoka pande zote mbili ambao wanakubaliana kuwa kuna tatizo fulani katika Idara. Sasa kwanini wabunge wasitumie umoja wao huu wa misimamo kufanya jambo lililo ndani ya uwezo wao?
Wabunge ndio watunga sheria wa nchi hi (law makers). Rais hatungi sheria hata moja; yeye kwake ni kuzipitisha tu. Siyo tu wabunge wanatunga lakini pia wanaweza kufanya marekebisho sheria na Katiba!
Sasa kuna pendekezo la Zitto kuchunguza matukio mbalimbali ambayo yanadaiwa kutokea hivi karibuni na Idara kuhusishwa. Njia hii ya Kamati Teule inaweza kutangulia – kama alivyodokeza – mabadiliko yoyote ya idara. Kamati Teule inaweza kuwaita watendaji na wakuu wote wa idara za usalama na kuwahoji chini ya kiapo – mbele ya camera au nje ya camera – na kutaka kujua nini kinaendelea. Na kwa vile Kamati ina nguvu za kibunge na mahakama inaweza kumlazimisha yeyote kati yao kufika mbele ya kamati hiyo au kuagizwa kukamatwa na kufikishwa mbele ya kamati hiyo.
Hiyo inaweza kuwa ni njia sahihi ya kutaka kutafuta ukweli. Pamoja na kuwaita hawa wote inaweza kuwaita hata waathirika wa vitendo hivi. Bashe kwa mfano anaweza kuitwa mbele ya Kamati hiyo na kutoa ushahidi wa madai ya kuwa kuna “mawaziri” ambao wamempa taarifa kuwa yeye ni mlengwa wa kutekwa; Zitto mwenyewe vile vile n.k Lengo ni kutaka kujua ukweli zaidi ili watakapotaka kufanya mabadiliko wajue wapi pa kuanzia.
Mkurugenzi wa TISS Dkt. Modestus Kipilimba
Hata hivyo, hilo linahitaji kuungwa mkono sana na wabunge wa CCM. Njia ya pili ambayo binafsi naipenda zaidi kama njia ya haraka ni kwa wabunge wenye kuona tatizo hasa – Bashe, Ridhiwani, Zitto, na wengine wakutane pamoja na kuandaa mswaada wa pamoja (bipartisan bill) ya kuivunja Idara ya Usalama wa Taifa na kuiunda upya ikiwa imetengenezwa kukidhi mahitaji ya kiusalama ya taifa hili na ikisimamiwa moja kwa moja na Bunge. Mswada huu uletetwe hata kwa hati ya dharura ili kabla ya Bunge hili kuisha usomwe unavyohitajika na upitishwe na Bunge na hatimaye upelekwe kwa rais kwa kuudhinisha.
Nina uhakika Rais Magufuli ataridhia kwani atakuwa amesaidiwa kazi ambayo labda ingemchukua muda yeye mwenyew ekuifanya. Na kama hatoridhia na kutishia Veto Bunge linaweza kuipiku veto hiyo kwa kura nyingi na kumlazimisha aisaini na kama haitowezekana basi Bunge litavunjwa na watu watarudishwa kwenye uchaguzi mkuu mpya ambapo wananchi watapata nafasi ya kwenda kuchagua wabunge na Rais mwingine kulingana na ajenda watakazosimama nazo.
Lakini kulalamika tu wakati nyenzo wanazo ni kupoteza muda wa watu. Ni wakati wa kufanya wanachoamini ni sahihi kufanya na wana uwezo wa kukifanya. Lakini pia utakuwa ni wakati wa watu kuhesabiwa. Kwa sisi wengine ambao tumekuwa tukilalamikia idara hii kwa muda mrefu tunaona labda hii ni nafasi ya pekee ya kuileta Idara hii kwenye karne ya 21. Inapofikia watu tena wazito wanadai kuwa Idara inajihusisha au watumishi wake wanajihusisha na vitendo ovya kighaidi hakuna namna namna nyingine ya kufanya isipokuwa kuivunja idara hiyo na kuiunda upya toka chini. Mkitaka mawazo tupo wengine tunaweza kuwasaidia.