Ni Muhimu Watoto Wenye Ulemavu Kuwezeshwa Kuwa Washiriki Hai Katika Jamii Zao Na Kuishi Maisha Bora

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
746
2,102
IMG_20220801_135523_746.png


Ni muhimu kwa watu wenye ulemavu kuwa washiriki hai katika jamii zao na kuishi maisha yenye kuridhisha. Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu unasema kuwa watu wenye ulemavu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika jamii.

Watoto na watu wazima wenye ulemavu mara nyingi hukabiliwa na ubaguzi, unaosababisha kupungua kwa upatikanaji wa huduma za msingi za kijamii na kutotambuliwa kwa ujumla.

Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) linasema kuwa asilimia 15 ya idadi ya watu duniani - takribani watu bilioni moja - wana aina fulani ya ulemavu, iwe ni wa kuzaliwa nao au uliopatikana baadaye maishani. Takribani milioni 240 kati yao ni watoto.

Hata hivyo, watoto wenye ulemavu wamekuwa ni miongoni mwa watu wasiojiweza zaidi, wakikabiliwa na ongezeko la unyanyasaji na ubaguzi na kupungua kwa ufikiaji au upatikanaji wa huduma za msingi katika maeneo mengi duniani.

Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) ulipitishwa mwaka 2006 ili kukabiliana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa dhidi ya watu wenye ulemavu duniani kote. Unafafanua kwamba kuishi na ulemavu wa muda mrefu wa kimwili au kiakili umekuwa ukikwamisha ushiriki katika jamii kwa viwango sawa na wengine. Vizuizi vingi huzuia uwezo wao wa kufanya kazi katika maisha ya kila siku, kufikia huduma za kijamii (kama vile elimu na huduma za afya) na kushiriki katika jamii zao.

Unyanyapaa na ubaguzi ndio mzizi wa kutengwa kwa watoto wenye ulemavu katika kila nyanja ya maisha. Hivyo ni vema kufanya kazi kubadilisha mitazamo, desturi na kanuni za kijamii kuhusu ulemavu ili kuzifanya familia, jumuiya, shule, huduma za afya, na huduma za kijamii kuwa shirikishi na zinazoweza kufikiwa, na kusaidia ushiriki kamili wa watoto wenye ulemavu katika jamii.

Kiwango ambacho watoto wenye ulemavu wanaweza kufanya kazi, kushiriki katika jamii na kuishi maisha yenye kuridhisha inategemea ni kwa kiwango gani wanashughulikiwa na kujumuishwa. Bila kujali changamoto zao, kila mtoto ana haki ya kustawi.

Ili kuwajumuisha watoto wenye ulemavu, ni vema kuwa na mikakati ya kupambana dhidi ya vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwakwamisha kuwa sehemu ya jamii zao kama vile:

Vikwazo vya kimwili - kwa mfano, majengo, usafiri, vyoo na viwanja vya michezo ambavyo haviwezi kufikiwa na watumiaji wa viti vya magurudumu.

Vikwazo vya mawasiliano na taarifa - kama vile vitabu vya kiada ambavyo havipatikani katika nukta nundu au matangazo ya afya ya umma yanayotolewa bila tafsiri ya lugha ya ishara.

Vikwazo vya kimtazamo - kama vile mawazo potofu, matarajio madogo, unyanyasaji na uonevu.

Kila moja ya haya yamejikita katika unyanyapaa na ubaguzi unaoakisi mitazamo hasi ya ulemavu inayohusishwa na uwezo.

IMG_20220801_135518_276.png


Baadhi ya watoto wenye ulemavu pia wanakabiliwa na na changamoto zaidi pale wanapokuwa ni wasichana, maskini, wanaotoka kwenye makabila madogo, jumuiya za wahamiaji au makundi mengine yaliyotengwa. Mazingira hayo huwafanya kuwa na wakati mgumu sana kupata mahitaji yao.

CRPD inawajibisha Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu wanapata na kufurahia kikamilifu haki zao zote za msingi.

Kiwango ambacho watoto wenye ulemavu wanaweza kuishi maisha ya furaha kinategemea nia yetu wenyewe ya kukabiliana na vizuizi vya mabadiliko.

Kwa mujibu wa UNICEF ushahidi katika baadhi ya nchi unaonesha kuwa watoto wenye ulemavu wana uwezekano mkubwa wa kutengwa shuleni kuliko wenzao wasio na ulemavu - katika baadhi ya nchi, hadi mara nne zaidi. Hata wanapojiunga na shule, watoto wenye ulemavu wana uwezekano mdogo wa kumaliza elimu ya msingi au sekondari, na ukosefu wa usawa unakua kadri kiwango cha elimu kinavyosonga mbele.

Kwa kuhitimisha, hakuna mtu anayependa kutengwa kwa sababu zozote zile ambazo hazipo chini ya uamuzi wake. Kutoshirikishwa kwa namna yoyote kijamii kunaweza kuleta hisia za kuumiza, wasiwasi, aibu, upweke, na huzuni, kati ya hisia nyingine nyingi.

Ikiwa kutengwa ni jambo linalosababisha maumivu ya kihisia, basi kujumuishwa kunaweza kusababisha furaha na ustawi wa kila mwanajamii. Ni wakati sasa kwa jamii zetu kuhakikisha kila mtoto mwenye ulemavu anatendewa yale yanayostahili ili ajhisi kuwa ni sehemu muhimu katika jamii anayoishi.
 
Back
Top Bottom