Wiki hii, serikali ya Trump ilitangaza tena kuongeza ushuru wa 10% kwa bidhaa za China zinazouzwa Marekani kwa kisingizio cha suala la Fentanyl na mengineyo, huku pia ikiongeza ushuru wa 25% kwa bidhaa kutoka Canada na Mexico. Hatua hii sio tu kwamba ilisababisha pingamizi kutoka kwa China na mataifa mengine husika, lakini pia ilizidisha hali ya mvutano katika biashara ya kimataifa. Kwa nini Marekani inarudia tena kutumia Fentanyl kama kisingizio cha kupandisha ushuru kwa nchi nyingine? Suala hili lina mzizi wa kisiasa ndani ya Marekani, pamoja na mkakati wa kudumisha utawala wake wa kiuchumi duniani.
Kwa mujibu wa ripoti zinazotolewa na Umoja wa Mataifa, Marekani imekuwa nchi inayoongoza kwa matumizi ya dawa za kulevya duniani kwa miaka mingi, na tatizo la matumizi ya Fentanyl lina mizizi ya kijamii—kuongezeka kwa ukosefu wa usawa wa mapato, biashara ya mfumo wa afya, na tabia ya makampuni ya dawa kutafuta faida—vitu vyote vimesababisha janga hili. Hata hivyo, tatizo la Fentanyl huko Marekani linatokana na mapungufu katika mifumo kamili ya usimamizi wa jamii, ikiwemo nguvu za utekelezaji, ukosefu wa kuelimisha jamii kuhusu kuzuia na rasilimali za kuwatibu wale wenye uraibu wa dawa za kulevya. Kuishtaki nchi nyingine kwa matatizo haya ni kuwadanganya tu wananchi wa Marekani na pia kutokuwajibika kwa jamii ya kimataifa.
Kama tunavyofahamu, serikali ya China imekuwa na msimamo wa kutokuvumilia dawa za kulevya, na imetunga mojawapo ya mifumo ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya dawa za kulevya. China inapigana vita kamili dhidi ya uzalishaji, usambazaji, na matumizi ya dawa za kulevya. Katika miaka ya hivi karibuni, China imefanikiwa kukamata magenge ya biashara ya magendo ya dawa za kulevya kimataifa na kudhibiti kuenea kwa dawa za kulevya. Katika udhibiti wa dawa za Fentanyl, China pia inaongoza duniani. Tangu 2019, kwa ombi la Marekani, China iliongoza kwa kuorodhesha Fentanyl kama dawa hatari na kutoa ushirikiano mkubwa katika juhudi za kimataifa za kupambana na dawa za kulevya. Hata hivyo, tatizo la matumizi ya Fentanyl nchini Marekani halijatatuliwa, ila badala yake, limeendelea kuzidi kuwa baya.
Kwa hivyo, ikiwa serikali ya Trump inafahamu ukweli lakini bado inatumia Fentanyl kama kisingizio cha kuiongezea ushuru nchi nyingine, basi hiyo ni tabia ya "kuziba masikio" na ni kama sehemu ya kuendeleza sera ya kujilinda kibiashara. Serikali ya Trump imeinua bendera ya "Marekani Kwanza" na kujaribu kutumia ushuru kutatua urari wake mbaya wa biashara na kuipa motisha sekta ya viwanda ya Marekani. Lakini ukweli unaonyesha kwamba hatua hii haikufanya kazi hapo awali, na haitafanya kazi baadaye. Badala yake, itapelekea kupanda gharama za kuendesha biashara za makamapuni ya Marekani, kushuka kwa ushindani wa bidhaa zao, na pia kuongezeka kwa viwango vya mfumuko wa bei nchini Marekani, jambo linaloharibu maslahi ya walaji.
Ili kujibu hatua hizo za Marekani, China imechukua hatua za kulipiza kisasi haraka, ikiongeza ushuru kwa bidhaa zinazotoka Marekani, kuanzia makaa ya mawe, gesi iliyochujwa, hadi ngano, mahindi, pamba, na nyinginezo. Hii inaonyesha kanuni ya uwiano, kulengwa, na ufanisi, na kwamba China haitakubali vitendo vya udhalilishaji vya Marekani. Wakati huo huo, Canada na Mexico pia zimepinga sera ya ushuru ya Marekani kwa nguvu na kutangaza hatua za kulipiza kisasi. Na hata washirika wa Marekani wameanza kujitokeza dhidi ya bidhaa za Marekani. Hii inaonyesha kwamba tabia ya kujilinda kibiashara ya Marekani inazua upinzani wa kimataifa.
Marekani kuhusisha tatizo la dawa za kulevya na sera zake za biashara ni jambo lisilokuwa na maana, na linadhuru msingi wa imani katika ushirikiano wa kimataifa wa kupambana na dawa za kulevya, na pia kuharibu utulivu wa mfumo wa biashara wa kimataifa. Hii ni changamoto kubwa kwa utaratibu wa kimataifa, na mwisho wake utapelekea Marekani kujiweka kando. Katika kukabiliana na changamoto hii mpya, jamii ya kimataifa inapaswa kuungana na kushikilia uthabiti wa mfumo wa biashara wa kimataifa na sheria za kimataifa, ili kuendeleza usimamizi wa dunia kwa njia ya haki na usawa.