Samahani
JF-Expert Member
- Oct 29, 2018
- 221
- 335
Utangulizi
Katika Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, Sura ya 29; ndoa imetafsiriwa kuwa ni ‘muungano wa hiari’ kati ya mwanamke na mwanaume unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao yote. Kumbe, mojawapo kati ya mambo ambayo wanandoa wanapaswa kuyaweka vema katika fahamu zao ni kuwa, lengo la uwepo wa ndoa ni kuendelea kubaki katika muunganiko huo “katika kipindi chote cha maisha yao”. Hili linathibitika katika aina zote za ndoa zinazotambulika katika sheria hii, yaani ndoa za kimila, ndoa za kidini na ndoa za kiserikali.
Kisheria, zipo sifa ambazo zimeainishwa ili kuipa nguvu za kisheria ndoa. Sifa hizi zinapaswa kuwepo kabla na wakati wa kufungwa kwa ndoa yenyewe. Hizi zinajumuisha utayari/ hiyari baina ya wanaofunga ndoa, wanaofunga ndoa kuwa mwanamke na mwanaume, umri unaotambulika kisheria kuzingatiwa, ndoa ilenge kwenye msingi wake wa awali, yaani kudumu (isiwe ndoa ya mkataba), wanandoa kutokuwa ndugu wa damu, ndoa kutangazwa kabla ya kufungwa na zingine (TLS, 2015).
Hata hivyo, katika kipindi cha karne moja iliyopita, tafsiri, lengo na mwelekeo wa “ndoa” umebadilika kwa kiasi cha kuleta mashaka makubwa. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la ndoa kuvunjika, kuwepo kwa ‘dhana ya ndoa’ ambapo wanawake na wanaume wameendelea kuishi pamoja pasi na kufunga ndoa, pamoja na ongezeko la ‘waliowahi kuwa wanandoa’ kuamua kufunga ndoa na wenzi wengine baada ya talaka au kuachana (Weiss Yoram 2005 Uk. 1).
Pamoja na kutufikirisha, hali hii inatupa kila sababu ya kuangazia tena kile hasa kinachoendelea katika muunganiko huu wa “hiyari” ambao tunataka kuuona ukidumu.
Hali Halisi
Ingawa ndoa kwa asili inalenga kuwa ni chanzo cha maisha ya amani, furaha na upendo kwa wanandoa, katika miaka ya hivi karibuni tunashuhudia kubadilika kwa kiasi kikubwa kwa dhana hii. Ndoa nyingi sasa zimekuwa ni sababu ya kuvumilia mateso, visa vya unyanyasaji na ukatili uliopitiliza baina ya wanandoa (Amato, P. R. et al, 2001). Matukio ya ukatili yameendelea kushuhudiwa kila siku, na mengine yamepeleka mauaji ya kutisha, ulemavu wa kudumu, majeraha na makovu makubwa, kudhalilishana mbele ya kadamnasi, Maisha ya vitisho, fedheha, masimango na kejeli, magonjwa ya zinaa yatokanayo na kukosa uaminifu katika ndoa, sonona, kukimbia familia na wengine wakiishia kuyadhuru maisha yao wenyewe.
Unapoingia katika mtandao na kutafuta habari za mauaji baina ya wanandoa, unahitaji muda wa kutosha kuanza kupitia moja baada ya nyingine maana ni nyingi mno, na zinatokea maeneo tofauti na kwa njia pia zinazotofautiana. Wapo ambao wanakufa kwa kupigwa na vitu vizito, kuchinjwa, kuchomwa moto, kupigwa risasi, kucharangwa kwa mapanga, kuchomwa na vitu vyenye ncha kali au kunyongwa mpaka kufa. Ingawa katika kila habari kunakuwa na kisa fulani, mara nyingi utakuta kabla ya kutokea kwa maafa hayo makubwa, kumekuwapo na chokochoko “zinazovumiliwa kwa muda mrefu!”.
Mwaka 2018 peke yake, takwimu za jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kuwa wanawake 137 waliuawa kwa kupigwa na waume zao, huku kati ya Januari na Septemba 2019, idadi ya wanawake waliouawa ilikuwa ilifikia wanawake 120 (Msemaji wa jeshi la Polisi, David Misimbe alipohojiwa na Gazeti la Mwananchi 09/12/2019)
Katika utafiti uliofanywa na Mamlaka ya taifa ya Takwimu, kati ya wanawake wawili (2) wenye umri kati ya miaka 15 na 49 waliokuwa wameolewa, mmoja (1) aliwahi kukutana na aina mojawapo ya ukatili kihisia, kimwili au kimaumbile kutoka kwa mume aliyekuwa akiishi naye au aliyekuwa ameolewa naye awali. Kwa mwaka 2014, wanawake 26 katika ndoa waliuwawa na wenzi wao mkoani Mbeya pekee (Tanzania Human Rights Report, 2014 Uk 178).
Ripoti ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu (UNODC) ya mwaka 2018, inasema nyumbani ni mahali hatari zaidi kwa wanawake na hususan kwa mauaji na ukatili. Ripoti hiyo inasema wanawake 87,000 waliuawa duniani mwaka 2017, huku 50,000 au asilimia 58 ikiwa ni mikononi mwa wenzi wao au jamaa watu wa familia. Idadi hiyo inamaanisha kuwa wanawake 6 waliuawa kila saa moja na watu wanaowafahamu duniani kote. (Gazeti la Mwananchi 09/12/2019)
Soma:
Yote haya yanafanyika, iwe kwa uwazi au kificho, chini ya kivuli cha “uvumilivu katika ndoa”.
Tanzania tulijiwekea lengo kuwa, kufikia mwaka 2025 tutakuwa tumefikia usawa wa kijinsia katika uchumi, kijamii, kisiasa na kielimu kwa kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizokuwepo (Tanzania Vision 2025, Uk 3). Sasa ni mwaka 2022, na bado tumeendelea kuweka takwimu zinazoongezeka za ukatili mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa chini ya mgongo “wa ndoa zinazopaswa kudumu”. Nusu ya ndoa tunazoziona ni “kiwanda cha unyanyasaji”!
Wengi wamejikuta wakiwa ni waathirika wa yote haya kutokana na baadhi ya kauli, mafundisho, sheria au semi mbalimbali ambazo tumejiwekea kama vile; ‘ndoa ndoano’, ‘ndoa ni uvumilivu’, ‘ndoa yataka moyo’, ‘kuachika au kuachana ni aibu’.
Sheria inasemaje?
Kwa mujibu wa sheria ya ndoa, pamoja na mafundisho hasa katika dini ya kiislamu, upo ukomo unaoweza kuwekwa kisheria katika ndoa, bila kujali kuwa tulilenga uwe ni “muunganiko wa daima”. Mahakama inaruhusu talaka ikiwa itajiridhisha kuwa, hali ya ndoa husika haiwezi kurekebishika tena! Vigezo kadhaa vimewekwa ili kujiridhisha juu ya hilo ikiwa ni pamoja na;
Kwa kuziangalia sababu hizi zinazotambulika kisheria, ni wazi kuwa, wazo la “ndoa yangu haipaswi kuninyanyasa” linapata maana kubwa zaidi. Ubakaji katika ndoa limekuwa ni jambo la kawaida sana, na kwa namna ya ajabu, wapo wasioelewa kuwa, ubakaji unaweza kuwepo hata baina ya wanandoa (TAMWA, 2019). Ukatili umeendelea kuwa gumzo lisilochosha masikio yetu. Visa vya mauaji vinaendelea kuwa ni sehemu ya vichwa vya habari katika vyombo vingi nchini. Wapo wanawake wanaoingiliwa kinyume na maumbile, lakini wamebaki kuwa kimya (SIAC, 2016). “Ugumu wa maisha” umewakimbiza wanaume wengi mbali na familia zao na kuziacha katika dhiki isiyoelezeka kwa muda mrefu, huku wenzi wao wakiendelea kusubiri “miujiza” ya kuwaona tena.
Si ajabu tena kwa wengi kati ya wanandoa sasa kuwa na ‘mahusiano ya kingono’ nje ya ndoa zao zinazotambulika. Misamiati mingi imezuka ikiwepo ‘Mchepuko, ‘Nyumba Ndogo’, ‘Mpango Kando’, ‘Kibanda Muafaka’ na mingine mingi inayoendana na hii, yote ikionesha kuwa, ‘ndoa nyingi’ ziko mashakani. Katika mazungumzo yetu, pengine tunafikia hata kuwasifia wenye tabia kama hizi!!
Kutokana na kukua na kukomaa kwa tabia hizi, visa vya kufumaniwa, kuwa na watoto nje ya ndoa na baadae kutelekeza familia limekuwa jambo la kawaida. Haya pia ndiyo yanayopelekea MANYANYASO KATIKA NDOA, na wakati mwingine, VIFO! Lakini ajabu inabaki kuwa, wapo ambao wanabaki katika msingi wa “uvumilivu katika ndoa”, uvumilivu ambao mara nyingi zaidi umeleta mateso makubwa zaidi badala ya nafuu na faraja!
TUNAWEZA KUFANYA NINI?
Uhalisia unatupa kila sababu ya kufikia hitimisho kuwa, “Ndoa” sio LAZIMA yawe ‘makubalioao ya daima’. Katika miaka ya karibuni, tunashuhudia viashiria vingi vya ukweli huu na mojawapo ni kupungua kwa idadi ya ‘ndoa’ mpya, kuongezeka kwa wenzi wanaoishi bila ndoa zinazotambulika (kuishi kinyumba), kuongezeka kwa idadi ya wanaaolewa au kuoa kwa mara ya pili baada ya kuvunjika kwa ndoa za awali, huku kiwango cha talaka au kuachana kikiongezeka (Stevenson, Betsey; Wolfers, Justin 2007). Lakini pia, ndoa nyingi zimekuwa kisababishi cha mateso kinyume kabisa cha lengo kuu la ndoa; kuishi kwa furaha, amani, upendo na umoja/ ushirikiano.
Ufike wakati tuungane na wanaharakati wa haki za binadamu katika kuukubali ukweli kuwa, “NDOA SIO PAHALA PA MANYANYASO!”. Inapobidi kuvunjika kwa ustawi wa wanandoa wenyewe na wanaowazunguka, ni vema zaidi hilo likafanyika kwa amani kabisa ili kuepusha madhara ambayo tumekuwa tukiyashuhudia kila siku. Uhalisia katika jamii yetu, sheria pamoja na mafundisho ya kidini vinatupa njia ya kufikia hili kwa amani kabisa bila kuwepo na vurumai zisizo za lazima.
Kwa kuanza, ni vema yafuatayo yakawepo katika mawazo ya taasisi za kiusimamizi, wanandoa wenyewe na jamii inayotuzunguka kwa ujumla.
1. Wanandoa kujiwekea mipaka
“Uvumilivu” katika ndoa unapaswa kuwekewa mipaka na kupimwa katika mizani ya haki. Katika kila jambo zuri, ni muhimu mwanadamu kuwa na uvumilivu (Health and Safety Professionals Alliance, 2012). Hii haina maana kuwa uvumilivu huu usiwe na mipaka. Wanandoa wanaopitia manyanyaso kama vile ya kingono (ubakaji, kuingiliwa kinyume na maumbile na/ au kunyimwa unyumba) wanapaswa kuweka mipaka katika kuvumilia kwao vitendo hivi. Pale wanapomaizi kuwa vimevuka mipaka waliyojiwekea pamoja na ile iliyowekwa kwa mujibu wa sheria, ni wakati muafaka wa kukataa ndoa kuwa sababu ya manyanyaso!
2. Kutambua viashiria vya hatari
Ni vema wanandoa wakawa makini kiasi cha kutambua mapema tabia, vitendo na mienendo hatarishi katika ndoa zao. Tabia kama vile ulevi uliopitiliza, vipigo vya mara kwa mara, lugha za matusi, unyanyasaji wa kingono pamoja na usiri katika mambo msingi katika ndoa ni baadhi tu ya dalili kuwa, ndoa hii inaweza kuanza kuwa sababu ya manyanyaso ikiwa hazitatafutiwa ufumbuzi mapema. Palipo na mazingira Rafiki, viashiria hivi vijadiliwe na kutafutiwa ufumbuzi na ikiwa vimefikia katika hatua isiyoweza kurekebishika, viwekwe wazi ili sheria na miongozo mingine ianze kuingilia kati.
3. Kurekebisha kwa kiasi tuwezacho misimamo na mitazamo yetu juu yetu na wenzi wetu
Sheria inaweka wazi kuwa, ndoa ni makubalioano baina ya watu wawili; mwanamke na mwanaume. Ni vema watu hawa, kwa kuwa wanakuwa wamefikia makubaliano haya kwa hiyari; kila mmoja kutathmini na kurekebisha kwa kiasi awezacho mitizamo na misimamo yake. Kuridhiana kunapaswa kuwa kipaumbele kwa wanandoa wote wawili. Baadhi ya tabia na misimamo ambavyo tunakuwa navyo kabla ya kuingia kwenye ndoa vinapaswa kuangaliwa tena kwa umakini iwapo bado vitakuwa na tija baada ya ndoa, na ikiwa vinahatarisha “udaima wa ndoa”, ni busara kuamua mara moja kuviacha ili kuihami ndoa.
4. Kuongeza uelewa wa sheria zihusuzo ndoa
Kuna kila sababu ya kuongeza uelewa wa sheria na kanuni za jadi zinazosimamia ustawi wa ndoa. Zipo ambazo zimeandikwa na zipo ambazo zimekuwa zikitekelezwa bila kuwepo katika maandishi rasmi. Kabla ya ndoa, wakati wa kufunga ndoa n ahata baada ya ndoa, wanandoa waendelee kuwezeshwa katika kuzijua sheria na haki katika ndoa. Pia, viongozi wa dini, wa kimila na wa jamii kwa ujumla wajengewe uwezo wa kutosha katika sheria hizi ili wawe wapatanishi na wasuluhishaji wanaoangalia kwa upana usalama wa maisha ya ndoa.
5. Kuwepo kwa Mizani ya Haki wakati wa usuluhishi
Wakati wa usuluhishi katika mabaraza yanayosimamia ndoa (BAKWATA, mabaraza ya ndoa ya kanisa, baraza la kata na baraza la kamishna la ustawi wa jamii), msukumo na lengo kubwa limekuwa ni kuzinusuru ndoa hizi kuvunjika. Hili ni lengo zuri kwa kuwa linalenga hasa msingi mkuu wa ndoa kudumu. Hata hivyo, huu umekuwa ni mwanya wa kuuacha “msamaha na suluhu zisizo na mabadiliko chanya” kutawala. Ni muhimu katika kusuluhisha ndoa zenye migogoro, mizani ya haki, ukweli na uadilifu kutumika. Sio kosa kusema kuwa rangi nyeupe ni ‘nyeupe’ au kuwa rangi nyeusi ni ‘nyeusi’. Huu ndio ukweli! Ikiwa kuna viashiria vinavyolazimisha wanandoa hawa kutengana, mabaraza yetu yawe mstari wa mbele kusimamia ukweli ili kuepusha madhara makubwa zaidi.
6. Marekebisho ya sheria ya ndoa na kukuza uelewa kwa jamii
Kilio juu ya mabadiliko ya sheria ya ndoa 1971 kimekuwepo kwa miaka mingi kwani katika kipengele cha umri, sheria hiyo inakinzana na sheria ya Mtoto 2009. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ndoa za utotoni duniani. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mnamo mwaka 2010, asilimia 37 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kufikisha miaka 18. Maana yake ni kwamba wasichana wawili (2) kati ya watano (5) nchini Tanzania waliolewa wakiwa Watoto (TLS, 2015 Uk.13). Si rahisi kuthibitisha “uhiyari wa mtoto” katika kufikia maamuzi ya kuoa au kuolewa. Ili kuthibitisha hili, mikoa ambayo ilikuwa ikiongoza kwa ndoa za utotoni ndiyo pia ilikuwa ikiongoza kwa takwimu za wingi wa ukatili katika ndoa.
Jamii ieleweshwe kwa kutumia takwimu hizi kuwa, ndoa za utotoni ni janga kubwa zaidi ya ile furaha tunayoipata katika ‘machezo na mashangilio’ wakati wa harusi hizi. Ni dhuluma ambazo hazipaswi kuendelea kufichwa katika kivuli cha ndoa!
7. Kukubali kuachana “kwa hiyari”
Upo msemo maarufu sana katika jamii kuwa ‘ni afadhali kukosea kujenga nyumba kuliko kukosea kuoa/ kuolewa’. Kuna ambao mara baada ya kuoa au kuolewa hutambua kuwa, walishapotea njia! Ni busara ya wazi kabisa, pindi hili linapogundulika, na ikiwa haliwezi kubadilishwa, wanandoa hawa kufikia makubaliano ya “kuachana”. Ndio, yanaweza kuwa maamuzi magumu na yenye kufedhehesha, lakini sio kwa kiasi kikubwa kama kuendelea “kuishi uvumilivu” usio na tija huku vitendo vya unyanyasaji vinavyohatarisha misingi ya ndoa kuendelea kuwepo.
8. Nafasi ya viongozi wa dini na serikali washirikishwe pasipo kificho
Wakati mwingine, kukwaruzana kwa hapa na pale kunashuhudiwa sana katika ndoa nyingi. Hili ni jambo la kawaida. Katika kila wanandoa wawili waliohojiwa katika wilaya ya Kinondoni, mmoja alikiri kuwepo kwa kutokuelewana katika ndoa mara kwa mara (Malinda 2017). Kutokuelewana huku sio sababu ya kuvunja ndoa. Migogoro hii ifikishwe kwa viongozi wa kidini na kijamii pasi na kificho, hasa ikiwa ni ile inayoweza kupelekea hali ya hatari katika siku za usoni. Vitendo kama ukatili wa kingono, bila kujali “unyeti na usiri” wake, visifichwe, bali vijadiliwe na kuwekewa mkazo unaolenga kuvibadili na kuviondoa na sio kuwadhalilisha wahusika.
9. Sheria ifuate mkondo wake
Mbele ya sheria, haijalishi upendo baina ya wanandoa ni mkubwa kiasi gani! Mwanandoa anayepigwa mpaka kufikia kubaki na ulemavu hawezi kuendelea kubaki akiugulia maumivu yake kwa kigezo cha kumpenda sana anayemsababishia maumivu hayo. Upendo na msamaha ni tiba dhidi ya mateso na chuki, lakini vinapaswa kuwa na vipimo sahihi. Pale mwanandoa mmoja anapogundua anaishi chini ya mateso kwa kujipa faraja ya kivuli cha uvumilivu wa ndoa, ni wakati wake sahihi kutafuta msaada wa kisheria bila kupepesa macho ili kuokoa uhai na usalama wake.
10. Huruma na upendo wa wazazi/ walezi visipoe
Hakuna asiyetambua ni kiasi gani wazazi wanakuwa na huruma juu ya watoto wao, na pengine ndio maana wanaitwa “mungu wa pili”. Busara na mahusia yao havipaswi kupoa pale watoto wao wanapooa au kuelewa. Kama walivyowalea kwa mapenzi wakati wakiwa chini ya mikono yao, ni vema pia wakaendelea kuwapa ushauri mwema na kuwasikiliza pale wanapopitia migogoro mikubwa katika ndoa. Ikumbukwe kuwa, naadhi ya vitendo vya kikatili katika ndoa vinahusisha usiri mkubwa, na wakati mwingine, wanaotendewa vitendo hivi hujisikia aibu kuwashirikiswa watu wengine, lakini wanaweza kupata ujasiri wa kuwashirikisha wazazi au walezi wao kwa uhuru zaidi juu ya madhila wanayopitia.
11. Sheria juu ya ukatili wa majumbani
Changamoto nyingi za ukatili katika ndoa zimebaki hewani kisheria kwa kuwa, ukatili wa majumbani haujawekewa sheria ya moja kwa moja (TLS, 2015). Ni vema serikali ichukue hatua muhimu ili kutunga Sheria dhidi ya ukatili wa majumbani kwa kufanya ukatili wa majumbani kuwa kinyume na Sheria na hivyo adhabu kali zitolewe. Ukatili huu pia utolewe ufafanuzi wa kutosha ili kuwasaidia wale ambao hawana taarifa kuwa hata katika “vifungo vya ndoa” kunaweza kuwepo na ukatili. Jamii inayowazunguka wanandoa; hasa wasimamizi/ mashahidi wa ndoa, ndugu, jamaa na marafiki wenye nia njema wanaweza kuwa chanzo kizuri cha msaada katika usambazaji wa taarifa hizi kwa vyombo vinazyosimamia haki na ustawi wa jamii.
12. Tuipe heshima ndoa na Kuchochea majadiliano
Biblia takatifu inanukuliwa ikitahadharisha kuwa; “Ndoa na iheshimiwe na watu wote” (Waebrania 13:3). Ni vema heshima ya ndoa ikatolewa na watu wote, walio na wasio katika ndoa. Tuna kila sababu ya kuibua mijadala ya kijamii juu ya usalama wa ndoa zetu na umuhimu wake. Waliooa wazipe heshima ndoa zao, hasa katika mazingira wanapokuwa na uhuru wao binafsi. Wapo ambao, kwa sababu zao binafsi hujitambulisha kuwa wajane, wagane au wasio na ndoa ili kupata maslahi fulani. Hii sio njia nzuri ya kuziheshimisha ndoa zetu. Wanaotuzunguka wanapaswa kuelewa hali zetu za ndoa ili wasiwe kikwazo kinachoweza kupelekea kuvunjika baadhi ya maagano na ahadi za ndoa.
13. Wanaume na vijana wa kiume wahusishwe kama wenzi
Kwa mujibu wa TDHS 2010, 44% ya wanawake ambao walikuwa/ waliwahi kuolewa, waliwahi kupitia ukatili wa kingono au ukatili wa kimwili kutoka kwa wenzi wao. Katika kipindi cha kuishi, mwanaume ana uwezekano wa kujihusisha na wanawake wengi zaidi kingono (6.7) ikilinganishwa na wanawake (2.3). Kumbe, wanaume wanapaswa kuhusishwa moja kwa moja katika harakati zinazofanyika kuirudisha heshima ya ndoa. Mwanaume anapaswa ahusishwe kama mwenzi, wakala wa mabadiliko na pia, mhusika mkuu katika harakati za kuisimamia misingi ya ndoa.
JE, NIKO “TAYARI” KWA NDOA?
Kigezo cha “utayari na hiyari” ni cha lazima kabla ya kufungwa kwa ndoa. Pamoja na vyote hivyo nilivyoviainisha hapo juu, ni lazima kabla ya kuamua kuingia katika ndoa, kila mmoja ajiulize swali hili na kujipa majibu yanayoridhisha. Yafaa sana ikiwa, anayefanya maamuzi anakuwa na uhakika pasi na shaka juu ya kile alichoamua kwa kuwa, wengi huingia kwenye ndoa bila ya kuwa na “sababu za kufanya hivyo”. Sababu za kuingia kwenye ndoa ni vema pia zikawa zenye mashiko na zinazojitosheleza na zinazoweza kuihakikishia ndoa uimara na uendelevu wake.
MAMBO YA KUZINGATIA
Wapo wengi wanaoendelea kuvumilia madhila makubwa katika ndoa zao kwa kigezo cha “malezi na ustawi ya watoto”. Ni ukweli usio na mashaka kuwa, kuvunjika kwa ndoa hupelekea madhara hasi kwa wanandoa wenyewe na hasa watoto. Tafiti nyingi zinathibitisha kuwa, watoto wengi wanaathirika zaidi kiuchumi, kihisia, kijamii, kimalezi, kielimu na hata kiimani pale wazazi wanapotengana (Gabriella D. B, 2017, Afifi T. O et al 2006) Malinda M.S, 2017, Ubong E. Eyo, 2018).
Hata hivyo, katika tafiti hizo, madhara ya ukatili yanaelezwa waziwazi jinsi yanavyomomonyoa na/au kuzibomoa kabisa familia hizi. Inapotokea mwanandoa mmoja anasababisha maumivu, ulemavu au kifo cha mwenzi wake, majeraha yanayoipata familia na hasa watoto yanakuwa ni mara dufu kwa yale yatokanayo na kutengana.
Kwa mujibu wa sheria ya ndoa, mzazi yeyote anaweza kuomba apewe amri ya kukaa na mtoto baada ya ndoa kuvunjika. Mahakama ina mamlaka ya kuamua mtoto ataishi na nani pindi ndoa inapovunjwa na baada ya ndoa kuvunjika. Amri ya kubeba dhamana ya malezi ya watoto inaweza kutolewa kwa baba, mama au ndugu wa karibu wa watoto. Hata hivyo, bila kujali kuwa watoto watakaa na nani, mume na mke watatakiwa kuchangia kutoa matunzo kwa ajili ya watoto, na kuhakikisha haki zao za msingi kama elimu, chakula, mavazi, kutibiwa, hazipotei (TLS 2015 Uk. 12).
Uwepo wa sera zinazohamaisha usawa, sheria pamoja na maazimio mbalimbali vinapaswa kuwa chachu ya kuzifanya ndoa kuwa sehemu salama za kuishi na sio “pahala pa manyanyaso”.
HITIMISHO
Mwanamuziki nguli katika miondoko ya Pop, Madonna, aliwahi kunukuliwa akisema; “Maisha ni mafupi. Mawazo yangu ni kuwa, ninapotaka kufanya jambo, nalifanya mara moja” (David Evans, 2008 Uk. 42).
Ingawa msingi mkuu tunaoupata katika tafsiri ya ndoa ni ‘ndoa kuwa muunganiko wa kudumu’, msingi huu usiwe sababu ya namna yoyote, ya yeyote aliyeko katika ndoa kushiriki kwa namna yoyote kuyafanya maisha ya mwingine kuwa handaki lenye moto. Uvumilivu wa manyanyaso kwa kigezo cha kuidumisha ndoa ni ukatili dhidi ya binadamu. Ni wakati wa kila anayepitia maumivu yasiyohimilika kuamua kubadili mtazamo wake haraka kabla “ndoa yake haijawa handaki la manyanyaso”.
(Unaweza kupakua andiko zima kwa mfumo wa PDF kupata rejea zilizotumika na pia kulitumia andikohili kama rejea katika kazi zingine)
TIMOTHY PETER KIRAKA MSUYA
timothyzone10@gmail.com
+255 763 305 605 | +255 674 656 539
ARUSHA, TANZANIA

- Ukatili baina ya wanandoa, iwe kwa maneno, matendo au kutokutimiza wajibu; unaoweza kuthibitishwa.
- Usaliti, ugoni, kufumaniwa au kukataa makusudi kushiriki tendo la ndoa
- Kuingiliwa kinyume na maumbile
- Kutengana kati ya wanandoa kwa zaidi ya miaka mitatu bila kuwepo sababu ya msingi
- Kichaa kisichotibika kilichothibitishwa na madaktari
- Kifungo cha mwenza kisichopungua miaka 5 au kifungo cha maisha na zingine